ZINAA HAITAKIWI KUWAKO KWA WATU WA MUNGU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU la uzima.

◼️Zinaa haitakiwi kuwapo kwa wateule wa MUNGU waliookolewa na YESU KRISTO Mwokozi.

 2 Kor 6:18 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.''

Zinaa ni nini?

➡️Zinaa ni tendo la uasherati au uzinzi.

✔️Uzinzi na uasherati ni tabia ya kuzini.

✔️Uzinzi na uasherati kwa jina lingine unaitwa ukware.

✔️Ukware ni tamaa ya kupenda kufanya tendo la kujamiana.

◼️Uzinzi na uasherati kwa jina lingine unaitwa uzinifu.

Katika Kanisa la MUNGU hakutakiwi kuwako wazinzi wala waasherati wala wakware wala wazinifu lakini leo kuna baadhi ya watu walio Kanisani  ni wakware, wazinzi, waasherati na wazinifu.

◼️Uzinzi na uasherati ni moja ya dhambi kuu zilizowafanya Sodoma na Gomora kuchomwa moto.

Yuda 1:7 ''Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele.'' 

◼️Njia mojawapo ya mtu kuepuka zinaa ni kuoa au kuolewa na mtu huyo akawa mwaminifu kwa mwenzi wake wa Ndoa.

1 Kor 7:2 '' Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.''

Lakini wapo pia baadhi ya  wanandoa sio waaminfu katika ndoa zao maana husaliti ndoa zao, hivyo hata kuwa ndani ya Ndoa hakujawasaidia kuacha zinaa hivyo jehanamu kuwangoja kwa spidi kali wasipopata neema ya kutubu na kuacha uzinzi.

◼️Kumbuka sku zote kwamba siku zote Mshahara wa dhambi zote zikiwemo dhambi za uzinzi na uasherati ni jehanamu.

Warumi 6:23 ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu.''

◼️Biblia inakataza kila mtu kufanya uzinzi na uasherati.

 Waefeso 5:3 '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; ''

Wazinzi ni watu gani?

✔️Wazinzi ni watu waliooa au kuolewa wanapotoka kingono nje ya ndoa zao.

✔️Waasherati ni watu ambao hawajaoa au kuolewa  wanapofanya ngono na mtu yeyote.

◼️Biblia inamtaka kila aliye Kanisa la MUNGU kuikimbia zinaa yaani kuukimbia uzinzi na uasherati.

 2 Kor 6:18 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.''

◼️Hivyo hakuna Mtu mwenye ruhusa ya kufanya uzinzi au uasherati.

Mama mmoja  Mume wake kwa muda wa  mwaka mmoja na nusu alikuwa anaumwa amepooza mwili, Mama huyu ni Mtumishi wa MUNGU kabisa lakini baada ya miezi kadhaa alisema neno la ajabu sana, alisema anahitaji kuhudumiwa kingono maana Mume wake hawezi tena kushiriki tendo la Ndoa,  na aliyekuwa anamwambia hivyo ni Mtumishi mwingine na ana Mke na Watoto, yaani alitamani mara moja moja yule Mtumishi awe anaenda kuzini na Mama yule kwa sababu tu Mume wake hawezi tena, nilitamani kulia niliposikia kauli hiyo mbaya na chafu sana.

Baba mmoja alipoona Mke wake hazai aliamua kwenda kutafuta Mtoto nje ya Ndoa na huko akapata ukimwi ulioangamiza hadi Ndoa yake.

Baba mmoja kwenye ndoa yake alipata watoto wa kiume tu na yeye alitamani Mtoto wa kike hata mmoja hivyo aliamua kwenda nje ya ndoa yake na huko aliangukia kwa wakala wa shetani ambaye alifanya hadi mipango ya kuua Mke na Watoto.

Inawezekana uko pia hapa unayetamani kufanya uzinzi  kwa kigezo cha mwenzi wako anaumwa n.k

◼️Ndugu, ni dhambi kuisaliti ndoa yako.

Kama unaitaka mbingu huruhusiwi kuzaa nje ya Ndoa yako kwa kigezo kwamba mwenzi wako wa Ndoa hana uwezo wa kuzaa.

Kama unaitaka mbingu huruhusiwi  kuoa Mke wa pili kwa sababu Mke wa kwanza kuna kitu unaona amepungukiwa.

Ndio maana kila mtu kabla ya kuoa au kuolewa huwa yuko makini sana maana mkifunga Ndoa ni huyo tu ndio wa kwako, mpende na madhaifu yake na heshimu Ndoa yako, ulimchagua mwenyewe kwa umakini mkubwa, ulimuona ni huyo tu miongoni mwa vijana au mabinti wengi hivyo ukaridhika kabisa kwamba ni huyo atakufaa kwa ajili ya Ndoa Takatifu ambayo huwa haitenganishi na chochote isipokuwa kifo.

Marko 10:7-9 ''Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe;  na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.
 Basi alichokiunganisha MUNGU, mwanadamu asikitenganishe.''
 
 ◼️Kama unaitaka mbingu huruhusiwi  kufanya mapenzi na mchumba wako kabla ya kufunga ndoa.

 ◼️Kama unaitaka mbingu huruhusiwi kufanya uzinzi na uasherati.

Inawezekana Kanisani kwenu sio wote wameikimbia zinaa ila wewe jitahidi kuikimbia dhambi hiyo.

Inawezekana katika familia yenu sio wote wameukimbia uzinzi na uasherati lakini wewe unayesoma ujumbe huu hakikisha unaukimbia uzinzi na uasherati.

Inawezekana sio wanandoa wengi unaowafahamu wamejitenga mbali na uzinzi lakini wewe jitenge mbali na dhambi hiyo.

Waebrania 13:4 ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. ''

Inawezekana kwenye ukoo wenu sio wote wameukimbia uzinzi na uasherati lakini wewe unayesoma ujumbe huu hakikisha unaikimbia dhambi hiyo inayonajisi mwili na roho.

Inawezekana sio marafiki zako unaowafahamu wamejitenga mbali na uzinzi au uasherati au ngono kinyume na maumbile lakini wewe hakikisha dhambi hizo chafu hazikuhusu.

Inawezekana katika mtaa wenu au katika eneo lako la kazi sio wote wamejitenga mbali na dhambi ya uzinifu lakini wewe unayesoma ujumbe huu nakuomba ikimbie dhambi hiyo.

◼️Jitenga na dhambi hizo ili uepukane na laana.

2 Petro 2:14 '' wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; ''

Leo kuna hadi watumishi wa Kanisani ambao badala ya kuikimbia zinaa wao wameikaribisha na wanaiishi siku zote.

Leo kuna mpaka Wachungaji ni wazinzi,ni hatari sana sana.

Leo kuna mpaka wa Mama Wachungaji ni wazinzi, hiyo ni hatari sana na ni kujipoteza.

Leo mpaka kuna waimbaji au wahubiri ni wazinzi na waasherati kuliko hata makahaba.

Leo kuna mabinti ambao hawajaolewa wamekuwa waasherati na watoa mimba, ni mbaya sana na ni laana.

Inawezekana kabisa katika baadhi ya jamii za leo ni nadra sana kukutana na Binti ambaye hajatoa mimba, ni hatari sana na kutoa mimba ni kujitafutia laana maana chanzo kimoja wapo cha laana kibiblia ni kumwaga damu isiyo na hatia.

Mwanzo 4:10-12 ''Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.''

Sasa wanaotoa mimba wanaingia katika kundi lililolaaniwa maana wameua mtu asiye na hatia, katika jamii ya leo wapo wengi sana waliomwaga damu isiyo na hatia kwa sababu ya kutoa mimba. Na laana ni laana tu hivyo usipojua namna ya kuifuta laana hiyo ujue kuna maeneo mengi ya maisha yako yataathiriwa na laana hiyo.

Wapo watu hadi wametoa mimba zaidi ya mbili  yaani ni laana iliyobeba laana na juu ya laana yenye laana.

Na laana ya kuua damu isiyo na hatia sio laana ya kuifuta tu kwa kusema ''Kwa imani naifuta laana ya kuua mtu asiye na hatia'' kama ni hivyo tu tambua haifutiki.

Waone watumishi wa MUNGU wakusaidie na uwe na kiapo moyoni mwako kwamba hutatoa mimba tena.

Lakini kwanini ipelekee laana?
◼️Ni kwa sababu ya uzinzi na uasherati.

◼️Kumbe ukiepuka uzinzi na uasherati umeepuka madhara mengi sana kiroho na kimwili.

Uasherati na uzinzi unaweza kukuondolea haki zako kiroho na ukawa mtu wa majanga na mikosi na kuadhalaulika na  vifungo vya giza, Mfano ni huu Ezekieli 23:29-30 '' nao watakutenda mambo kwa chuki, watakuondolea kazi zako zote, watakuacha uchi, huna nguo na aibu ya mambo yako ya kikahaba itafunuliwa, uasherati wako na uzinzi wako. Utatendwa mambo hayo kwa sababu umezini na hao wasioamini, na kwa sababu umetiwa unajisi kwa vinyago vyao.''

➡️Ndugu, hakikisha uzinzi na uasherati haupo kwako.

◼️Hakikisha unalitii Neno la MUNGU kuanzia leo kwa kuacha zinaa.

◼️Okoka na anza kuishi maisha matakatifu.

◼️Kumbuka zinaa inaweza kukufarakanisha na MUNGU na ukakosa hata mbingu au ukakosa baraka zako.

Hosea 5:4 ''Matendo yao hayatawaacha kumgeukia Mungu wao; maana roho ya uzinzi imo ndani yao, wala hawamjui BWANA.''

 Inawezekana wewe una mchumba na akili yako inakutuma kwamba kwa sababu huyo mtaoana hivyo hata mkizini sio tatizo sana, ndugu kuzini ni dhambi na dhambi hiyo itatengeneza matatizo makubwa sana hivyo acha uzinzi na uasherati.

Kwanza uzinzi na uasherati ni sehemu ya ibada ya sanamu.

Wakolosai 3:5-6 '' Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;  kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya MUNGU.''

Je hufanyi ibada ya sanamu wewe?
Kwa sababu ya uzinzi au uasherati?

Ndugu, zinaa haitakiwi kuwako katika watu wa MUNGU.

◼️Uwe ni mwanaume au mwanamke hakikisha unajitenga mbali na dhambi ya uzinzi na uasherati.

"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments