![]() |
Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU la maombi kisha tuombe maombi ya ushindi.
◼️Kibiblia neno nyumba linaweza kuwakilisha familia, ndoa, ukoo au jengo la mahali ambako watu wanaishi.
◾Nyumba inaweza ikabeba vitu kiroho na vitu hivyo vinaweza kuwa ni vitu vizuri au vitu vibaya.
◼️Nyumba ikiwa na maana ya nyumba ya kuishi, ndoa, familia au ukoo pasipo ulinzi wa MUNGU huyo mwanadamu anayeamua kuilinda anafanya kazi bure.
✓✓Hivyo ndoa, nyumba, familia au ukoo vinahitaji sana ulinzi wa MUNGU na si vinginevyo.
Zaburi 127:1 ''BWANA asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. BWANA asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure. ''
✓✓Hakika ndoa yako au nyumba yako inahitaji ulinzi wa MUNGU.
✓✓Ukoo wako au familia yako inahitaji ulinzi wa MUNGU.
Mambo machache kuhusu nyumba hata upate msukumo wa kuombea.
1. Nyumba/familia inaweza ikabeba adhabu kwa sababu ya makosa ya mmoja kutoka familia hiyo.
Mwanzo 20:18 ''Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu.''
✓✓Nimesema neno nyumba kibiblia lina maana zaidi ya moja, hapa tunaona kwamba familia ya Abimeleki yote yaani wote wa jamaa yake alioishi nao matumbo yao ya uzazi yalifungwa ili wasipate kuzaa kwa sababu tu ya kosa la Abimeleki kumchukua mke wa Mtu wa MUNGU akitaka kumuoa.
Je familia yenu au ukoo wenu unapata adhabu kwa sababu ya kosa la nani?
◼️Ukiona hivyo ujue dawa ya kufuta adhabu hiyo ni kutubu toba ya kweli itakayokubalika mbele za MUNGU.
Sasa unaweza kujiuliza kwanini akosee mtu mmoja harafu adhabu iwapate familia nzima au ukoo?
✓✓Ndugu, wewe unaunganishwa na familia yako kiroho hivyo usipojua kujinasua kimaombi unaweza kuteswa hata na vifungo vya giza kwa sababu ya kosa la babu yako aliyeamua kumkataa YESU Mwokozi na akaamua kufuata miungu na mashetani.
2. MUNGU anaweza kuizingira familia kwa sababu ya ucha MUNGU wa kiongozi wa familia.
Ayubu 1:10 ''Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.''
✓✓Ayubu kama kiongozi wa familia alikuwa mcha MUNGU safi na kitendo hicho kilipelekea familia yake kuzingirwa na MUNGU kwa ukigo pande zote.
✓✓Ukiona ucha MUNGU umesababisha kuzingirwa na MUNGU basi ujue kwamba kuna familia viongozi wa familia sio wacha MUNGU hivyo hakuna kuzingirwa na MUNGU ndio maana majanga hayaishi.
◼️Ndugu, ukiokoka wewe na ukajitambua kiroho wewe unakuwa rango la familia na kiroho unakuwa kiongozi wa familia au ukoo hivyo familia yako wanaweza kukaa salama kwa maombi yako.
3. Nyumba/ukoo/familia inaweza kubeba laana.
Mithali 3:33 '' Laana ya BWANA i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki.''
Sasa inawezekana unatokea familia iliyolaaniwa labda kwa sababu kiongozi wa familia alimwaga damu ya mtu asiye na hatia.
Inawezekana unatokea ukoo uliolaaniwa kwa sababu ya maovu mabaya yaliyokithiri kwa watu wanaotokea ukoo huo.
✓✓Wewe uliyepata neema ya kuokolewa na Bwana YESU inakupasa sana kujinasua kwenye laana za ukoo au familia au nyumba maana usipojua kuomba unaweza hata wewe ukashikiliwa na laana hiyo hiyo.
◼️Daudi alikuwa ameokoka kuliko hata wewe, alikuwa muombaji kuliko wewe na alikuwa Mtumishi wa MUNGU lakini ikulu au ofisi aliyoirithi ilikuwa na adhabu kwa sababu ya makosa ya mtangulizi wake, madhara ya adhabu ya ofisi hiyo yalimpata hadi Mtumishi wa MUNGU Daudi ambaye ni kosa la mtangulizi wake na sio kosa lake, adhabu ilimfuata na yeye lakini kwa sababu Daudi alikuwa muombaji ilibidi aombe maombi ya kuuliza chanzo cha tatizo na MUNGU akamwambia kwamba ni kwa sababu ya mtangulizi wake kwenye ofisi hiyo, hata wewe unaweza kuadhibiwa kiroho kwa kosa la baba yako au babu yako kama hutajitambua na kuomba ili kujitenga na adhabu hiyo.
2 Samweli 21:1 '' Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.''
✓✓Hivyo kuombea familia, nyumba au ofisi unayoingia huku alikuwepo mtangulizi hapo lifanye kuwa jambo la lazima.
✓✓Inawezekana ofisi yako ina laana hivyo hata anayeingia hapo laana inaambatana naye, ndugu jitambue na omba ili kujiondoa wewe kwenye laana ya familia, ukoo au nyumba.
✓✓Kuna nyumba zimejengwa juu ya ardhi iliyobeba laana hivyo lazima ujue kuomba ili kujitenga na laana iliyo katika ardhi kwa ajili ya watakaojenga juu yake.
Yoshua 6:26 '' Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.''
Vipi kama unakaa katika ardhi ambayo kila mtoto wa kwanza kuzaliwa lazima afe?
✓✓Ndugu, unahitaji sana kuomba juu ya familia, nyumba au ukoo na ardhi yake.
4. Familia inaweza kubarikiwa na MUNGU kwa sababu ya uwepo wa Mtumishi wa MUNGU anayeishi maisha matakatifu.
Mwanzo 39:5 '' Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, Bwana akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.''
✓✓Vipi kwenu kama hamna Mteule wa KRISTO, Babu zako na wazazi wako kila siku wanapishana tu kwa waganga wa kienyeji, hapo ujue kwamba kwenu hakutakuwa na baraka bali laana, hivyo inakupasa sana kuombea nyumba yenu, uzao wa mama yako, familia yenu na ukoo.
5. Kuna nyumba/Familia/ukoo miguu ya wahusika haikaagi nyumbani.
Mithali 7:11-12 '' Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake. Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia.''
✓✓Inawezekana wewe huwa hutulii nyumbani yaani miguu yako kila muda inatamani kutembea, inawezekana ulirithi kwa baba yako, inawezekana nyie ukoo mzima wanaume huwa kazi yenu ni kuzunguka tu, wakati mwingine hata ndoa zinakufa kwa sababu baba wa familia miguu ni kama inawasha akikaa nyumbani, kila muda anatamani kutembea tu.
✓✓Kama familia yenu au ukoo mna tatizo hilo wakati mwingine ni kwa sababu ya nguvu za giza, hivyo omba ukikomboa miguu yako kiroho.
✓✓ Kuna mpaka familia au ukoo watu wa familia hiyo au ukoo wakijenga nyumba hawana kibali cha kukaa katika nyumba hizo, kwa sababu ya vifungo vya giza vya kuwazuia kukaa kwenye nyumba zao.
6. Kuna nyumba/familia/ukoo mabaya hayaishi.
Mithali 17:13 '' Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake. ''
✓✓Inawezekana mama yako au baba yako alirudisha mabaya badala ya mema kwa watu fulani na hiyo ikapelekea mabaya kutokuondoka katika nyumba yake yaani nyumba, familia au ukoo kama ataanzisha ukoo.
✓✓Inawezekana babu yako au bibi yako alikuwa mtu wa kurudisha mabaya kwa watu hata waliomtendea mema hivyo kutengeneza kifungo kwenye ulimwengu wa roho kinachoitwa''Mabaya hayataishi kwenye nyumba'' sasa kwa sababu mtu huyo alianzisha familia maana yake mabaya hayatakiwi kuisha katika familia yake, kwa sababu amezaa watoto na wajukuu hivyo amekuwa na ukoo na bado mabaya hayatakiwi kuisha katika nyumba yake.
◼️Ndugu, kama kuna tatizo kama hilo kiroho shughulikia kimaombi na MUNGU atakupa neema hivyo mabaya hayo hayatakupata wewe na familia yako mpya uliyoanzisha.
Zaburi 91:10 '' Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.''
7. Kuna nyumba/familia ni salama.
Ayubu 21:9 '' Nyumba zao zi salama pasina hofu, Wala fimbo ya Mungu haiwapigi.''
Sasa vipi kama nyumba yenu sio salama?
Vipi kama familia yenu sio salama?
✓✓Ndugu ombea nyumba yako na familia yako na ukoo wako.
8. Kuna nyumba/familia ni watumishi wa KRISTO na kuna familia ni watumishi wa shetani.
Yoshua 24:15 '' Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA.''
◼️Kuna faida kubwa kuwa na familia yenye watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU na ni hasara kuu kuwa na familia au ukoo ambako kumejaa watumishi wa shetani.
✓✓Watumishi wa shetani ni pamoja na wachawi, waganga wa kienyeji, wanajimu na watu maarufu kwenye jamii wanaotumia nguvu za giza au wanaomtumikia shetani, wakiwemo waimbaji wa nyimbo za kidunia au waigizaji maarufu ila wanatumia nguvu za giza, au wacheza mpira maarufu ila wanatumia nguvu za giza..
✓✓Inawezekana familia yenu au ukoo kumejaa watumishi wa shetani, ndugu inakupasa sana kuiombea familia yako au ukoo ili kusiweko watumishi wa shetani.
Kumbuka mtumishi wa shetani anaweza kutoa hata kafara kwenye madhabahu za giza, vipi kama ukichaguliwa wewe au mtoto wako ili kutolewa kafara?
Kumbuka mtumishi wa shetani anaweza kuadhibiwa na anayemtumikia hivyo adhabu ikaelekezwa kwa familia au nyumba na wewe unahusika.
Ni hatari sana kuwepo mtumishi wa shetani yeyote katika familia yenu au ukoo.
✓✓Unayo nafasi leo ya kuomba na Bwana YESU atakutenga mbali na adhabu za kipepo zinazowafuatilia watu wa familia yako au ukoo wako na wewe ukiwemo.
Baadhi ya aina ya maombi unayopaswa kuomba juu ya nyumba au familia au ukoo wako.
1. Tubu kwa ajili ya makosa ya wahusika wa nyumba au familia au ukoo wako.
Isaya 59:1-2 '' Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.''
◼️Unapotubu kama kuna adhabu au laana basi toba hiyo itazuia adhabu yaani MUNGU atawandolea laana au adhabu.
2. Ombea familia yako au nyumba au ukoo juu ya kufunguliwa vifungo vya giza na adhabu za kipepo.
Luka 4:18 '' ROHO wa BWANA yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, ''
3. Ombea familia yenu mafanikio ya kiroho na kimwili na kiuchumi.
Zaburi 112:3 '' Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele. ''
4. Futa kumbukumbu mbaya kwenye ardhi ya nyumba yenu.
Yeremia 22:29-30 '' Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la BWANA.
BWANA asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda.''
5. Ombea nyumba yako au nyumba yenu au familia iwe moto kwa adui ili isichezewe na mawakala wa shetani.
Obadia 1:18 '' Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa BWANA amesema hayo.''
6. Ombea usingizi mzuri na mtamu kwa nyumba yako au familia.
Mitahli 3:24 '' Ulalapo hutaona hofu; Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu.''
7. Ombea neema ya Wokovu wa KRISTO YESU iambatane na kila mwanafamilia yenu au mwana ukoo wenu.
2 Kor 13:24 ''Neema ya Bwana YESU KRISTO, na pendo la MUNGU, na ushirika wa ROHO MTAKATIFU ukae nanyi nyote.''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa na somo hili kuna wakati nitalifafanua zaidi ndani ya kitabu.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu
Hapa chini ni MAOMBI YA KUOMBEA FAMILIA, UKOO AU NYUMBA UNAYOKAA. Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda.
MAOMBI YA KUOMBEA FAMILIA, UKOO AU NYUMBA UNAYOKAA.
MUNGU Baba Mwenyezi ninakushukuru kwa kunilinda na kunipa uzima.
Nikakushukuru kwa kuilinda nyumba yangu na familia yangu.
Ninakushukuru maana umeachilia neema ya ajabu katika KRISTO YESU hivyo BWANA kwa ulinzi wako na neema yako ya ajabu ''Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako.'' Kama Zaburi 18:49 inavyosema.
Niko mbele zako sasa ninatubu kwa ajili yangu mwenyewe, natubu pia kwa ajili ya nyumba yangu na nyumba ya baba yangu, ninatubu kwa ajili ya familia yangu na ukoo wangu.
Neno lako linajulisha katika Isaya 59:1-2 kwamba dhambi na uovu vinaweza kuuficha uso wako MUNGU hata usitusaidie hivyo ninatubu leo kwa ajili ya kila chanzo cha tatizo la familia au ukoo au nyumba yetu, JEHOVAH uliye hai ninaomba unisamehe mimi na familia yangu na ukoo wangu.
Nimejifunza mambo mengi juu ya nyumba, familia, ardhi na ukoo kupitia somo hili hivyo ninaomba MUNGU wangu unisaidie na kunifungua ili nisifuatiliwe tena na nguvu za giza zilizokamata familia au ukoo wetu.
Mwanzo 20:18 inaonyesha kwamba kosa la mtu mmoja katika familia linaweza kusababisha adhabu kwa watoto wake au ndugu zake au ukoo wake, MUNGU Baba kama iko adhabu au laana au tatizo la kiukoo lililo na chanzo katika ulimwengu wa roho kwa makosa ya mwana familia au mwana ukoo, Ee MUNGU Baba ninaomba utusamehe na damu ya YESU KRISTO ya agano jipya ninaomba kwako sasa ifute adhabu hiyo na laana hizo.
Ninajitenga sasa na kila adhabu iliyotokana na wazee wangu kuabudu miungu, ninajitenga na laana za ukoo zilizotokana na ukoo wangu kuwa wauaji au waabudu mizimu.
Ninajitenga na kila mpango wa shetani juu ya ukoo wangu, ninajitenga na kila ajenda ya kichawi juu ya ukoo wangu, ninajitenga na kila mpango wa wakuu wa giza juu ya nyumba yangu, katika jina la YESU KRISTO ninajitenga hivyo kuanzia sasa hakuna nguvu za giza za kiukoo au kifamilia zitanipata.
Kila laana ya ukoo naifuta kwa kutumia damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu.
Kila laana iliyo katika ardhi yangu au nyumba yangu, naifuta kwa kutumia damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu.
Kila majini na wakuu wa giza waliochaguliwa kuzimu ili kufuatilia familia yangu tu au ukoo wangu ninawafukuza sasa kwa jina la YESU KRISTO na hawatarudi kwangu tena.
Kama watu wa familia yangu au ukoo wangu walirogwa ili wasiwe wanakaa nyumbani, nafuta huo uchawi, naufuta kwa jina la YESU KRISTO.
Kama kuna mabaya yamekusudiwa kutupata sisi tu na familia yetu au ukoo wetu, sasa nafuta ratiba hiyo kwa jina la YESU KRISTO.
Katika jina la YESU KRISTO ninabomoa na kuvunja kila madhabahu ya kipepo iliyo katika nyumba yetu, naibomoa madhabahu hiyo na kuivunja katika jina la YESU KRISTO.
Kila mtu wa ukoo wetu au familia yetu anayetumika kishetani hadi kusababisha vifungo vya giza, kuanzia sasa mtu huyo ninaziharibu nguvu za giza zinazomtumia kipepo, naachilia damu ya YESU KRISTO juu ya madhabahu ya giza anayoitumia na nafuta kila kusudi la giza kwake.
Kila ratiba ya kishetani juu ya ukoo wangu au familia yangu, hiyo ratiba iliyotengenezwa kuzimu ninaichoma kwa moto wa jina la YESU KRISTO.
Kila kalenda ya mateso, majanga au mikosi iliyoelekezwa katika nyumba yangu au familia yangu, hiyo kalenda naifuta kwa jina la YESU KRISTO.
Kila ramani iliyochorwa na kutengeneza na wakuu wa giza ili sisi kama familia au ukoo tutembee katika ramani hiyo, sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninaifuta hilo ramani na kuichoma moto kwa damu ya YESU KRISTO.
Nawakomboa sasa ndugu zangu wote, nawakomboa watoto wangu, nawakomboa ndugu zangu wa kuzaliwa, nawakomboa wazazi wangu, ninamkomboa kila ndugu katika familia yetu au ukoo wetu, ninawakomboa wote kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Kila laana au adhabu iliyo katika ardhi ya nyumba yangu au ya familia yetu, hiyo laana naifuta kwa kutumia damu ya YESU KRISTO, hiyo adhabu naibatilisha kwa damu ya YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Nafuta kila misingi ya kipepo katika nyumba yangu na familia yangu, naifuta kwa jina YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai milele.
Sasa niko mbele zako MUNGU wa Wokovu wangu nikiomba mambo haya matano juu ya nyumba yangu, familia na ukoo wangu.
Ninaomba neema ya Wokovu wa YESU Mwokozi katika familia yangu na nyumba yangu na ukoo wangu kama 2 Kor 13:24 inavyosema kwamba ''Neema ya Bwana YESU KRISTO, na pendo la MUNGU, na ushirika wa ROHO MTAKATIFU ukae nanyi nyote.''
Ninaomba nyumba yangu na familia yangu na ukoo wangu kuwe na uchumi mzuri na baraka zinazodumu kama Zaburi 112:3 inavyosema kwamba '' Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele.''
Kuanzia leo katika jina la YESU KRISTO nyumba yangu na familia yangu tutalala salama bila kukabwa wala kufuatiliwa na majini ndotoni, tutalala salama kama Ayubu 11:19 inavyosema kwamba '' Tena utalala, wala hapana atakayekutia hofu; Naam, wengi watakutafuta uso wako.''
Ninafuta kila kumbukumbu yangu au ya familia yangu au ya nyumba yangu iliyo kwenye ulimwengu wa roho wa giza, naifuta kumbukumbu hiyo kwa kutumia damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai milele.
Imeandikwa katika Mathayo 7:7 kwamba ''ombeni nanyi mtapewa'' hivyo nimeomba ili kufuta kila kumbukumbu yangu iliyotunzwa katika ulimwengu wa roho wa giza, hivyo kuanzia sasa hakuna kumbukumbu yangu kuzimu au kwa wachawi au kwa waganga au kwa mizimu na majini, tena hakuna kumbukumbu yangu kwenye madhabahu za giza, nakushukuru Bwana YESU Mwokozi wangu maana jina lako limeniweka huru leo.
Eee MUNGU Baba ninaomba sasa nyumba yangu na familia yangu iwe na moto wako ambao hakuna wakala wa shetani anaweza kuingia na kuroga au kufanya chochote.
Imeandikwa katika Obadia 1:18 kwamba '' Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa BWANA amesema hayo.''
Hivyo kuanzia sasa mimi ni mwali wa moto dhidi ya wachawi na majini na kila majeshi ya pepo wabaya.
Kuanzia sasa katika nyumba yangu na familia yangu kutakaa moto wa MUNGU unaounguza nguvu za giza na hizo nguvu za giza zitakuwa kama mabua makavu yaliyo tayari kuungua yakiguza tu moto.
MUNGU Baba ninakushuru maana najua sasa nimekombolea kwa damu ya thamani sana ya YESU KRISTO, Nyumba yangu na familia yangu imekombolewa kwa damu ya YESU KRISTO.
Najua mimi sasa ni mshindi niliyeshinda.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.
Ni katika jina la YESU KRISTO nimeomba na ninamshukuru MUNGU Baba.
Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza hata kuwa na maombi ya kufunga unaweza, pia baada ya maombi yako unaweza kufanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka n itakayoambatana na maombi juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho, huo ni utashi wako na sio agizo.
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na whatsapp).
Ubarikiwe sana.
Comments