![]()  | 
| Na Mwl Peter Mabula  Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi  | 
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Leo tunaangalia Sifa za viongozi wa Kanisa.
Sifa hizi kama zinavyoelezewa katika 1 Timotheo 3:1-7 zikimzungumza Askofu ambaye ndiye Kiongozi mkubwa zaidi wa kiroho, hivyo sifa za Askofu kiroho zinatakiwa pia kuwa sifa za Viongozi walio chini yake.
Katika hii 1 Timotheo 3:1-7 Biblia inasema "Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya Askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa Askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha;
 si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu;  (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la MUNGU?)  Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi."
Sifa hizi za Kiongozi mzuri wa Kanisa kama zinavyoelezewa katika 1 Timotheo 3:1-7 ni hizi.
1. Awe ni Mtumishi asiyelaumika.
2. Awe ni Mume wa mke mmoja.
✓✓Naamini viongozi walio Wanawake wote wako katika ndπoa ya Mume mmoja tu maana sijawahi kusikia Mwanamke aliye na waume zaidi ya mmoja.
Hivyo kiongozi wa kiroho lazima awe katika Ndoa ya Mke/Mume mmoja tu.
3. Kiongozi lazima awe mwenye kiasi na busara.
4. Awe mtu wa utaratibu mzuri na awe pia mkaribishaji.
5. Kiongozi wa Kanisani lazima awe anajua kufundisha Neno la MUNGU.
6. Kiongozi wa Kanisani hatakiwi kamwe kuwa mlevi wala mpiga watu.
✓✓Kama ambavyo ni marufuku kwa waenda Mbinguni kunywa pombe, basi na Kiongozi anatakiwa kutokuwa mnywa pombe kamwe.
7. Kiongozi anatakiwa kuwa na upole na awe mtu wa majadiliano.
✓✓Upole haina maana asikemee maovu Bali akemee, aonye na akaripie pale watu wa MUNGU wanapotaka kwenda kinyume na Neno la MUNGU.
8. Kiongozi wa kiroho hatakiwi kuwa mpenda fedha.
✓✓Yaani hatakiwi kufanya mbinu ya hila ili kupata fedha, hatakiwi kufanya huduma hadi alipwe, hatakiwi kuiba n.k
10. Kiongozi wa kiroho anatakiwa kujua kuisimamia vyema familia yake.
✓✓Yaani sio anawaonya kanisa kujitenga na uzinzi, pombe, na n.k wakati Watoto wake mwenyewe ni makahaba na wanalala mitaloni baada ya kulewa.
✓✓Maana yake kiongozi wa kiroho anatakiwa kusimamia vyema Kanisa na familia yake pia.
◼️Mwisho kabisa zingatia maneno haya.
Tito 2:7-8 "katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu."
◼️Sifa zingine za Kiongozi wa kiroho inakupasa kuwa mzalendo.
✓✓Musa aliambiwa na MUNGU achague watu safi 70 ili MUNGU aweke ndani hao roho ya uongozi iliyokuwa juu ya Musa ili wawe viongozi kumsaidia Musa kazi.
Hesabu 11:16-17 " Kisha BWANA akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe. Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako."
✓✓Inawezekana hata kwako Maaskofu au Wachungaji au Kanisa wamekuchagua au kukuteua ili uwe kiongozi safi wa kiroho.
◼️Swali langu je unatumika vyema na kwa utakatifu tena kwa kusudi la MUNGU?
◼️Je hujabadilika na kujiinua baada ya kupewa uongozi?
◼️Je nafasi uliyopewa haijakutumia vibaya?
✓✓Ushauri wangu katika ujumbe huu nakuomba uwe kiongozi wa kiroho aliye mzalendo.
◾Kiongozi wa kiroho mzalendo ni yupi?
✓✓Kiongozi wa kiroho mzalendo ni Mtumishi wa MUNGU ambaye anaipenda kazi yake na anatimiza majukumu yake vyema kwa kusudi la MUNGU.
✓✓Mzalendo wa kweli hawezi kuonea watu, hawezi kutoa wala kupokea rushwa tena mzalendo hawezi kufanya kazi ya MUNGU kwa ulegevu.
◼️Ndugu uliyeitwa kumtumikia Bwana YESU hakikisha unakuwa mzalendo kwenye kazi yako ya kiroho uliyopewa na MUNGU.
◼️Ngoja nikutajie Kibiblia baadhi ya kazi za viongozi wa kiroho.
1. Kulitunza na kulilinda kundi la MUNGU.
Matendo  20:28" Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo ROHO MTAKATIFU amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe."
✓✓Yaani kuhakikisha mafundisho ya mashetani ama hayawafikii Kanisa la MUNGU au kuhakikisha hayo mafundisho ya mashetani hayawageuzi Kanisa hata wakamuacha YESU Mwokozi.
◾Unalindaje kundi la MUNGU? 
✔Kwa wewe kuwafundisha Kanisa kweli ya MUNGU ya Wokovu wa KRISTO YESU.
✔Kwa kuwaonya Kanisa ili wasitekwe na mafundisho yaliyo kinyume na Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
◼️Hakikisha pia unajua kufundisha Neno la MUNGU kwa usahihi wake(1 Timotheo 3:2)
✓✓Kama hujui jifunze na soma sana Biblia.
2. Kulilisha Kanisa na kulichunga.
1 Petro 5:1-3 " Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya KRISTO, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la MUNGU lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama MUNGU atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi."
◼️Unalilisha Kanisa kwa kulifundisha Neno sahihi la MUNGU.
◼️Unalichunga Kanisa kwa kuhakikisha hakuna kondoo anatekwa na mawakala wa shetani.
3. Kutawala vyema.
1 Timotheo 5:17-18 " Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake."
✓✓Kutawala vyema ni jukumu lako kama kiongozi wa kiroho.
✓✓Viongozi wengi wa Kiroho husema kwamba lawama huwa hazikosekani lakini Mimi nakumbia kwamba isiwemo lawana hata moja uliyoisababisha wewe.
✓✓Pia katika kutawala kumbuka na epuka kutumikiwa wewe.
✓✓Bwana YESU mwenyewe alisema kwamba alikuja kutumika na sio kutumikiwa, yaani kipindi Bwana YESU yuko duniani katika mwili kama wa kwetu alikuwa anatumika na sio kutumikiwa, hata sisi katika mwili tutumike na sio kutumikiwa.
◼️Kwa sasa tunatakiwa tumtumikie sana Bwana YESU maana yuko sasa katika utukufu wake, hivyo sisi wote yaani viongozi na wasio viongozi tumtumikie Bwana YESU na sio sisi viongozi tuwe watu wa kutumikiwa.
✓✓Ndugu tawala huku ukiwa Mtumishi na sio mtumikiwa.
4. Kulishika Neno la MUNGU na kulifanyia kazi.
Tito 1:9 "akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.'
✓✓Kiongozi wa kiroho lazima uwe na mfano katika kulitii Neno la MUNGU na kulifanyia kazi kwa kusudi la MUNGU.
✓✓Hakikisha unakuwa kielekezo chema kwa mema.
Sio wewe unaagiza kwa ukali kwamba Kanisa waingie katika maombi ya kufunga huku wewe wala huna mpango wa kufunga, sio unaagiza watu kutoa fungu la kumi huku wewe huwa hutoi.
◼️Ndugu, hakikisha unakuwa kielelezo chema katika mema yote.
5. Kuwatembelea watu na kuwaombea.
Yakobo 5:14-15" Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa Kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.
 Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa."
✓✓Kuwatembelea watu sio mpaka ufike kwao ila hata kujua hali zao inapobidi kisha unawaombea ni jambo jema.
✓✓Ikiwepo nafasi ya kuwatembelea basi fanya hivyo na kuwaombea.
 ◼️Ni jukumu la Viongozi wa kiroho kulijenga Kanisa la MUNGU.
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments