WATU WAPUMBAVU ZAIDI DUNIANI.

Na Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu wote walio na mpango wa kwenda uzima wa milele.
Karibu ujifunze kitu kwa ajili yako au kwa ajili ya mtu wako wa karibu anayestahili msaada wa Neno hili  la MUNGU utakalojifunza Leo.
Sio kila siku utakutana na Neno la MUNGU utakalo tu wewe, siku nyingine unaweza kukutana na Neno la MUNGU aina ya nyundo pia kama Biblia inavyosema katika Yeremia 23:29 kwamba Neno la MUNGU ni nyundo, Leo tuna Neno aina ya nyundo, fanyia  tu kazi na itakusaidia.

✓✓Neno ""mpumbavu"" limeandikwa Mara nyingi katika Biblia hivyo hata Mimi nalitumia katika ujumbe wa leo hivyo kama unahusika usidhani ninakutukana kwa kukuita mpumbavu bali Neno la MUNGU liko wazi sana juu ya mtu mpumbavu, hivyo sio tusi bali ni onyo ili upumbavu umtoke mtu.

Baadhi ya maandiko yanayoonyesha Neno mtu mpumbavu ni hili.
Mithali 26:4 ''Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Usije ukafanana naye.''

✓✓Nini maana ya Mpumbavu?

Mpumbavu ni mtu anayeshindwa kuelewa jambo hata kama akielekezwa sana.

Pia mpumbavu ni mtu ambaye anafahamu jambo jema lakini halitendi, mfano wa mpumbavu ni mtu ambaye anajua kabisa kwamba inampasa kuishi maisha matakatifu ya Wokovu yeye  haishi maisha hayo matakatifu.

Wapo watu wapumbavu duniani wengi sana.
Yapo makundi mengi ya wapumbavu duniani, baadhi ya makundi ya watu wapumbavu zaidi ni haya.

1.   Wanaokataa wokovu wa Kristo yaani wanaokataa kuokoka.

Yohana 3:16-18 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."

Wanaompokea YESU kama Mwokozi wao sio wapumbavu bali ni wenye akili, lakini wanaomkataa YESU hao ni wapumbavu kwa sababu wakifa bila Wokovu wa KRISTO wataenda jehanamu.

2. Wanaosema MUNGU hayupo.

Zaburi 14:1 "Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna MUNGU; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema."

Hili ni kundi lingine la watu wapumbavu zaidi duniani.
Ni watu ambao wanajua kwamba kila kitu duniani kina chanzo wanasahau kwamba uhai wao wenyewe chanzo chake ni MUNGU huyo wanayesema hayupo.

Biblia iko wazi sana kwamba ni wapumbavu tu ndio wanaoweza kusema kwamba MUNGU hayupo.

Je wewe ni mpumbavu katika hili?
Nakuomba usikubali kamwe kuwa mpumbavu kwa ajili ya kusema MUNGU hayupo wakati yupo milele na atakuwepo milele yote ijayo.
MUNGU wa kweli ni mmoja tu ni MUNGU katika KRISTO YESU.
1 Wafalme 8:23 "Akasema Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote."

3. Waabudu shetani au sanamu au miungu.

Kutoka 20:4-5 " Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni MUNGU mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,"

Kuabudu miungu na kuabudu sanamu ni jambo moja yaani huko kote ni kuabudu shetani.
Kumwabudu yeyote nje na MUNGU aliyejifunua katika KRISTO YESU ni kuabudu shetani.

Isaya 41:29 "Tazama, hao wote ni ubatili; kazi zao si kitu; sanamu zao ni upepo na fujo."

Waabudu shetani ni wapumbavu kwa sababu wanaabudu kazi za mikono ya wanadamu yaani wanasujudia sanamu iliyotengenezwa na mwanadamu, wanasujudia jiwe au mnyama vitu ambavyo viliumbwa tu na hairuhusiwi kuviabudu.

Warumi 1:25 "Kwa maana waliibadili kweli ya MUNGU kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina."

Waabudu shetani ni wapumbavu kwa sababu wanamwabudu Lucifer ambaye ameandikiwa jehanamu hivyo na wao wanakuwa wanajiunga naye jehanamu, huo ndio upumbavu mkubwa zaidi.
Shetani huabudiwa pia kupitia mizimu, majini, wakuu wa giza na kila maroho wa kuzimu wanajifunua kwa namna tofauti tofauti ili yaabudiwe.
Biblia inasema wale ambao majina yao hayapo katika kitabu cha uzima cha Bwana YESU mbinguni ndio wanaomsujudia shetani kupitia mnyama ambaye ni roho ya kuzimu.
Ufunuo  13:8 "Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu(shetani), kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo(YESU KRISTO), ....."

 Kwa hiyo wanaomwabudu shetani majina yao hayako katika kitabu cha uzima mbinguni.
Kumwabudu shetani ni upumbavu wa kiwango cha juu sana, kuabudu sanamu au mizimu au chochote ni upumbavu.
Je wewe ni mpumbavu katika hili?
Ndugu usikubali kuwa mpumbavu.
Mkimbilie YESU  na Wokovu wake ili upishane na upumbavu huo.

4. Wanaojiua.

Kumbu 5:17 "Usiue."
Biblia inaposema "usiue" ina maana ya kwamba wewe usimuue mtu yeyote na pia wewe mwenyewe usijiue.

Hili la watu wanaojiua ni kundi lingine la watu wapumbavu zaidi duniani.
Kujiua ni kufanya dhambi ya kuua hivyo kujiua ni kujipeleka jehanamu.
Hata kama ulikuwa mtakatifu kiasi gani lakini baada tu ya kujiua unakwenda kuzimu  na sio mbinguni kwa sababu unapomalizia tu kujiua umefanya dhambi na kuua na hakuna tena nafasi ya kutubia dhambi hiyo maana unakuwa haupo duniani na baada tu ya kufa Biblia inasema ni hukumu, hivyo hakuna tena nafasi ya kutubu.

Waebrania 9:27 ''  Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; ''
Wengi wanaojiua kwa upumbavu wanadhani wanakimbia matatizo duniani kumbe wanaikimbilia jehanamu maana hakuna mtu anayejiua akaenda uzima wa milele.
Kuna upumbavu mwingi katika kujiua, kwanza unakatisha uhai wako, unaacha maumivu kwa ndugu zako au watu wako wa  karibu na unamkosa MUNGU milele kwa sababu hutaenda uzima wa milele.

5. Wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na wanaofanya mapenzi kinyume na maumbile.

Warumi 1:26-28 "Hivyo MUNGU aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;
 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. Na kama walivyokataa kuwa na MUNGU katika fahamu zao, MUNGU aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa."

Hili ni kundi lingine la wapumbavu zaidi duniani.
Wanaofanya mapenzi ya jinsia moja ni mashoga kama ni wanaume na wasagaji kama ni wanawake, hawa ni wapumbavu maana wamechagua jehanamu, wamechagua kumkosa MUNGU maishani mwao.
Wanaofanya mapenzi kinyume na maumbile ni mashoga, wafiraji na  walawiti, ni upumbavu wa kiwango cha juu sana.
Sio kwamba kufanya ngono isiyo kinyume na maumbile sio dhambi bali pia ni dhambi kama unafanya na asiye Mke/Mume wako sahihi.
1 Wakorintho 6:9 "Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,"

Ni upumbavu mkubwa kufanya mapenzi kinyume na maumbile.
Ni upumbavu wa hali ya juu sana kufanya mapenzi ya jinsia moja.
Je wewe ni mpumbavu katika hili?
Ndugu ukatae upumbavu huo kuanzia leo.

6.  Wazinzi na waasherati. 

1 Kor 6:18 ''Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. ''

Hili ni kundi maarufu zaidi la wapumbavu duniani.
Ni kundi la wapumbavu sana lenye wanachama wengi.
Biblia kwa kuonyesha upumbavu wao inasema Mithali 6:32 " Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake."

Wazinzi ni akina nani?
Wazinzi ni walio ndani ya ndoa wanapotoka nje ya ndoa zao.
Yaani mtu aliye katika ndoa anapofanya ngono na mtu yeyote nje na mwenzi wake wa ndoa.

Waasherati ni watu gani?
Waasherati ni wale ambao hawajaingia ndani ya ndoa wakifanya uzinifu.

Akikutana kimapenzi mtu aliye ndani ya ndoa na mtu asiye ndani ya ndoa maana yake hapo wamekutana mzinzi na mwasherati ili wafanya uzinifu, ni dhambi mbaya sana. Wapumbavu tu ndio hufanya uzinzi na uasherati.
Na uzinifu wao huwafanya wawe rafiki wa dunia na kuwa adui wa MUNGU.
Yakobo 4:4 "Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU."

Je wewe ni adui wa MUNGU kwa sababu ya uzinzi na uasherati?

Je wewe ni rafiki wa dunia kwa sababu u mzinzi au mwasherati?
 Biblia inasema kwamba kuna hukumu ya MUNGU kwa wazinzi na waasherati.
Waebrania 13:4 " Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu."
Je wewe ni mpumbavu katika hili?
Ndugu kuanzia leo kataa kuwa mpumbavu.
Usikubali kuisaliti ndoa yako, usikubali kutembea na mchumba wako, usikubali kufanya mapenzi na mtu yeyote ambaye hujafunga nae ndoa takatifu.

7. Wanaomwacha YESU.

Hili ni kundi la wapumbavu linalohuzunisha sana.
1 Timotheo 5:15 Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka(Wameacha Wokovu) na kumfuata Shetani. "

Hili ni kundi ambalo mwanzo walikuwa wameokoka lakini kwa sasa ni wapagani.
 Zamani walikuwa watumishi wa MUNGU lakini kwa sasa ni watumishi wa shetani maana wamemwacha YESU Mwokozi.
Zamani walikuwa wanamwimbia MUNGU lakini kwa sasa wamemwacha YESU Mwokozi na kwa sasa wanamwimbia shetani.
Walikuwa wateule wa MUNGU lakini kwa sasa wameshamwacha YESU Mwokozi na kwa sasa wao ni wazinzi au waasherati au waabudu shetani au waabudu majini, au wauaji n.k
Je wewe ni mpumbavu katika hili?
Ndugu, rudi kwa YESU Mwokozi haraka maana nje na YESU hakuna uzima wa milele.
Ndugu usikubali kuwa mpumbavu kwa kumwacha YESU Mwokozi, kumbuka Mithali 10:21b  kwamba " wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu."
Ndugu usikubali kuwa mpumbavu katika niliyokuambie leo.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na siku moja nitalifafanua zaidi katika kitabu.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments