![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tena karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
◼️Kwanini MUNGU akujulishe jambo kwa ndoto au kwa maono?
Tuanze na maana ya ndoto na maono.
◼️Kwa ujumla ndoto au maono ni lugha ya rohoni inayoelezea mambo yaliyopita, yaliyopo au yajayo.
Ayubu 33:14-16 '' Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,''
◾Ndoto ni nini?
✓✓Ndoto ni matukio unayoyaona kupitia utu wako wa ndani wakati umesinzia.
◾Maono ni nini?
✓✓Maono ni matukio unayoyaona kwa kutumia utu wako wa ndani wakati hujasinzia.
◼️Tofauti ya ndoto na maono ni kwamba huwezi kuota ndoto ukiwa hujasinzia ila unaweza kuona maono kipindi hujasinzia.
Yoeli 2:28 '' Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;''
✓✓Kuna njia nyingi MUNGU hutumia kuongea na wanadamu, ndoto na maono ni moja ya sehemu hizo anazotumia MUNGU kusema na watu wake.
MUNGU kusema na watu kwa ndoto ni mara nyingi sana, na nina hakika hakuna mtu ambaye MUNGU hajawahi kusema na yeye kwa ndoto.
Njia nyingine ambazo MUNGU hutumia kusema na watu wake nje na ndoto, baadhi ni hizi; MUNGU husema na watu wake kwa Neno lake la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU, MUNGU husema na watu/mtu fulani kwa kuwatumia watumishi wake wengine, MUNGU husema kwa njia ya Malaika, husema kwa wewe kujifunza Biblia n.k
✓✓Changamoto ya watu wengi leo ni kwamba MUNGU anaposema nao kwa ndoto au maono hukimbilia kutafuta kujua maana ya ndoto hiyo ila hata wakijua hawafanyii kazi ujumbe ulio ndani ya ndoto waliyopewa.
✓✓Kutafuta maana ya ndoto yako ni jambo jema sana ila kitu chema zaidi ni wewe kufanyia kazi ndoto yako katika kusudi la MUNGU.
✓✓MUNGU anataka akikusemesha kwa ndoto anataka utembee kwenye ujumbe huo katika kusudi lake, mfano kama ndoto inakuonya juu ya dhambi basi anza muda huo kujitenga na dhambi zote.
✓✓Ndoto au maono ni lugha ya rohoni hivyo kuitambua vyema inakupasa uwe rohoni ukishirikiana vyema na ROHO MTAKATIFU pamoja na Neno la MUNGU.
◼️Bila Neno la MUNGU na ROHO MTAKATIFU hakuna Mteule wa MUNGU anayeweza kutafasiri ndoto iliyotoka kwa MUNGU kama ndoto hiyo ina mafumbo ndani yake, maana lugha ya rohoni wakati mwingine ni fumbo hivyo lazima uwe rohoni na uwe na ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU ndipo utaelewa.
◼️ROHO MTAKATIFU ndio pekee anayeweza kutufunulia siri zote kutoka ulimwengu wa roho maana kazi yake mojawapo kwa Kanisa la KRISTO ni kutufumbulia mafumbo yote.
1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''
◼️Uwe makini pia maana sio ndoto zote zinatoka kwa MUNGU, hivyo uwe makini sana maana moyo wako pia ni kama Memory card inayohifadhi matukio hivyo usishangae usiku matukio uliyoyaona na kuyawaza sana mchana ukayaota huku ukidhani ni MUNGU anakusemesha.
Mfano hai unaweza kuangalia sana filamu ya wanyama na ajabu usiku unaota sana wanyama na unajua kabisa umeota sio ujumbe wa MUNGU ila moyo ulichohifadhi kwa muda mrefu ndio umekiona ndotoni, hivyo usishangae hata binti au kijana akimuwazia sana kijana fulani au binti fulani kwamba anamfaa kufunga nae ndoa, anaweza akawa anamuota kila mara kwa sababu tu moyo ulihifadhi taarifa hiyo muda mrefu na sio ujumbe wa MUNGU.
◼️Ndoto zote anazokupa MUNGU zina majibu yake ndani ya Biblia hivyo inakupasa sana uwe msomaji wa Biblia ili ROHO MTAKATIFU akupe andiko ulilowahi kujifunza katika Biblia lenye majibu na maana ya ndoto yako.
Ngoja nikupe mifano mitatu ili ujue namna ya kutafasiri ndoto yako.
◼️Mfano wa kwanza, Nebkadneza aliota ndoto mti unaanguka.
Danieli 4:4-16 utasoma yote ila maandiko machache ni haya '' .....Nikaota ndoto iliyonitia hofu; mawazo niliyokuwa nayo kitandani mwangu, na njozi za kichwa changu, zikanifadhaisha. ...... Njozi za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi; naliona, na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana. ..... ''
✓✓Tafasiri ya ndoto hiyo ilikuwa hii, Danieli 4:20-22 '' Ule mti uliouona, uliokua, ukawa na nguvu, urefu wake ukafika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka dunia yote; ambao majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha wote; ambao chini yake wanyama wa kondeni walikaa, na ndege wa angani walikuwa na makao yao katika matawi yake; ni wewe, Ee mfalme, uliyekua, na kupata nguvu; maana ukuu wako umekua na kufika mpaka mbinguni, na mamlaka yako yamefika mpaka mwisho wa dunia.''
✓✓Hivyo Mti unawakilisha mtu na shina la mti linawakilisha utawala(Ufalme) Danieli 4:26 ''Na kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala.''
✓✓Ufalme wa Nebkadneza haukuondolewa kabisa ndio maana baada ya nyakati saba(Miaka 7) akarudishwa katika nafasi yake kama Mfalme.
◾Nini tunajifunza?
✓✓Mti mkubwa unawakilisha mtu mkubwa katika jamii, hiyo ni sehemu ya kujua maana ya ndoto yako kama inahusika na mti.
Mtumishi mmoja siku moja alinikaribisha nikahubiri Kanisani kwake na kabla ya kunikaribisha alisema kwamba ameota ndoto akiniona mimi Peter Mabula ninatembea huku nimeshika Biblia na nilikokuwa natembea kulikuwa na miti mingi sana na kila nikiifikia miti hiyo huku nimebeba Biblia inakuwa miti ya kijani sana yenye afya na kupendeza sana.
Aliponiambia niligundua kabisa kwamba baadhi ya watu(Miti) wanabadilishwa na Neno la KRISTO ninalofundisha na hivyo waanza kumpendeza MUNGU na kuwa na afya ya rohoni, nilimshukuru MUNGU kwa hilo.
✓✓Mtu mmoja siku moja aliona ndoto akiona mti mkubwa sana unaanguka na kesho yake kiongozi mkubwa wa serikali katika eneo hilo alifariki, hivyo ilikuwa ni rahisi tu kujua juu ya mti kwenye ulimwengu wa roho.
✓✓Mtu mmoja siku moja alikimbizwa na wanyama wakali na akakimbilia mti fulani akapanda juu na akawa salama, hapo tunagundua kwamba katika vita ya kiroho aliyopo anatakiwa kushirikisha watumishi wa MUNGU ili wamsaidie maombi, yaani vita aliyopo anayopambana na nguvu za giza anahitaji msaada wa maombi ili kushinda.
◼️Mfano wa pili, andiko Mithali 6:32 '' Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.''
Tunajifunza nini?
✓✓Ni kwamba Mwanamke au Mwanaume anapofanya uzinzi au uasherati maana yake hana akili kabisa yaani hana akili hata moja na tukio alifanyalo la uzinifu linatangulia tu ili kuyakaribisha maangamivu.
✓✓Hivyo wewe unapozini ndotoni usifurahi maana maana mojawapo kujua ni kwamba huna akili maana umeruhusu kumilikiwa na majini mahaba.
✓✓Kwahiyo andiko linaweza kukujulisha maana ya ndoto yako.
✓✓Maana zingine za kuota unazini ni kwamba umeungwa kipepo na mawakala wa shetani,
1 Kor 6:16 '' Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.''
baaadhi ya mawakala wa shetani ni majini ndio maana ukiota umezini na mtu unayemfahamu au humfahamu, mwenzi wako au sio mwenzi wako maana yake umeingia agano na majini mahaba na baada ya hapo unakufuata uharibifu.
✔️✔️Kataa sana mpango huo wa shetani kwa maombi kupitia jina la YESU KRISTO na futa maagano kati yako na majini, futa maagano hayo kwa kutumia damu ya YESU KRISTO ya agano.
✓✓Kumbe umeota unazini maana yake huna akili kabisa na umeingia agano na majini mahaba.
™✓Maana nyingine ya kuota unafanya mapenzi ni kwamba umeingia agano au patano la kishetani yaani umeingia makubaliano mabaya sana na watu wabaya,
Ufunuo 18:3 '' kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake.''
✓✓Wamezini naye hapo ina maana ya wameingia mkataba naye wa kipepo, wameingia agano nae la kipepo, wameingia patano la dhambi.
✓✓Sasa unajulishwa ili ujitenge na watu hao wabaya na uvunje mapatano mabaya uliyoingia na watu hao.
✓✓Kwahiyo unapoota unazini na mtu yeyote yule maana yake ama huna akili kabisa, ama umeungwa kipepo na jini, ama umeingia patano baya na watu wabaya hata kama hukujua patano hilo kama ni baya.
◼️Mfano wa tatu andiko Mitahli 14:1 '' Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.''
✓✓Hapa tunajifunza kwamba nyumba kwenye ulimwengu wa roho inaweza kuwakilisha Ndoa au Familia au Nyumba unapoishi n.k
✓✓Sasa unapoota unaibomoa Nyumba yako maana yake inaweza kuwa ni wewe unataka kuiharibu Ndoa yako au Familia yako kwa tabia zako chafu au kwa maamuzi yako ya kipepo.
✓✓Unapoota watu wengine wanavunja nyumba yako maana yake uwe makini ili watu wa nje wasiivunje Ndoa yako au familia yenu hivyo jitenge nao au omba ukiharibu mipango yao ya kukuharibia ndoa yako.
✓✓Unapoota nyoka au kitu kibaya kinaingia ndani ya nyumba maana yake Ndoa yako au Familia yako imevamiwa na nguvu za giza, hivyo pambana kimaombi kupitia jina la YESU KRISTO na adui huyo aliyevamia Ndoa au Nyumba au kazi au ukoo au unapokaa ataondoka.
✓✓Unapoota umemuua nyoka au mnyama au mdudu ndani ya nyumba maana yake roho ya kuzimu iliyotumwa kuvunja ndoa au kuivuruga familia yenu umeishinda.
✓✓Mtu mmoja aliota nyoka anazunguka nyumba yake na baada ya muda ndoa yake ikasambaratika, sababu ni kwamba adui alikuwa anatafuta nafasi ya kuvamia ndoa ile na akaipata maana aliyeota ndoto hakufanyia kazi kimaombi.
✔️✔️Yaani kutokana na andiko hilo tu unaweza hata kupata maana zaidi ya kumi ya ndoto kuhusu nyumba kama ambavyo ROHO MTAKATIFU atakufunulia, hivyo mhitaji sana ROHO MTAKATIFU katika maisha yako.
✓✓Na hatua ya mwanzo kabisa hata ROHO MTAKATIFU aje kwako ni wewe kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako yaani kuokoka na kufanyika mtoto wa MUNGU.
✓✓Unaweza kuota unasafisha nyumba, maana yake unatakiwa kuingia katika maombi ya toba ili kuisafisha ndoa, au familia au Kanisa unapoabudu n.k
✓✓Ndoto ni lugha ya rohoni wakati mwingine ni lugha ya mifano inayowakilisha tukio halisi.
✔️✔️Mfao wa lugha ya rohoni soma mifano ya Bwana YESU aliyokuwa anaitoa alipokuwa anafundisha kuhusu ufalme wa MUNGU ulivyo au utakavyokuja, mfano wa mifano hiyo ya Bwana YESU ni Luka 8:5 '' Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila. '',
✓✓Mbegu ni Neno la MUNGU, Hivyo unaweza kuota ndoto unapanda mbegu nzuri maana yake anza kuwahubiria watu Injili ya KRISTO YESU inayookoa.
✓✓Unapoota unapanda mbegu iliyooza maana yake acha kueneza uongo, acha kuwatoa watu kwa YESU, acha uzushi unaowatoa watu kwa YESU.
◼️Bwana YESU alikuwa anazungumza wakati mwingine kwa mifano ya lugha ya rohoni ndio maana waliokuwa mwilini hawakumwelewa, kwanini? Kwa sababu lugha rohoni inawahitaji watu wawe rohoni ili waelewe.
Kwa nini MUNGU akujulishe jambo kwa ndoto au maono?
1. Ili kukuonya kwa sababu ya mambo mabaya unayoyatenda au unayotaka kuyatenda.
Mwanzo 20:3 '' Lakini MUNGU akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu.''
✓✓Abimeleki alikuwa anaonywa kama ambavyo wewe pia unaweza kuonywa na MUNGU juu ya jambo lolote ili usilifanye.
Mathayo 2:12 ''Nao wakiisha kuonywa na MUNGU katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.''
✓✓Hawa nao walionywa kwa ndoto kama ambavyo wewe pia unaweza kuonywa kwa ndoto au maono, usidharau ndugu maonyo ya MUNGU kwako.
2. Ili kukujulisha yajayo kukuhusu wewe.
Mwanzo 37:5-7 '' Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.''
✓✓Yusufu alikuwa anajulishwa juu ya atakuja kuwa nani na wengine watakuwa chini yake.
✓✓Yusufu alijulishwa kwa ndoto kwamba atakuja kuinuliwa kuliko ndugu zake.
Mwanzo 40:5 '' Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. ''
✓✓Ukiendelea kusoma juu ya ndoto za hawa ndugu na tafasiri zake unagundua kwamba mmoja alikuwa anajulishwa kwamba atakufa siku chache zijazo na mwingine alikuwa anajulishwa kwamba japokuwa alifukuzwa kazi lakini atarudishwa kazini na kuendelea kufanya kazi yake ya awali, hivyo kwa ndoto unaweza kujulishwa juu ya yajayo kukuhusu wewe.
◼️Kama ni mambo mabaya na yanazuilika basi inakupasa kuyazuia kwa maombi na kubadilika tabia.
◼️Jina la Bwana YESU KRISTO lipo kukupa ushindi wewe uliyeokolewa na yeye Bwana YESU.
Yohana 14:13 '' Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.''
3. Ili kukujulisha usitende dhambi.
Mwanzo 20:6 '' Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. ''
✓✓Huyu alijulishwa kwa ndoto ili asitende dhambi, hata wewe unaweza kujulishwa kwa ndoto ili usitende dhambi.
✓✓Jitahidi sana kuzingatia ndoto inayokujulisha kwamba usitende dhambi.
4. Ili kukutoa hofu, wasiwasi na mashaka juu ya ahadi za MUNGU kwako alizokuahidi kabla.
Mwanzo 15:1 '' Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.''
✓✓Kwa ndoto MUNGU anakuonyesha nguvu zake na utukufu wake ili kukupa uhakika kwamba uendelee kumtegemea na kumtumaini yeye, usiwe na hofu, wasiwasi wala mashaka.
5. Kukujulisha mambo ambayo yatakuwa yako, umejulishwa sasa ili uvumilie maana mambo hayo kwako sio kwa wakati huu.
Habakuki 2:2-3 '' BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.''
✓✓Kuna ndoto ni ujumbe wa MUNGU kwako ili kukupa uhakika wa unachohitaji ila kitu hicho sio cha muda huo unaohitaji wewe.
Unajulishwa kwa ndoto ili usifute tumaini na sasa uendelee mbele, kama ulikuwa mtu wa Ibada ili uendelee mbele, kama ulikuwa mtoaji ili uendelee mbele, kama ulikuwa mtu wa maombi ili uendelee mbele maana ahadi hiyo itatimia hakika.
6. Ili kukubadilishia mtazamo.
✓✓Utasoma maandiko yote ila kwa ufupi ni kwamba Matendo 10:9-35'' Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na MUNGU, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni. ..... Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa MUNGU hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. ''
✓✓Petro hakujua mwanzo kama Wokovu wa KRISTO unawahusu hata watu wasio wayahudi, hakujua kwamba Injili ni kwa watu wote wa kila Taifa na Nchi, alikuwa na mtazamo kwamba wanaotakiwa kuokoka ni Wayahudi tu.
✓✓Alikuwa sahihi kwa mtazamo wake maana yeye alipewa Injili kwa Wayahudi huku akina Paulo wakipewa injπili kwa mataifa yote.
✓✓Sasa ili kuubadili mtazamo wa Petro kwamba hata watu wasio Waisraeli inawapasa kumpokea YESU na kuokoka ilibidi MUNGU amfunulie Petro kwa maono.
✓✓Maono yale ndio yalimfanya Petro kutamka neno hili kwamba ''Hakika natambua ya kuwa MUNGU hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.''
✓✓Hata wewe MUNGU anaweza kukujulisha kwa maono au ndoto jambo fulani ili tu kuubadili mtazamo wako uliokuwa sio sahihi na sasa uwe na mtazamo sahihi wa kibiblia.
Yaani ulikuwa na mtazamo mbaya na sasa kupitia ndoto au maono unapewa au mtazamo sahihi unaotakiwa kuufanyia kazi.
7. Ili kukufunulia siri iliyokuwa huijui au iliyokuwa imejificha.
Mathayo 1:20 ''Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa BWANA alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa ROHO MTAKATIFU.''
✓✓Yusufu kuna siri moja alikuwa haijui, alikuwa hajui kwamba mimba aliyokuwa nao Mariamu ni kwa uweza wa ROHO MTAKATIFU. Yusufu hadi alikuwa amemwacha Mchumba wake kwa sababu ya mimba maana akili zake zote zilimtuma kwamba amemsaliti kwa kuzini hadi akapata mimba na kumbe yeye ndio alikuwa anakosea sana maana Mariamu hakuzini popote ila mimba aliyokuwa nayo ni kwa uwezo wa ROHO MTAKATIFU ili kumleta Bwana wa utukufu Mwokozi YESU KRISTO.
✓✓Kama Yusufu asingefunuliwa kwa ndoto nina hakika asingeamini maneno ya mtu yeyote juu ya mimba ya Mariamu, lakini MUNGU wakati mwingine hutumia ndoto ili kutujulisha siri fulani zinazotupasa kujua.
✓✓Hata wewe kwa ndoto au maono unaweza ukajulishwa na MUNGU siri nyingi tu, fanyia tu kazi na tembea kwenye kusudi la MUNGU.
8. Ili kujulisha yaliyoamuliwa mbinguni ambayo yatatokea.
Mwanzo 41:5 ''Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema.''
✓✓Farao alikuwa anajulishwa juu ya miaka ya njaa ambayo itakuja.
✓✓Kwenye ulimwengu wa roho yaliyokuwa yamepangwa ni hayo kwamba iwepo miaka 7 ya shibe kisha miaka 7 ya njaa, hatuoni hapa mtu akiomba kwamba miaka ya njaa izuiliwe, hata Yusufu aliyekuwa na ROHO MTAKATIFU hatuoni akipata msukumo wa kuomba ili kuzuia njaa bali alijulisha juu ya nini kifanyike wakati wa shibe na wakati wa njaa.
✓✓Kuna mambo huamuliwa kwenye ulimwengu wa roho wa nuru, hayo hayabadiliki kamwe hata ukiomba maana yameagizwa na MUNGU mwenyewe, ikitokea umeota ndoto yenye maagizo kama hayo inakupasa kufanyia tu kazi maelekezo ya MUNGU ya ndani ya ndoto ili uwe salama wewe na wanaohusika.
✓✓Mfano kuna siku ya mwisho, wako watu wamewahi kuona maono au kuota juu ya siku za mwisho, hawawezi kufunga na kuomba ili kuizuia siku ya mwisho bali inawapasa kuokoka na kuishi maisha matakatifu katika KRISTO ili waende uzima wa milele siku ya mwisho.
✓✓Kuna ndoto huwa ni maagizo ya kufanyia kazi tu maana lazima itakuwa kama ilivyoamuliwa na mbingu.
✓✓Usiogope ukiona maagaizo ambayo ni sharti yatimie ila inakupasa kuishi maisha matakatifu katika KRISTO na itakuwa heri kwako.
✓✓Mfano ni Mtume Yohana aliona kwenye maono juu ya mpinga KRISTO kwamba atakuja kutawala Duniani kabla ya kuja kwa Bwana YESU, Sasa Yohana hawezi kufunga na kuomba ili kumzuia mpinga Kristo bali anatakiwa kuwaonya Kanisa na kuwafanya kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU.
✓✓Kuna vitu havizuiliki ila inakupasa kuzingatia tu utakatifu katika KRISTO YESU.
Siku moja Mimi Peter Mabula nilikuwa namuombea Baba mmoja kwa simu na nikaona maono kwamba ni wakati wake wa mwisho kuishi duniani, nilichofanya ni kumwambia Binti yake aite Wachungaji haraka katika eneo la Hospitalini huko ili wamuongoze Sala ya Toba maana nilipojaribu Mimi kumuongoza sala ya toba alikataa, walipokuja wakamuongoza Sala ya Toba na muda mfupi baadae akafariki, yaani ni kama alikuwa tu anawasubiri waje wampatanishe na MUNGU ndipo aondoke.
✓✓Sio kila kitu unachokiona ni jambo lisilobadilika hivyo unamhitaji sana ROHO MTAKATIFU ili kuyatambua mambo ya namna hiyo maana unaweza ukaliona jambo kumbe unatakiwa uombe sana ili kuharibu mipango mibaya lakini wewe unaweza kudhani ni lazima jambo hilo litokee na kwa sababu hukuomba linatokea kweli na kumbe ulikuwa na uwezo wa kulizuia.
9. Ili kukujulisha siri za adui zako kiroho.
Waamuzi 7:13 ''Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini. ''
✓✓Gideoni alipata siri ya ajabu kuhusu adui zake na ndio maana alishinda vita hiyo kirahisi sana.
✓✓Hata wewe kwa Ndoto unaweza kuona mipango ya maadui zako hivyo ukawashinda kirahisi sana.
Zingatia na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili, Ushauri, Whatsapp n.k)
Ubarikiwe sana.

Comments