NINI UFANYE ILI ROHO MTAKATIFU AKUONGOZE.




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze somo hili muhimu sana.

◼️Nifanye nini ili niweze kuongozwa na ROHO MTAKATIFU?

◼️Nifanye nini ili ROHO MTAKATIFU awe ndani yangu?

◼️Nifanye nini ili nijazwe nguvu za ROHO MTAKATIFU na niweze kunena kwa lugha?

◼️Nifanye nini ili niwe na ROHO MTAKATIFU?

Maswali haya nimewahi kuulizwa mara nyingi sana na watu mbalimbali, inawezekana na wewe unajiuliza ufanye nini ili uweze kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.

Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.'' 

✓✓ROHO MTAKATIFU katika Kanisa la MUNGU duniani ni wa muhimu sana sana, na dhehebu lolote bila ROHO MTAKATIFU haliwezi kuwa dhehebu la kiroho na haliwezi kumpendeza MUNGU kamwe.

✓✓ROHO MTAKATIFU ndiye anayetukamilisha sisi tuliompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wetu, bila ROHO MTAKATIFU Kanisa linakuwa  ni kama gari bila mafuta hivyo haliwezi kusafiri, ni  kama samaki ziwani/Baharini  bila maji hata kidogo, hao samaki watakufa tu, ndivyo ilivyo kwa kila Mkristo bila kuwa na ROHO MTAKATIFU,  inatakiwa sana kumhitaji sana ROHO MTAKATIFU katika maisha yako.

◼️Kumbuka pia ninapokufundisha juu ya ROHO MTAKATIFU ni muhimu ukajua kwamba kuna kujazwa ROHO MTAKATIFU na kuna  kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.

◼️Kuna ROHO MTAKATIFU kuwa ndani yako na kuna ROHO MTAKATIFU kuwa juu yako.

✓✓Kujazwa ROHO MTAKATIFU ndio ubatizo wa ROHO MTAKATIFU ndani ya mtu aliyemwamini YESU KRISTO kama Mwokozi.

 Matendo 2:4 '' Wote wakajazwa ROHO MTAKATIFU, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama ROHO alivyowajalia kutamka.''

✓✓Kuongozwa na ROHO MTAKATIFU ni kukubali kuenenda katika yeye huku ukimtii.

Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.'' 

✓✓ROHO MTAKATIFU kuwa ndani yako ni pale ulipompokea na unamtii kutokea ndani yako.

1 Yohana 4:4 ''Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.'' 
 
✓✓ROHO MTAKATIFU kuwa juu yako ni lazima kwanza awe ndani yako yaani ulishampokea na sasa kuwa juu yako maana yake amekupa Nguvu zake nyingi ili umtumikie MUNGU katika KRISTO YESU, Amekuteua kwa kazi maalum, anakupa maelekezo ya kiutumishi na huduma katika Injili ya KRISTO.

Luka 4:18 ''ROHO wa BWANA yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,''

Mambo hayo yote manne(4) kuhusu ROHO MTAKATIFU ndani ya mteule wa KRISTO Mwaminifu yanakusubiria wewe  Mkristo.

Unasubiriwa kubatizwa ubatizo wa ROHO MTAKATIFU, unasubiriwa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU, unasubiriwa ROHO MTAKATIFU kuwa ndani yako na unasubiriwa ROHO MTAKATIFU kuwa juu yako, ni muhimu sana sana kama kweli unataka kumtumikia MUNGU aliyeziumba mbingu na dunia.

◼️ROHO MTAKATIFU ni ahadi ya MUNGU kwa waliompokea YESU KRISTO wote.

  Matendo 2:17-18 '' Itakuwa siku za mwisho, asema MUNGU, nitawamwagia watu wote ROHO yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake ROHO yangu, nao watatabiri.''
hivyo ndugu ihitaji sana ahadi hiyo ya MUNGU ili itimie kwako, leo ninazo njia za kukusaidia katika hili, soma kwa makini somo hili na zingatia itakusaidia sana.

Ufanye nini ili uongozwe na ROHO MTAKATIFU?

Futa hatua hizo zote saba.

1. Fanyika mtoto wa MUNGU.

✓✓Utafanyika Mtoto wa MUNGU kwa wewe kumpokea YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi wako binafsi.

Yohana 1:12-13 '' Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''

2.  Jifunze Neno la MUNGU kuhusu ROHO MTAKATIFU na kazi zake huku ukiishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.

 Ayubu 22:21 ''Mjue sana MUNGU, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia. ''

✓✓Unajifunza kuhusu MUNGU kwa kusoma ufunuo alioufunua kwetu kumhusu, ufunuo huo ni Biblia takatifu.

◼️ROHO MTAKATIFU yuko ndani ya MUNGU hivyo unapojifunza kumjua MUNGU ujue na ROHO MTAKATIFU anahusika maana ROHO MTAKATIFU ndio Roho wa MUNGU.

3. Jazwa ROHO MTAKATIFU.


Unajazwaje ROHO MTAKATIFU?

(a). Mwambie Bwana YESU akujaze.

Yohana 20:22 ''Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni ROHO MTAKATIFU.''

(b) Jazwa kwa kuombewa na watumishi wa MUNGU wenye ROHO MTAKATIFU.

1 Kor 14:19 '' lakini katika Kanisa napenda kunena maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha. '' 

✔️✔️Uwe tu na kiu ya kumhitaji ROHO MTAKATIFU hakika utajazwa.

4.  Tembea katika Nguvu za ROHO MTAKATIFU.

Matendo 1:8 '' Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. ''

5. Jifunze tena kuhusu ROHO MTAKATIFU huku wakati huu ukiwa ndani yake.
 
(a) Jifunze kuielewa sauti ya ROHO MTAKATIFU.

1 Kor  2:10 ''Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU. ''

(b) Kubali kufundishwa na ROHO MTAKATIFU.

Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.''

(c) ROHO MTAKATIFU hutufundisha Kumtukuza Bwana YESU KRISTO, Yohana 16:14 '' Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.'' hivyo tembea katika kumtukuza Bwana YESU.

Yohana 15:26 '' Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba(MUNGU), huyo ROHO wa kweli atokaye kwa Baba(MUNGU), yeye atanishuhudia.'' 

(d)  Ukipata Connection na nguvu za ROHO MTAKATIFU itumie Connection hiyo  kujazwa zaidi.

Matendo 2:2-4 ''  Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.  Wote wakajazwa ROHO MTAKATIFU, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama ROHO alivyowajalia kutamka. ''

◼️Connection na nguvu za ROHO MTAKATIFU unaipata kwenye Ibada yenye Nguvu za ROHO MTAKATIFU.


(e) Kubali kumkaribia MUNGU kila mara katika ROHO MTAKATIFU.

Waefeso 2:18-19 ''Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba(MUNGU) katika ROHO mmoja. Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake MUNGU.''

6. Kubali siku zote kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.

Yohana 16:13 '' Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.''

7. Kubali ROHO MTAKATIFU awe anakuombea kwa MUNGU.

Warumi 8:26 '' Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.''

(a)Kwa wewe kunena kwa lugha.

Marko  16:17 '' Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; ''

(b) Kwa wewe kuwa mtu wa maombi kila mara.

Waefeso 6:18 ''kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;   '' 

8. Yaishi matunda tisa(9) ya ROHO MTAKATIFU.

Wagalatia 5:22-23 '' Lakini tunda la ROHO ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.''

9. Achana na tabia za kimwili ili sasa uwe na uwezo wa kupokea mambo ya ROHO MTAKATIFU anapokusaidia.

1 Kor 2:14 ''Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya ROHO wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.''

✓✓Achana na tabia za kimwili ambazo ndio tabia za asili, achana na dhambi na achana na taratibu chafu za kimila au za madhehebu ambazo ni machukizo kwa MUNGU.

10. Usikubali kumzimisha ROHO MTAKATIFU.

1 Thesalonike 5:19 '' Msimzimishe ROHO; ''

◾Kumzimisha ROHO MTAKATIFU maana yake kumpinga, hivyo popote na wakati wote usikubali kumpinga ROHO MTAKATIFU.

'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''

Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments