Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
✓✓Ni vyema sana kila mtu akautambua wakati wake uliokubalika.
Upo wakati uliokubalika wa namna nyingi na kwa ajili ya mambo mengi.
✓✓Kuna wakati uliokubalika kwa ajili ya mavuno.
Mathayo 24:32-33 " Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu; nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni."
Usipofanyia kazi wakati wa mavuno, huo wakati ukipita hutaweza kuvuna au hutavuna mazao bora.
Kuna wakati wa Kuokoka, huo wakati upo Sasa na ni wakati Muhimu sana.
Baadhi ya watu hawakuujua wakati huo uliokubalika kwa ajili ya Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako hivyo walipoondoka Duniani hawakwenda Mbinguni Bali walienda kuzimu.
Ndio maana Biblia hapo juu inasema
"tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni." Yaani YESU KRISTO yu Karibu hivyo ni vyema kila Mtu akampokea kama Mwokozi wake haraka bila kuchelewa.
Kwanini ni Muhimu kuutambua wakati uliokubalika?
✓✓Usipoutambua wakati wako uliokubalika unaweza kujikuta unapata hasara maana hukuujua wakati wako uliokubalika.
Luka 19:44 "watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako."
✓✓Waisraeli kipindi fulani MUNGU aliwapa Neema ya kuutambua wakati uliokubalika kwao kwa Kujus kwamba kuna Mtumishi Wamepewa kwa majira hayo
1 Samweli 3:20 "Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa BWANA."
✓✓Walipomtambua Mtumishi waliyepewa kwa majira hayo walimshirikisha mengi na walisaidika mengi sana, walishinda Maadui zao na walistawi sana.
Vipi Wewe unayesoma somo hili, vipi kama MUNGU amekupa Mtumishi wake mwaminifu ili awe msaada kwako katika Mambo yote ya kiroho ili ufanikiwe na Wewe unamdharau Mtumishi huyo?
Hakika hutafanikiwa ndio maana ni Muhimu sana kuutambua wakati uliokubalika na kutambua wale watu Muhimu ambao MUNGU amekuletea katika Wakati wako uliokubalika.
Waisraeli wasingemtambua Samweli kwamba ndiye Nabii katika Wakati wao uliokubalika wangeteseka sana Tena kwa mengi.
◼️Usipotambua wakati wako uliokubalika ni vigumu kufanikiwa na ni rahisi kupata madhara.
Farao mmoja Kuna kipindi hakuutambua wakati hadi Watumishi wake wakamjulisha wakati huo kwamba ni wakati wa Misri kuharibika maana MUNGU wakati huo Yuko na Israeli.
Kutoka 10:7 "Ndipo watumishi wa Farao wakamwambia, Mtu huyu atakuwa tanzi kwetu sisi hata lini? Wape hawa watu ruhusa waende zao, wamtumikie BWANA, Mungu wao; hujatambua bado ya kuwa Misri imekwisha haribika?"
Farao huyu hata baada ya kujulishwa wakati huo ni wakati gani alidharau akidhani atawatesa Waisraeli kama alivyozoea zamani Matokeo yake akapigwa mapigo 10 na MUNGU na jeshi lake likafia baharini.
Ndugu yangu unayesoma somo hili, Mimi Peter Mabula Niko hapa leo kukujulisha rafiki yangu kwamba utambue wakati wako uliokubalika.
Namfahamu Mtu mmoja ambaye wakati wake uliokubalika wa kuoa alidharau akijua hata baadae ataoa maana anaamini hakuna msichana wa kumkataa katika Makanisa yote kwenye eneo lile.
Katika Wakati wake uliokubalika MUNGU alisema naye na akamjulisha na Binti wa kumuoa ila Kijana akakataa. Baada ya Miaka 2 akataka Sasa aoe jambo la ajabu kila Binti anayemfuata yule Binti anakataa, jamaa alijiona mzuri sana lakini hakuna Binti aliyekuwa na mpango naye wakati huu, Kijana baada ya kutafuta Makanisa kadhaa akakosa akaamua kuhamia Mji Mwingine na huko akakosa, akasema "Ngoja nitafute hata mpagani nioe" hata huyo mpagani akakosekana.
Baadae akagundua kwamba alidharau wakati wa MUNGU uliokubalika na akagundua alilikataa kusudi la MUNGU ndipo akatubu na kurudi kule kule kwa yule Binti wakafunga Ndoa.
Ninachotaka kukuonyesha ni nini?
Ilipita Miaka zaidi ya 5 ya kuhangaika tu.
Maana yake usipojua kuutumia vizuri wakati wa MUNGU uliokubalika unaweza kupoteza muda na kupata hasara.
Kuna Mtu mmoja anaitwa Labani siku Moja akagundua uwepo wa Yakobo pale nyumbani kwake ulikuwa ni wakati wa MUNGU uliokubalika kwa ajili ya Baraka zake maana alibarikiwa sana.
Mwanzo 30:27 "Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba BWANA amenibariki kwa ajili yako."
Katika majira hayo Labani angemfukuza Yakobo siku tu anafika angekuwa anaifukuza baraka yake.
Hata Wewe Inawezekana umewahi kufukuza baraka zako kwa kutokuutambua wakati wa MUNGU uliokubalika.
◼️Upo wakati mwingi uliokubalika ambao ukiufanyia kazi katika kusudi la MUNGU utapata faida.
✓✓Tunajua kwamba kila jambo lina wakati wake hivyo ukiujua wakati wako huu na ukajua inakupasa kufanya nini katika MUNGU ujue utafanya vyema na kupata faida njema.
Mhubiri 3:1" Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu."
✓✓Unajua wakati huu kwako ni wa kufanya nini kulingana na mbingu?
Ukijua unatakiwa ufanye nini katika wakati huu basi ukifanya jambo hilo jema utapata faida.
◼️Kama wakati wako kumtumikia Bwana YESU KRISTO ni huu basi mtumikie MUNGU kwa uaminifu na juhudi, ukipita wakati huu ujue baadae itakuwa vigumu kutumika kwa viwango.
✓✓Kuna wakati wa mtu kufunga ndoa, ukipita huo wakati inaweza ikakusumbua sana baadae wewe kufunga ndoa.
✓✓Kuna ajira zinahitaji umri fulani tu kuajiriwa, umri huo kwako ukipita ujue hutaweza kuipata ajira hiyo tena, hata kama unaipenda sana kazi hiyo.
✓✓Kuna wakati wa kufunga na kuomba sana maana baadae unaweza ikakosa nafasi kama uliyonayo sasa, itumie vyema nafasi ya sasa.
✓✓Kuna wakati usipoutumia vyema kwa kusudi la MUNGU ujue mbeleni unaweza kupata hasara, kwa maana hukuujua wakati uliokubalika kwako.
Mfano kuna watu walipata nafasi za kuokoka ila wakakataa kuokoka kisha baada ya hapo wakafa katika dhambi na kuukukosa uzima wa milele.
Ndugu, Biblia iko wazi sana kwa hilo
2 Wakorintho 6:2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)
Je unajua wakati huu kwako ni wakati wa kufanya nini kulingana na mbingu?
◼️Ndugu tafuta kujua majira hayo kwako kulingana na mbingu inakupasa kufanya nini katika KRISTO.
✓✓Wakati mwingine unaweza kuwa na msukumo rohoni wa kufanya jambo fulani jema la ki MUNGU, usipofanyia kazi na majira haya yakipita ujue baadae utataka kufanya jambo hilo usiweze maana majira yanakuwa yamepita.
Ndugu hakikisha unautambua wakati huu kiroho kwako unatakiwa ufanyeje.
◼️Ukiutambua wakati wako katika MUNGU ujue hakuna kitu kitakachoharibika .
✓✓Ukiyatambua majira yako katika MUNGU na ukayatumia vyema majira hayo ujue hutapata hasara.
◼️Kila jambo duniani limewekwa kwa majira yake, muhimu tu hakikisha majira yako yote upo katika KRISTO kwa utakatifu ili usipate hasara.
Mhubiri 3:2-6 "Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia;
Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa;"
✓✓Kama ambavyo kulikuwa na wakati wako wa kuzaliwa basi hata wakati wa kufa pia upo, tatizo sio kufa ila muhimu je umejiandaaje baada ya kifo?
Wenye akili humpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao ili baada ya duniani iwe uzima wa milele na sio jehanamu.
Yohana 3:35-36 " Baba(MUNGU) ampenda Mwana(YESU), naye amempa vyote mkononi mwake. Amwaminiye Mwana(YESU) yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana(YESU) hataona uzima, bali ghadhabu ya MUNGU inamkalia."
Je unautumiaje wakati wako huu mfupi wa kuishi duniani?
Wakati wa kuishi duniani ni mfupi sana ukilinganisha na milele ijayo, hata kama utaishi miaka 100 duniani basi hiyo ni wakati mfupi sana ukilinganisha na milele ijayo.
Ndugu majira haya unayafanya nini?
Kila jambo lina majira yake, unajua unatakiwa ufanye nini sasa katika KRISTO?
✓✓Kuna wakati wa kupanda ili kuuruhusu kuja wakati wa kuvuna, usipoutumia wakati huu kupanda ujue baadae hutavuna chochote maana hawezi kuvuna kama hukupanda.
✓✓Kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka, ni heri kuutumia wakati huu kwa kulia mbele za MUNGU kwa maombi ili uje na wakati wa kucheka baadae baada ya MUNGU kujibu maombi yako.
Kuna watu pia sasa wanacheka katika shetani kwa kushiriki mambo ya kishetani, watu hao wanacheka sasa ili waje walie jehanamu kwa sababu ya dhambi zao, ndugu naomba usiwe wewe.
Utumie wakati wako huu katika KRISTO YESU kwa utakatifu.
◼️Ukiutambua wakati wako wa kuishi kwamba unatakiwa uokoke na uishi maisha matakatifu ujue baada ya kufa kuna uzima wa milele.
✓✓Ukiujua wakati wa kupanda na ukautumia kupanda ujue utapata wakati wa kuvuna, wasiojua wakati wa kupanda ujue hawatapata wakati wa kuvuna.
Kwa kila jambo kuna majira yake.
Mhubiri 3:1 ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu."
✓✓Usipoujua wakati wa kung'oa mapando ya giza katika maisha yako, ndoa yako, familia yako au nyumba yako, usipong'oa mapando hayo ya shetani ujue utakuja baadae uharibifu, na wakati huo utakuwa umechelewa au itakubidi utumie nguvu nyingi sana ndipo upate ushindi.
✓✓Ndugu utambue wakati wa kutafuta ili upokee na hiyo itakusaidia kubaki na kitu hicho ulichopokea na kukusaidia hata wakati majira hayo yamepita.
Mimi nakushauri kwa wakati huu tumia muda wako mwingi zaidi kuutafuta ufalme wa MUNGU.
Mathayo 6:33 "Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa."
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili,whatsapp, ushauri n.k).
Ubarikiwe
Comments