MAKUNDI MANNE(4) YA MAOMBI YA UFUNUO KUOMBEA MWILI WAKO KIROHO.

 
Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Huu ni ufunuo ambao Mimi Peter Mabula nilipewa, ukipenda fanyia kazi ki maombi na mwili wako utakuwa salama kiroho.

Napitia tu dondoo katika somo hili na siku moja nitafafanua vyema hadi kitabuni.

1. KUNDI LA KWANZA LA MAOMBI YA KUOMBEA MWILI WAKO.

◼️Kwa njia ya maombi kataa kuitwa na wachawi kwenye ulimwengu wa roho.

1 Samweli 28:11 "Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekupandishia? Naye akasema, Nipandishie Samweli."

Maandiko haya yanaonyesha Sauli alikwenda kwa mganga wa kienyeji na kisha kumwambie yule Mganga/mchawi amwite pale Nabii Samweli kiroho na ikawezekana.

✓Wapo watu huota ndoto akiona yuko katikati ya kikao cha kipepo na wanayomfanyia huko kwenye ulimwengu wa roho yanakuja kutimia katika ulimwengu wa mwili.

◼️Leo kwa Jina la YESU KRISTO kataa kuitwa kichawi mahali popote.
Omba katika Jina la YESU KRISTO na hutaitwa Tena kichawi.

Dada mmoja siku moja ndotoni alijiona yuko baharini na kuna kikao cha wakuu wa giza, wakapanga mipango mibaya kisha mmoja akamtuma nyoka na nyoka yule akaambiwa aingie ndani ya tumbo la Dada yule na kuwa uvimbe, nyoka akaingia mdomoni kwa Dada hadi tumboni. Dada yule aliloamka asubuhi alidhani ni ndoto tu ila kuanzia siku hiyo akaanza kuumwa sana uvimbe tumboni.

Dada mmoja alijishangaa ndotoni akijiona yuko kuzimu na mzimu wa ukoo ukimwambia kwamba hiyo mimba aliyonayo wanaitoa maana wao ndio wasimamizi wa ukoo wao na aliyewakaribisha kwenye ukoo ni Baba wa ukoo huo aliyefanya matambiko na kuukabidhi ukoo mzima kumilikiwa na mkuu wa kuzimu mmoja.

Katika andiko tunaona Mtumishi wa MUNGU akiitwa kwa mganga na anatokea, hata kwako inawezekana kuitwa na mawakala wa shetani na wewe unaona matukio hayo ndotoni huku hujui jinsi ya kuomba ili kuharibu nguvu hizo za giza.

Nina mifano hai mingi sana kutoka kwa watu ninavyowasiliana na watu wengi na kuwaombea na kuwashauri.

Dada mmoja alipokuwa anamaliza kusoma degree ya pili aliona ndotoni yuko mahali na mawakala wa shetani wameshikilia vyeti vyake wakisema "Hatukumzuia kusoma ila tunamzuia kupata kazi" kisha vyeti vyake wakavichovya kwenye vitu kama vinyesi na wakamrudishia vyeti, akatoka ndotoni lakini tangu muda huo hajawahi kupata kazi.

Mtu mmoja baada ya tu kufunga ndoa akaota yuko sehemu amezungukwa na mawakala wa shetani kisha wakamwibia pete yake ya ndoa, tangu wakati huo ndoa yake haiko sawa.

Kuna mtu aliota akiwa amekalishwa mahali kwenye kikao cha wachawi akapigwa mapigo na kesho katika hali ya mwili ni kweli akakutana na mapigo hayo ya kichawi.

✓✓Ndugu ukiona mipango ya kipepo dhidi yako ndotoni omba ukiiharibu hiyo maana wakati mwingine hawawezi kukudhuru live, hivyo wanakuita na kukudhuru kwenye ulimwengu wa roho na utashangaa usipomkimbilia YESU KRISTO Mwokozi inakuwa vilevile kama ulivyoona.

Ndugu zingatia hii.

A. Futa sumu za kishetani ulizowekewa ndani yako, futa kwa kutumia damu ya YESU KRISTO ya agano jipya.

B. Haribu vifungo vyote ulivyofungwa na mawakala wa shetani.

C. Futa kila kilicho mwilini mwako chenye muunganiko na nguvu za giza.

Kuna mifano mingi sana ya watu jinsi walivyoitwa kwenye madhabahu za giza na yakawapata yaliyopangwa na wakuu wa giza.

Leo omba maombi haya.

✓✓ Katika Jina la YESU KRISTO kataa kuitwa popote kwenye ulimwengu wa roho wa giza.

 ✓✓Katika Jina la YESU KRISTO Omba nyumba yako iwe moto kwa wote wanaotumia nguvu za giza.

Obadia 1:18 "Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa BWANA amesema hayo."

✓✓Omba MUNGU akufanye kuwa mwali wa moto kwa mawakala wa shetani.

Hata wakikuita wataona moto tu ukiwaunguza.

Zaburi 104:4 "Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali."

✓✓ Futa vikao vya kipepo vinavyokaa kukujadili wewe kwa lolote.

Isaya 54:15 "Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako."

2. KUNDI LA PILI LA MAOMBI YA KUOMBEA MWILI WAKO.

◼️Osha/takasa mwili wako kwa damu ya YESU KRISTO.

Zaburi 51:2 "Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu."

✓✓Kumbuka kinachoweza kukuosha, kukutakasa na kukusafisha na damu ya YESU KRISTO pekee, hivyo hakikisha umeokoka na omba maombi haya ya kutakasa mwili wako ili usitumiwe kivyovyote na shetani.

1 Yohana 1:7 " bali tukienenda nuruni, kama yeye(MUNGU) alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote."

✓✓Kwa maombi uweke wakfu mwili wako ili utumike na MUNGU na sio kutumika na shetani.

✓✓Weka agano na damu ya YESU KRISTO katika mwili wako.

3. KUNDI LA TATU LA MAOMBI YA KUOMBEA MWILI WAKO.

◼️Ondoa alama za kipepo katika mwili wako na sasa vaa chapa za KRISTO ndani ya mwili wako.

Wagalatia 6:17 "Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake YESU."

Ninaposema chapa za KRISTO sina maana ya mikufu au rozali au bangili za kidini au vitambaa vya upako au joho lolote la kitumishi au chochote avaacho mtu yeyote mwilini, vitu hivyo sio chapa za KRISTO katika mwili wa Mkristo.

✓✓Chapa za KRISTO ni alama ya kuwa mwanafunzi wa YESU KRISTO anayetimiza kusudi la MUNGU duniani.

4. KUNDI LA NNE LA MAOMBI YA KUOMBEA MWILI WAKO.

◼️Funga milango ya adui kuvamia mwili wako kiroho.

Mathayo 16:18 " Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.''

Kumbe huwa kuna milango ya kuzimu.

✓✓Ndugu ifunge milango yote ya kuzimu iliyofunguliwa katika maisha yako, Ifunge kwa Maombi katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi.

✓✓Wewe ni Kanisa na milango ya kuzimu haitakiwi kukushinda.
Funga mlango huo kwa maombi katika Jina la YESU KRISTO.

✓✓Hata maombi ya kuambatanisha na sadaka kama una ufunuo huo au msukumo huo Fanya Wala usiache maana utauona ushindi mkuu wa MUNGU.

Unaweza pia kuwa na maombi ya kufunga.
Unaweza kumshirikisha Mchungaji wako au Mtumishi wa kweli wa Bwana YESU unayemwamini aliye mwombaji.

Kwanini nasema kuhusu kanuni hizo za maombi?

✓✓Ni kwa sababu mlango wa shetani kuingia kwako, mlango huo unaweza kuwa jina lako ulilopewa na wazazi na kumbe lilitoka kwenye madhabahu za giza wao waliambiwa tu na Bibi au Babu wakuite jina hilo, kama ni hivyo jina hilo linatakiwa kutakaswa kwa damu ya YESU KRISTO, linahitaji ubatizo wa kiroho.

✓✓Mlango unaweza kuwa ni kazi, ardhi unayokaa ikiwa na vitu vya kishetani n.k

Milango hiyo ni mingi wakati mwingine hivyo omba na hata ombewa inapobidi.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili,whatsapp, ushauri n.k).
Ubarikiwe.

Comments