![]()  | 
| Na Mwl Peter Mabula  Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi  | 
 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifune Neno la MUNGU la maombi ya ushindi mkuu.  
Ngoja nianze na shuhuda hizi za kweli ili ikurahisishie kunielewa vyema katika ufunuo wa leo.
◾Siku moja Mimi Peter Mabula nilikuwa namuombea mtu kwa simu na wakati naendelea na kumuombea ghafla alianza kupiga kelele kisha mapepo ndani yake yakaanza kuzungumza yakisema ''Wewe ni nani unayetaka kutuondoa ndani ya mtu  huyu wakati tuna uhalali wa kukaa ndani yake?'' 
 yaliendea kidogo kuzungumza na nikagundua kabisa kuna nguvu za giza ziko ndani ya watu fulani kwa sababu tu zina uhalali.
Mathayo 12:43-45 '' Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate. Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya.'' 
◼️Kulingana na maandiko haya tunagundua kwamba nguvu za giza kuna mahali zina uhalali wa kukaa, hata kama zikifukuzwa na kuondoka wakati mwingine zikikosa penye uhalali wa kukaa hutaka kurudi kule kwa mwanzo,  zikikuta bado uhalali wa kukaa upo basi zinaingia, zikikuta uhali haupo zinaondoka ili kutafuta mtu ambaye zitapata uhalali kwake kukaa.
◼️Kuna nguvu za giza  hutafuta uhalali wa kuvamia maisha ya Mtu na Mtu huyo akifungua mlango basi nguvu za giza huingia kwake na kuwa na uhalali wa kumtesa. 
◼️Dawa kuu ya kufuta uhalali wa Nguvu za giza kwako ni Wewe Kuokoka kwa Kumpokea YESU KRISTO Mwokozi kama Mwokozi wako, unaanza kuishi Maisha matakatifu ya Wokovu katika yeye.
◾Dada mmoja alikuwa anateswa sana na vifungo mbalimbali vya giza, siku moja akanipigia simu ili nimuombee na Mimi nikamuombea,  baada ya maombi usiku wa siku hiyo akaota ndoto akiona majitu ya ajabu  yakisema ''Tuna uhalali wa kukutesa kwa sababu umekataa kiti cha enzi cha umalikia wa kichawi ambacho ni bibi yako alitujulisha kwamba ni wewe ndio utakuja kuchukua nafasi yake katika ukoo wenu, sasa kwa sababu umekataa tutakupa mapigo mpaka  urudi kwenye nafasi hiyo maana mkataba alioingia bibi yako hauwezi kuvunjwa hata kama kwa sasa yeye ameshakufa''
Dada yule alinijulisha hayo aliyoyaona na alikuwa na hofu sana, tena akasema kwamba ni mara nyingi ameota ndoto akiona kiti kikiwa hakijakaliwa na mtu ila hakujua maana yake, kumbe ni kiti(Nafasi) ya kipepo aliyopangiwa tangu akiwa mtoto mdogo, sasa alipoamua kumpokea YESU KRISTO wakuu wa giza waliona wamemkosa hivyo wakati hajaimarika kiroho walijaribu kumpa mapigo na kumtesa ili arudi katika nafasi ya uchawi aliyoingizwa na bibi yake kwa maagano na kafara.
◾Dada mmoja tulikuwa tunamuombea Kanisani na wakati tunaendelea kuomba alidondoka na mapepo ndani yake yakaanza kusema ''Hatuwezi kutoka ndani ya mtu huyo maana tuna uhalali wa kukaa kwake, kwanza  jina lake ni sisi tulimpa, hivyo tuna uhalali wa kukaa kwake''
◾Ndugu mwingine tena tulikuwa tunamuombea Kanisani na nguvu za giza ndani yake zikasema kwamba ''Hatuwezi kutoka kwa huyu maana ana vitu vyetu na hivyo ndivyo vinatupa uhalali wa kukaa kwake''
✓✓Wako watu nguvu za giza zilipata uhalali kwa sababu ya kujiambatanisha na mambo ya kishetani, mfano mmojawapo kati ya mingi ni  mtu anaambiwa ana nyota yake kulingana na mwezi aliozaliwa kisha anapewa maelekezo na wanajimu juu ya tarehe fulani na nini afanye ili afanikiwe jambo fulani, vitu hivyo humfanya mtu kumilikiwa na majini hivyo kujikuta baadae anateseka.
 ✓✓Mkristo mwenye akili timamu hatakiwi kuwa na nyota yake aliyoambiwa na wanajimu, ukifanya hivyo ujue unazipa nguvu za giza uhali wa kukaa kwako.
◼️Unajimu ni wavu wa shetani ili kuwakamata watu wa MUNGU, ndio maana wanajimu wote hakuna Mkristo aliyeokoka  hata mmoja, wote ni waganga wanaotumia majini n.k
◼️Biblia inasema kwamba Wanajimu, wachawi wala waganga wa kienyeji hawawezi kumfunulia mtu  kitu cha maana hata kimoja.
Danieli 2:27 '' Danieli akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu; ''
✓✓Wewe unayehitaji msaada wa waganga wa kienyeji au wanajimu ujue unamfungulia tu mlango shetani ili aje akumiliki na kukufunga vifungo.
✓✓Wewe unayejiona una nyota yako ujue umenaswa kwenye wavu mbaya wa kipepo ili nguvu za giza ziwe na uhalali kwako .
◾Dada mmoja siku moja aliniambia kwamba kila mara huwa anaota ndoto akiwa kwa mganga wa kienyeji, sasa alijaribu kuwashirikisha watu wake wa karibu na wakamwambia kwamba aende kwa waganga wa kienyeji. Aliniponijulisha nilisikitika sana maana watu wake wa karibu walitaka kumpoteza, nilimjulisha kwamba ndoto hiyo inaonyesha ni wapi alifungwa vifungo vya giza vinavyomtesa, tulianza maombi ya kuharibu kila vifungo vya giza alivyofungwa kwa waganga wa kienyeji na tatizo lake likaisha.
◼️Ndugu, nguvu za giza kama zina uhalali kwako, kwa afya yako, kwa uzao wako, kwenye ndoa au uchumba, kwenye kazi au kwenye biashara yako leo kuna nafasi ya maombi ya kufuta uhalali wa hizo nguvu za giza na kuanzia leo hazitakufuatilia tena.
✓✓Kuna nguvu za giza hutafuta uhalali wa kukaa kwa mtu baada ya kumlaghai mtu huyo, ni hatari sana.
◼️Wana wa Isareli MUNGU aliwaonya mapema ili wasitoe nafasi ya nguvu za giza kuwa na uhalali kwao kupitia maagano n.k maana ingekuwa tanzi kwao kama wangenaswa na uhalali wa nguvu hizo za giza.
Kutoka 23:32-33 ''  Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao. Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni tanzi kwako.''
✓✓Uwe makini sana maana kuna nguvu za giza zinaweza kukaa ndani yako kwa sababu tu zina uhalali wa kukaa kwako, ukiuondoa uhalali huo zitaondoka na hazitakurudia tena.
Kuna majini wanaweza kumtesa mtu kwa sababu tu wana uhalali kwa mtu huyo baada ya mtu huyo kuingia agano la kishetani.
◾Inawezekana unajiuliza inakuwaje hadi nguvu za giza zinakuwa na uhalali kwako?
Ngoja nikujulishe.
Vyanzo vya nguvu za giza kuwa na uhalali kwa mtu.
Baadhi ya maeneo yanayoweza kuzipa uhalali nguvu za giza kukushikilia ni.
1. Jina lililo na maagano ya kipepo.
Mithali 22:1 '' Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu. ''
✓✓Ni heri kuwa na jina jema kuliko utajiri.
Kuna watu majina yao wamepewa  kutokea kuzimu kwa siri sana hivyo jina hilo kuzipa uhalali nguvu za giza kumtesa mtu.
Inawezekana una jina ulipewa na wazazi wako na wao waliambiwa na watu wao wa karibu na kumbe jina hilo chanzo chake lililetwa na mizimu, ni hatari sana.
✓✓Jina lako kama lina maagano ya kipepo ujue utateseka sana hadi utakapojua aina ya maombi ya Kuomba kulingana na ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
2. Adhabu za kipepo za  urithi ulizorithi kwa wazazi wako au babu zako au nafasi kazini uliyorithi kutoka kwa mtu aliyekutangulia.
Maombolezo  5:7 '' Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao.''
Adhabu za kipepo za kurithi pamoja na maagano ya kipepo ya kurithi vinaweza kuwapa  nguvu za giza uhalali wa kukuonea kama hutajua namna ya kujinasua kimaombi.
◼️Daudi alirithi tatizo ambalo lilifanyika katika utawala wa kabla yake.
2 Samweli 21:1 '' Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni. ''
✓✓Yaani nafasi ya Daudi ya ufalme ilikuwa ina adhabu ya kosa la mtangulizi wake katika nafasi hiyo hiyo.
✓✓Inawezekana ni wewe umefungua biashara katika flemu ambayo aliyehama hapo aliingia mikataba ya giza inazozipa nguvu za giza uhali hapo.
✓✓Inawezekana umepewa nafasi kiserikali na mtu wa kabla yako katika nafasi hiyo alitakiwa kuadhibiwa hivyo adhabu kwa sababu ni ya kiti basi wewe unayechukua nafasi hiyo unapatwa na madhara.
◼️Ndugu inatakiwa sana kuomba  katika Jina la YESU KRISTO ili kuondoa uhalali wa nguvu za  giza katika kila maeneo yako na baraka zako.
3. Kutunza vitu vya kipepo.
Mwanzo 35:2-4 ''Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu. Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia MUNGU madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu.''
Watu wa nyumba ya Yakobo walikuwa na miungu migeni na miungu lazima iambatane na nguvu za giza na kupitia miungu hiyo ujue umezipa uhalali nguvu za giza kukufunga vifungo, Yakobo kwa kujua madhara ya miungu aliwaambia kwamba waondoe miungu migeni yote maana ingewakosesha.
✓✓Nguvu za giza zinaweza kupata uhalali kwa mtu kwa sababu mtu huyo anahusika na miungu.
Je wewe una miungu gani? iondoe miungu hiyo na jitenge nayo.
4. Kurogwa.
Nahumu 3:4 '' Kwa sababu ya wingi wa ukahaba wa yule kahaba mzuri, yule bibi wa mambo ya uchawi, auzaye mataifa kwa ukahaba wake, na jamaa za watu kwa uchawi wake.''
✓✓Yuko bibi wa mambo ya uchawi, yuko babu wa mambo ya uchawi.
✓✓Kazi ya mchawi ni kuroga hivyo wako watu wamerogwa na uchawi huo umezifanya nguvu za giza kuwa na uhalali kwa mtu husika.
Ndugu kama yuko mtu amerogwa au ni wewe mwenyewe unahisi ulirogwa basi futa uhalali wa nguvu za giza kukuonea kwa Maombi katika Jina la YESU KRISTO.
5. Ardhi iliyobeba vitu vya giza vya kuwafunga wanaokaa juu yake.
Isaya 13:20-21 ''Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi. Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko. Lakini huko watalala hayawani wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko. ''
✓✓Ziko ardhi za namna hii na yako maeneo ya namna hii ambayo kuna vitu vya kishetani vingi na maeneo hayo hayajatakaswa kwa damu ya YESU KRISTO.
✓✓Ukikaa maeneo yaliyobeba vitu vya giza ujue unaweza kuzipa uhalali nguvu za giza kukuonena na kukufuatilia.
✓✓Kuna ardhi zimelaaniwa hivyo kama utaishi maeneo hayo unaweza kujikuta unateseka bila kujua chanzo cha tatizo.
Mfano ni huu, Yoshua 6:26 ''Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.''
6. Kujiunganisha na madhababu za za giza.
Isaya 28:15 '' Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli;   ''
✓✓Madhabahu za giza ndio wawakilishi wa kuzimu hivyo ukiingia  agano na madhabahu za giza ujue umeingia agano na kuzimu na watenda kazi wa kuzimu ambao ni nguvu za giza lazima tu zitakuwa na uhalali kwako.
✓✓Madhabahu za giza ziko kwa waganga wa kienyeji, wachawi n.k
✓✓Ukijiunganisha na madahabahu yeyote ya giza ujue umezipa uhalali nguvu za giza kukuonea.
7. Kuabudu miungu na kuingia mapatano na mawakala wa shetani.
Kutoka 20:4-5 '' Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.  Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni MUNGU mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,''
◼️Lakini pia mtu anaweza kuingia kwenye vifungo  na mateso kwa sababu mtu huyo amemwasi MUNGU katika maeneo yafuatayo.
1. Kumwacha MUNGU na kufuata miungu.
Yoshua 24:20 '' Kama mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema.''
2. MUNGU hatamkemea wakala wa shetani kama hutoi Fungu la kumi na Dhabihu.
Malaki 3:11 '' Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi.''
✓✓Inawezekana wewe sio mwaminifu katika kutoa Zaka hivyo MUNGU hawezi kuwakemea maadui zako, hivyo unaweza kujikuta mawakala wa shetani wanakufanya kila wanachotaka kwa sababu tu wewe huwa hutoi zaka kamili.
3. Unapoacha kumtegemea MUNGU wala kumtumainia katika KRISTO YESU.
Yeremia 17:5 '' BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.''
◼️Jinsi ya kuondoa uhalali wa nguvu za giza kwako.
1. Tubu kwa ajili ya chanzo cha nguvu za giza kupata uhalali kwako.
Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''
2. Hakikisha YESU KRISTO ni Mwokozi wa maisha yako.
Mathayo 11:28 '' Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.''
3. Omba au ombewa maombi ya kufunguliwa kutoka nguvu za giza.
Yakobo 5:16 '' Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.''
4. Kwa maombi ondoa uhalali wa nguvu za giza kwako.
Isaya 54:14 ''Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.''
5. Ziangamize kwa maombi nguvu za giza zilizokuwa na uhalali kwako.
Yeremia 51:20-21 ''Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake; ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa na somo hili kuna wakati  nitalifafanua zaidi ndani ya kitabu.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu
Hapa chini ni MAOMBI YA KUUFUTA UHALALI WA NGUVU ZA GIZA  ZILIZOKUWA NA UHALALI KWAKO.
 Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 
MAOMBI YA KUUFUTA UHALALI WA NGUVU ZA GIZA  ZILIZOKUWA NA UHALALI KWAKO.
 Baba katika jina la YESU KRISTO ninakuabudu na ninakushukuru kwa kunilinda na kunipa uzima.
Ninaomba MUNGU Muumbaji wangu unisamehe dhambi zangu zote, maovu yangu yote na makosa yangu yote.
Ninaomba BWANA kwa neema yako katika Damu ya YESU KRISTO unitakase dhambi zangu zote, maovu yangu yote na uovu wangu wote.
Niko hapa YAHWEH ninaomba unisamehe kila kosa langu na dhambi zangu zilizowapa uhalali nguvu za giza kunionea mimi(taja Jina lako)
Ninatubu kwa ajili ya makosa na dhambi za wazazi wangu na wote walionitangulia ila adhabu zao zimeelekezwa katika maisha yangu.
Ninakushukuru Bwana YESU maana kuanzia sasa wewe ni Mwokozi wa roho yangu na maisha yangu, naomba unipe neema Bwana YESU nitembea katika kusudi lako na katika neno lako nitembee na kufanikiwa kimwili na kiroho.
Ninakuomba MUNGU Baba unifungue kutoka vifungo vyote vya giza nilivyofungwa tangu nikiwa tumboni mwa Mama yangu, nakuomba BWANA Mwenyezi unipe neema ya kufunguliwa na kuwa huru mbali na nguvu za giza zote.
Katika jina la YESU KRISTO  kila nguvu za giza zilizokuwa na uhalali kwangu, huo uhalali naufuta sasa kwa kwa jina YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
Kila uhalali wa mapepo kuvamia baraka zangu, huo uhalali naufuta kwa kutumia damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO.
Kila uhalali wa wachawi kunitesa au kunifunga vifungo, huo uhalali naufuta kwa kutumia damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO.
Kila uhalali wa wakuu wa giza kunishikilia popote, huo uhalali naufuta kwa  jina la YESU KRISTO.
Kila uhalali wa washirikina na wanga kunifunga vifungo, huo uhalali naufuta kwa jina la YESU KRISTO.
Kila uhalali wa wanadamu wanaotumika kipepo kunitesa,
huo uhalali naufuta kwa  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai milele.
 Kila uhalali majini na mizimu kufuatilia maisha yangu au ndoa yangu au uchumba wangu au uchumi wangu au uzao wangu, huo uhalali naufuta kwa  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu.
 Kila uhalali nguvu za giza zilizotumwa kutoka kwa mganga wa kienyeji kuja kwangu, huo uhalali naufuta kwa kutumia damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai milele.
 Kila uhalali wa mawakala wa shetani wa kila namna, huo uhalali naufuta kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Kuanzia dakika hii hakuna nguvu za giza zenye uhalali kwangu ndio maana  kwa kutumia damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO nazifukuza hizo nguvu za giza zote zitoke kwangu na hazitarudi tena milele.
Imeandikwa Yeremia 51:20-21  kwamba mimi ni rungu la MUNGU la kuharibu nguvu zote za giza, Biblia inasema  ''Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;''
 Hivyo sasa naachilia mapigo kwa kila wakala wa shetani aliyetuma nguvu za giza kwangu, naachilia mapigo kwa jina la YESU KRISTO.
Mapigo na yawafuate wachawi wote, waganga wa kienyeji wote, wakuu wa giza wote, majini wote, mizimu wote na kila nguvu za giza zilizokuwa zinatesa maisha yangu.
Imeandikwa katika Isaya 54:14 kwamba  ''Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.''
 Hivyo kuanzia sasa, kwa  jina la YESU KRISTO nitakuwa mbali na kuonewa na majini kama Isaya 54:14 inavyosema.
 Kuanzia sasa, kwa  jina la YESU KRISTO nitakuwa mbali na kuonewa na wachawi na wakuu wa anga na wakuuu wa giza  kama Isaya 54:14 inavyosema.
 Kuanzia sasa, kwa  jina la YESU KRISTO nitakuwa mbali na kuonewa na magonjwa ya kichawi na laana zote  kama Isaya 54:14 inavyosema.
 Kuanzia sasa, kwa  jina la YESU KRISTO nitakuwa mbali na kuonewa na kila mganga au aliyeniendea kwa mganga  kama Isaya 54:14 inavyosema.
 Kuanzia sasa, kwa  jina la YESU KRISTO nitakuwa mbali na kuonewa na wanadamu wanaotumika kipepo  kama Isaya 54:14 inavyosema.
 Kuanzia sasa, kwa  jina la YESU KRISTO nitakuwa mbali na kuonewa na majini mahaba au roho za kukataliwa  au mizimu  kama Isaya 54:14 inavyosema.
 Kuanzia sasa, kwa  jina la YESU KRISTO nitakuwa mbali na kuonewa na kuzimu kama Isaya 54:14 inavyosema.
 Kuanzia sasa, kwa kutumia damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO nitakuwa mbali na kuonewa na shetani na mawakala zake wote  kama Isaya 54:14 inavyosema.
 Ninakushukuru MUNGU wangu wa mbinguni maana katika wewe mimi(taja Jina ) sasa ni mshindi katika KRISTO YESU.
Niseme nini kwako JEHOVAH MUNGU wangu? 
Mimi sina cha kusema zaidi ninakushukuru kwa ukuu wako ulinzi na ushindi ulionipa katika jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Ni hakika kwamba kuanzia sasa mimi niko huru na nitaendelea kuwa huru mbali na nguvu za giza.
Ni katika jina la YESU KRISTO nimeomba na ninamshukuru MUNGU Baba.
Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza hata kuwa na maombi ya kufunga unaweza, pia baada ya maombi yako unaweza  kufanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka  itakayoambatana na maombi juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho, huo ni utashi wako na sio agizo.
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili, Ushauri, Whatsapp n.k)
Ubarikiwe sana.

Comments