ADUI ZAKO WAJIKWAE.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Ujumbe wa May 2019.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Ni kama mwezi mmoja na nusu umepita tangu siku nilipopata ajali mbaya ila MUNGU akaniokoa, ilikuwa tarehe 25 March 2019 asubuhi ndio siku nilipata ajali hiyo, namshukuru MUNGU mimi ni mzima na sina dhara lolote kutokana na ajali hiyo. Baada ya hapo niliwajulisha baadhi ya ndugu na marafiki. Namshukuru sana MUNGU kwa watu ambao walitoa pesa zao ili nitibiwe, nilibaki nimeduwaa nikimshukuru MUNGU maana sikutarajia, nilishangaa tu kuona nimetumiwa .
Namshukuru MUNGU kwa ajili ya watu ambao walitaka kunitumia pesa nitibiwe nikawaambia wasitume na wawe na amani kabisa, yaani nilimshangaa sana MUNGU kwa ajili ya marafiki zangu ambao tumefahamiana tu mtandaoni kupitia Neno la MUNGU ninalofundisha kila mara mtandaoni.

Pia nilimshukuru sana MUNGU kwa ajili ya Wateule mbalimbali wa MUNGU ambao waliguswa sana kuniombea, wengine walinijulisha na wengine hawakunijulisha ila naamini hivyo.

Sasa baada ya hapo nikawa naomba maombi nikimshukuru MUNGU kwaajili ya watu hao wa kipekee sana kwangu, katika maombi hayo nikasikia sauti ikisema "Omba adui zao wajikwae, Yeremia 20:11"

✓✓Baada ya kufunuliwa ufunuo huo wa andiko niliwaombea marafiki hao wa kipekee kwamba adui zao kiroho na kimwili wajikwae.

Niliitafakari sana hiyo Yeremia 20:11 ambayo inasema " Lakini BWANA yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe."

Baadae niliingia katika tafakari juu ya maadui kiroho kujikwaa nikagundua mambo haya;

1. Maadui wanaweza kujikwaa na kurudi nyuma wasikufuatilie tena.

Zaburi 27:2 "Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka."

2. Adui anaweza kujikwaa na mabaya yakamfuata yeye na sio wewe.

Zaburi 9:3 "Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako."

3. MUNGU akiunyoosha mkono wake juu ya adui zako wanaweza kujikwaa wao na wanaowasaidia.

Isaya 31:3 "Basi Wamisri ni wanadamu wala si MUNGU, na farasi zao ni nyama wala si roho; na BWANA atakaponyosha mkono wake, yeye asaidiaye atajikwaa, na yeye asaidiwaye ataanguka, nao wote pamoja watakoma."

4. Kuna adui anaweza kujikwaa na asiwepo wa kumnyanyua tena.

Yeremia 50:32 "Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote."

✓✓Sijui wewe unapambana na nguvu gani za giza, hao maadui MUNGU anaweza kuwafanya wajikwae na wasikufuatilie tena.

✓✓Kinachoweza kuwafanya adui zako wajikwae ni pale ambapo MUNGU atawaondolea nuru yaani uwezo wa kukuona wewe.

Yohana 11:10 "Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake."

✓✓Inawezekana unateswa na mchawi, kwa maombi yako anaweza kujikwaa na asikufuatilie tena katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.

✓✓Inawezekana umetumiwa majini ili wakunyonge, ukiomba maombi anaweza kujikwaa huyo jini na aliyemtuma na usikupate Miaka Yako yote.

✓✓Inawezekana kuna wakala wa shetani anakufukuzisha kazi kwa hila, unaweza kuomba katika Jina la YESU KRISTO na huyo akajikwaa na asinyanyuke tena au asifanikiwe tena maishani mwako.

Je ni nani anataka kukufukuza katika ndoa yako takalifu?

Ni nani anakuchongea ili ufukuzwe kazi?

Je ni nani anakuwinda ili akudhuru?

Ni nani anatamani ufe?

◼️Ukiwa muombaji  katika Jina la YESU KRISTO basi adui zako hao wanaweza wakajikwaa na wasinyanyuke tena kamwe.

Ni nani anataka huduma yako ufe?

Nani anataka uchumba wako ufe?

Nani anataka bishara yako ifilisike kwa uchawi wake?

Je ni nani anaroga uchumi wako?

◼️Hao maadui zako ukiomba leo katika jina la YESU KRISTO watajikwaa na hawatainuka tena kukufuatilia kama neno la MUNGU linavyosema hapo juu.

✓✓Ndugu, hakikisha tu umeokoka na unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Amua kuomba  kwa Imani katika Jina la YESU KRISTO na MUNGU akubariki sana.
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments