KUITOWESHA ROHO YA MAUTI.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Siku Moja rafiki yangu mmoja aliniandikia hivi hapa chini, nakuletea ujumbe wake kama ulivyo.

"Bwana YESU KRISTO atukuzwe Mtumishi wa MUNGU.
Mtumishi, mimi nafuatiliwa sana na roho ya mauti, nisaidie maandiko ambayo nitayatumia ili kuomba kuitowesha hii roho ya mauti kwangu na kwa familia yangu. "

◾Majibu ya Mtumishi Peter Mabula, Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

MUNGU akubariki sana ndugu.

  ◼️Nakushauri kwanza okoka kama hujaokoka na anza kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU Mwokozi.

Yohana 10:28 "Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu."

✓✓Ukiokoka YESU KRISTO atahusika na Wewe hivyo adui wa kiroho aitwaye roho ya mauti hatakuweza.

✓✓Ukiokoka hutakuwa unaishi tu bali KRISTO YESU atakuwa anaishi ndani Yako hivyo adui aitwaye roho ya mauti hatakuwa na mamlaka kwako ya kukufanya lolote.

✓✓Kama umeokoka tayari hakika umelichagua fungu lililo jema sana ambalo hakuna atakayekuondoleae.

◼️Kuhusu roho ya mauti inayokufuatilia ni rahisi sana kuishinda kama unaomba katika jina la YESU KRISTO huku ukitumia maandiko.

✓✓Yako maandiko mengi unaweza kuyatumia katika maombi yako na hiyo kalenda ya kichawi ya kukuua haitafanikiwa kamwe.

Hapa chini nimekuwekea baadhi ya maandiko ambayo unaweza ukayatumia katika Maombi yangu ili kuishinda roho ya mauti unayoiona.

1. Omba MUNGU akukomboe wewe na familia yako dhidi ya hiyo roho ya mauti inayokufuatilia.

Hosea 13:14 "Nitawakomboa na nguvu za kaburi; nitawaokoa na mauti; ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Kujuta kutafichwa na macho yangu."

2. Omba MUNGU afute huo mpango wa mawakala wa shetani wa kukuua au kumuua mtu wako wa karibu.

Zaburi 102:19-20 " Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu, Toka mbinguni BWANA ameiangalia nchi, Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa."

3. Omba MUNGU akuokoe na abatilishe mipango yote ya maadui zako dhidi yako.

Ayubu 5:12-15 " Yeye(MUNGU) huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao. Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao wenyewe; Na mashauri ya washupavu yaharibika kwa haraka. Wao hupatwa na giza wakati wa mchana, Hupapasa mchana vilevile kama usiku. Lakini yeye huokoa na upanga wa kinywa chao, Hata kumwokoa mhitaji na mkono wake aliye hodari."

4. Omba MUNGU afute kila mipango ya mawakala wa shetani dhidi ya uhai wako, hivyo utaishi idadi ya miaka aliyokupangia MUNGU na sio wachawi, wakuu wa giza, wanadamu wasiokupenda, majini wala waganga wa kienyeji wote.

Kutoka 23:26-27 "Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; NA HESABU YA  SIKU ZAKO NITAITIMIZA. Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao."

◼️Kumbuka njia za wewe kutoka kwenye uharibifu wowote njia hizo zina MUNGU, hivyo omba katika jina la YESU KRISTO utatoka kwenye kila uharibifu uliopangwa kuhusu Wewe.

Zaburi 68:20 "MUNGU kwetu sisi ni MUNGU wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana."

✓✓Baada ya kuitowesha roho ya mauti kumbuka na huyo mpambe wa shetani aliyeituma hiyo roho ya kuzimu, pambana kimaombi pia na huyo ili asitume tena hiyo roho chafu.

◼️Namna ya kuomba juu ya huyo wakala wa shetani inategemea na msukumo wako wa rohoni unataka iweje, Biblia inazungumza mambo mengi juu ya hilo, baadhi ya haya.

1. Unaweza ukamponda kwa fimbo ya chuma huyo wakala wa shetani.

Zaburi 2:9" Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi."

2. Kwa maombi unaweza ukawavunja kiroho na kuvunja kazi zao za kishetani na kuharibu falme zao za giza.

Yeremia 51:20-21 "Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;"

3. Kwa maombi unaweza ukawafukuza hao mawakala wa ili watoke katika eneo lako na watoke katika Maisha Yako.

Yoshua 23:10 "Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana BWANA, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia."

4. Kwa maombi unaweza kung'oa falme za giza, kubomoa falme za giza, kuharibu na kuangamiza falme za giza na madhabahu za giza.

Yeremia 1:10 "angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda."

Hayo ni baadhi tu ya maombi.
Je unapata msukumo wa kuomba maombi gani juu ya mawakala wa shetani ili wasikutumie tena roho za mauti?
Omba na Utashinda katika jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments