MWILI, MOYO, ROHO NA NAFSI NI NINI?

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
Leo tunaangalia Mwili, Nafasi,Roho na Moyo ni nini.

Wakati Mimi Peter Mabula naanza kujifunza Biblia mwaka 2009 Kuna mambo 2 yalikuwa yananichanganya sana nikisoma Biblia. Mambo hayo ni pale ambapo nikisoma baadhi ya maandiko naona kwamba Mtu akifa anakwenda mavumbini yaani ardhini lakini maandiko mengine yanaonyesha Mtu akifa anaenda Mbinguni kwa MUNGU na maandiko mengine yanasema Kuna Mtu akifa anaenda kuzimu.

✓✓Adamu anaambiwa akifa ataenda mavumbini yaani ardhini.

Mwanzo 3:19 kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.

✓✓Mfano hapa Paulo anasema watakatifu wakifa wanaenda kukaa na Bwana YESU maana yake wanaenda Mbinguni.

2 Wakorintho 5:8 "Lakini tuna moyo mkuu; nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana."

✓✓Ukisoma Luka 16:22-23 unaona Lazaro baada ya kufa anaenda Eneo la Mbinguni na tajiri akifa akaenda kuzimu.

✓✓Hata YESU alimwambia mfungwa pale gerezani kwamba akifa ataenda pema peponi ambako ni sehemu ya Mbinguni.

Luka 23:43 "YESU akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi."

◼️Kwa habari ya Lazaro na tajiri niligundua mapema kwamba Mtu mwovu akifa katika uovu wake huenda kuzimu na Mteule wa KRISTO akifa katika Wokovu huenda paradiso yaani pema peponi ambako ni Mbinguni.

Swali ambalo likabaki likinichanganya ni kwamba Inawezekanaje Mtu mwema afe na andiko Moja liseme ameenda kwa MUNGU Mbinguni na lingine liseme Mtu huyo huyo ameenda mavumbini yaani ardhini.
Maswali haya yalinichanganya sana hadi pale nilipojifunza tofauti ya Mwili, nafasi na roho ndipo nikagundua Nini huenda ardhini na Nini huenda Mbinguni au kuzimu kwa waovu wasio na YESU KRISTO.
Naamini na Wewe utajifunza, Karibu sana.

Tuanze Moja kwa Moja kuangalia kipengele kimoja kimoja.

1. Roho ni nini?

✓✓Neno "roho" asili yake ni katika lugha ya Kiyunani likiitwa 
"Pneuma” ambalo maana yake kwa kiswahili ni “ pumzi ya uhai”.

Mwanzo 2:7 "Bwana MUNGU akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai."

◼️Roho au pumzi ya uhai huwekwa na MUNGU tu.

Mhubiri 12:7 "Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia MUNGU aliyeitoa."

✓✓Katika andiko hili tunaona tofauti ya Mwili na roho, mwili ni mavumbi na mavumbini hurudi ila roho hurudi kule MUNGU amepanga Kulingana na Maisha ya Mtu husika aliyoishi akiwa hai.

◼️Pumzi ya namna hii ambayo ni roho ni pumzi iletayo uzima yaani mtu anakuwa hai.

✓✓Bila roho hakuna mtu anaweza kuwa hai.

◼️Roho hasa ndio Mwanadamu mwenyewe na roho shetani Wala majini Wala Wanadamu hawawezi kuiua, Anayeweza kuiua roho ni MUNGU tu.

Mathayo 10:28 "Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.''

◼️Kama Kuna kitu Cha kwanza kabisa kwa umuhimu ambacho Mwanadamu yeyote anatakiwa kukuponya Cha kwanza ni roho yake dhidi ya jehanamu.
Na ataiponya roho yake kwa Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake na Kuokoka.

Yohana 3:16-18 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."


2. Nafsi ni nini?

✓✓Neno "Nafsi" ni sehemu ya mwanadamu inayohifadhi akili na hisia.

Zaburi 103:2 "Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, Wala usizisahau fadhili zake zote."

✓✓Hivyo kusema nafsi ya mwanadamu ni sawa na kusema akili,ufahamu na hisia zinakokaa.

◼️Maamuzi yote ya Mwanadamu hutoka katika nafsi.

2 Wakorintho 2:1 "Lakini nafsini mwangu nalikusudia hivi, nisije kwenu tena kwa huzuni."

✓✓Nafasi ya Mtu iliharibika ni vigumu sana Mtu huyo Kumcha MUNGU.

Kumbu 11:16 ""Jitunzeni nafsi zenu, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kutumikia miungu mingine na kuiabudu;""

✓✓Ilazimishe nafasi Yako kumtii KRISTO.

2 Wakorintho 10:5" tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya MUNGU; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii KRISTO;'

◼️Kwenye Maombi ikomboe nafsi Yako kwa kutumia Damu ya YESU KRISTO ukiomba katika Jina la YESU KRISTO.

3. Moyo ni nini?

✓✓Kimwili Moyo ni kiungo Cha mwili kinachoshughulika na kusukuma Damu ila kibiblia Moyo ni tofauti.

◼️Kibiblia moyo ni sehemu ya kiroho ya Mtu ambako hisia  na matamanio hukaa.

Marko 7:21-23 " Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi."

✓✓Moyo  kitovu cha maisha ya kiroho, maamuzi, hisia, dhamira, na fikra za ndani. 

◼️Hata leo Moyo wako unaweza ukaamua kumpenda YESU KRISTO Mwokozi na unampokea na Kuokoka, ni maamuzi ya Moyo.

Warumi 10:10 ''Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.''

✓✓Ni mahali ambapo mtu huamua kumpenda MUNGU au kutenda mabaya.

Mathayo 22:37 "Akamwambia, Mpende Bwana MUNGU wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote."


4.Mwili ni nini?

✓✓Mwili ni gamba la nje linaloibeba roho.

Mithali 11:17 "Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake."

✓✓Kwa lugha nyingine mwili ni nyumba ya kuwa kuishi roho Yako.

✓✓Kipindi roho inatengana na mwili mwili hufa.

Mwanzo 35:18 "Ikawa hapo katika kutoa roho yake, maana alikufa, akamwita jina lake Benoni, lakini babaye alimwita Benyamini."

✓✓Hakikisha dhambi haitawali mwili wako, huo ndio ushauri wa Neno la MUNGU.

Warumi 6:12 "Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake;"

✓✓Mwili una Tamaa 

Wagalatia 5:13 Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo.

◼️Biblia inatutaka tujifunze kuiitisha miili yetu ili tusitende dhambi.
1 Wathesalonike 4:4-5 " kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua MUNGU."

Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana.

N.b
Katika baadhi ya maandiko kwenye Biblia yanazungumza Moyo yakiwa na maana ya Nafsi na pengine yanazungumza Nafsi yakiwa na maana pia ya Moyo wa Mtu.
Kwa sababu Nafsi na Moyo ni kama kitu kimoja.

Comments