BINTI MTEULE WA KRISTO ANAYEJIELEWA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 




Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

Katika somo hili nimetumia neno "Binti" katika somo hili nikiwa na maana ya mwanamke ambaye hajaolewa ila anategemea siku moja kuolewa, hivyo hata kama amechelewa kuolewa kwa miaka mingi sana bado Mimi nimemwita binti katika somo hili, hivyo linamhusu sana.

Binti mteule anayejitambua ni nani?

◼️Binti huyu ni yule mwenye uwezo wa kuhisi mema na mabaya, kutambua mema na mabaya, kuelewa mema na mabaya ila yeye hufuatana na mema wala sio mabaya.

Kumbu 30:19 "Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako;"

✓✓Chagua uzima ili uwe hai maana yake nyingine chagua mema maana hayo ndio yanayokufaa.


◼️Binti mteule anayejielewa ni binti anayejifahamu yeye ni nani mbele za MUNGU na mbele za Kanisa na anajitambua binafsi kama mteule wa KRISTO na ana uwezo wa kugundua hila za mawakala wa shetani.

2 Wakorintho 2:11 "Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake."

✓✓Sio mabinti wote wanajielewa na kubaki katika kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU, wapo pia mabinti hadi wa watumishi wa MUNGU lakini binti hao hawajielewi, ndio maana hutenda dhambi hasa uasherati hivyo kuchafua hadi huduma njema za wazazi wao.

 Zamani za Biblia binti za namna hiyo walikuwa wanauawa lakini siku hizi hao hufa kiroho na kubaki kama wasindikizaji wa waenda Mbinguni huku wao hawana mpango wa kwenda.

Walawi 21:9 "Na binti ya kuhani ye yote atakapojitia unajisi kwa ukahaba, amemtia unajisi baba yake; atachomwa moto."

◼️Lakini pia wapo mabinti wanaojielewa na sifa yao huwa wazi kabisa, mfano ni huu

Ayubu 42:13-15 " Tena(Ayubu) alikuwa na wana waume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume."

✓✓Binti za Ayubu walikuwa wazuri kuliko mabinti wote katika nchi hiyo, sio uzuri tu bali tabia njema inayosababishwa na kujielewa vyema kama watu wa MUNGU.

✓✓Tena walikuwa wazuri kuliko mabinti wote kwa sababu wao walikuwa wanamcha MUNGU.

Mithali 31:30 "Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye BWANA, ndiye atakayesifiwa."

◼️Sasa Binti mteule wa KRISTO anayejielewa yukoje?

1. Binti Mteule wa KRISTO anyejielewa ana tabia njema.

Mithali 11:16a " Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; ...."

✓✓Neno adabu maana yake tabia njema, hivyo mwanamke mwenye adabu maana yake mwanamke mwenye tabia njema.

2. Binti Mteule wa KRISTO anayejielewa ataolewa na mwanaume mcha MUNGU, lakini ni Binti huyo ndio atampenda huyo kijana na sio kupangiwa na watu mtu wa kumuoa.

Hesabu 36:6 " BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao."

✓✓Yaani waolewe na wateule wenzao, sio kuolewa na watu wa mataifa yaani kuolewa na wapagani au wapinga KRISTO.

✓✓Yaani kwa sababu binti ni mteule wa KRISTO anayejielewa basi wazazi au watu wa karibu hatawaruhusu wamchagulie mtu wa kufunga naye ndoa. Bali kwa sababu binti huyu anajielewa basi ataolewa na mteule mwenzake wa  KRISTO aliyeokoka kama yeye.

3. Binti Mteule wa KRISTO anayejielewa anavaa mavazi ya kujistiri.

1 Timotheo 2:9 "Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;"

✓✓Katika nyakati za Leo mabinti wengi wanajikwaa katika mavazi, wakati Mwingine watu wanaweza kumdhania  Binti fulani ni kahaba kwa sababu ya mavazi ya kikahaba anayovaa, na kumbe sio kahaba.
Sasa kwanini Binti yangu watu wakufikilie tofauti?
Acha kuvaa kikahaba ili uwe Binti anayejielewa.


4. Binti anayejielewa lazima ameokolewa na Bwana YESU KRISTO.

Waefeso 2:8 "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;"

◼️Binti Mteule wa KRISTO anayejielewa hana wokovu wa kuigiza bali anaishi maisha matakatifu.

5. Binti Mteule wa KRISTO anayejielewa anamtumikia Bwana YESU.

1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

Kuna mambo mengi sana yanayoweza kumuonyesha mtu au kumfunua mtu kwamba yeye anamtumikia Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

Sio lazima kuhubiri au kuomba Kanisani hata tu Maisha yake safi yatawafanya watu wasema "Huyu Binti ni Mtumishi wa MUNGU"

6. Binti Mteule wa KRISTO anayejielewa siku zote amejitenga mbali uasherati.

1 Wakorintho 6:18 " Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe."

✓✓Binti huyu hayuko katika kundi la wasio na akili maana waasherati na wazinzi hawana akili.

Mithali 6:32 "Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake."

7. Binti Mteule wa KRISTO anayejielewa anastahili kuwa mke mwema wa mtu.

Mithali 31:29 "Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote."

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
Mwisho kabisa Binti yangu mzuri nakuomba sana usimpe nafasi shetani kwenye Maisha Yako yote.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments