![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu katika sehemu ya pili ya somo hili linalosema JINSI YA KUWASHINDA MAWAKALA WA SHETANI WALIOKUSUDIA JAMBO KWAKO MWAKA HUU, Kipengele cha leo ni kuharibu ratiba za kishetani zidi yako.
◼️Mimi naamini wewe binafsi katika KRISTO YESU umepanga mambo kadhaa au malengo unayopanga yatokee mwaka huu, umefanya vyema ila usisahau kuharibu ratiba ya kishetani kama imepangwa kuhusu wewe mwaka huu.
✓✓Jana nilikupa andiko la Zaburi 102:20 likionyesha kwamba mawakala wa shetani wanaweza kumpangia mtu uharibifu ila leo ngoja nizungumzie ratiba za kishetani na jinsi ya kuziharibu ili zisitokee kwako mwaka huu.
◾Ratiba za kishetani ni nini?
✓✓Ratiba za kishetani ni mpango wa mambo mfululizo yaliyopangwa na mawakala wa shetani ili yafanyike kulingana na jinsi walivyopanga wao kwenye ulimwengu wa roho wa giza.
Ngoja tuone mfano hai huu.
Esta 3:12-13 " Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza; na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza vyote, kwa maakida wa mfalme, na maliwali waliokuwa juu ya kila jimbo, na wakuu wa kila taifa; kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jinsi la mfalme Ahasuero, na kutiwa muhuri kwa pete yake. Barua zikapelekwa kwa mikono ya matarishi mpaka majimbo yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyachukua mali yao kuwa nyara."
✓✓Ukisoma hii Esta sura ya tatu kuanzia mstari wa kwanza unaona kwamba wakala wa shetani aitwaye Hamani alipandishwa cheo na raisi wa nchi, baada ya kupandishwa cheo na Mfalme aliona huo ndio muda wa kutimiza ajenda yake ya kuwaua Waisraeli wote katika nchi ile, kwanza akajipendekeza kwa mfalme ili kumnasa mfalme, yaani ili mfalme akubaliane na kila maamuzi ya Hamani.
Alifanikiwa kujipendekeza kipepo kwa mfalme hadi mfalme akajikuta amempa kibali cha ajabu sana, kibali cha kukabidhiwa watu ili afanye chochote anachotaka.
Baada ya mambo yote kukaa sawa ndipo alifanya ujanja mwingine na ikaandikwa barua ya kifalme kwenda wilaya zote, mataifa na mikoa yote ikiagiza kwamba Watu wa MUNGU wote wauawe, hiyo ndio ratiba ya kishetani ilivyopangwa.
✓✓Ashukuriwe MUNGU maana watu wa MUNGU wote waliingia kwenye maombi ya kufunga ya siku 3 na ratiba ile ya kishetani dhidi yao ikamwangamiza aliyeitengeneza.
Lakini wana wa Israeli waliingia katika mwaka huo kwa furaha kama uliyokuwa nayo wewe ila mwezi huo huo wa kwanza wa mwaka tarehe 13 ndipo ratiba mbaya kwao iliandaliwa na ilitiwa saini na mkuu wa nchi na ratiba hiyo kama maandiko yanavyosema hapo juu ilionyesha kwamba mwezi wa kumi na mbili tarehe 13 watu wa MUNGU wote wauawe.
Biblia inasema "Barua zikapelekwa kwa mikono ya matarishi mpaka majimbo yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyachukua mali yao kuwa nyara.-Esta 3:13"
◾Yaani ratiba ya kipepo ilipangwa ya mwaka mzima ilipanga January 13 mwaka huo huo ili itimizwe December 13 mwaka huo huo.
◾Ilikuwa ratiba ya kuwaua watu wa MUNGU na kuwaibia Mali zao zote.
Sasa inawezekana kabisa kuna mwisraeli mmoja alikuwa amepanga mwaka huo atafunga ndoa, mwingine mwaka huo atanunua kiwanja n.k lakini hawakujua kwamba mawakala wa shetani wamepanga kifo juu yao, ni hatari sana.
Inawezekana kuna mtu alipanga mwaka huo angeongeza biashara au angepanua biashara yake lakini kumbe kuzimu imepanga kuibiwa, roho za mauti na uharibifu.
Ratiba kama hiyo unaweza hata kupangiwa wewe mwaka huu.
Umepanga kufunga ndoa, wachawi ratiba yao juu yako inasema mwaka huu uachwe na mchumba.
Umepanga mwaka huu upate kazi au upate mtoto kwenye ndoa yako na kumbe kuna ratiba ya majini kwako ili usifanikiwe kamwe, na kama huombi na kutembea kwenye kusudi la MUNGU ujue ratiba ya kipepo inaweza kutimia kwako.
◼️Kama ipo ratiba ya wachawi, wanadamu wabaya, majini na mizimu juu yako mwaka huu hakikisha kwa kutumia jina la YESU KRISTO, damu ya YESU KRISTO na Neno la MUNGU la ufunuo kama hili unaomba na kufuta ratiba hizo za kipepo, unaweza pia hata kuambatanisha maombi yako na sadaka, yaani kumtolea MUNGU sadaka ya agano(Zaburi 50:5) ili kutia muhuri maombi yako kwamba ratiba ya kishetani ya kila namna haifanikiwi kwako mwaka huu.
Mtu mmoja alimwendea mtu mwingine kwa mganga ili kumharibia katika mambo Fulani ambayo sitayataja sana. Mganga alichofanya ni kuita jini(joka) lake na kulipa damu ya mnyama aliyetoa huyo aliyeenda kwa mganga, baada ya joka(jini) kushiba damu lilielekezwa kwa mtu husikwa aliyekusudiwa ili mambo yake yaharibike. Yule mtu ndoa yake, afya yake, biashara yake, kazi na n.k vilianza kuharibiwa na joka lile ambalo likitumwa na mganga baada ya adui yake kumpeleka huko.
Mtu huyu akaanza kuota akiona joka lile, akapambana kimaombi muda mrefu sana mwaka ule, wakati mwingine akiomba sana na kuombewa lile joka linaondoka lakini baada ya siku linarudi.
◼️Ndugu, kama na kwako iko hivyo, leo kwa damu ya YESU KRISTO futa kafara zote zilizotolewa kwa waganga kwa ajili yako, achilia mapigo hadi kwa aliyetuma na aliyeshirikiana na alituma.
Ziko ratiba nyingi za kipepo za wanadamu au za kuzimu au za mawakala wa shetani wengine, usiogope Bali mwaka huu futa ratiba hizi za kipepo.
◼️Mwite Bwana YESU KRISTO ili akushindie maana yeye hufuta mipango ya wabaya wako kama ukimwita.
Ayubu 5:12 "Yeye(MUNGU) huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao."
✓✓Ni kweli wanaweza kupanga ratiba ya magonjwa, ajali, mikosi,balaa, kuteseka, kufilisika, ndoa kufa n.k lakini wewe simama katika nafasi yako kama muombaji na utashinda na ratiba hiyo ya kipepo kwako mwaka huu haitafanya kazi.
Nini ufanye?
1. Chana kwa damu ya YESU KRISTO hiyo ratiba ya kipepo zidi yako au familia yako mwaka huu.
Kumbuka kwa damu ya YESU KRISTO utashinda shetani na walio upande wake wote(Ufunuo 12:11)
2. Futa kila kumbukumbu kuhusu wewe iliyo katika wa roho wa giza.
✓✓Kumbuka utakusudia jambo lolote katika MUNGU nalo litadhibitika(Ayubu 22:28) leo kimaombi kusudia kufuta ratiba za kipepo na kimaombi zifute na zitafutika zote.
3. Mpige kwa moto wa jina YESU KRISTO kila mpanga ratiba wa kipepo aliyepanga chochote kwa ajili yako mwaka huu.
Tumia Zaburi 2:9
4. Mtegemee MUNGU kukulinda na omba akulinde.
Isaya 26:3
✓✓Omba ndugu na ratiba za kishetani zote hazitafanya kazi kwako.
✓✓Omba na utamuona MUNGU aliyeziumba mbingu na nchi.
Zingatia na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments