![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
◼️Leo tunaangalia faida za kumcha MUNGU.
Zaburi 34:11" Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha BWANA."
Kumcha MUNGU ni nini?
◼️Kumcha MUNGU ni kuishi maisha yanayompendeza MUNGU.
◾Maisha yanayompendeza MUNGU ni maisha ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
◾Kwa hiyo tunaweza kusema kwamba kumcha MUNGU ni kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi kisha unaanza kuliishi Neno la MUNGU.
◼️Kumcha MUNGU ni kuambatana na MUNGU Moyoni mwako.
◼️ Kumcha MUNGU ni kuwa na hofu ya MUNGU ndani yako ambayo hukupelekea kumheshimu MUNGU katika KRISTO YESU kwa kiwango cha juu, kumpa nafasi ya kwanza anayostahili, kumtii, kushika maagizo yake yote, kumwabudu katika ROHO MTAKATIFU, kumpa heshima na utukufu na maisha yako kuamua kumtumikia kwa moyo wa upendo.
◼️Kumcha MUNGU ni kuchukia dhambi zote na uovu wote ili uambatane na YESU KRISTO.
◼️ Kumcha MUNGU ni kulishika Neno lake na kuenenda katika njia za kumpendeza.
✓✓Kuna faida kubwa sana katika kumcha MUNGU.
✓✓Tangu zamani watu wa MUNGU wanafundishwa kumcha MUNGU aliyeziumba mbingu na dunia.
2 Wafalme 17:28 "Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha BWANA."
✓✓Hata wewe inakupasa kujifunza kumcha MUNGU Baba wa mbinguni.
✓✓Hata wewe inakupasa kuwafundisha watoto wako na watu wa familia yako jinsi ya kumcha MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Nini kinatengenezwa na mtu kumcha MUNGU katika KRISTO YESU?
1.Kumcha MUNGU hutengeneza hekima safi.
Zaburi 111:10 "Kumcha BWANA ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake zakaa milele."
Hekima ya ki MUNGU ni nini?
✓✓Hekima ya ki MUNGU ni akili inayotokana na uzoefu wa muda mrefu wa kuhusika na mambo ya ki MUNGU.
✓✓Unapokuwa unajifunza Neno la MUNGU kila Mara kwa kuzingatia na kulifuata baada ya muda utakuwa na hekima ya ki MUNGU, hiyo ni faida kubwa sana iliyotengenezwa na wewe kumcha MUNGU katika KRISTO YESU.
Mithali 9:10 "Kumcha BWANA ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu."
2. Kumcha MUNGU huleta maarifa sahihi.
Mithali 1:7 "Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu."
Maarifa ya ki MUNGU ni nini?
✓✓Maarifa ya ki MUNGU ni ujuzi au elimu vinavyotengenezwa na Neno la MUNGU kwa kumcha MUNGU.
✓✓Neno tu "Maarifa" lina maana ya njia inayotumiwa kujitoa katika tatizo au ni njia inayotumiwa ili kupata kitu.
3. Kumcha MUNGU hutengeneza kuchukia dhambi.
Mithali 8:13 "Kumcha BWANA ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia."
✓✓Kipimo cha kwanza cha kumjua mtu anayemcha MUNGU ni mtu huyo kama anachukia dhambi na hazitendi.
✓✓Maana mojawapo ya kumcha MUNGU ni kuchukia dhambi, kama mtu anafanya dhambi wala hachukii dhambi huyo hamchi MUNGU hata kama mtu huyo ni Mtumishi wa MUNGU.
Mithali 16:6 "Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha BWANA watu hujiepusha na maovu."
✓✓Maisha ya kumcha MUNGU ndiyo hutengeneza kuchukia dhambi na maovu.
✓✓Kumcha MUNGU sio maneno tu bali na vitendo pia.
✓✓Wateule wa KRISTO lazima waishi maisha ya kumcha MUNGU, matokeo ya mtu kumcha MUNGU ni mtu huyo kuwa wa kuchukia dhambi na maovu.
2 Wakorintho 7:1 "Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha MUNGU."
4. Kumcha MUNGU huongeza siku za kuishi.
Mithali 10:27 "Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa."
✓✓Hii ni siri ya ajabu sana na faida ya ajabu sana ya kumcha MUNGU kwamba kumcha MUNGU huongeza miaka ya mtu ya kuishi.
Mithali 19:23 'Kumcha BWANA huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya."
✓✓Yaani hesabu ya miaka ya mtu mcha MUNGU hutimia kama alivyopangiwa na MUNGU.
✓✓Mcha MUNGU huwezi kumkuta katika waliokufa kwa sababu walikutwa wanaiba wakapigwa wakafa.
✓✓Mcha MUNGU huwezi kumkuta katika waliofanya uzinzi na uasherati wakapata magonjwa ya zinaa na magonjwa hayo yakawaua kabla ya muda wao.
✓✓Ukiona binti amekufa akijaribu kutoa mimba, huyo hakuwa mcha MUNGU.
✓✓Ukiona mwizi kapigwa hadi kufa, ujue huyo hakuwa mcha MUNGU ndio maana akaiba.
✓✓Kumcha MUNGU kuna faida kubwa sana na moja ya faida hizo ni kwamba kumcha MUNGU huongeza siku za kuishi, maana MUNGU atakulinda kwa sababu unamcha yeye hadi muda wako stahiki ufike.
[✓Kumcha MUNGU huongeza miaka ya kuishi kwa sababu hiyo ni ahadi ya MUNGU mwenyewe kwa wanaomcha yeye katika KRISTO YESU.
◼️Hata katika historia dhambi na maovu ndivyo vilivyosababisha miaka ya mwanadamu kuishi ikapungua.
Kabla ya gharika ya Nuhu watu kuishi miaka mia tisa lilikuwa jambo la kawaida kabisa, lakini dhambi zikasababisha watu kuishi mwisho miaka 120 na sio 900 tena.
Mwanzo 6:3 "BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini."
Wanadamu walipoendelea na dhambi miaka 120 ikawa mingi sana kuishi, ikapunguzwa na kuwa 70 hivyo anayevuka miaka 70 ni kwa neema ya MUNGU ila labda mtu huyo atapata akili na ufahamu hata akampokea YESU KRISTO na kuokoka.
Kwa sasa miaka ya mwanadamu ya kuishi duniani ni 70 hivyo wanaovuka hapo ni bonus au ofa wamepewa na MUNGU.
Zaburi 90:10 " Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara."
✓✓Kumcha MUNGU hutengeneza kuongezeka kwa miaka ya mcha MUNGU.
Wako wateule wa MUNGU wakiongezewa siku za kuishi kwa sababu walikuwa wanamcha MUNGU.
Mithali 14:27 "Kumcha BWANA ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti."
5. Kumcha MUNGU huleta Roho ya kumcha MUNGU ndani ya mtu huyo.
Isaya 11:2-3 " Na roho ya BWANA atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA;
na furaha yake itakuwa katika kumcha BWANA; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;"
✓✓Kuna roho saba za MUNGU na hizi anazo Bwana YESU KRISTO, moja ya roho hizo ni roho ya kumcha MUNGU.
◼️Roho hizo saba za MUNGU zinamilikiwa na ROHO MTAKATIFU na kuwapa wateule wa KRISTO wanaomcha MUNGU.
✓✓Kwa hiyo unaweza ukawa unamcha MUNGU na ukapata faida ya ajabu ya kupewa na roho ya kumcha MUNGU.
Kama kuna watu hupewa roho ya utumishi n.k wewe unaweza kupewa pia na roho ya Kumcha MUNGU, ni faida muhimu sana.
Zingatia na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments