![]()  | 
| Na Mwl Peter Mabula  Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi  | 
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno hai la MUNGU aliye hai milele.
◼️Leo tunaangalia faida za kujidhili mbele za MUNGU.
Luka 14:11 ''Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.''
◾Kujidhili ni nini?
◼️Kujidhili ni hali ya kunyenyekea na kujishusha.
✓✓Kinyume ya kujidhili ni kujikweza.
◾Kujikweza ni nini?
◼️Kujikweza ni hali ya kujiinua au kujipandisha juu na kujiona wewe ni bora kuliko wengine.
◼️Kwa mujibu wa Biblia mtu binafsi huna kibali cha kujikweza ila MUNGU ndiye anaweza kukukweza kulingana na jinsi unavyomtii.
◾MUNGU kukukweza ina maana gani?
◼️MUNGU kukukweza ina maana ya MUNGU kukuinua na kukupandisha juu kuliko wengine.
✓✓Ila hata kama ni MUNGU amekuinua hauna kibali wewe cha kujiinua, ukijiinua MUNGU atakushusha haraka sana.
Mathayo 23:12 '' Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.''
◼️Kwa hiyo ndugu, katika maisha yako yote chagua kujidhili mbele za MUNGU na sio kujikweza.
◼️Katika huduma yako chagua kujidhili na sio kujikweza.
◼️Katika wito wako uliopewa na MUNGU katika KRISTO YESU hakikisha unaambatana na kujidhili siku zote mbele za MUNGU na mbele za wanadamu pia.
✓✓Kuna faida kubwa sana ukijidhili mbele za MUNGU, zingatia sana kujidhili mbele za MUNGU siku zote.
◼️Jidhili sana mbele ya Bwana YESU KRISTO Mwokozi na jidhili daima mbele za ROHO MTAKATIFU ndipo utakwezwa.
Faida nne(4) za kujidhili.
1. Mabaya yaliyokusudiwa kwako yatazuiliwa kwa sababu umejidhili mbele za MUNGU.
1 Wafalme 21:25-29 '' (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.) Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole. Neno la BWANA likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.''
✓✓ Ahabu alikuwa amefanya mabaya sana mbele za MUNGU, adhabu kutoka ulimwengu wa roho ilikuwa kwamba Ahabu afe na mabaya mengi yaachiliwe katika nchi yake maana yeye ndio alikuwa mfalme wa nchi ile na aliwakosesha hadi wananchi wake.
✓✓Kilichomwokoa Ahabu hata asife wakati huo ni yeye kujidhili mbele za MUNGU.
◼️Kujidhili mbele za MUNGU kuna faida na matokeo ya haraka sana kwa mtu huyo aliyeamua kujidhili mbele za MUNGU.
◾Ahabu alijidhili kwa namna gani?
✓✓Biblia inasema aliposikia Neno la MUNGU akararua mavazi yake, akavaa magunia, akaanza maombi ya kufunga, akajilala juu ya magunia, akaanza kwenda kwa upole yaani akaacha ukali na dharau.
✓✓Kujidhili kule kuliondoa adhabu mbaya wakati yeye akiwepo, lakini kwa sababu taifa zima walikuwa wamemwacha MUNGU wa mbinguni basi mabaya hayo yalikuja kutokea baada ya Ahabu kufa.
✓✓Unaona sasa jinsi kulivyo na faida kubwa sana ukijidhili mbele za MUNGU?
Yaani inaweza hata kuzuiliwa adhabu mbaya kwako, kwa familia yako, kwa nchi yako, au ukoo wako kwa sababu tu wewe umejidhili mbele za MUNGU.
◼️Ndugu, hakikisha unakuwa mtu wa kujidhili mbele za Bwana YESU siku zote.
2. Utahesabiwa haki na kuinuliwa, kwa sababu umejidhili mbele za MUNGU.
Luka 18:10-14 '' Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee MUNGU, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee MUNGU, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.''
◼️Kujidhili mbele za MUNGU kunaleta kuhesabiwa haki mbele za MUNGU kuliko kujiinua.
Hapo kwenye maandiko tunaona kuna mtu anajisifu kwamba yeye sio kama wengine, anajiona yeye ni mtu special sana, anajiona anastahili mno, hana haja ya kutubu,anajiona hana dhambi ni mkalimilifu, hana haja ya kunyenyekea, kwenye maombi mbele za MUNGU anatoa tu CV yake na sio kuomba, anajihesabia haki na Biblia inahitimisha kwamba mtu huyo anachokifanya ni kujikweza.
Lakini yuko pia mtu yeye alijidhli mbele za MUNGU na Biblia inasema alihesabiwa haki yeye yaani alisamehewa na kutakaswa kwa sababu amejidhili mbele za MUNGU.
◾Alijidhili kwa namna gani?
✓✓Alijinyenyekea sana mbele za MUNGU, aliomba maombi ya toba akimaanisha, alihitaji msaada wa MUNGU na alimtegemea MUNGU.
3. MUNGU atakukuza, kwa sababu ya kujidhili kwako mbele zake.
Yakobo 4:10 '' Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza.''
✓✓MUNGU kukukuza ina maana nyingi zikiwemo MUNGU kukubariki, MUNGU kukutumia katika kazi yake kwa viwango vikubwa, MUNGU kukufanya uonekane wa thamani, MUNGU kukufanya uheshimiwe na watu,Kukupa hitaji lako uliloomba, MUNGU kuizidisha huduma yako na kazi yako, kukuletea ushindi kila eneo n.k
✓✓Hayo yote yatakuja kama matokeo ya wewe kujidhili kwako mbele za MUNGU.
4. MUNGU atakupandisha juu.
1 Petro 5:6-7 ''Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa MUNGU ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.''
✓✓MUNGU kukupandisha juu maana yake kukufanya uende juu kihuduma, kimaisha, kikazi n.k
Lakini matokeo hayo mazuri yatakuja kwa sababu ya wewe kujidhili mbele zake, na maana mojawapo ya kujidhili ni kunyenyekea, hivyo unaponyenyekea chini ya mkono wa MUNGU ulio hodari maana yake unajidhili mbele za MUNGU.
◼️Ndugu, hakikisha unajidhili mbele za MUNGU katika KRISTO YESU siku zote.
✓✓Lakini pia kujidhili kwako kusiwe katika maneno tu bali kuwe katika vitendo.
◼️Ishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU, huko ndiko kujidhili mbele za MUNGU.
◼️Hakikisha YESU KRISTO ni Bwana na Mwokozi wako binafsi, huko ndiko kujidhili mbele za MUNGU.
◼️Hakikisha unaishi maisha ya toba huku ukijitenga na kila maovu, dhambi na makosa, huko ndiko kujidhili mbele za MUNGU.
Yakobo 4:8-10 '' Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza.''
◼️Hakikisha unamtii ROHO MTAKATIFU, huko ndiko kujidhili mbele za MUNGU.
◼️Hakikisha unatoa fungu la kumi na sadaka safi maana hiyo ni sehemu muhimu ya kujidhili mbele za MUNGU.
◼️Hakikisha unalitii Neno la KRISTO siku zote na liluhusu kuingia kwa wingi moyoni mwako, huko ndiko kujidhili mbele za MUNGU.
✓✓Usiwe msikiaji tu wa Neno bali uwe mtendaji wa Neno la MUNGU, huko ndiko kujidhili mbele za MUNGU.
Yakobo 1:21-24 '' Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.''
◼️Maombi ya leo.
✓✓Leo jifungue vifungo vya giza kwa maombi na maamuzi sahihi kama umefungwa.
Isaya 52:2-3" Jikung'ute mavumbi; uondoke, Uketi, Ee Yerusalemu; Jifungulie vifungo vya shingo yako, Ee binti Sayuni uliyefungwa. Maana BWANA asema hivi, Mliuzwa bure; nanyi mtakombolewa bila fedha."
✓✓Leo jikung'ute kimaombi na uondoke ili nguvu za giza zilizokushikilia zikuachie.
✓✓Jikung'ute kimaombi na uondoke ili huo ugonjwa wa kichawi udondoke na wewe uwe huru.
✓✓Ikung'ute kimaombi ndoa yako uondoke ili ndoa yako mkuu wa giza aliyeishikilia aiachie.
Je umeshikiliwa na kifungo gani?
✓✓Jikung'ute leo kimaombi na uondoke ukikitaja kifungo hicho ili kikuachie.
Je nini chako kimekamatwa na nguvu za giza?
Je ni uzao au uchumi au ndoa au kibali au afya au nini?
◼️Kimaombi unaweza kuomba leo ukitumia jina la YESU KRISTO, damu ya YESU KRISTO na Neno la ufunuo ukikung'uta maeneo yako ili nguvu za giza zilizoshikilia ziachie na uwe huru.
✓✓Jifungulie vifungo vyako ulivyofungwa, jifungue kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
✓✓Ifungue ndoa yako, ifungue familia yako, fungua uchumia, fungua kazi yako, wafungue watoto wako.
Uliuzwa bure na utakombolewa bure.
Ondoka jikung'ute kimaombi na cha kipepo kilichokushikilia kitaachia.
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana
 
Comments