UZINZI NA UASHERATI HUUCHAFUA MWILI WOTE.




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

◼️Ujumbe wa leo unasema kwamba uzinzi na uasherati huuchafua mwili wote.

◾Uzinzi ni nini?

✓✓ Uzinzi ni kitendo cha mtu aliye kwenye ndoa kufanya mapenzi na mtu yeyote nje na mwenzi wake wa ndoa.

✓✓Wazinzi Ni Wanandoa Wanaotoka kingono nje Ya Ndoa Zao.

◾Uasherati ni nini?

✓✓Uasherati ni kitendo cha kuzini anachokifanya mtu ambaye hajaingia katika ndoa.

✓✓Waasherati Ni Wale Ambao Hawajafunga Ndoa Wakifanya Ngono Wao Kwa Wao Au  Wakifanya Ngono Na Wale Walio Kwenye Ndoa.

 ✓✓Kama kuna mtu yuko katika ndoa anapozini na mtu ambaye hayuko katika ndoa maana yake mzinzi na mwasherati wanakutana kuzini.

✓✓Aliye kwenye ndoa anapotoka nje ya ndoa yake kingono ni mzinzi na mtu ambaye hajaingia kwenye ndoa anapozini huyo ni mwasherati.

✓✓Kitendo wanachokifanya wazinzi au waasherati kinaitwa uzinifu au zinaa.

◼️Biblia iko wazi sana kwamba uzinzi na uasherati ni dhambi na dhambi hiyo mtu asipoitubia na kuacha anaweza kuishi jehanamu milele.

1 Kor 6:9-11 '' Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; WAASHERATI hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala WAZINZI, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana YESU KRISTO, na katika ROHO wa MUNGU wetu.'' 

✓✓Uzinzi na uasherati ni dhambi ambayo imewaangusha wengi na imewachafua wengi hadi wanadhani wamevamiwa na nguvu za giza kumbe dhambi yao hiyo ya kuzini ndio mlango na msingi wa vifungo vyao.

◼️Sasa kwanini uzinzi na uasherati huuchafua mwili wote kiroho?

✓✓Unaweza ukakosa baraka zako kwa sababu ya uzinzi na uasherati maana dhambi hiyo huuchafua mwili wako kiroho.

✓✓Uzinzi na uasherati hufungulia milango mawakala wa shetani ili kumtesa mtu huyo.

◼️Katika maagizo ya Torati Waisraeli waliambiwa kwamba mtu akizini anakuwa najisi yaani mchafu kiroho hivyo anatakiwa kuoga kwenye maji ndipo atakuwa safi.

Walawi 15:18 ''Huyo mwanamke naye ambaye mtu mume amelala naye kwa shahawa, wote wawili wataoga majini, nao watakuwa najisi hata jioni. '' 

◼️Katika agano jipya ambalo sisi tunaishi ni kwamba uzinzi na uasherati ni ibada ya sanamu, yaani ibada ya kishetani.

Wakolosai 3:5 '' Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; ''

✓✓Na unajisi wa ibada ya sanamu unaweza kumchafua mtu mwili kiroho mpaka siku atakapotubu  na kusafishwa na damu ya YESU KRISTO Mwokozi.

✓✓Uzinzi na uasherati unaweza kumchafua mtu kiroho  na kimwili.

◼️Mtu aliyechafuka maana  yake hafai, hivyo anaweza hata kukosa haki zake kwa sababu ni mchafu mwili wake kiroho.

◼️Katika wakati huu wa Kanisa kuoga kwetu ni kujitakasa kwa damu ya YESU KRISTO kwa kutubu, kutakaswa  na kuacha dhambi hiyo.
1 Yohana 1:8-9 '' Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.''

Labda ngoja tuzungumzie kidogo juu ya mwili ni kitu gani.

◾Mwili ni nini?

✓✓Mwili ni gamba la nje linaloibeba roho.

✓✓Kwa lugha nyingine mwili ni nyumba ya kuwa kuishi roho.

✓✓Mwanadamu ni roho anayeishi katika mwili, sasa tunapozungmzia uzinzi na uasherati huuchafua mwili wote maana yake mwili wote unaweza kuwa najisi maana najisi na uchafu zina maana sawa.

◾Tunajuaje kama uzinzi na uasherati huuchafua mwili wote?

1 Kor 6:18 ''Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.'' 

✓✓Dhambi  hii ni uchafu wa kiroho na mtu anapozini hufanya dhambi juu ya mwili wake mwenyewe, yaani moja ya madhara ya kuzini ni kuuchafua mwili wako mwenyewe.

◼️Sasa tunajua kwamba kuna tendo la ndoa, hilo ni takatifu na hilo linahusika tu na mwanamke mmoja na mwanaume mmoja waliofunga ndoa na tendo hilo linahusisha tu matumizi ya asili ya mwanadamu na sio vinginevyo.

✓✓Kama wako wanandoa na wanafanya mapenzi kinyume cha maumbile basi hao walishaachwa na MUNGU, na hakuna kitu kibaya kama kuachwa na MUNGU maana usipotubu na kuacha huwezi kuurithi uzima wa milele.

Warumi 1:26-28 '' Hivyo MUNGU aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. Na kama walivyokataa kuwa na MUNGU katika fahamu zao, MUNGU aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.''

✓✓Kwahiyo kama yuko mtu ni shoga basi huyo ameshaachwa na MUNGU.

✓✓Kama yuko mtu ni mfiraji au mlawiti kama 1 Kor  6:9-11 inavyosema hapo juu, huyo ameachwa na MUNGU na asipotubia uchafu huo na kuacha hawezi kuingia uzima wa milele.

✓✓Hata anayekubali kufanyiwa ulawiti au ufiraji kama Biblia inavyoita, huyo ameachwa na MUNGU, Ni hatari sana kuachwa na MUNGU.

✓✓Kwa hiyo matukio ya uzinzi na uasherati, ulawiti na ufiraji huunajisi mwili wote, yaani kiroho mtu huyo anakuwa mchafu sana hata kama katika ulimwengu wa mwili watu wanamuona ni msafi tu.

✓✓Mtu akiwa ni mchafu mwili kwenye ulimwengu wa roho ni rahisi sana mapepo kuingia ndani yake, maana shetani ni mchafu kiroho na hupenda kukaa sehemu chafu.

✓✓Majini wote wanaitwa pepo wachafu hivyo pepo mchafu anapata nafasi ndani yako kama wewe ni mchafu mwili kiroho, na uzinzi na uasherati huuchafua mwili kiroho hivyo watu kwa sababu ya uzinzi na uasherati wamejikuta wakikaribisha mapepo ndani yao na hivyo mapepo hayo kuwafanya wazidi sana kutenda dhambi hiyo na kuwa mbali na MUNGU Muumbaji wao.

✓✓Kuna mabinti kwa sababu ya uasherati walishachafuliwa kiroho miili yao kiasi kwamba hata kupata Mtu wa kumuoa ni vigumu sana sana.

✓✓Kuna vijana wameshachafuliwa kiroho kwa sababu ya uasherati na uzinzi kiasi kwamba majanga ni mengi na kama hawajaoa basi kupata mke mwema ni ngumu sana, sana sana hupata wachafu wenzao.

✓✓Unaweza ukaendekeza uzinzi kisha ukashangaa unafukuzwa kazi, wewe unadhani umerogwa au kuna mtu hakupendi kumbe mwili wako ulishachafuka kiroho kwa sababu ya uzinifu kiasi kwamba shetani anakuonea kwa sababu ana mlango kuingia kwako wewe mchafu mwenzake.

✓✓Kuna watu wanasema wana roho za kukataliwa na kumpe hawana ila ni wachafu mwili kiroho, ni najisi kiasi kwamba mtu wa rohoni anayehitaji mchumba hawezi kutokea kamwe.

✓✓Mabinti wengi leo kwa sababu ya unajisi ya miili yao huishia tu  kutongozwa  waume za watu maana hao wanaume nao ni wachafu mwili kiroho, hivyo mchafu anamfuata mchafu mwenzake.

✓✓Kuna watu hawatulii kwenye ndoa zao kwa sababu ua miili yao ni najisi kiroho kwa sababu ya uzinzi na uasherati.

◼️Kama tu ulikuwa hujui ni kwamba ardhi ya eneo mlilofanyia uzinzi au uasherati hutunza kumbukumbu hiyo na kama kuliambatana na kifungo cha giza basi usishangae baadae ulishakuwa mtu wa Kanisa lakini  ndoto zako unakuwa unaona maeneo ambapo ardhi ilitunza kumbukumbu zako mbaya za dhambi hivyo unatakiwa utubu kwa ajili ya uchafu huo wa mwili na futa kwa damu ya YESU KRISTO hizo kumbukumbu mbaya ili zisikushikilie na kufuatilia maisha yako.

Ninayo  mifano hai mingi juu ya watu waliojikuta mambo yao mema yanagoma kwa sababu tu ya miili yao kiroho ni michafu kwa sababu ya uzinzi na uasherati.

Kwa jinsi gani uasherati na uzinzi huuchafua mwili wote?

1. Uzinzi na uasherati huwapa kibali mawakala wa shetani kukuonea.

Ezekieli 23:29 '' nao watakutenda mambo kwa chuki, watakuondolea kazi zako zote, watakuacha uchi, huna nguo na aibu ya mambo yako ya kikahaba itafunuliwa, uasherati wako na uzinzi wako. ''

2. Uasherati ni mapatno ya kipepo na hayo humkosesha mtu kupata haki zake.

2 Nyakati 21:11 '' Tena ndiye aliyefanya mahali pa juu milimani pa Yuda, na kuwaendesha katika uasherati wenyeji wa Yerusalemu, na kuwakosesha Yuda.''

3. Uliozini nao watafarakana na wewe na kukuachia mateso mengi.

Ezekieli  23:17 '' Na watu wa Babeli wakamwendea katika kitanda cha mapenzi, wakamtia unajisi kwa uzinzi wao, akatiwa unajisi nao, kisha roho yake ikafarakana nao.''

4. Dhambi ya uzinzi na uasherati itakutenga mbali na MUNGU.

Hosea 5:4 '' Matendo yao hayatawaacha kumgeukia MUNGU wao; maana roho ya uzinzi imo ndani yao, wala hawamjui BWANA.'' 

5. Dhambi ya uzinzi na uasherati itakufanya utapanye mali zako ambazo zingekusaidia.

Luka 15:13 '' Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.'' 
Huyu mwana mpotevu ni mfano hai wa kutumia mali kwa anasa na uasherati hadi akawa masikini mkubwa.

6. Kwa dhambi hiyo wewe utakuwa sio mtakatifu.

Waefeso 5:3 ''3 Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; '' 

7. Uzinzi na uasherati ni ibada ya sanamu na huleta ghadhabu ya MUNGU.

Wakolosai 3:5-6 '' Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya MUNGU.'' 

8. Usipotubu na kuacha uzinzi na uasherati ujue jehanamu inakungoja.

Yuda 1:7 '' Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele.'' 

◼️Kwa anayefanya uzinzi au uasherati nafasi ya kutubu na kuacha ni leo.

◼️Tubu katika KRISTO YESU na jitenge mbali na uasherati na uzinzi.

✓✓Kama kweli unaitarajia mbingu mpya ya MUNGU kwa ajili ya watakatifu basi hakikisha unashinda dhambi na kuziacha.

✓✓Kama kweli unautaka uzima wa milele basi mpokee Bwana YESU, tubu na kuacha dhambi zikiwemo kuacha uzinzi na uasherati. 

◼️Kataa uzinifu, jitenge na uzinifu. ikimbie zinaa na usifanye uzinzi  na uasherati tenaaaaaaaaa.

Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments