HERI YA MWAKA MPYA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Heri ya mwaka mpya rafiki yangu mpendwa.

Bwana YESU KRISTO asifiwe sana.
Namshukuru MUNGU amekulinda na kukupa kibali cha kuishi mwaka huu mpya, hata Mimi nimepata neema hiyo na ninamshukuru MUNGU sana.

Ngoja niseme machache juu ya mwaka mpya uliouingia.

Mwaka ni nini?

◾Mwaka ni kipindi cha miezi kumi na miwili.
Kipindi hiki ulichopewa na MUNGU kina sababu yaani umepewa tu kwa kusudi la MUNGU.

✓✓Kama kusudi la MUNGU la duniani kwako lingekuwa limeisha basi usingekuwa hai Leo.

Waefeso 1:11" na ndani yake(YESU) sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na KUSUDI lake yeye(MUNGU), ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake."

Kusudi la MUNGU ni nini?

◼️Kusudi la MUNGU ni kitu cha ki MUNGU kinachosababisha kitu kingine cha ki MUNGU kitokee.

✓✓Kwa mtu binafsi "Kusudi la MUNGU" ni nafasi yenye sababu unayopewa na MUNGU.

Nafasi hiyo imebeba sababu hivyo ni vyema kuomba kwa MUNGU ili uzijue baadhi ya sababu zilizosababisha wewe upewe nafasi ya kuishi.

Warumi 8:28 "Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote MUNGU hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake."

✓✓Zipo sababu nyingi zinazoweza kubeba kusudi la MUNGU lililopelekea wewe uwe hai Leo.

✓✓Sababu zangu za kuishi mwaka huu zinaweza kuwa tofauti kidogo na sababu zako za kuishi mwaka huu kulingana na kusudi la MUNGU.

Baadhi ya sababu zilizobeba kusudi ni hizi.

1. Kuna watu wamepewa nafasi na MUNGU ya kuishi mwaka huu ili waokoke na kuanza kumtumikia Bwana YESU.

Waebrania 3:7-8 " Kwa hiyo, kama anenavyo ROHO MTAKATIFU, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu ......"

2 Wakorintho 6:2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)

◼️Wakati wa Wokovu/Kuokoka/Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi ndio sasa, kuna watu wanasubiriwa kwa ajili ya hilo, wamepewa nafasi ya kuishi mwaka huu ili waokoke, ndugu kama ni wewe hujaokoka kimbilia haraka kusudi hili la MUNGU kwako watu wote ambao bado hawajaokoka.

2. Kuna watu ni watumishi wazuri wa MUNGU katika KRISTO YESU na wamepewe kuishi mwaka huu ili waendelee kumtumikia zaidi Bwana YESU na kuleta matunda mema mengi kwa MUNGU.

1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

✓✓Watu hawa wanasubiriwa kuzaa matunda, yaani utumishi wao kwa KRISTO umletee faida MUNGU.

Mathayo 13:23 "Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini."

✓✓Inawezekana ni wewe umepewa nafasi hiyo mwaka huu, ndugu tembea kwenye kusudi hilo la MUNGU.

3. Kuna watu wamepewa nafasi ya kuishi ili waitengeneze boma.

Ezekieli 22:30 "Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu."

✓✓Kuitengeneza boma kunahusisha mambo mengi baadhi ni haya yaani wazifanye familia zao kuokoka, kuwafanya ndugu au ukoo kuachana na kufuata uganga, kuacha kuroga, kuacha kuabudu sanamu n.huko ndio kutengeneza boma.

4. Kuna watu wamepewa nafasi ya kuishi mwaka huu ili waendelee kupanda zaidi katika ufalme wa MUNGU maana watavuna kwa ukarimu.

Wagalatia 6:7 "Msidanganyike, MUNGU hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna."

5. Kuna watu wamepewa nafasi ya kuishi mwaka huu ili waendelee na maombi na maombezi.

Isaya 62:6 "Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya;"

6. Kuna watu wamepewa nafasi ya kuishi mwaka huu ili waache mabaya na waanza kutenda mema kama kusudi la MUNGU linavyotaka.

Zaburi 34:14 "Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie."

