BAADHI YA MAMBO YA KUJUA KUHUSU SAUTI YA ROHO MTAKATIFU NDANI YAKO.




Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Kwa sehemu chache ngoja tuangalie  mambo kadhaa kuhusu umuhimu wa sauti ya ROHO MTAKATIFU ndani yako na ndani yangu pia.

◼️Sauti ya ROHO MTAKATIFU ni ya muhimu sana na ndio sauti pekee ya kweli.

✓✓Sauti ya ROHO MTAKATIFU inaweza kuleta mawazo ya MUNGU anayokuwazia sasa.

✓✓Sauti ya ROHO MTAKATIFU inaweza kukujulisha nini ufanye ili upate kitu fulanj unachokihitaji kwa MUNGU.

◼️Ukitii sauti ya ROHO MTAKATIFU hakika umeamua kuwa mtoto wa MUNGU.

Warumi 8:14 "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU."

Mambo ya kujua kuhusu sauti ya ROHO MTAKATIFU ndani yako.

1. Sauti ya ROHO MTAKATIFU hukufunulia kile kilichojificha ambacho unatakiwa ukijue.

1 Wakorintho 2:10 "Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."

2. Sauti ya ROHO MTAKATIFU hukushauri na kukuonyesha njia sahihi na salama ili usiangukie pabaya.

Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."

3. Sauti ya ROHO MTAKATIFU hukuongoza kwenye kweli yote katika KRISTO YESU.

Yohana 16:13" Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake."

4. Sauti ya ROHO MTAKATIFU hukujulisha nini cha kusema katika mazingira yanayohitaji msaada wa MUNGU katika kuongea kwako mbele za watu wenye hila au mashtaka kuhusu wewe mteule wa KRISTO.

Mathayo 10:19-20 "Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni ROHO wa Baba yenu asemaye ndani yenu."

5. Sauti ya ROHO MTAKATIFU hukujulisha Neno la MUNGU.

Mithali 1:23" Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu."

6. Sauti ya ROHO MTAKATIFU hukupa uhakika wa kiroho kama unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.

Warumi 8:16 "ROHO mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa MUNGU;"

7. Sauti ya ROHO MTAKATIFU huleta mpango wa MUNGU wa sasa kwako na mpango wa MUNGU wa wakati ujao kwako.

Matendo 13:2 "Basi hawa walipokuwa wakimfanyia BWANA ibada na kufunga, ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia."

8. Sauti ya ROHO MTAKATIFU hukujulisha uhubiri nini kama wewe ni Mtumishi wa kweli wa Bwana YESU KRISTO.

1 Wakorintho 2:4" Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za ROHO na za nguvu,"

✓✓Naamini kuanzia leo utatamani sana kuisikiliza sauti ya ROHO MTAKATIFU na kuitii na kuifuata maana ndio sauti ya kweli ya kwanza inayopita sauti zote.

◼️Akisema ROHO MTAKATIFU ujue amesema MUNGU aliyeziumba mbingu na dunia.

◼️Akisema ROHO MTAKATIFU ujue amesema YESU KRISTO Mwokozi.

Warumi 8:9 "Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake."

✓✓Kama huna ROHO MTAKATIFU okoka na omba upewe na utapewa maana ROHO MTAKATIFU ni ahadi ya MUNGU kwa wateule wake wote.

Luka 24:49 "Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu."

Kama ulijazwa ila ukapoteza sifa za kuwa na ROHO MTAKATIFU basi mrudie YESU KRISTO kwa usahihi, tubu na kujitenga na mabaya yote.

Zingatia mteule wa KRISTO na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments