FAIDA ZA KUMSHUKURU MUNGU (3)



Peter na Jemimah Mabula 
Watendakazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Sehemu ya tatu.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe sana ndugu zangu wote.
Karibuni sana katika mfululizo wa somo hili, somo la kumshukuru MUNGU katika KRISTO YESU.
Siku ya kwanza tuliangalia utangulizi na maana ya KUMSHUKURU MUNGU, Siku iliyofuata tuliangalia KWANINI UMSHUKURU MUNGU? na leo tunaangalia UNAMSHUKURU MUNGU KWA NJIA GANI?

Kabla sijakueleza kiini cha ujumbe wa leo ngoja nikueleze mambo machache kuhusu umuhimu wa kumshukuru MUNGU.
Kwanza maana ya ''kumshukuru MUNGU'' ni kuonyesha ishara ya kuridhika na jambo la wema alilokufanyia MUNGU.
Maana ya pili ya  kumshukuru MUNGU ni kusema kwa maneno mazuri ya kutoa shukrani kwa kwake kwa wema aliokufanyia.

Zaburi 107:1-2 ''Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi. ''

Kila mwanadamu unayo sababu ya kumshukuru MUNGU  ukianzia na kumshukuru kwa sababu ya ulinzi aliokupa hata uko hai leo.

Kuna watu mwaka huu walipitia katika hatari kubwa sana lakini MUNGU akawalinda, ndugu mshukuru MUNGU.

Kuna watu mwaka huu MUNGU aliwapa kufaulu masomo na wengine sasa wako chuo kikuu, ndugu mshukuru MUNGU sana.

Kuna watu walihangaika sana kupata kazi lakini ni mwaka huu walipata kazi, kwanini iwe tu mwaka huu, ndugu mshukuru MUNGU sana.

Kuna watu ni mwaka huu walipata uzao, kuna watu ni mwaka huu walijenga nk

Hakika kila mtu ana sababu nyingi sana za kumshukuru MUNGU kwa maombi na sadaka.
Kuna mtu mmoja mwanaume mwaka huu waliokuwa jirani naye walimshangaa maana aligeuka ghafla na kuanza kuwa anaongea peke yake kumbe alirogwa ili awe kichaa, hali ikawa mbaya sana hadi ndugu yake mmoja alinishirikisha akishangaa sana kaka yake alivyogeuka na kuwa mwehu, baadae kwa maombi ikagundulika ni uchawi alifanyiwa. Ni neema ya MUNGU tu lakini wakuu wa giza walikuwa wamemfanya mwehu anayevua nguo hata mbele za watu, ndugu, wewe kuwa salama leo ni kwa neema ya MUNGU na ulinzi wake hivyo Mshukuru MUNGU sana.

Kuna mteule wa KRISTO mmoja mwaka huu alitafutiwa msichana wa kazi na kumbe msichana yule ni Mchawi aliyefundishwa na Babu yake kuroga, alianza kufanya mambo ya ajabu katika familia hiyo, siku moja alichukua soksi za Baba wa familia na kusafiri nazo kichawi usiku kutoka Dar es salaam hadi mpakani mwa Morogoro na Iringa na alipomaliza kuzifanyia uchawi alizirudisha usiku huo huo na tangu siku ile uchumi wa Baba yule ukayeyuka, na katika familia ile Binti yule alikwenda pale kwa sababu mama wa familia ile alikuwa amejifungua hivyo alitakiwa kupatikana mlezi wa mtoto, lakini binti huyo kwa sababu ya uchawi  siku moja alifumwa na mama wa familia akiwa anamnyoa mtoto mchanga nywele ili azipeleke kwao usiku kuzifanyia uchawi na vifungo, hapo ndipo ilibidi binti yule ahojiwe na kupigwa sana ndipo akaweza wazi kila alichokifanya cha uchawi pale, akasema pia kwamba yeye alifundishwa uchawi na Babu yake mzaa Baba na nilipomhoji mimi juu ya kazi yake katika uchawi alisema kwamba Babu yake ana misukule 52 na yeye kazi yake ni kuwalisha chakula, nilipomuuliza ni chakula gani na ni muda gani huwalisha akasema kwamba chakula cha hiyo misukule  ni pumba za mchele akichanganya na maji na huwalisha usiku. Yaani hata alipokuwa  Dar es salaam alikuwa anaondoka usiku ili kwenda kusimamia misukule na kuichapa kisha anaipa chakula, na ajabu siku hiyo ndipo nilishangaa roho ya uchawi  iliyovyo ya ajabu na mbaya sana maana Binti yule alisema kwamba moja ya misukule ya Babu yake ni kaka yake mwenyewe yaani kaka yake na binti huyo alikufa miaka minne iliyopita na kumbe aliyemuua ni Babu yake na kumfanya msukule, hatua ya kwanza alisema kwamba huwa wanawakata ulimi hao misukule na huku kwenye ulimwengu wa mwili huwa wanazika mgomba na sio mtu hata kama wao wanaona mtu halisi, nilishangaa sana lakini ndugu yangu kwanini nakumbia haya ambayo ni ya kweli kabisa, ni kwa sababu MUNGU amekulinda wewe ndio maana uko salama, hivyo hakikisha unamshukuru MUNGU kwa maombi na kwa sadaka nzuri.

Zaburi 121:4-5 ''Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. BWANA ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.''

Biblia inasema kwamba MUNGU halali wala hasinzii daima hivyo muda wote unalindwa na MUNGU, ndugu mshukuru MUNGU hakika, mwendelezo unaofuata wa somo hili nitakuambia faida unazoweza kuzipata kwa sababu ya kumshukuru MUNGU.
Ndugu, unapoona upo sasa mwisho wa mwaka ukiwa hai basi mshukuru MUNGU sana, maana unalindwa na nguvu za MUNGU.

1 Petro 1:5 '' Nanyi mnalindwa na nguvu za MUNGU kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.''

Ndugu hakikisha unaona umuhimu mkubwa sana wa kumshukuru MUNGU kwa kukulinda mwaka huu.

UNAMSHUKURU MUNGU KWA NJIA GANI?

1. Kwa kumtolea sadaka ya kumshukuru/shukrani.

Zaburi 50:23 '' Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa MUNGU. ''

Kama kuna kitu muhimu katika kumshukuru MUNGU basi sadaka ya shukrani ni jambo la muhimu sana.
Kumbuka maana ya kumshukuru MUNGU  ni kuonyesha ishara ya kuridhika na jambo la wema alilokufanyia MUNGU.
Sasa ishara mojawapo ya kibiblia ya shukrani kwa MUNGU ni sadaka ya shukrani.

Kwa neema aliyokupa MUNGU kuwa salama hadi leo ukiwa mwishoni mwa mwaka basi usiache kumtolea sadaka ya shukrani.

Mkumbuke Nuhu ambaye baada ya kupona katika gharika alimtolea MUNGU sadaka za shukrani zilizopelekea MUNGU kufuta adhabu ya gharika na akaweka upinde ili uwe unamkumbusha , sadaka njema na inayotoka katika moyo wa furaha, na inayotolewa kwa imani na maombi huwa kuna matokeo makubwa sana.

Mwanzo 8:20-21 '' Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.''

2. Kwa wimbo wa kumsifu na kumtukuza.

Zaburi 28:7 '' BWANA ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru ''

Mshukuru MUNGU pia kwa wimbo wa kumshukuru maana amekupa neema ya kuishi hadi leo.
Kuna nyimbo nyingi za injili za kumshukuru MUNGU unaweza ukamwimbia MUNGU kwa neema moyoni mwako ukimshukuru kwa neema aliyokupa ya ulinzi  hadi leo ukiwa mwishoni mwa mwaka huu.
Wakati mwingine ROHO MTAKATIFU anaweza kuweka moyoni mwako wimbo wa kumsifu MUNGU, kumtukuza na kumshukuru, unaweza ukatamka kwa maneno yako ya furaha na utauwa mbele za MUNGU ukimshukuru kwa kinywa chako kupitia wimbo.

3. Kwa kupitia vifaa vya mziki  kucheza.

Zaburi 33:2 '' Mshukuruni BWANA kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.''

Kama wewe ni mtaalamu wa kupiga vyombo vya mziki, ngoma, kinanda n.k hakikisha hata kwa kipaji chako hivyo unamtukuza MUNGU na kumshukuru ukiambatananisha na nyimbo za kumtukuza MUNGU huku ukiwafanya watu kucheza kwa furaha mbele za MUNGU wakimtukuza..

4. Kwa maombi ya Shukrani.

Wakolosai  4:2 ''Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; ''

Moja ya njia kuu ya kumshukuru MUNGU ni kwa njia ya maombi ukitamka shukurani, ukimshukuru na hata ukitaja ni nini amekutendea maana vipo vingi.
Maombi ya shukurani kwa MUNGU ni ya muhimu sana.
Usiache kuingia katika maombi ya kumshukuru MUNGU.

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
By Mwl Peter  Mabula.
+255714252292
MUNGU akubariki sana kwa kusoma somo hili.

Comments