7. Kuna watu wamepewa nafasi na MUNGU ya kuishi mwaka huu wapokee walichowekeza kwa MUNGU zamani.

Wagalatia 6:9 "Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho."

Kuna sababu hata zaidi ya 100 za MUNGU kukufanya uishi mwaka huu.

✓✓Ndugu tafuta kujua ni nini kimemfanya MUNGU kukupa mwaka huu uishi.

✓✓Kuna watu wamepewa nafasi kuishi kumbe ni ili watengeneze na MUNGU maana muda wao wa kuishi duaniani umeisha, yaani wamepewa ofa na MUNGU ili tu wajitambue na kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi ili wasiende jenahamu.

Mwaka fulani kuna Baba mmoja alikuwa anaumwa, nikasikia sauti rohoni kwamba muda wa kuishi kwa mwanaume yule ulikuwa umefika mwisho, sikumwambia ila nikamwambia kwamba anatakiwa kumpokea YESU KRISTO na kutubu dhambi zake zote, nilipomwongoza sala ya toba alikataa ila nikamsihi mtoto wake akaite wachungaji na walipokuja waliongea naye na kumuongoza sala ya toba, siku hiyo hiyo akafariki.

Ndugu usiende kinyume  na kusudi la MUNGU juu yako juu ya mwaka.

Ukipishana na kusudi la MUNGU ni hatari sana kwako.

Jambo la kujua tu ni kwamba kusudi la MUNGU halihusiki na dhambi wala upinga Kristo.

Ukiona mtu anampinga YESU huyo yuko kutimiza kusudi la shetani na sio la MUNGU.

Ukiona mtu anatenda dhambi yeyote au machukizo ujue huyo analitimiza kusudi la shetani na sio la MUNGU.

◼️Ukilifanyia kazi kusudi la MUNGU utaitwa heri, utafanikiwa na kubarikiwa.

◼️Hakikisha tu mipango yako ya kutafuta Mali haizuii kusudi la MUNGU na wewe kuishi mwaka huu.

Kuna watu sana mipango mingi sana mwaka huu lakini mipango yao karibia yote iko kinyume na kusudi la MUNGU, ni mbaya sana.

◼️Ndugu hakikisha unatembea kwenye kusudi la MUNGU.

◼️Wakati mwingine kusudi unaweza kulijua kwa msukumo ambao ROHO MTAKATIFU anakupa ndani yako.
Kuna watu wanamsukumo wa kujenga Kanisa, kuna watu wanamsukumo wa kushuhudia injili mitaani mwaka huu, kuna watu wanamsukumo rohoni wa kuombea nchi au watumishi.

Iko misukumo mingi rohoni inayoweza kuwa njia mijawapo ya kukujulisha kusudi la MUNGU kwako ambalo ni kusudi hilo ndilo lilisababisha MUNGU akakupa nafasi ya kuishi mwaka huu.

Ngoja nikupe baadhi ya maangalizo.

1. Dhambi yeyote haihusiki na kusudi la MUNGU, hivyo usifanye dhambi mwaka huu maana dhambi zote sio mipango wa MUNGU.

1 Yohana 3:8 "atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. "

2. Kuipenda dunia na machukizo ya duniani haiko katika kusudi la MUNGU.

✓✓Hivyo epuka kuipenda dunia na machukizo yake.

1 Yohana 2:15 "Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake."

3. Kutokuleta matunda kwa KRISTO sio kusudi la MUNGU.

Mathayo 7:17-19 " Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni."

Hakikisha unaleta matunda mengi kwa MUNGU katika KRISTO YESU.

Nakutakia mwaka mpya wa baraka na ushindi ila tambua kwamba unaishi kwa kusudi la MUNGU hivyo hakikisha unaliishi kusudi hilo la MUNGU.
Inawezekana wewe umepewa kuishi mwaka huu ili utimize makusudi 7 ya MUNGU, ndugu timiza kila kusudi la MUNGU lililomfanya MUNGU kukupa kuishi mwaka huu.
Nitakuletea masomo mbalimbali ya kusudi la MUNGU kwako mwaka huu.
Bwana YESU KRISTO akubariki sana sana.
Heri ya mwaka mpya.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU.

Comments