![]() |
Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu ujifunze kitu kutokana na maswali ambayo baadhi ya rafiki zangu waliniuliza kisha nikawajibu, naomba majibu ya maswali hapa chini yamsaidie kila mmoja ambaye anahusika. Pia wapo watu wengi sana wamewahi kuniuliza maswali na sikuwajibu, kama ni wewe sikukujibu subiri, siku moja nitakujibu au watumishi wengine watakujibu.
Mbarikiwe wote.
1. Swali la kwanza.
Bwana Yesu asifiwe Mtumishi wa Mungu, samahani Mtumishi wa Mungu, naomba kuuliza swali,samahani mtumishi wa Mungu, kama ulikuwa unamwomba Mungu swala la Mume na akakuonyesha huyo mwanaume katika ulimwengu wa Roho na kwa watu wengine wawili tofauti mwanaume huyo huyo,na huyo mwanaume akaona katika ulimwengu wa Roho kama mimi nilivyoona,na akaja katika ulimwengu wa damu na nyama,halafu huyo mwanamume mimi nimemzidi umri sasa hapo swali langu mtumishi wa Mungu, sasa hapo utaingia tena kwenye maombi ya kumwomba Mungu akuletee mwanaume aliyekuzidi umri au unatakiwa kukubaliana na hilo kusudi la Mungu, naomba unisaidie kiroho nisikosee,asante mtumishi wa Mungu
◾MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.
MUNGU akubariki sana.
✓✓Kama ni MUNGU amesema basi funga ndoa na mtu huyo.
✓✓MUNGU akisema anakuwa anajua kila kitu hivyo hakuna tatizo kama ni MUNGU amesema, ila iwe ni kweli aliyesema na MUNGU.
✓✓Ukilifuata kusudi la MUNGU na kuitii sauti yake basi hutapata hasara hata moja na huyo mwenzi wako hatapata hasara hata moja.
✓✓Itii sauti ya MUNGU kama yeye MUNGU amekupa huyo.
Kuna kaka mmoja alifufuliwa kwamba dada fulani ndiye mkewe, yule kaka akafurahi lakini baadae alipomwendea dada husika ili wafunge ndoa alishangaa pale alipokuta yule dada amewahi kuzaa, kipindi hajaokoka.
Kaka huyo alinitafuta kwenye simu akisema kwamba hawezi kuoa mwanamke ambaye ameshazaa, ilimsumbua sana hali hiyo, ila ukweli ni kwamba sio kweli kama mtu ambaye amewahi kuzaa hafai kuwa mke mwema au mume mwema, sio kweli kwamba mtu aliyekuzidi umri hafai kuwa mke mwema au mume mwema.
Kama MUNGU amesema basi fuata sauti ya MUNGU maana hutapata hasara, kama MUNGU hajasema basi omba sana kisha chagua ukifuata amani ya KRISTO ndani yako.
Mke mwema au mume mwema hahusiani na umri bali tabia njema, utakatifu na kuwa na hofu ya MUNGU.
Ubarikiwe
2. Swali la pili
Shalom Mtumishi Mabula.
Nimesoma somo linasema kuombea watoto na kutoa sadaka kwa ajili yao, sasa mimi nilitaka kujua hivi kutoa sadaka kwa ajili ya watoto au kwa niaba ya watoto natoaje? Naomba unifafanulie.
Nimesoma somo linasema kuombea watoto na kutoa sadaka kwa ajili yao, sasa mimi nilitaka kujua hivi kutoa sadaka kwa ajili ya watoto au kwa niaba ya watoto natoaje? Naomba unifafanulie.
◾MAJIBU YA MTUMISHI MABULA.
Ubarikiwe.
✓✓Unapowatolea sadaka watoto wako unakuwa unawakabidhi watoto wako kwa MUNGU kupitia sadaka kwa ajili yao.
✓✓Sadaka humfanya mtu kumilikiwa na madhabahu, ndio maana kuna waliotoa sadaka kwa madhabahu za giza kwa ajili ya watoto wao na baadae watoto hao kwa sababu wanamilikiwa na madhabahu za giza basi watajikuta wanafanya mambo ya kishetani yaliyotengenezwa na hiyo madhabahu ya giza ambapo ni wazazi wao waliwakabidhi huko kwa sadaka.
Kuna familia au ukoo kila mtoto wa kiume ni mlevi kwa sababu ya madhabahu za giza za ukoo, kuna familia au ukoo wanaume wote wanaona wake zaidi ya mmoja kwa sababu ya madhabahu ya giza za ukoo na madhabahu hizo zilikuja na kupata nguvu kwa sadaka.
◼️Wewe watolee watoto wako sadaka kwa MUNGU katika KRISTO YESU ili madhabahu ya kiroho ya MUNGU aliye hai iwatetee na baadae watajikuta wana adabu njema na wakiwa hawaambatani na mambo ya kishetani.
✓✓Hivyo ukitoa sadaka kwa MUNGU kupitia watumishi wake waaminifu ujue Umewakabidhi watoto wako katika madhabahu ya kiroho ya MUNGU hivyo baadae watajikuta wanamtumikia MUNGU na kumpendeza.
Sadaka ina kazi nyingi mno.
✓✓Ushauri wangu ukitoa sadaka mtolee kila mtoto wako sadaka yako ili mtumishi amuombee kila mtoto kivyake akimwambatanisha na madhabahu ya MUNGU katika ulimwengu wa roho, hivyo utashangaa baadae watoto wako hawafanyi mambo ya ajabu maana wanamilikiwa na madhababu ya MUNGU.
Wapo watu pia wamekabidhi watoto wao kwa shetani kupitia sadaka/kafara walizotoa kwa mawakala wa shetani.
✓✓Hivyo Ukisikia msukumo wa kutoa sadaka kwa ajili ya kila mtoto wako fanya hivyo na hapo utakuwa Unawakabidhi kwa MUNGU.
Sadaka hutengeneza agano na MUNGU,
Zaburi 50:5 "Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu." hivyo unaweza kutoa sadaka kwa ajili ya watoto wako na hivyo madhabahu ya MUNGU itawafuatilia baadae kwa ajili ya kusudi la MUNGU lililopo kulingana na sadaka na maombi ya mtumishi mwaminifu wa KRISTO aliyeomba maombi sahihi.
Ayubu alikuwa anatoa sadaka kwa ajili ya kila mtoto wake, unaweza ikafanya hivyo na wewe, sadaka zina maana sana kwenye ulimwengu wa roho, na zina nguvu sana.
Ayubu 1:5 "Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote."
✓✓Hata kama watoto wako ni wakubwa sasa na hukuwahi kufanya hivyo, Ukisikia msukumo rohoni kutoa sadaka kwa ajili yao unaweza kufanya hivyo pia.
Unaweza kuwatolea sadaka watoto wako kama Ayubu alivyofanya.
Elikana alikuwa anahakikisha ipo sadaka kwa ajili ya kila mtoto wake na mke,
1 Samweli 1:4 "Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao;"
✓✓Unapotoa sadaka kwa MUNGU kuhusu mtoto wako unakuwa unaruhusu baraka za MUNGU zilizo ndani ya sadaka husika zifanye kazi.
✓✓Ibrahimu alipotoa sadaka ya kondoo baraka zilizokuwa ndani ya sadaka hiyo zilileta baraka za ajabu kwa watoto wake, baraka mojawapo ni kwamba watoto wa Ibrahimu wamiliki milango ya adui, hiyo ni baraka ya MUNGU iliyokuwa ndani ya sadaka ya Ibrahimu.
Mwanzo 22:13-18 "Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire,kama watu wasemavyo hata leo,Katika mlima wa BWANA itapatikana. Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu."
✓✓Ni jambo la maana sana kutoa sadaka kwa MUNGU kwa ajili ya kila mtoto wako maana adui hatawashikilia.
3. Swali la tatu.
Bwana Yesu asifiwe mtumishi Mabula.
Unaweza niambia maana ya kukesha, au Biblia inaposema kesheni mkiomba inataka tukeshe masaa mangapi?
Unaweza niambia maana ya kukesha, au Biblia inaposema kesheni mkiomba inataka tukeshe masaa mangapi?
MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.
✓✓Biblia inaposema kesheni mkiomba maana yake muwe na maombi ya kila mara.
✓✓Kukesha ina maana ya kuwa macho kiroho na kimwili kwa muda fulani huku ukiutumia muda huo kuomba mbele za MUNGU katika KRISTO YESU.
Maombi ya kukesha ndio maombi ya muda mrefu.
Maombi ya kukesha huanza na kuomba saa moja nzima na kuendelea.
Mathayo 26:40 "Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?"
Kwa hiyo ukiomba kuanzia saa moja mfululizo na kuendelea kwa muda uuwezao hapo uko kwenye maombi ya kukesha.
Kuna watu huwa na mikesha ya masaa 6 wengine masaa 12 wengine masaa 7 n.k
Ni muhimu kila Mkristo kuwa na maombi ya kukesha.
Ubarikiwe
4. Swali la nne.
Shalom mtumishi, hongera kwa kazi ya MUNGU, nimekuwa nikikufatilia katika group lako hakika naona kupitia wewe MUNGU anainuliwa, kutoka kwako mtumishi naomba utoe unabii juu ya maisha yangu.
◾Majibu ya Mtumishi Peter Mabula baada ya hitaji hilo gumu.
Ni vigumu mimi kutoa unabii maana mimi sio nabii au sijafunuliwa chochote kuhusu wewe ila kanuni ya Kibiblia ni kila mtumishi wa MUNGU kuwabariki wateule wa KRISTO wenzake hivyo ombi langu kwa MUNGU ni kwamba akutendee haya mambo 6 sawasawa na Neno lake takatifu.
Hesabu 6:24-26 " BWANA akubarikie, na kukulinda;
BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani."
Mbarikiwe sana wote mliojifunza kitu leo.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU Baba wa mbinguni.
Comments