CV YA BWANA YESU KRISTO ILIYOSOMWA NA MALAIKA.



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.

◼️Je unaijua CV ya Bwana YESU KRISTO?

Ngoja nianze na maana ya CV.
CV ni Neno ambalo watu Duniani hutumia kuelezea wasifu wao.
CV ni kifupi Cha neno la kiingeleza "curriculum vitae" likiwa na maana ya wasifu wa kazi wa Mtu likiwa limebeba historia ya Mtu, uzoefu, Elimu,ujuzi n.k

Ndio maana Mtu akiomba kazi utasikia "Hebu lete CV yake tuone kama anatufaa katika kazi "
Sasa Mimi Wala siko huko kwenye CV za watu Bali namzungumzia Bwana YESU KRISTO Mwenye CV kubwa na kuu kuliko watu wote waliowahi kuishi Duniani.

✓✓Tangu zamani sana kabla hajaja duniani Bwana YESU tangazo la ujio wake lilitangazwa na Mbingu kwamba siku moja atakuja duniani, ni tukio muhimu sana.

Isaya aliyeishi miaka 700 kabla ya Bwana YESU hajaja rasmi duniani kwa ajili ya makusudu maalumu ya MUNGU, alisema maneno haya.
'' Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli. -Isaya 7:14.''

✓✓Na ishara hiyo ya MUNGU ilikuja kutimizwa kwa njia nyingi tu, njia mojawapo ni Kuzaliwa kwa Yohana mbatizaji, na tangazo la Malaika la kujulisha juu ya YESU ni nani na alikuja kufanya nini duniani.

Mimi  binafsi nimewahi kuishi katika jamii ya watu ambao asilimia zaidi ya 95 sio Wakristo, sasa watu hao maneno yao kumhusu YESU muda wote ninapokutana nao ni maneno ya kumfanya YESU kuwa Mwanadamu na kumfanya YESU kuwa chini ya baadhi ya Wanadamu ambao wao wanaamini Wanadamu hao ndio bora zaidi, lakini ashukuriwe MUNGU maana siku moja niliposoma CV ya YESU KRISTO iliyoletwa na Malaika nilijua ukweli na hakika nina ujasiri siku zote za Maisha yangu kujiamini na kujikubali kwa sababu tu YESU KRISTO ndio Mwokozi wa maisha yangu.

✓✓Ndugu Mkristo uliyeokolewa na Bwana YESU nakuomba sana jiamini, jikubali na uwe na amani ya milele maana kama uko kwa YESU KRISTO hakika uko mahali salama na mahali sahihi sana.

✓✓YESU KRISTO ni Mkuu sana, ufalme wake ni juu ya falme zote na utawala wake ni utawala ambao hauna mwisho, yaani ufalme wa Bwana YESU ni ufalme ambao hautakuwa na mwisho milele.

Je unataka kuona CV ya Bwana YESU KRISTO kama ilivyosomwa na Malaika?

✔️✔️Ni hii hapa ''Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa MUNGU. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita YESU. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na BWANA Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. -Luka 1:30-33''

◼️Hakuna Duniani mwenye CV kama ya Bwana YESU KRISTO.

◼️Kwanza jina lake halikutoka duniani bali lilitoka mbinguni na anayetangaza jina lake ni Malaika.

◼️Ni jina hili YESU KRISTO ndilo jina lipitalo kila jina, ni jina hili pekee ambalo hakuna nguvu ya giza haiwezi kuliogopa.

◼️Neno lenyewe ''YESU' maana yake ''Mwenye kuokoa'' Hivyo kusema YESU KRISTO ni sawa na kusema ''Mfalme wa mbinguni anayeokoa''

◼️Malaika tena anatutangazia wanadamu kwamba YESU KRISTO ni mkuu, yaani hakuna mkuu mwingine duniani kuliko YESU KRISTO na hatatokea mkuu mwingine kuzidi YESU KRISTO.

◼️Malaika hakuishia hapo tu kutoa CV ya Bwana YESU bali alisema kwamba Bwana YESU jina lake lingine ataitwa Mwana wa MUNGU, hivyo wanaopinga kwamba YESU sio mwana wa MUNGU wanakuwa hawajui na hawajui kwanini hawajui.

◼️Sio hayo tu bali Malaika pia alitangaza kwamba kiti cha enzi kilichoahidiwa katika Daudi kitakuwa chake, na ni Bwana YESU atawamiliki wateule wake milele yaani watakuwa uzima wa milele milele yote waliompokea kama Mwokozi na wanaishi maisha matakatifu katika yeye.

◼️Na tena Malaika akamalizia kwa kusema kwamba Bwana Ufalme wa Bwana YESU ni wa milele yaani hauna mwisho.

✓✓Niliposoma maandiko hayo nilipata ujasiri sana maana hajawahi kutokea duniani ambaye ufalme wake ni wa milele ila ni Bwana YESU KRISTO tu.

◼️ Ukiwa kwa YESU hakika uko sehemu salama, rudia kusoma katika ROHO juu ya CV hiyo kumhusu Bwana YESU hakika hutamkana YESU milele maana ni yeye tu wa kweli na wa haki.

✓✓Ingawa huo ndio ukweli wa milele ni vyema sasa tukajifunza pia kwanini Bwana YESU aliacha enzi yake na kuja duniani?

◼️Je unafahamu kwanini Bwana YESU alikuja duniani?

Kuna sababu nyingi ila baadhi ya sababu za kwanini Bwana YESU alikuja duniani ni hizi;

1. Bwana YESU alikuja duniani ili watakaotubu kwa MUNGU katika yeye wasamehewe dhambi zao.

1 Yohana 1:9 '' Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.''

✓✓Unapotubu kwa MUNGU katika KRISTO na wewe kuokoka hakika ROHO MTAKATIFU atakuja kwako na utafanyika mwana wa MUNGU kuanzia hapo.

◼️Ni ahadi ambazo MUNGU alizisema tangu zamani za kusamehe dhambi za watakaotubu, na sasa MUNGU anatimiza katika KRISTO YESU Mwokozi.

Isaya 43:25 ''Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.''

2. Bwana YESU alikuja ili tutakaomtii tuupate uzima wa milele.

Yohana 3:16-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

◼️Kazi yetu ni kumpokea Bwana YESU KRISTO kama Mwokozi na kuendelea kuishi maisha matakatifu ya Wokovu, na uzuri ni kwamba Bwana YESU kwa sasa anatuandalia Makao Mbinguni, siku moja atakuja na kutupeleka uzima wa milele.

Yohana 14:1-3 '' Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini MUNGU, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.''

✓✓Kwa sasa anatuandalia Makao yetu, ni furaha sana kwa kuwa katika KRISTO YESU, ukimtii na kuliishi Neno lake.

3. Bwana YESU alikuja ili MUNGU atuhamishe kutoka ufalme wa giza na sasa tuwe katika ufalme wa YESU KRISTO.

Wakolosai 1:13-15 '' Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa MUNGU asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.''

✓✓Hili ni jukumu mojawapo lililosababisha Bwana YESU aje duniani, ni jukumu lako tu kuhakikisha umehamishwa kutoka nguvu za giza na sasa uwe katika ufalme wa Bwana YESU.

✓✓Kama unahisi bado hujahamishwa kutoka kwa shetani basi unayo nafasi leo ya kimaombi ya kuhamishwa na utahamishwa.

✓✓Kumbuka kazi mojawapo ya Bwana YESU ni kuziharibu nguvu za shetani, hivyo hakikisha Bwana YESU anaziharibu nguvu za giza zinazofuatilia maisha yako, fuata maombezi na jifunze kuomba.

1 Yohana 3:8b '' Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.''

4. Bwana YESU alikuja ili kutuondolea vifungo vyote.

Mathayo 9:35 '' Naye YESU alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.''

✓✓Biblia inatufunulia kwamba Bwana YESU anaponya magonjwa yote na kila aina ya udhaifu.

◼️Kuponya magonjwa na kuondoa vifungo vya giza ni moja ya kazi za Bwana YESU hivyo kama unahisi kuna kifungo kwako ni nafasi yako leo kuomba au kuombewa na vifungo vya giza vitaachia maisha yako.

✓✓Kumbuka Bwana YESU anakungoja tu uokoke na uingie kwake hakika atakuponya.

Mathayo 11:28 ''Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. ''

5. Bwana YESU alikuja ili kutupa madaraka/mamlaka ya kuzishinda nguvu za giza zote.

Luka 10:19 '' Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. ''

◼️Bwana YESU alikuja na akatuachia mamlaka ya kuzishinda nguvu za giza zote.

✓✓Mamlaka ya kuzishinda nguvu za giza ipo ndani ya wateule wa KRISTO tu, hakuna anayeweza kuiga.

✓✓Hata wewe kama umeokoka hakika una madaraka ya kuzishinda nguvu zote za giza.

◼️Hiyo ni neema ya MUNGU ya ajabu sana kwamba Bwana YESU alikuja ili tuwe na mamlaka ya kuzishinga nguvu za giza.

Mathayo 16:19 ''Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. ''
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ushauri, Maombezi, Whatsapp n.k)
Share ujumbe huu kwenye magroup ya Whatsapp uliyopo.
Ubarikiwe

Comments