NINI UFANYE JUU YA MTUMISHI WA MUNGU ANAYEKUCHUNGA KIROHO NA KUKUSAIDIA SANA KIROHO KWA KUSUDI LA MUNGU.
![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe.
Wapo Watumishi wa MUNGU ambao waliobeba dhamana kubwa kwa ajili ya watu fulani.
◼️Mfano hai ni Musa ambaye kwa Maombi yake aliepusha MUNGU asiwaangamize Waisraeli wote.
Kutoka 32:11,14 " Musa akamsihi sana BWANA, Mungu wake, na kusema, BWANA, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? ........... Na BWANA akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake."
◼️ Mfano Mwingine ni Mtume Paulo anasema hakujiepusha kuwahubiria Neno la KRISTO.
Matendo 20:27 "Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la MUNGU."
✓✓Wakati Mwingine Inawezekana Mtume Paulo angechoka sana lakini alijilazimisha hivyo hivyo ili Neno la MUNGU liwafikie watu waliokusudiwa.
Wakati Mwingine alifanya kazi ya MUNGU kwa machozi na maumivu makubwa ila hakuacha.
Matendo 20:31 "Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi."
✓✓Wakati Mwingine Watumishi wa MUNGU wanaweza wakafanya kazi ya MUNGU katika mazingira magumu sana na kwenye vita Kali sana ya kiroho na kimwili.
Yote hayo ni ili Neno la MUNGU limfikie Mtu aliyekusudiwa kwa ajili ya ushindi wake, baraka zake na uzima wake wa milele.
◼️Je umewahi kujiuliza ufanye Nini kwa ajili ya Mtumishi wa kweli wa MUNGU katika KRISTO anayekuchunga kiroho au kukusaidia kiroho kwa kusudi la MUNGU?
Haya hapa chini ni Mambo 7 ambayo unaweza ukayafanya kwa ajili ya Mtumishi wa kweli wa MUNGU anayekuchunga Wewe na kukusaidia kiroho kila mara kwa kusudi la MUNGU wa Mbinguni.
1. Mtambue Mtumishi huyo wa MUNGU aliyewekwa na MUNGU kwa ajili yako.
1 Wathesalonike 5:12" Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika BWANA, na kuwaonyeni;"
✓✓Ukimtambua utamtia Moyo maana inawezekana wasiomtambua ni wengi na kazi yao ni kumvunja Moyo, kumtukana, kumdharau, kumzushia uongo n.k
✓✓Watu wabaya wa ulimwengu wanaweza wasimtambua na wasitambue na kuthamini kile ambacho MUNGU amempa kwa ajili ya Injili. Wewe usiungane na Watu wabaya kumsema vibaya Mtumishi wa kweli wa MUNGU, Bali kwa sababu unamtambua basi mthamini.
2. Mstahi na kumheshimu Mtumishi wa KRISTO aliyewekwa na MUNGU kwa ajili yako.
1 Wathesalonike 5:13 "mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi."
Sio Mimi Peter Mabula ndio naagiza haya Bali ni Biblia Takatifu ndio inaagiza kwamba tuwasitahi sana Watumishi wa kweli wa KRISTO ambao MUNGU ametupa sisi.
◼️Kumstahi Mtumishi maana yake ni kumpa heshima kama Mtumishi wa MUNGU.
3. Muombee Mtumishi wa MUNGU aliyewekwa na MUNGU kwa ajili yako.
2 Wathesalonike 3:1 "Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la BWANA liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu;"
✓✓Hata kama Mtumishi anayekuchunga kiroho au anayekusaidia kiroho ana Nguvu za MUNGU kiasi gani, bado Mtumishi huyo anahitaji sana Maombi Yako.
✓✓Muombee Mtumishi wa MUNGU anayekuchunga kiroho kwa Neno la MUNGU.
✓✓Muombee Mtumishi wa MUNGU ambaye una uhakika ni MUNGU amekupa ili huyo Mtumishi akusaidie kiroho.
4. Msapoti kwa matoleo ili azidi kuipeleka injili ya KRISTO mbali zaidi.
1 Wakorintho 9:11" Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini?"
✓✓Ndio maana usione jambo baya kushirikishwa katika changizo ili injili ya KRISTO iende mbele.
1 Wakorintho 16:1" Kwa habari ya ile changizo kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo."
✓✓Pale inapihitaji kwa ajili ya kuipeleka Injili ya KRISTO mbele msapoti Mtumishi huyo hata bila kuambiwa. Hata kama hajakuomba umsapoti Wewe msapoti sawasawa na uwezo wako, Sadaka za namna hiyo zina Nguvu sana na zitaleta Matokeo makubwa kwako.
5. Mwamini huyo Mtumishi wa MUNGU ambaye umejiridhisha kwamba ni Mtumishi wa kweli wa Bwana YESU kwa ajili yako pia.
2 Nyakati 20:20b " ..... mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa."
✓✓Usipomwamini Mtumishi wa kweli wa KRISTO ambaye MUNGU amekupa ujue utapishana na baraka zako nyingi kwa sababu hutamsikiliza Mtumishi huyo Wala kumzingatia.
✓✓Kuwezi ukizingatia Neno la MUNGU kama Mtumishi anayelitoa hilo Neno humwamini.
Ndio Biblia katika andiko inasema utafanikiwa kama utamwamini na kutamsikiliza Mtumishi wa MUNGU aliyepewa na MUNGU kitu kwa ajili Yako.
6. Mshirikishe hitaji lako ili akuombee.
Yakobo 5:16 "Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii."
✓✓Inawezekana unangaika sana kwa sababu hujamdhirikisha Mtumishi uliyepewa, Kumbuka kila Mtu ana Neema yake. Kuna mambo unaweza ukayaombea muda mrefu lakini bila mafanikio lakini ukamshirikisha Mtumishi uliyepewa akaomba kwa ufupi tu Wewe ukafanikiwa kwa sababu kila Mtu ana Neema yake.
7. Kama kuna mambo yanahitaji ushauri basi usiache kumshauri vyema.
1 Wakorintho 8:2 " Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua."
✓✓Sii kwamba kuwa Mtumishi wa MUNGU ndio unajua kila kitu, yapo mengi tu Mtumishi hayajui na anaweza kuhitaji msaada kwa anaowahubiri au kuwachunga au kuwaongoza kiroho.
✓✓Hata Mtumishi anahitaji kujifunza sana maana sio kwamba kuwa Mtumishi basi unajua kila kitu.
Mithali 1:5 "mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia."
MUNGU akubariki Sana kwa kujifunza somo hili nililokuletea Leo.
Zingatia na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments