Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
◾Rafiki yangu mmoja siku moja aliniuliza swali hili alisema "Samahani mtumishi Mabula kwa hili swali.... nilikuwa na mchumba tukaachana miaka nne imepita wala sina mawasiliano na yeye, mwezi ulioisha nilimuota na leo asubuhi nikamuota tunaoga wote. Na mimi kwa sasa niko na mchumba mwingine tunataka kuoana, je itakuwa na maana gani hii ndoto?
◾Mama mwingine ambaye yuko katika ndoa kwa zaidi ya miaka 15 siku moja aliniambia hivi " Kabla sijaolewa na huyu Baba nilikuwa na mchumba na tulikosea kwa kufanya dhambi ya uasherati uliopelekea kuachana, sasa kila Mara namuota ndotoni Mara akiwa kama mume wangu, Mara tukifanya mambo mbalimbali na kiukweli sijawahi kumuona tangu wakati huo ila japokuwa tuliachana lakini ndoto kumhusu yeye ninazoota zimenifanya nimuone ni mwanaume wa kipekee kwangu na ninampenda sana, natamani hata nimuone"
◾Kijana mwingine siku moja aliniambia hivi "Wakati nakaribia kufunga Ndoa na Mke wangu niliota ndoto kuhusu Dada ambaye tuliachana zamani na alinisaliti sana, sasa hata siku moja kabla ya kufunga Ndoa nilimuota huyo Dada akiwa kapendeza na akiwa kama Mke wangu, akili yangu ilivurugika kiasi nikadhani labda yule wa zamani ndie anapaswa kuwa Mke wangu na sio huyu ambaye masaa machache baadae nafunga nae ndoa"
◼️Ndugu hao niliwajibu kama nilivyojariwa kuwajibu ila jambo hilo lilibaki kama ujumbe moyoni mwangu ili kuwasaidia watu wengi zaidi, hili sio somo kamili ila siku moja nitafafanua vyema ila kwa sehemu unaweza kujifunza na kufunguliwa.
✓✓Katika utumishi kwa KRISTO nimekutana Mara nyingi na maswali ya watu kuwaota watu waliowahi kuwa na uhusiano nao kimapenzi zamani.
✓✓Zipo ndoa zimevunjika na ziko ndoa ziko matatani sana kwa sababu ya mwanandoa kuota Mara kwa Mara akiwa na mtu aliyewahi kuwa na uhusiano nae kabla ya ndoa.
Ndugu nisikilize vizuri itakusaidia.
◼️MUNGU anapokukataza kufanya uasherati ni kwa faida yako ndugu.
1 Wakorintho 6:18 " Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe."
✓✓Uasherati na uzinzi hutengeneza agano la kipepo, je umeingia agano la kipepo la uasherati na watu wangapi?
✓✓Maana wote uliozini nao uliingia agano nao.
✓✓Maagano hayo huweza hata kukuvunjia uchumba au ndoa n.k
◼️Neno la MUNGU linamtaka kila mtu kutokufanya uzinifu.
✓✓Kukutana kimwili kunatakiwa katika ndoa tu basi, na huko sio uzinzi wala uasherati tena Bali ni tendo la ndoa na tendo hilo huhusika na agano la ndoa.
✓✓Sasa watu wengi uzinzi na uasherati umewakosesha sana na kuwavuruga.
◼️Sasa unapomuota mtu uliyewahi kuwa naye kwenye uhusiano maana yake ni kwamba mlipokuwa wachumba mlitamkiana maneno yaliyotengeneza agano, yaani mfano alikuambia "Wewe ni wangu tu hata uende wapi" au ukamwambia "Nakupenda hadi siku nakufa"
maneno kama hayo na ya aina hizo yanaweza kukushikilia na kukuzuilia kuolewa na mtu mwingine hivyo yafute maneno yote, viapo vyote na kila connection ya kiroho kati yako na mtu uliyewahi kuhusiana naye kimapenzi.
✓✓Wadada wengi wamewakataa watu sahihi wa kufunga nao ndoa kwa sababu tu maagano na watu wao wa zamani yapo na yanajidhihilisha kwa ndoto.
✓✓Wapo wanaume wanapiga wake zao kwa sababu tu ndotoni huwaona waliowahi kuzini nao zamani hivyo hudhani walikosea kuoa, hali hiyo inapelekea kupunguza upendo kwa wenzi wao sahihi wa ndoa.
◼️Yanayowashikilia watu ni agano la kipepo la uasherati.
◼️Yanayowashikilia watu ni maneno ya kujitamkia wakati ukiwa katika furaha za uhusiano.
✓✓Maneno yanaumba.
Mithali 18:21 " Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake."
✓✓Maana yake unaweza kujiumbia uharibifu kwa maneno yako na unaweza kupata matunda ya ulivyoumba kwa kutamka, kama ulitamka katika mpango wa shetani ujue unaweza kupata madhara baadae.
◾Dada mmoja aliwahi kuwa na uhusiano na kijana Fulani, wakiwa shuleni, kwa sababu ya uasherati shetani alipanda magugu, na yalipoota hayo magugu uhusiano ukafa. Baadae yule mwanaume akapata mke na kuoa, Dada huyo baadae alipokuwa anahitaji kuolewa alikuwa anaingia kwenye maombi na ajabu akawa anamuota yule mwanaume ambaye tayari yuko kwenye ndoa. Dada huyu ilifika kipindi alidhani kwamba mwanaume yule ndie mume wake hivyo alingoja eti mke wa huyo mwanaume afe ili aolewe yeye. Yeye alipokuwa anamuota ndotoni alidhani anafunuliwa juu ya mume wake kumpe alikuwa anajulishwa kufuta maagano ya kipepo na mwanaume Huyo maana maagano hayo ndio yanamzuiliwa kuolewa.
✓✓Yeye alielewa tofauti alichoona ndotoni, wapo wengi wanapowaota watu wao wa zamani hudhani wamefunuliwa hao kumbe wanajulishwa juu ya kufuta maagano na viapo walivyoapiana na hao wa zamani maana hivyo ndivyo vizuizi vyao.
Dada huyo wakati katika uhusiano na mwanaume huyo walipokuwa shuleni waliapiana na kuahidiana mambo mengi,viapo hivyo ndivyo vilivyomshikilia.
◼️Madhara ya uasherati yapo mengi, baadhi tu katika kipengele cha Leo ni
1. Uasherati hutengeneza na kuambatana na viapo vya kipepo.
2. Uasherati ni agano la kishetani.
3. Uasherati huufanya mwili kuwa najisi kiroho.
✓✓Wengi kwa sababu ya unajisi huu husema wana roho ya kukataliwa.
4. Uasherati unaweza kutengeneza tabia mbaya na chafu sana.
✓✓Nimewahi kuwasiliana na watu wakihitaji msaada wa kiroho kwa sababu hawaoni furaha katika ndoa zao wakilinganisha na enzi za uasherati walizopitia zamani zilizowatengenezea mazoelea mabaya.
5. Uasherati humfanya shetani alete mtu wake ili ufunge nae ndoa, na sio yule ambaye MUNGU amekusudia kwa ajili yako.
Nini ufanye ili kujinasua kwenye hili.
1. Tubu kwa MUNGU kwa dhambi yako ya uzinzi na uasherati.
Zaburi 51:1-4 " Ee MUNGU, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu. Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima. Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu."
2. Futa kwa damu ya YESU KRISTO maagano yote yaliyotokana na uzinzi au uasherati.
1 Yohana 1:7-8 " bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote."
Mathayo 5:34 "lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;"
4. Elewa vyema maana ya unachokiona ndotoni kuhusu mtu uliyewahi kuwa na uhusiano naye na chukua hatua za kimaombi.
Ayubu 33:14-15 " Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;"
5. Ujue uongo wa shetani na uepuke.
Waefeso 6:11 "Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani."
Ayubu 42:6 "Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu Katika mavumbi na majivu."
7. Futa kumbukumbu ya kipepo iliyotunzwa ardhini katika eneo mlilofanyia uzinzi au uasherati au eneo ambalo mlitamkiana maneno na viapo.
Isaya 57:8 "Na nyuma ya milango na miimo umeweka kumbukumbu lako; kwa maana umejifunua nafsi yako kwa ajili ya mwingine, si kwa ajili yangu, ukakwea juu; umekipanua kitanda chako, nawe umefanya maagano na hao; ulikipenda kitanda chao hapo ulipokiona."
✓✓Kama hujui ni kwamba ardhi husikia na kutunza kumbukumbu, hivyo ardhi ya eneo uliliapiana au kuzini ilitunza kumbukumbu hizo.
Zingatia na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana.

Comments