![]() |
Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Rafiki yangu mmoja aliniandikia hivi.
"BWANA YESU APEWE SIFA Kaka Peter Mabula,
Habari za uzima
mimi naendelea vizuri namshukuru MUNGU kwahili. Kaka ninatatizo
Ninapokua kwenye Maombi sioni Upenyo au uwepo Haupo naomba lakini naona kabisa Mawasiliano hakuna, Nimefunga na kufanya Toba lakini Bado siombi rohoni, Naimba nasoma neno lakini Hakuna upenyo Bado tatizo litakua ni nini
leo ni siku ya tatu ya maombi ya Toba lakini hakuna upenyo nakosea wapi itakua
kazi njema Kaka
Ubarikiwe"
Majibu haya yakusaidie na wewe unayesoma ujumbe huu na wakati mwingine unapitia haki hiyo katika maombi yako.
◼️Kukosa upenyo wa maombi kunaweza kusababishwa na;
1. Dhambi au kukosa toba ya kweli.
Isaya 59:1-2 " Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."
✓✓Dhambi hukausha Nguvu za kuomba, Ukitaka kuwa na mpenyo katika Maombi na uwepo wa Nguvu za MUNGU uwe na Wewe basi tubu dhambi na kuziacha.
2. Kuomba kimazoea au kutokuzama rohoni.
Wagalatia 5:16 "Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."
✓✓Kuna watu hawako serious na Maombi bali huomba bila Imani.
3. Kutokuomba kwa bidii.
Yakobo 5:17" Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, AKAOMBA KWA BIDII mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita."
✓✓Hakikisha unaomba kwa bidii ukihitaji Matokeo, bidii ya Maombi itaongezea Nguvu za MUNGU kwako
4. Kutokumsikikiza ROHO MTAKATIFU katika maombi.
Yuda 1:20 "Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU,"
✓✓Bila ROHO MTAKATIFU huwezi kushinda katika ulimwengu wa roho, baada ya Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi unayemhitaji zaidi baada ya hapo ni ROHO MTAKATIFU.
Sasa kama ROHO MTAKATIFU amekuambia jambo ukaenda kinyume uwe na uhakika Nguvu za MUNGU zinaondoka ndani Yako na hutaona mpenyo wa Maombi Wala uwepo wa Nguvu za ROHO MTAKATIFU hutaziona hadi utakapotubu na kurejea.
5. Imani haba.
Yakobo 1:6-7 "Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa BWANA."
✓✓Imani hapa maana yake huomba kwa Imani kubwa, hivyo huwezi kupokea.
Mfano ni Mtu katika Maombi yake Kanisani anaomba Bwana YESU KRISTO amponye lakini alipotoka tu Kanisani Kuna Mtu akamuuliza "Naamini umepona" yeye aliyetoka kwenye Maombi anajibu "Mimi siwezi kupona" huyo hawezi kweli kupona maana hana Imani ya kupona.
Kumbuka bila Imani kubwa huwezi kumpendeza MUNGU wa Mbinguni.
Waebrania 11:6 "Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye MUNGU lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao."
6. Kuomba kwa tamaa.
Yakobo 4:3 "Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu."
✓✓Wengi huomba wakipata wanamwacha YESU KRISTO na kuendeleza anasa za Dunia, huwezi kupata mpenyo kama Nia Yako ni hiyo.
◼️Na Kumbuka hata kama kwa Sasa huna Nia mbaya ndani Yako lakini MUNGU hujua wazo la Mtu kutokea mbali.
Zaburi 139:2 "Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali."
MUNGU anaweza kuja akikubariki Sasa Miaka 20 ijayo wazo lako la ujinga litaanza kazi hivyo anaweza asikupe hitaji hilo ili usije baadae ukamwacha.
✓✓Wengi hufanya Maombi ili wapate Kisha wawakomeshe watesi wao, huwezi kupokea.
7. Kutokuvaa silaha za MUNGU.
Waefeso 6:11 "Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani."
✓✓Silaha za MUNGU ni nyingi kubwa silaha hizo ni Neno la MUNGU ni silaha,Jina la YESU KRISTO ni silaha, Imani ni Silaha, tumaini kwa MUNGU ni silaha, Maombi ni silaha n.k
8. Kutokuwa na nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Mithali 24:10 "Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache."
✓✓Zihitaji kwanza nguvu za ROHO MTAKATIFU, yaani badili maombi yako.
Zaburi 105:4 "Mtakeni BWANA na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote."
9. Kuomba nje na mapenzi ya MUNGU.
1 Yohana 5:14 "Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia."
✓✓Ukiomba kitu ambacho ni nje na mapenzi ya MUNGU huwezi kupata mpenyo.
Mfano unaomba MUNGU akupe Wewe kuwa rais wa Nchi wakati huu na wakati huo MUNGU ameshamweka tayari kwenye ulimwengu wa roho Mtu Mwingine kwenye nafasi hiyo ujue hata ukiomba hadi ujichane na Wembe huwezi kupokea kwa sababu uko kinyume na MUNGU, huwezi kupata mpenyo.
Mfano unaomba kwa Imani na kwa Kufunga kwamba mlima Kilimanjaro uhamie Tabora, hapo umeomba kinyume na mapenzi ya MUNGU.
Uko katika Maombi kwamba Mtu fulani afe, kama MUNGU ametaka aishi Mtu huyo ujue unaomba kinyume na mapenzi ya MUNGU hivyo hutaona Matokeo kamwe.
10. Pambana na nguvu za giza zilizokufunga au zilizofunga anga lako, au ufahamu wako, au ardhi ya mahali ulipo au zinazokuondolea utulivu na uwepo.
Luka 10:19" Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru."
✓✓Wakati Mwingine Ukiona huna dhambi, una YESU KRISTO na mambo hayo hapo juu yote uko vizuri nayo mbele za MUNGU basi badili Maombi, pambana na nguvu za giza zinazokuzuia.
Kumbuka umepewa mamlaka na Bwana YESU KRISTO hivyo itumie mamlaka hiyo katika Maombi.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na whatsapp).
Ubarikiwe sana.
Comments