KANISA LENYE NGUVU ZA KIROHO LIKOJE?

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Hapa alikuwa ameenda kufundisha Kanisa la P A G(T) Vijibweni Kigamboni Dar es salaam.



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Bwana YESU KRISTO alipoondoka duniani aliacha Kanisa lenye washirika 120.

Matendo 1:15 "Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema,"

✓✓Kanisa hili lenye washirika 120 lilikuwa na umoja wa ajabu sana.

✓✓ Kanisa hili walikuwa wamejaa ROHO MTAKATIFU.

✓✓Kanisa hilo walikuwa watoaji na wanaoishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.

✓✓Japokuwa Kanisa hili walikuwa watu 120 tu lakini ndio hao waliupindua ulimwengu hata ulimwengu ukamgeukia YESU KRISTO Mwokozi.

Ni Kanisa hili lenye washirika 120 ndilo lilipeleka Injili Asia, Afrika, Ulaya na Amerika.

◼️Sasa Ukitaka kulijua Kanisa lenye Nguvu za rohoni kwa Sasa usiangalie idadi ya watu Bali angalia Nguvu za MUNGU zinazotendeka pale.

Kuna tofauti ya dini na Kanisa, Kuna watu wako katika dini ila wao rohoni hawajaamua kufanyika Kanisa hai la MUNGU wa Mbinguni.

◼️Ninaposema Kanisa lenye Nguvu katika somo hili sizungumzii dhehebu Bali ni Kanisa la mahali wanapokutana kumwabudu MUNGU wa Mbinguni pamoja Haijalishi wanatokea dhehebu gani. Maana unaweza ukakuta Kanisa A la dhehebu fulani katika mtaa fulani Kijiji fulani au Mji fulani Wana nguvu za MUNGU lakini Kanisa A la dhehebu hilo hilo katika Mji Mwingine hawana Nguvu za MUNGU. Lakini pia Inawezekana dhehebu B Kanisa zima kila maeneo hawana Nguvu za MUNGU kwa sababu ya mafundisho yasiyo yanayotokana na miongozo ya dhehebu.

◼️Sasa Kanisa lenye Nguvu za rohoni ni lile utakaloliona linahusika na Mambo haya Saba yote.

1. Viongozi na washirika wa hilo Kanisa wameokolewa na Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

Waefeso 2:8 "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;"

✓✓Kanisa la hili Nguvu za MUNGU huambatana nao maana mahubiri yao msisitizo wao watu wampokee YESU KRISTO kama Mwokozi wao na waishi Maisha matakatifu ya Wokovu.

2. Viongozi na washirika wa hilo Kanisa wamejaa ROHO MTAKATIFU.

Matendo 5:32 "Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na ROHO MTAKATIFU ambaye MUNGU amewapa wote wamtiio."

✓✓Kujaa Nguvu za ROHO MTAKATIFU ni Muhimu sana kama tunataka kuwa Kanisa lenye Nguvu.
Ni lazima watu Wafundishwe kuhusu ROHO MTAKATIFU, wampokee ROHO MTAKATIFU baada ya Kumpokea YESU KRISTO Mwokozi.
Hawa lazima wawe Kanisa lenye Nguvu sana za rohoni.

3. Viongozi na washirika wa hilo Kanisa ni watoaji.

2 Wakorintho 9:6-7 "Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu."

✓✓Utoaji Sadaka na Zaka kwa uaminifu na kwa Moyo wa  upendo huongeza Nguvu ya Madhabahu kiroho  hivyo Nguvu za MUNGU kuwa nyingi Madhabahu hapo na nguvu hizo kuwapata watu wote.

Ukiangalia maandiko mengi katika Biblia ilipotajwa Madhabahu na Sadaka zilitajwa. Changamoto ya watu wengi hawajui Nguvu ya sadaka kiroho.

Mwanzo 8:20 "Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu."

✓✓Baada ya Nuhu kutoa Sadaka MUNGU alitoa tamko.

✓✓Sadaka husababisha mambo mengi kiroho juu ya Madhabahu na wanaomwabudu MUNGU mahali hapo.

Sadaka ya Nuhu ilisababisha MUNGU atoe tamko.

Sadaka za Waisraeli wakati wa Sulemani zilivuta Nguvu za MUNGU kubwa sana.

1 Wafalme 8:5 "Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli waliokutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng'ombe, wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao kwa kuwa wengi."

Baada ya hapo wingu la Nguvu za MUNGU nilijaa.

1 Wafalme 8:10-11" Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya BWANA ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya BWANA ilikuwa imejaa utukufu wa BWANA."

ndugu nadhani unajua jambo hili maana baadhi kabla ya Kuokoka walijihusisha na waganga wa kienyeji, Kwenye madhabahu za giza kwa waganga wa kienyeji bila sadaka hakuna utendaji wa kiroho.
Hao mawakala wa shetani waliiga kwa MUNGU maana ni Kanuni ya kiroho Utoaji wa sadaka za upendo hufanya mambo makubwa.

✓✓Ulishawahi kujiuliza vipi kama watu sio watoaji, wanung'unikaji katika Utoaji wao? Hawa wanapata madhara kiroho wao hadi Madhabahu inaathirika.
Makanisa ya namna hii hutembea tu kwenye upako wa Mchungaji tu  Kulingana na Neema ya MUNGU juu yake, akihama Kanisa hata linaweza kufa, ilitakiwa Kanisa lote lijae Nguvu za ROHO MTAKATIFU.

✓✓Utoaji sahihi wa Matoleo una uhusiano mkubwa na nguvu za MUNGU.

Wewe Anza uchunguzi wako hata kuanzia Leo Makanisani Waamini ambao ni wabishi sana, wasiokua kiroho na wapingaji wa Mambo mazuri ya ki MUNGU Kanisani kila mara wengi zaidi au wote  sio watoaji, maana yake roho ya kifalisayo imewavaa.

✓✓Ndugu, ni Kanuni ya kiroho tukitaka kuwa Kanisa lenye Nguvu za rohoni ni Muhimu kujua Kuna uhusiano mkubwa kati ya Utoaji Matoleo na nguvu za MUNGU.

◾Eliya alipotoa Sadaka ndipo Nguvu za MUNGU zilionekana(1 Wafalme 18:36-39)

◾Ibrahimu baada ya kutoa Sadaka ndipo tamko la Mbinguni lilitoka. 

Mwanzo 22:15-17 " Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;"

4. Viongozi na washirika wa hilo Kanisa wana umoja.

Waefeso 4:3-6 " na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa ROHO katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na ROHO mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. MUNGU mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote."

◼️Umoja kwa watu wa MUNGU waliookoka ni jambo la lazima kama tunataka tuwe Kanisa lenye Nguvu za MUNGU.

Zaburi 133:1 "Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja."

◾Kama hamna umoja Mchungaji anaweza kufundisha mfano MADHARA YA UZINZI na baada ya Ibada watu wabaya wakaanza kusema "Mchungaji mbona amefundisha somo hili si heri angefundisha somo la UPENDO"
Hapo hata aliyezingatia Neno atajikuta anamdharau Mchungaji na anadharau Neno sahihi alilofundisha Mchungaji. Safari ya Kanisa lenye Nguvu za rohoni katika Kanisa hili itakuwa ngumu sana maana hakuna umoja bali Kuna kinyume Cha umoja.

✓✓Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya Kanisa lenye Nguvu za MUNGU na umoja safi kwa washirika mahali hapo.

5. Viongozi na washirika wa hilo Kanisa ni watu wamjuao MUNGU Baba wa mbinguni.

Ayubu 22:21 "Mjue sana MUNGU, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia."

✓✓Wanaomjua MUNGU hawana masihara na mambo ya MUNGU.

✓✓Wanaomjua MUNGU huwezi kuwadanganya ili kuwatoa kwa YESU KRISTO.

✓✓Wanaomjua MUNGU wanaisikia sauti ya ROHO MTAKATIFU na kuzingatia maelekezo yake.
✓✓Wamjuao MUNGU lazima wame Kanisa lenye Nguvu za rohoni daima.


6. Viongozi na washirika wa hilo Kanisa ni watu wenye kuthubutu.

Danieli 11:32 " ........ LAKINI WATU WAMJUAO MUNGU WAO WATAKUWA HODARI, NA KUTENDA MAMBO MAKUU."

✓✓Wateule wa KRISTO wenye uthubutu ndio huambatana na Nguvu za MUNGU.

✓✓Watu wenye uthubutu sio waoga Bali wako tayari siku zote kutenda mambo kwa msaada wa MUNGU.

Zaburi 18:29 "Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi, Kwa msaada wa MUNGU wangu naruka ukuta."

Hawa hawaogopi Wachawi Bali wanaweza kushuhudia Injili hata mtaa wenye Wachawi wengi, hata kwa mchawi wanaweza kufika kuhubiri Injili.
Hawa lazima wawe Kanisa lenye Nguvu za MUNGU.

✓✓Kanisa ambalo lina washirika wengi wenye uthubutu huwa litafanikiwa sana.

✓✓Wako tayari kuipeleka Injili ya KRISTO.
✓✓Wako tayari kufungua Biashara, kulima n.k ni wathubutu wa Kila Mambo mazuri yenye faida kwa MUNGU, kwao na kwa Kanisa.
Hawa watakuwa Kanisa lenye Nguvu za MUNGU maana ni Wathubutu sio waoga.

7. Viongozi na washirika wa hilo Kanisa msingi wao wa imani ni KRISTO YESU Mwokozi.

1 Wakorintho 3:11" Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, YESU KRISTO."

✓✓Hiki ndicho kiini Cha Watu kuitwa"Kanisa"

✓✓Hakuna Kanisa bila YESU KRISTO, Ukiona watu wanajiita Kanisa ila hawamtaki YESU KRISTO ujue hao ni Sinagogi la shetani kama wanavyosema katika Ufunuo 2:9.
 
✓✓Ni heri kila Mkristo akafanyika Kanisa la namna hii.

✓✓Ni heri kila Mkristo akawa wa namna ya Kanisa hili.

✓✓Ni heri kila dhehebu wakati wa namna hii.
✓✓Nakuomba Wewe unayesoma somo hili fanyika Kanisa la namna hii.

◼️Nini nataka niseme kwa Kanisa hai la KRISTO leo?

✓✓Ni kwamba, tukitaka tuwe Kanisa lenye nguvu lazima tuwe tunaokolewa na Bwana YESU KRISTO Mwokozi, lazima tuwe na nguvu za ROHO MTAKATIFU, lazima tuwe na umoja.

Zaburi 133:1 "Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja."

✓✓Tukitaka tuwe Kanisa lenye nguvu lazima tuhubiri Injili ya kweli KRISTO YESU, tena tuhubiri bila kuogopa wanadamu au mazingira.

Isaya 58:1" Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao."

✓✓Tukitaka la MUNGU lenye nguvu lazima tufuate nyayo za Kanisa la kwanza.

Matendo 2:41-42 "Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali."

Ni ajabu watu 120 walipindua ulimwengu wote, lakini kwa sasa kuna wateule wa KRISTO kila taifa wengi zaidi ya Milioni 2 lakini wameshindwa kulifanya taifa lao kufanyika wateule wa KRISTO YESU Mwokozi.

◼️Tatizo kubwa kwa Kanisa la sasa ni kukosekana kwa umoja, kuwa walegevu katika kazi ya MUNGU, kutokuwa watoaji ili kupeleka wahubiri kila pahali, kuwa watu wa mashindano, mbwa mwitu kujiingiza kwenye uongozi wa kundi la watu wa MUNGU, kukumbatia dhehebu huku umemwacha YESU KRISTO Mwokozi n.k

✓✓Inatupasa sana kama Kanisa hai la KRISTO duniani kuwa na umoja kwanza.

Mambo 5 ambayo huambatana na umoja wa watu wa MUNGU ni haya;

1. Kila mtu kutembelea kwenye wito alioitiwa na MUNGU.

2. Unyenyekevu na Upole.

4. Kuwa naa uvumilivu.

4. Kuchukuliana kwa upendo wa ki MUNGU.

5. Kuhifadhi umoja wa ROHO MTAKATIFU.

Maambo hayo matano yanapatikana katika Waefeso 4:1-3 ambapo Biblia inasema " Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani."

✓✓Natamani wewe uwe Kanisa lenye nguvu.
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments