ZIFUTE KALENDA ZA KICHAWI ZILIZOPANGWA KUHUSU WEWE MWAKA HUU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.

 Leo  tunaomba tukizifuta kalenda  zote za kichawi

Kalenda za kichawi ni nini?

✓Kalenda za kichawi ni mipango ya kichawi iliyopangwa kumpata mtu kwenye tarehe maalumu iliyopangwa.

✓Kalenda za kichawi ni mipango iliyopangwa kishetani iliyoanza zamani kwenye maisha ya mtu na inaendelea wakati huu na wakati ujao kwa usimamizi wa nguvu za giza.

✓✓Ukisoma Esta 3:12-13 unaona mawakala wa shetani walipanga tarehe 13 December waisraeli wauawe na kunyang'anywa Mali zao.

Esta 3:12-13 " Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza; na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza vyote, kwa maakida wa mfalme, na maliwali waliokuwa juu ya kila jimbo, na wakuu wa kila taifa; kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jinsi la mfalme Ahasuero, na kutiwa muhuri kwa pete yake. Barua zikapelekwa kwa mikono ya matarishi mpaka majimbo yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyachukua mali yao kuwa nyara."

✓✓Ukisoma 2 Wafalme 6:8 Biblia inasema " Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani."

Mfalme wa Shamu ni mfano wa wakala wa shetani anayepanga kuwapiga watu wa MUNGU. Akaamua kupanga vituo vya kufikia akifanya vita na watu wa MUNGU, neema ya MUNGU ni kwamba kwa watu wa MUNGU alikuwepo Elisha aliyekuwa anaona kinachokuwa kinaendelea kwenye ulimwengu wa roho hivyo akawasaidia watu wa MUNGU wasiuawe.

Lakini nini nataka ujue?
Mfalme wa shamu alipanga vituo, hata wewe kwako nguvu za giza zinaweza kupanga vituo vya kukushambulia, wanaweza kuiacha ndoa yako ila wakakutesa afya yako, kituo chao kinaweza kuwa uchumi na sio afya.
Je kwenye maisha yako unahisi ni eneo gani mawakala wa shetani wameweka kituo?

Kuna watu shetani hajawazuia kuwa matajiri ila kawazuia kukaa bila kuumwa, hivyo wanateswa na magonjwa.

Kuna watu shetani hajawazuia kupata kazi ila kawazuia kuishi bila madeni hivyo wamejaa madeni.

Kuna watu shetani hajawazuia kufunga ndoa ila kawazuia kuwa na furaha katika ndoa, kawazuia uzao, kawazuia upendo.

Kuna watu shetani hajawazuia kufaulu mitihani na kumaliza chuo ila kawazuia kupata kazi.

Kuna watu shetani hajawazuia kufungua biashara ila kawazuia kupata faida.

 Kalenda za kichawi juu ya mtu zinaweza kupangwa hata kwa miaka mitano au miaka yeyote, mtu huyo asipojua kumwita Bwana YESU KRISTO anaweza kushangaa matatizo ya mwaka juzi ndio yamekuwa matatizo ya mwaka jana na hata mwaka huu ni matatizo hayo yanaendelea, hiyo ni kalenda ya kichawi kwa mtu huyo, kalenda ya muda mrefu.

Kuna mama mmoja ndoa yake ilikuwa na mgogoro kwa zaidi ya miaka 5, aliomba na kufunga lakini vita katika ndoa haikuishi, siku moja alipata Neno la MUNGU la ufunuo na alipolifanyia kazi  Neno Hilo ndipo furaha ya ajabu katika ndoa yake ndipo ilirudi.

Ndugu, ni kweli inawezekana una maadui wengi na wengine hadi wamekutengenezea kalenda ya mateso, lakini kwa maombi leo kupitia jina la YESU KRISTO hao adui wa watarudi nyuma ghafla na kuyaachia maisha yako. Imeandikwa " Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika.-Zaburi 6:10

 Ukiwa na mamlaka ya jina la YESU KRISTO imeandikwa " Nitawafuatia adui zangu na kuwapata, Wala sitarudi nyuma hata wakomeshwe. Nitawapiga-piga wasiweze kusimama, Wataanguka chini ya miguu yangu.-Zaburi 18-37-38

Kuna mamlaka kuu sana katika jina la YESU KRISTO ukitumia Damu ya YESU KRISTO na Neno la MUNGU.

Ngoja nikujulishe jambo hili, mawakala wa shetani wanaweza kukaa kikao cha siri na kupanga mambo mabaya ambayo anayehusika anaweza asijue. Kumbuka nao wanaweza kutenda kwa akili.
Mfano 
Kutoka 1:9-10 "Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii."

Farao ni mfano wa shetani na hapa kwenye maandiko tunaona akikaa kikao cha kipepo na watenda kazi wake akiwaambia kwamba wawatende waisraeli kwa akili ili waisraeli wasiongezeke.
Ndipo unavyoweza kupangiwa wewe na mawakala wa shetani ili biashara yako iziongezeke, uchumi wako usikue.
Mawakala wa shetani hutenda kwa akili wakati mwingine, ndio maana mtu anaweza kuishi hata miaka kumi bila kujua kama ana mapepo ndani yake waliyomuwekea ili kumvuruga.

Unaweza ukashangaa mtu anaishi na mchawi hata miaka 20 na asijue kama anaishi na mchawi.

Ndugu, hakikisha unafuta kalenda zote za shetani kuhusu wewe mwaka huu.

 Futa hata kalenda ya kipepo ya muda mrefu katika familia yenu au ukoo ambapo kalenda hiyo inaendelea kutoka mababu zako na imekupata na wewe mjukuu.
Masomo kama haya ni muhimu sana katika jamii zetu kwa sababu ni nadra sana kukuta ukoo hauko katika kalenda ya kishetani, ni wateule wachache tu walioamua kujitenga kiroho na ukoo ulioshikwa kipepo na nguvu za giza, inawezekana hujanielewa, ngoja nifafanue jambo moja tu kati ya mengi yanayoleta ukoo au familia kuwa katika kalenda ya kipepo.
Familia nyingi au koo nyingi zimewahi kuhusika na matambiko.
Kama hujui ni kwamba matambiko ni njia ya shetani kuwakabidhi familia kwa mkuu wa giza wa kuwasimamia.
Baba akifanya matambiko ujue amewaunganisha na uzao wake na wajukuu zake.

 Matambiko ndio chanzo cha mizimu na mizimu ni maroho ya kuzimu yaliyokabidhiwa familia ili yaisimamie kishetani, kama mizimu hiyo ilianza na mtu mmoja na huyo baada ya miaka mingi atakuwa ukoo, na bado mizimu ipo na inaendelea kuwasimamia watu wale kipepo, ni hatari sana ndio maana kuna watu hajawahi kwenda kwa mganga wala kushirikiana kivyovyote na nguvu za giza lakini akitaka kusoma Biblia anasinzia ghafla, hiyo ndio kalenda ya kipepo ili mtu huyo asisome Neno la MUNGU litakalomtoa katika nguvu hizo za giza, mizimu watamruhusu kusoma vitabu vyote, magazeti yote ha majarida yote hata kama atasoma kurasa 500 kwa siku lakini akishika Biblia ili kusoma nusu ukurasa anachoka ghafla na kusinzia na kichwa kinakuwa kizito, hiyo ni kalenda ya kuzimu ili mtu huyo asiipate kweli ya MUNGU akaokoka au akapata mbinu za kutoka katika tatizo.

Mizimu ni maroho ya kuzimu yaliyokaa kwenye ukoo kwa muda mrefu, ni watunza taarifa kipepo za ukoo ili shetani azitumie kuwatesa zaidi ukoo huo.

Usishangae ugonjwa uliomuua Bibi ndio ugonjwa unamtesa sasa mjukuu, usishangae familia Fulani au ukoo fulani wanawake wote huzalia nyumbani bila ndoa.
Leo mwambie MUNGU awaangamize mizimu na alifute jina lao kwako na kwa ukoo wako wote.
Zaburi 9:5 "Umewakemea mataifa; Na kumwangamiza mdhalimu; Umelifuta jina lao milele na milele;"

 Ukoo fulani kila  mwanamke aliye kwenye ndoa lazima mimba yake ya  kwanza ama itoke, ama azae mtoto aliyekufa, yaani walishajua kabisa ndio wao walivyo kumbe wanateswa na kalenda ya kichawi ya tangu kizazi na kizazi cha ukoo wao.

Ni koo chache sana katika jamii zetu wasiohusika na matambiko, na tambiko lolote akifanya mtu ujue amewaunganisha na watoto wake katika usimamizi huo wa kipepo wa mizimu.
Mizimu huwawekea mipaka ya kishetani wana ukoo husika.

Kuna ukoo mtu hawezi kukaa katika ndoa miaka zaidi ya 30, yaani ukifika muda huo ama kufa au kufiwa au kuachana.

Kuna koo ni marufuku kufikisha kiwango Fulani cha pesa, mtu akikikaribia kiwango hicho ama anafilisika ghafla yaani anaanza moja au anapatwa na mabaya mengine, ndio maana huwa unasikia mtu anaenda kwao kutengeneza na mizimu, kumbe ameenda kuimalisha agano la kipepo la kuwafanya maroho wa kuzimu wawe na uhalali zaidi.
Kumbu 18:10-12 "Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; ......."

 Je ukoo wenu mmewekewa kalenda gani na mizimu, ndugu futa leo kwa maombi katika jina la YESU KRISTO Mwokozi, maana ukiendelea pia kushirikiana na mizimu huwezi kwenda uzima wa milele.
Kwa sababu ya mizimu ya ukoo ndio maana nikasema ni watu wachache ambao ukoo wao hauko katika kalenda ya kipepo.

Baadhi ya vitu vya watu wenyewe vinavyoweza kuleta kalenda ya kipepo kwa familia au ukoo ni laana ya kulaaniwa na mawakala wa shetani, laana hiyo italeta wasimamizi wa kuzimu kuhakikisha inatimia, watakaopona hapo walio tu na YESU KRISTO na waombaji wanaojitambua na kujua haki zao kiroho.

Mazindiko ya kiukoo nayo ni njia mojawapo ya kuleta wasimamizi wa kipepo waliobeba kalenda ya kichawi juu ya ukoo husika au familia husika.

Kuchanjwa chale ni mlango mmoja wapo wa kishetani unaoleta nguvu za giza zikiwa na kalenda ya kuzimu juu ya mtu husika.
Walawi 19:28 "Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA."

Kwenda kwa waganga ni mlango mkuu wa kuleta mashetani yaliyo na kalenda za giza. 
Kwenda kwa waganga kutengeneza maagano ya kuzimu yatakayosimamiwa na majini, usimamizi huo ndio kalenda za kichawi.
Usiende kamwe kwa waganga wa kienyeji, Manase alifanya hivyo ikapelekea kupata adhabu kubwa na mbaya sana kutoka kwa MUNGU.
2 Wafalme 21:6 "Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, hata kumkasirisha."

 Kurogwa pia ni kuwekwa chini ya nguvu za giza zenye kalenda za kuzimu juu ya mtu husika au watu husika.

Ndio maana ni walio na YESU KRISTO tu ndio wanaoweza kujitenga mbali na kalenda za kipepo kwa maombi.
Mathayo 7:8 "kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."

Angalau baadhi ya familia unaweza kukuta tangu babu wa babu aliompokea YESU KRISTO tangu zamani ndio maana kwa miaka mingi hawakushirikiana na mizimu hivyo kalenda ya kipepo kuzikuifuatilia familia hiyo au ukoo, ni wachache sana sasa.
Kumbuka Ukristo uliingia afrika mashariki na kati si zaidi ya miaka 250 iliyopita hivyo waliopata neema ya Wokovu hata wakavunja mikataba na shetani ni wachache sana, ndio maana tunafundisha masomo kama haya ili wanaoendelea na mizimu waache.

Kuna watu wana magonjwa ya kurithi, kumbe ni kalenda ya kichawi inayoendelea, leo ifute hiyo kalenda ya kichawi kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO Mwokozi.

Kuna watu kalenda ya kichawi kwao ni ukoo mzima hakuna kufikia daraja Fulani la elimu, familia nzima hakuna kufunga ndoa takatifu kanisani, kuwa watu wa kunyanyaswa tu na kuonewa n.k

Ndugu, kama kuna kalenda ya kipepo yeyote kuhusu wewe hakikisha leo, kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO unaifuta kalenda hiyo ya giza.

Inawezekana kuna matatizo yanakuandama mfululizo kumbe kuna kalenda ya kichawi ilitengenezwa kuhusu wewe.
Kalenda za kichawi zinaweza kutengenezwa na wachawi, waganga au kuzimu na watekelezaji wa kalenda hiyo ni majini na kila maroho wa kuzimu, ndugu inakupasa kuomba na MUNGU atakushindia, kalenda za giza zitafutika na utajitenga kiroho na familia iliyofungwa, ukoo uliofungwa na eneo lililofungwa.

Nini ufanye ili usifuatiliwe na kalenda za kichawi ikiwa ulishampokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako?

1. Futa matukio ya kipepo yote yaliyopangwa katika tarehe yeyote ya mwaka kwako.

Futa kwa kuifunga hiyo mipango ili isifanyike kamwe.

Mathayo 18:18 "Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni."

2. Amuru wakichokipanga mawakala wa shetani dhidi yako kiwapate wao na sio wewe.

Una kibali cha kuwahukumu na ulichowahukumu kikawapata.

Isaya 54:17 "Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA."

3. Pambana kimaombi na wakuu wa giza walioandaa kalenda ya kipepo dhidi yako.

Waponde kwa fimbo ya chuma.
Zaburi 2:9 "Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi."

 4. Omba ulinzi wa MUNGU siku zote  zilizobaki za mwaka huu.

Zaburi 27:1-2 " BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka."

5. Amuru uharibifu wa ghafla uwapate mawakala wa shetani waliokupangia jambo lolote mwaka huu.

Zaburi 35:8 "Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake."
Omba ndugu na utashinda.
Omba kwa imani katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
MUNGU akubariki.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
+255714252292

Comments