KANISA LINAJENGWA NA HUDUMA TANO NA SIO MOJA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu.
Karibu nikujuze kitu katika somo hili kuhusu huduma 5 za ROHO MTAKATIFU ndani ya Kanisa la KRISTO duniani.

◼️Kanisa halijengwi na huduma moja au mbili, Kanisa limajengwa na huduma tano.

Waefeso 4:11-15 " Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa KRISTO ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa KRISTO; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, KRISTO."

✓✓Huduma hizi 5 za ROHO MTAKATIFU ndani ya Kanisa ni kwa ajili ya kuwakamilisha watakatifu, ili kuukuza mwili wa KRISTO na ili kuwafanya watu wasiwe wachanga kiroho, na ili  kuwafanywa watu wasiufuate upinga Kristo.

Ngoja nianze hivi;.
✓✓Ukiona kuna mtume ila yuko kinyume na KRISTO YESU, ujue huyo sio mtume aliyetumwa na MUNGU.

✓✓Ukiona kuna nabii yuko kinyume na KRISTO YESU, ujue huyo sio nabii wa MUNGU bali ni wa shetani.

✓✓Na manabii wengi wa uongo ni nadra sana kumtaja YESU KRISTO Mwokozi kwenye mahubiri yao, wengi wanajihubiri wao na kujitaja wao tu.

✓✓Ukiona mwinjilisti yuko kinyume na KRISTO YESU ujue huyo huyo hahubiri injili ya YESU KRISTO inayookoa.

✓✓Ukiona Mchungaji yuko kinyume na Bwana YESU ujue Mchungaji huyo sio Mtumishi wa MUNGU bali ni mpambe wa shetani.

✓✓Ukiona mwalimu yuko kinyume na Bwana YESU ujue huyo sio Mwalimu wa Neno la MUNGU la kuwapeleka watu uzima wa milele.

◼️Japokuwa sio wote ambao ni  mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji au walimu ni watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi, lakini watumishi wa kweli wa Bwana YESU KRISTO nao wapo na ni wengi.

◼️Sasa nimesema kwamba Kanisa halijengwi na huduma moja kwa sababu MUNGU alitoa huduma tano kwa Kanisa na sio huduma moja.

✓✓MUNGU ameachilia huduma 5 na zote MUNGU anataka ziwemo ndani ya Kanisa.

◼️Ngoja nikuambie kwanini huduma zote 5 ni za muhimu katika Kanisa la KRISTO duniani?

1. Utume lazima uwepo katika Kanisa.

◼️Utume hupeleka Injili ya KRISTO mbele, kuna ambako ilikuwa haijafika.

✓✓Maana ya neno "Mtume'' maana yake alitetumwa.

Yohana 13:16" Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka."

◼️Utume hulifanya Kanisa kufungua matawi mbalimbali sehemu mbalimbali.

◼️Mitume ni wapeleka injitli mbele hata kule ambako Injili haijawahi kufika.

✓✓Utume unalifanya Kanisa likue sana.

◼️Kanisa la KRISTO duniani linahitaji sana huduma ya utume ili likue.

2. Unabii lazima uwepo katika Kanisa la KRISTO duniani.

✓✓Neno Nabii lina maana ya msemaji wa mwingine, mjumbe wa MUNGU, mwonaji.

2 Petro 1:21 "Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa MUNGU, wakiongozwa na ROHO MTAKATIFU."

◼️Unabii unakemea dhambi, unalionya Kanisa.

◼️Unabii unajulisha yaliyopo na yajayo.

✓✓Kanisa linahitaji sana maonyo na kutahadhalishwa juu ya madhara ya kwenda kinyume na KRISTO YESU.

◼️Unabii lazima sana uwepo katika Kanisa.

3. Uinjilisti lazima uwepo katika Kanisa la KRISTO duniani.

✓✓Uinjilisti ni kitendo cha kuwaleta watu kwa YESU ili waokolewena YESU KRISTO.

◼️Maana nyingine ya uinjilisti ni uvuvi wa watu.

✓✓Maana ya Neno "Mwinjilisti" ni mpeleka injili ya KRISTO.

✓✓Unawavua watu ili watoke kwa shetani na waje kwa MUNGU.

◼️Mwinjilisti ni mtu yule anayeeneza habari njema za Wokovu wa YESU KRISTO kwa wanadamu.

Wafilipi 1:5-6 "kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya KRISTO YESU;"

✓✓Uinjilisti hupeleka injili ya KRISTO YESU mbele Sana.

◼️Ili Kanisa likue linahitaji sana huduma ya uinjilisti.

✓✓Huduma ya uinjilishi hairidhiki na waumini 20 tu au waumini 100 tu au waumini 1000 tu bali uinjilisti unataka sana watu wengi zaidi waokolewe.

◼️Huduma ya uinjilisti ni ya muhimu sana Kanisani na inahitajika sana katika Kanisa la MUNGU duniani.

4. Uchungaji lazima uwepo katika Kanisa la KRISTO duniani.

✓✓Kazi ya ya uchungaji ni kuchunga na kulisha kondoo.

Yohana 21:15-26 " Basi walipokwisha kula, YESU akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia , Naam ,Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, LISHA WANA-KONDOOWANGU. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, CHUNGA KONDOO ZANGU."

✓✓Kuna uchungaji wa aina mbili, kuna uchungaji wa cheo cha Kikanisa na kuna uchungaji wa kihuduma.

✓✓Hivyo wapo Wachungaji wanaongoza makanisa ila hawana huduma ya uchungaji maana uchungaji wa cheo na uchungaji wa huduma ni mambo mawili tofauti Kabisa.

✓✓ Ndio maana kuna wainjilisti kihuduma ila wanaongoza makanisa katika vyeo vya uchungaji, kuna manabii kihuduma ila kwa cheo cha dhehebu wamepewa cheo kuwa Mchungaji au Askofu.

◼️Kwa hiyo ninapozungumzia huduma ya kichungaji inahitajika sana katika Kanisa la KRISTO duniani Nina maana ya uchungaji wa huduma ya kupewa na ROHO MTAKATIFU na sio uchungaji wa cheo cha kupewa.

✓✓Kuna watu wana huduma ya uchungaji ndani yao ila wao sio wachungaji wanaongoza makanisa.

✓✓Kwa hiyo uchungaji wa huduma sio cheo ila huduma.

◼️Kanisa linatakiwa kuchungwa kama kundi la kondoo, na wachungaji wa kondoo hizo ni hao walio na huduma ya uchungaji.

◼️Wenye huduma ya uchungaji ndani yao hawawezi kukubali kondoo hata mmoja abaki porini na sio kuja zizini.

✓✓Mchungaji hulisha kondoo, husaidia kondoo kiroho kwa ukaribu sana.

✓✓Mchungaji hutunza kondoo, ni moja ya huduma muhimu sana katika Kanisa la KRISTO duniani.

◼️Ni huduma ambayo kama hukuitwa katika huduma hiyo kukimbia huduma au kuharibu huduma ni rahisi sana maana huduma hii inahitaji akili, hekima, upole unapohitajika, ukali unapohitaji na ulezi.

✓✓Kwenye ulezi ndio mtihani mgumu kidogo ndio maana ni wenye huduma ya uchungaji tu ndani yao ndio wanaweza kufanya kazi hiyo vyema.

✓✓Wenye huduma zingine wakati mwingine sio lazima sana wawe karibu na kondoo lakini Mchungaji lazima awe karibu sana na kondoo.

✓✓Hongera sana kwa wenye huduma ya uchungaji ndani yao na wanaifanyia kazi huduma yao waliyopewa na ROHO MTAKATIFU, kazi yenu sio bure katika MUNGU.

5. Ualimu lazima uwepo katika Kanisa la KRISTO duniani.

Mathayo 28:19-20 " Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;
 NA KUWAFUNDISHA kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari."

✓✓Kazi ya Mwalimu ni kufundisha.

Hata Mimi namshukuru sana MUNGU maana mimi binafsi kama Peter Mabula ualimu ndio huduma yangu maana ni ROHO MTAKATIFU aliniambia kwa sauti tarehe 20 April ya mwaka 2017.

✓✓Ualimu hutoa maarifa sahihi ya Neno la MUNGU.

✓✓Kama unahitaji sana kulielewa vyema Neno la MUNGU unamhitaji Mwalimu.

✓✓Ualimu hujulisha hasa Biblia inataka Nini  ufanye.

✓✓Ualimu hufungua watu ufahamu ili waelewe vyema Biblia inavyosema.

✓✓Ndio Maana ni rahisi kumuona Mwalimu anayefundisha akitumia maandiko hata 15 wakati akifundisha harafu Mwinjilisti akifundisha somo kama hilo hilo akatumia andiko moja tu.

✓✓Kwanini mwalimu anatumia maandiko mengi inapobidi wakati akifundisha?

◼️Ni kwa sababu Mwalimu hutaka Biblia ikujibu wewe kila unachohitaji, ni kwa sababu Mwalimu hufundisha huku akijibu maswali ambayo watu wengi wanayo na hawakuwa wamepata majibu.

◼️Ualimu husimamia misingi ya Biblia kwenye kila eneo kwa kusudi la MUNGU.

✓✓Kwa sababu kazi ya Mwalimu ni kufundisha na sio kuhubiri basi ndio maana mwalimu hufundisha akitamani anaowafundisha wanaelewa Neno la MUNGU hivyo anaweza hata kufundisha kwa vituo au kwa points ili hata iwe rahisi mtu kujua na kuelewa na kukariri.

◼️Huduma ya ualimu inahitajika sana katika Kanisa la MUNGU duniani.

◼️Huduma hizo 5 za ROHO MTAKATIFU ndani ya Kanisa ni za muhimu sana na zinahitajika zote Kanisani.

1 Wakorintho 12:28 "Na MUNGU ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha."

✓✓Changamoto tu watu wanakimbilia huduma ambazo hawakuitwa na kuzivuruga huduma hizo.

Wachungaji au wainjilisti wengi kihuduma hukimbilia huduma za kinabii ambazo wala hawakuitwa huko, huko ndiko kuvuruga huduma na Kanisa la KRISTO duniani.

◼️Kama kila aliyeitwa katika huduma fulani kiroho atatumika katika huduma yake, basi mwili wa KRISTO ungejengwa vyema.

◼️Mwili wa KRISTO ni jumuiko la waenda mbinguni wote ambao wameokolewa na YESU KRISTO duniani na wanaishi maisha matakatifu.

✓✓Unaitwa mwili wa KRISTO kwa sababu katika mwili huu wako watu kutoka madhehebu mengi na wa huduma mbalimbali.

Ushauri wangu.

1. Kaa kwenye huduma aliyokuitia YESU KRISTO.

1 Wakorintho 7:24 "Ndugu zangu, kila mtu na akae mbele za MUNGU katika hali iyo hiyo aliyoitwa nayo."

2. Ishi maisha matakatifu huku ukimtumikia Bwana YESU KRISTO.

1 Petro 1:15 "bali kama yeye(YESU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

3. Hakikisha unafanya kazi ya MUNGU huku ukiwa pamoja na MUNGU.

Warumi 8:28 " Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote MUNGU hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake."

4. Usikubali kuwa Mtumishi wa uongo.
1 Yohana 4:1 "............... kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani."

Ufunuo 2:2 " .......... tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo;"

5. Mhubiri YESU KRISTO tu anayeokoa na sio kuhubiri dini, au dhehebu, au kujihubiri wewe.

2 Wakorintho 4:5 "Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali KRISTO YESU ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya YESU."

6. Katika utumishi wako usijitukuze wewe au usitafute kutukuzwa na watu bali wewe mtukuze MUNGU.

Isaya 42:8 "Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu."

7. Usidharau huduma za wengine maana kwa MUNGU hakuna huduma kubwa na ndogo.

Luka 14:11 "Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa."

Kujidhili ni nini?

✓✓Kujidhili ni hali ya kunyenyekea na kujishusha.

✓✓Kinyume ya kujidhili ni kujikweza.

Kujikweza ni nini?

✓✓Kujikweza ni hali ya kujiinua au kujipandisha juu na kujiona wewe ni bora kuliko wengine.
Kwa mujibu wa Neno la MUNGU ukijiinua utashushwa, ukiwadharau wengine kwa sababu huduma yako unaiona ni bora kuliko wengine ujue utaishia kushushwa.
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana 

Comments