FAIDA ZA KUMSHUKURU MUNGU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Sehemu ya kwanza.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana katika mfululizo wa somo hili ambalo linaanza leo hadi mwisho mwa mwaka huu, somo la kumshukuru MUNGU katika KRISTO YESU.
Kwangu mimi Peter mwezi december huwa ni mwezi wa kumshukuru MUNGU hasa wiki 2 za mwisho wa mwezi wa 12.

Katika mwezi huu naweza kuomba pia  maombi mengine lakini kusudi kubwa la mwezi wa kumi na mbili kwangu ni mwezi wa shukrani kwa MUNGU, ukiweza hata wewe unaweza kuufanya mwezi huu kuwa mwezi wa kumshukuru MUNGU ila nje na kumshukuru MUNGU zingatia sana sauti ya ROHO MTAKATIFU anayokuelekeza na kukufunulia, fanyia kazi pia hiyo  maana hata kama uko katika mwezi wa kumshukuru MUNGU, ROHO MTAKATIFU anaweza kukupa maagizo hivyo usiache kufanyia kazi mnaagizo hayo.

Kama kuna jambo ni la muhimu sana katika maisha yako basi ni pamoja na kumshukuru MUNGU.

✓✓MUNGU hawezi kujishukuru mwenyewe bali amekuumba wewe, akakulinda, akakupa uzima na uhai na afya njema ili umsifu, umtukuze na kumshukuru.

✓✓Kumshukuru MUNGU ni jambo la muhimu sana na kwa Mteule wa KRISTO anayejielewa basi kumshukuru MUNGU ni jambo la lazima.

Mimi binafsi namshukuru MUNGU kwa mambo mengi sana lakini namshukuru sana pia MUNGU kwa ajili yako rafiki yangu unayejifunza somo hili muhimu  na namshukuru MUNGU kwa masomo yangu kupata kibali moyoni mwako hata huwa unajifunza na ninakuombea daima  '' Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru MUNGU bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la  MUNGU mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la  MUNGU; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini. 1 Thesalonike 2:13 ''

Nini maana ya neno ''Kumshukuru MUNGU''?
Zipo maana mbili za Neno Kumshukuru MUNGU.

1. Kumshukuru MUNGU ni kuonyesha ishara ya kuridhika na jambo la wema alilokufanyia MUNGU.

Zaburi 106:1 '' Haleluya. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. ''

2. Kumshukuru MUNGU ni kusema kwa  maneno mazuri ya kutoa shukrani kwa MUNGU kwa wema aliokufanyia.
Ni kusema  ''Asante'' kwa MUNGU kwa wema aliokutendea.

Zaburi 100:3-5  '' Jueni kwamba BWANA ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake; Kwa kuwa  BWANA ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi.''

Ni jambo jema sana kumshukuru MUNGU,
Kuwa hai tu ni kwa neema ya MUNGU.
Mwanadamu amewekewa kuzaliwa mara moja na kufa mara moja hivyo uhai ukiondoka huwa haurudi, hivyo kitendo cha wewe kuwa salama kwa miezi yote ya mwaka huu hakika unahitaji kumshukuru sana MUNGU sana.

Mtu mmoja siku moja aliniambia kwamba ''Mtumishi mimi nahisi MUNGU hanipendi na hanihitaji maana ninateseka sana japokuwa huwa naomba'' 
Mtu huyo nilimjibu kwamba ''MUNGU anakupenda sana maana angekuwa hakupendi usingekuwepo duniani''
Hiyo haina maana kwamba wanaokufa MUNGU hawapendi  bali maisha ni kama ukurasa, ukifungwa Ukurasa wa mtu duniani hautafunguliwa tena, hivyo kama wewe ukurasa wako  wa kuishi duniani  haujafungwa basi mshukuru MUNGU sana na elewa tu kwamba upo duniani kwa kusudi la MUNGU na upo kwa ajili ya kuitafuta toba ya kweli katika KRISTO ili ubaki kuwa wa uzima wa milele.
Kuna watu watakuwa hai mwaka mpya ujao kwa sababu tu MUNGU amewapa ofa waokoke na kutubu ili wasiende jehanamu.

Kuna watu MUNGU atawapa uhai mwaka mpya ujao ili wamtumikie katika KRISTO YESU.

Kuna watu MUNGU atawapa uhai mwaka mpya ujao ili tu waitegemeze kazi yake.
Hata wewe ndugu ni muhimu sana kujua kwamba MUNGU amekupa nafasi kuishi kwa kusudi lake hivyo lifanyie kazi kusudi la MUNGU lililo katika KRISTO YESU.
Siku muda wa kusudi la MUNGU ukiisha utaondoka duniani.

Ufanye mwezi huu wa 12 mwishoni  kuwa kipindi Cha kumshukuru MUNGU.
Una haki ya kumshukuru MUNGU maana amekulinda, amekuepushia na mabaya mengi.

 Inawezekana kuna watu walipanga mipango ufe mwaka huu lakini YESU KRISTO akasema utaishi mwaka huu wote ndio maana unaishi, ndugu mshukuru MUNGU.
Inawezekana kuna mahali uliwekewa mtego wa kipepo ili ufe, inawezekana uliwekewa sumu, inawezekana kuna watu walishaanza hata kuwaza kugawana mali zako maana walijua utakufa tu mwaka huu, lakini MUNGU kwa neema yake ya ajabu aliwatuma Malaika zake wakakulinda ndio maana uko salama.

Mfano hai ni Mtumishi wa MUNGU Danieli ambaye Mwaka fulani alipangiwa kufa ili tu asimalize mwaka huo akiwa hai, lakini Biblia inasema kwamba MUNGU alituma Malaika ili tu kuhakikisha Danieli anaishi.

Danieli 6:22 ''MUNGU wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; ''

Inawezekana kuhusu wewe kwa mwaka huu vilifanyika vikao vya wachawi zaidi ya kumi ili tu kukuondoa duniani lakini MUNGU akakulinda, ndugu yangu hivyo hivyo ulivyo tumia muda mwingi kumshukuru MUNGU.

Tembea kwenye utakatifu na mpe MUNGU heshima yake maana macho yako hayakuona tu kazi kubwa aliyoifanya MUNGU hata leo uko hai.
Hata mimi nina mambo mengi sana ya kumshukuru MUNGU kwa ajili ya mwaka huu tu, ni mengi sana.

Ngoja nikuambie kwa leo mambo matatu ambayo MUNGU alinilinda kiajabu sana na namshukuru sana sana.
Siku moja kuna rafiki yangu mmoja yuko Congo ambaye kuna kipindi kama miaka miwili nyuma alikuwa ananipigia simu namuombea mtoto wake aliyekuwa anaumwa sana pia nilikuwa naombea familia yake.
Ulipita muda mrefu sana tangu tumeongea kwa simu lakini mwaka huu  aliniandikia ndoto aliyoota kuhusu mimi.
Alisema kwamba ndotoni  alichukuliwa na mtu wa MUNGU asiyemjua ambaye kwa tafasiri ya kawaida ni kama Malaika au ni Bwana YESU mwenyewe ambaye alimleta nilipokuwa mimi nawahubiria watu na akawepo pale kisha huyo mtu wa MUNGU nilipomaliza tu kuhubiri akanisaidia kuwaponya watu wote pale waliokuwa na vifungo na magonjwa, kisha huyo mtu wa MUNGU akaniangalia na kuniambia kwamba kazi yangu ya utumishi ni njema ila kuna mtu(Mwanamke)  anapanga kuiharibu huduma yangu  akamtaja jina mtu huyo na ndoto ikaishia pale pale. Baada tu ya mtu yule aliye Congo kuniambia ndoto ile hata siku mbili hazikuisha  yule mwanamke akanitafuta kwa simu mara nyingi sana kiasi kwamba hadi nikashtuka maana sijawahi kuongea nae kwa simu, na alipojitambulisha jina aliongea mambo ya ajabu sana kiasi kwamba nilijua yule ni wakala wa shetani, na  kitendo cha kutaja jina lake na ndilo jina la ndotoni nilijiepusha nae hata kama alijifanya akihitaji sana msaada wa kiroho ila katika baadhi ya maneno alionekana haitaji msaada wa kiroho ila anataka tu kuonana na mimi ana kwa ana, yuko mkoa wa mbali sana na hapa Dar es salaam nilipo ila alitaka sana kuonana na mimi ana kwa ana, alisema yuko tayari kusafiri ili tu aonane na mimi ana kwa ana.
Nilimshukuru MUNGU kwa kuniepusha na hatari hiyo.

Jambo lingine ni kwamba siku moja nilikuwa naomba na ghafla nikaona maono nikiwaona Malaika 7 kila Malaika akija kwangu na kunishika kichwani kama ananiombea, akimaliza Malaika mwingine anakuja  hadi Malaika wote saba. Najua nini kiliongezeka katika utumishi wangu kwa KRISTO ndio maana hilo ni jambo la kumshukuru sana MUNGU aliyeziumba mbingu na nchi.

Siku moja asubuhi nilikuwa sehemu nakunywa chai na andazi. Nilipoanza kula andazi la kwanza tu nikashangaa andazi lile limekwamba kifuani sehemu ya kupitishia hewa.
Lilikuwa andazi laini tu na dogo lakini kifuani likawa kubwa na gumu sana sana.
Hali ikawa sio nzuri na niliomba na mke wangu akaniombea lakini hali ile haikuondoka, ilikuwa ni hatari sana. Ilipofika kesho yake nikaenda Hospitali ili kuona kipande hicho cha andazi kigumu kinatokaje kwenye njia ya hewa?
Kwanza daktari alinishangaa akisema ''Ni ajabu uko hai maana chakula kikizipa sehemu ya hewa hawezi mtu huyo kumaliza hata dakika 5 akiwa hai''  
Nilikosa msaada huko Hospitalini hivyo nikaamua kuingia kwenye maombi ya siku tatu, cha ajabu siku ya kwanza tu ya maombi ya kufunga kile kipande cha andazi kiliyeyuka hata nikapona muda ule ule.
Jambo la ajabu ni kwamba ijumaa ya wiko hiyo nilitoa ushuhuda kwenye ibada ya mkesha na watu 3 kila mmoja akasema kwamba aliona kwenye maono na ndoto wiki moja kabla juu ya hatari iliyokuwa inanikabili ila walisahau kunijulisha.
Nilijisikia vibaya kwa ajili ya wateule hao maana MUNGU anaweza kukupa ujumbe kwa ndoto au kwa maono ukichelewa kuupeleka sehemu husika kama ni agizo  la rohoni uupeleke hakika madhara uliyoyaona yanaweza kutokea.
Nilimshukuru MUNGU sana kwa kuniponya na hatari hiyo ambayo chanzo chake ni somo moja la maombi ya kuharibu nguvu za giza ambapo kuna wakuu wa giza walipanga nife kupitia chakula lakini MUNGU wa miujiza akaniokoa kiajabu sana.
Mimi hakika namshukuru MUNGU sana sana na nitamshukuru pia MUNGU kwa sadaka nzuri kama ambavyo kila mwisho wa mwaka  na mwanzo wa mwaka huwa nafanya hivyo.
Ninayo mengi sana ya kusema ila kwa leo ngoja niishie hapo.
Somo hili litanaendelea  maana leo ilikuwa utangulizi tu na kuweka msingi.

Wafilipi 4:6 '' Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.  ''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
By Mwl Peter  Mabula.
+255714252292(Whatsap, sadaka ya kuipeleka injili Mbele, Maombezi na Ushauri )
MUNGU akubariki sana kwa kusoma somo hili.

.

Comments