FAIDA ZA KUMSHUKURU MUNGU. (2)

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Sehemu ya pili.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe sana ndugu zangu wote.
Karibuni sana katika mfululizo wa somo hili, somo la kumshukuru MUNGU katika KRISTO YESU.
Leo tunajifunza KWANINI UMSHUKURU MUNGU?

Zaburi 9:1-3 ''Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote; Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu; Nitafurahi na kukushangilia Wewe; Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu. Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako.''

Kabla ya hapo ngoja niseme machache kuhusu kumshukuru MUNGU.

✓✓Kwanza maana ya kumshukuru MUNGU ni kuonyesha ishara ya kuridhika na jambo la wema alilokufanyia MUNGU.

Tena kumshukuru MUNGU ni kusema kwa maneno mazuri ya kutoa shukrani kwa kwake kwa wema aliokufanyia.
Kila mwanadamu mwenye pumzi ya uhai hadi leo tukiwa katika mwisho wa mwaka inampasa mwanadamu huyo kumshukuru sana MUNGU sana.
Sio kwamba kumshukuru MUNGU ni hadi mwisho wa mwaka bali maisha yetu kama wateule wa KRISTO yamejaa shukrani kwa MUNGU, lakini hii ni maelekezo malumu ya kuona kwamba hata mwisho wa mwaka inakupasa kutumia muda mwingi kumshukuru MUNGU kipekee sana.

Kumbuka kuna miujiza mikubwa zaidi miwili tu kwa mwanadamu awaye yote.
Miujiza hiyo ni.

1. Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako hata jina lako likafutwa kwenye kitabu cha hukumu na kuandikwa sasa katika kitabu cha uzima mbinguni, huo ndio muujiza mkubwa kuliko yote kwenye maisha ya mwanadamu, yaani muujiza wa kujitenga na jenahamu ili uingie uzima wa milele.

2. Muujiza mkubwa wa pili ni uhai, wewe kuwa hai ndio muujiza mkubwa kabisa  wa pili katika maisha yako na aliyekufanya uwe hai leo ni MUNGU tu na sio mwingine yeyote, hivyo mshukuru sana MUNGU aliyekuumba na sasa amekulinda hata uko hai.
Kumbuka uhai ukiondoka huwa haurudi, mtu akifa huwa amekufa na hatuwezi kumuona tena duniani, inawezekana walioondoka duniani walikuwa  na mipango yao mizuri sana ya mwakani au zaidi lakini leo hawako, ni huzuni kwetu lakini na hatuna namna hivyo kama wewe uko hai leo hakikisha unamshukuru MUNGU aliyekulinda na mpe haki yake kwa kumshukuru.

✓✓Ndugu, hakikisha unaiona thamani ya kumshukuru MUNGU na mshukuru maana anastahili kushukuriwa.

Nakumbuka miezi kadhaa iliyopita kuna ndugu mmoja ambaye  nilikuwa naenda dukani kwake mara kwa mara ili kununua vitu, alikuwa mtu wa stori na furaha na alikuwa mtu wa watu, alikuwa na mipango yake mizuri ya kununua magari n.k lakini siku moja mbaya kwake alifunga duka lake na kuchukua bodaboda ili arudi nyumbani kwake, akiwa njiani pikipiki ile iligongana na lori na akafariki pale pale mwili wake ukisagika vibaya sana.

Nakumbuka kuna rafiki yangu mmoja siku moja nilimkuta kajiinamia hana furaha nikamuuliza mbona yuko hivyo akasema jirani yake ambaye ni bodaboda amenunua pikipiki mpya na siku chache tu baada ya kununua alimbeba mteja mmoja usiku mapema kabisa na mteja huyo alikuwa anaelekea mitaa ile ile ambayo yule bodaboda alikuwa anaishi, kumbe jirani kabisa na anapokaa huyo bodaboda kulikuwa na mtu ambaye wamepanga dili na abiria aliyembeba ili kumwibia ile pikipiki yake mpya. Alipofika karibu na nyumbani kwake alikabwa na abiria na yule mwingine akatokea na kumkata shingo na kumtenganisha shingo na kiwiliwili na kisha wakachukua pikipiki na kuondoka, tukio hilo lilimuumiza sana rafiki yangu maana yule bodaboda alikuwa ni jirani yake na hakuna na uadui na mtu yeyote.
Kuna hatari nyingi katika dunia hii ila ashukuriwe MUNGU maana tukiomba ulinzi wake anatulinda.

Isaya 26:3-4 ''Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele.   ''

KWANINI UMSHUKURU MUNGU?

1. Unamshukuru MUNGU kwa sababu ni mapenzi ya MUNGU katika KRISTO YESU  kwamba tumshukuru.

1 Thesalonike 5:18 ''shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya MUNGU kwenu katika KRISTO YESU.''
Neno mapenzi ya MUNGU ni sawa na neno matakwa ya MUNGU.
Neno ''matakwa'' maana yake jambo  ambalo mtu analitaka.
Matakwa ya MUNGU maana yake ni jambo ambalo MUNGU analitaka, hivyo moja ya jambo ambalo MUNGU analitaka ni shukrani kutoka kwetu.
Hakikisha unamshukuru MUNGU maana ni mapenzi yake katika KRISTO YESU.

2.  Unamshukuru MUNGU kwa sababu yeye ni mwema na fadhili zake ni za milele.

1 Nyakati 16:34 ''Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele.''

Fadhili za MUNGU maana yake msaada wa MUNGU, Hivyo inakupasa kumshukuru MUNGU kwa sababu ni mwema na msaada wake kwako ni wa milele.
MUNGU katika mwaka huu tu amekusaidia katika mambo mengi sana sana hivyo mshukuru MUNGU sana.

Waebrania 13:6 ''Hata twathubutu kusema, BWANA ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? ''
Ndugu mshukuru MUNGU kwa maombi na kwa sadaka kwa maana amekusaidia katika mambo mengi mwaka huu.
Inawezekana kuna kipindi uliumwa ila ukapona, jambo la ajabu ni kwamba inawezekana wapo watu waliumwa ugonjwa kama ulioumwa wewe na wakanywa dawa zile zile ila wao hawakupona bali walikufa ila wewe kwa neema ya MUNGU iliyobeba msaada wa MUNGU ulipona, ndugu Mshukuru sana MUNGU.

Kipindi fulani niliona mtandaoni juu ya mtu mmoja maarufu ambaye alifariki mwaka huu kwa sababu ya ugonjwa wa malaria, unadhani ni yeye tu aliumwa malaria mwaka huu?
Je  yeye tu aliumwa na mbu mwaka huu hata akapata malaria? na licha ya kunywa dawa za malaria hakupona.
Ndugu, mimi najua hakika una jambo la kumshukuru MUNGU ambaye fadhili zake ni za milele kwako.

Zaburi 118:1 '' Haleluya. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. ''

3. Unamshukuru MUNGU kwa sababu amekulinda dhidi ya adui zako kiroho na kimwili.
 
Zaburi 124:2-8 '' Kama si BWANA aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia. Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu; Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo.  Na ahimidiwe BWANA; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi. -Zaburi 124:6-8 ''

Ndugu zangu, tuko katika wakati ambapo baadhi ya wanadamu wana roho za shetani  ila tu ashukuriwe MUNGU wetu katika KRISTO YESU maana hakutuacha tuwe mawindo ya maadui zetu, ndugu hakika unacho cha kumshukuru MUNGU kukupa uzima hadi leo.

4. Unamshukuru MUNGU kwa sababu wewe ni mali yake na uhai ulionao ni kwa agizo lake.

Ezekieli 18:4 ''Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa. ''
Roho yako ni mali ya MUNGU hivyo uhai ulionao ni kwa agizo lake.
Mshukuru MUNGU kwa uhai aliokupa maana wewe u mali yake.
Yaani wewe u mali ya MUNGU na kuishi kwako duniani kunategemea na ulinzi wa MUNGU.

Zaburi 24:1 ''Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Dunia na wote wakaao ndani yake.''
 Mshukuru MUNGU sana.

5. Unamshukuru MUNGU kwa sababu ni haki yake kushukuriwa.

Zaburi 7:17 '' Nitamshukuru BWANA kwa kadiri ya haki yake; Nitaliimbia jina la BWANA aliye juu. ''

Mwanadamu akikutendea mema kidogo huwa unamshukuru sana, Bosi wako hata ukimuona tu huwa unamshukuru hata hujui unamshukuru kwa ajili ya nini, dakitari aliyekutibu huwa unamshukuru. Hata mtu akikupa zawadi huwa unamshukuru lakini naomba nikuambie hivi ndugu yangu ni kwamba MUNGU ni zaidi ya wanadamu wote. Msaada wa MUNGU ni zaidi ya misaada ya wanadamu wote, na misaada mingine wanayokupa wanadamu ni kwa agizo la MUNGU na sio kwa matakwa yao hivyo ni MUNGU anakuwa amekupa kupitia wanadamu hao.
Kwa sababu watu  waliokusaidia ni haki yao wewe kuwashukuru basi kwa MUNGU ni zaidi.
Ndugu mshukuru sana MUNGU maana ni haki yake kushukuriwa.

6.  Unamshukuru MUNGU kwa sababu kumshukuru MUNGU ni sehemu ya ibada.

Zaburi 100:4 '' Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake; ''
Ukiangalia tafasiri ya BHN kwenye andiko hili la Zaburi 100:4a inasema ''Pitieni mlangoni mwa hekalu la MUNGU kwa shukrani'' hivyo Ingia Kanisani  au ibadani kwa shukrani kwa MUNGU.
Kumshukuru MUNGU ni sehemu muhimu ya ibada.
Hata Kanisani huwa tuna muda wa maombi  ya kumshukuru MUNGU, hata unapotoa ushuhuda wa ambacho MUNGU amekutendea hiyo ni sehemu ya ibada ya shukrani mbele za MUNGU.
Hakika una wajibu sana wa kumshukuru MUNGU.

7. Unamshukuru MUNGU kwa sababu ndiye akupaye kushinda.

1 Kor 15:57 ''  Lakini MUNGU na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu YESU KRISTO.''
MUNGU ndiye akupaye kushinda katika KRISTO YESU.
MUNGU asipokupa kushinda hauwezi kamwe kuwashinda wanadamu wabaya, huwezi kuwashinda majini, mizimu, wachawi na mawakala wa shetani wa kila namna.
Mshukuru MUNGU maana ndiye akupaye kushinda na zaidi ya kushinda katika KRISTO YESU Mwokozi.
Hii ilikuwa ni sehemu tu ya pili ya somo hili ambalo litaendelea, hivyo fuatilia na itakusaidia sana.
aamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo yangu.
By Mwl Peter  Mabula.
+255714252292(Hadi whatsap)
MUNGU akubariki sana kwa kusoma somo hili.

Comments