MASWALI NA MAJIBU(sehemu ya 13)

By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Haya ni baadhi ya maswali ambayo baadhi ya marafiki zangu waliniuliza nami nikawajibu.

1. Swali la kwanza.

Bwana Yesu asifiwe mtumishi Mabula, ubarikiwe kwa vipindi vizuri,
Nina swali
sijajua kama uliwahi kuulizwa swali kama hili
Ambalo nataka kukuliza
swali hili!!
Je kijana wa kiume anapochumbia binti akakubaliwa halafu anaenda kuchumbia sehemu nyingine zaidi ya 4 hadi tano na kati ya hizo chumba
Anazifuatilia zote
Hapa inakuwaje??
Cha ajabu kijana huyo kaokoka
Nini kina mfikishia kuwa na tatizo hilo??

◾MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.

✓✓Haitakiwi kuchumbia sehemu zaidi ya moja.

✓✓Hivyo kijana wa kiume akitaka kuchumbia basi achumbie sehemu moja tu.

✓✓Hata binti asikubali kuchumbiwa na wanaume wawili tofauti.

✓✓Yaani kifupi ni kwamba mwanamke au mwanaume yeyote ambaye hajaingia katika ndoa usikubali kuwa na wachumba wawili.

Biblia inasema ndio ya wateule na iwe ndio maana yanayozidi hapo yanaweza kuleta hukumu.

Yakobo 5:12" Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu."

Lakini pia inawezekana kabisa una mchumba mmoja lakini ukagundua hutaweza kuingia naye katika ndoa baada ya wewe kupata mtazamo mpya kuhusu huyo, basi Unachotakiwa kufanya ni kumweleza na kuvunja kwanza uchumba huo kabla ya kuanzisha uchumba mwingine sehemu nyingine.

✓✓Lakini usimwache mtu kwa siri kisha ukachumbiana na mwingine, hayo ni makosa.

✓✓Ushauri wangu, usiwe katika ahadi za kufunga ndoa na watu wawili kwa wakati mmoja.

✓✓Unapompenda binti fulani au kijana fulani jiridhishe kwanza ndipo uingie kwenye uchumba naye katika hali takatifu ili usije ukaghairi katika wakati ambao utamuumiza.

◼️Lakini pia kijana mwenye akili na binti mwenye akili hawawezi kukutana kimwili kabla ya ndoa.

✓✓Ukiona mchumba kaachwa na akaumia sana ujue asilimia kubwa amewahi kukutana kimwili na huyo anayemwacha.

✓✓Kwa mwanamke wenye akili na mwanaume mwenye akili timamu za kiroho hawezi kukutana kimwili na mchumba wake, hivyo mtu wa aina hiyo hata akiachwa na mchumba katika ya mahusiano hawezi kuumia sana maana hawajawahi kukutana kimwili, lakini waasherati ndio hao hata hutaka kujiua au kujidhuru au kudhuru watu na kujikuta katika vyombo vya dola.

Hivyo ingawa unaweza kumwacha mchumba wako ambaye umegundua sio mtu mzuri, basi mweleze kwanza na vunja uchumba kwanza ndipo uanze uchumba kwingine.
Ubarikiwe

2. Swali la pili.

Bwana Yesu asifiwe baba!
Wakati nasikiliza haya maombi yako uliyotuma kwa audio nimeona Mbwa wawili, huyo mbwa mmoja amekonda amepukutika manyoya na huyo mwingine mkubwa anafuatilia kama wanaulizana kitu lakn wanaondoka! Nimeshangaa nikajiuliza nini Maana yake Mtumishi!

◾MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.

Hayo maono ya kuona mbwa katika hali hiyo maana yake ni hii.

1. Mbwa aliyekonda ni roho ya uzinzi ikiambatana na magonjwa ya zinaa, hasa ukimwi.

✓✓Hivyo usikubali kamwe kufanya uzinzi au uasherati maana shetani anakuandalia na ukimwi pia kupitia hiyo dhambi ukifanya.

Ninao ushuhuda pia katika hilo.
Dada mmoja aliota mpya aliyekonda akimfuata, wiki hiyo hiyo alifanya uasherati na kuaambukizwa ukimwi, alipojikuta na ukimwi ndipo akaanza kuuliza maana ya ndoto hiyo kama inahusika na dhambi ya uasherati, akabaki akijuta.

◼️Wewe fanya maamuzi ya kujitenga mbali na kitu kinaitwa uzinzi na uasherati maana shetani kupitia dhambi hiyo anataka apitishe na magonjwa ya zinaa mubashara.

2. Mbwa mwingine ni roho ya uzinzi na ni roho ya mauti.

✓✓Muhimu uzinzi na uasherati huwa hauhitaji maombi sana ila unahitaji mtu husika kubadilika tabia kwa kumcha MUNGU katika KRISTO YESU na kujitenga mbali na uzinzi na uasherati.
Ubarikiwe.

3. Swali la tatu.

Bwana Yesu asifiwe Mtumishi!
Nina maswali haya,
Nikitubu dhambi zangu nitasamehewa? Je naweza kutubu kwa niaba ya yeyote? Je tukifa huwa tunakutana tunaojuana kwa mfano ndugu zangu waliokufa miaka mingi naweza kuwaona au kila mmoja atahukumiwa kadri ya matendo yake?
Je anapofariki mtu tunapomuombea anatuona au anatusikia?
Naomba unisaidie japo kidogo nielewe au unipe mistari nisome! Samahani kwa usumbufu.


◾MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.

Swali la kwanza.
◾Nikitubu dhambi zangu nitasamehewa?

◼️Ni kweli kabisa ukitubu dhambi zako katika KRISTO YESU unasamehewa.

Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

Swali la pili.
◾Je unaweza kutubu kwa ajili ya mtu mwingine?

✓✓Ndio unaweza kutubu kwa ajili ya mwingine ila aliye hai tu.

✓✓Mfano hai ni Musa alitubu kwa niaba ya Waisraeli na MUNGU akawasamehe kupitia toba ya Musa.

Hesabu 14:19-20 "Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa. BWANA akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa;"

Ukisoma pia Danieli 9:4-9 utaona Danieli akitubu kwa ajili ya Waisraeli.

Na hata katika Luka 23:34 utaona Bwana YESU akiwaombea msamaha kwa MUNGU watu waliomsulubisha.

✓✓Unapotubu kwa ajili ya mwingine maana yake ni ili mtu huyo avumiliwe na MUNGU maana atabadilika, ni ili mtu huyo asaidiwe kukaa kwenye kusudi la MUNGU.

✓✓Maombi ya kutubu kwa ajili ya mwingine hayawahusu wafu bali watu walio hai tu.

Mtu yeyote hawezi kuomuombea marehemu lolote na likafanyiwa kazi na MUNGU maana mtu husika anapokata roho tu kinachofuata ni hukumu na sio kingine chochote maana ukurasa wake duniani unakuwa umefungwa, hivyo kabla mtu hajamuombea aliyekufa ukurasa wa huyo aliyekufa unakuwa umefungwa duniani, kinachofuata ni hukumu ya MUNGU sawasawa na matendo yake .

Waebrania 9:27 "Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;"

Kutubu kwa ajili ya mwingine hakuna maana ya mtu huyo afutwe jina lake kwenye kitabu cha hukumu na jina lake liandikwe kwenye kitabu cha uzima, bali toba hiyo inaweza kufuta adhabu kwa mtu husika kama ilikuwepo adhabu, kutubu kwa ajili ya mwingine kunaweza kusababisha neema ya MUNGU kwa mtu husika ili aache tabia mbaya na aache mabaya na kuanza kutenda mema hata awe safi.

Ndio maana mfano unaweza kukuta familia ya Mchungaji au ya mtu wa MUNGU ambayo watoto wake wanatenda dhambi na machukizo mengi lakini MUNGU hajawapiga mapigo,

Yakobo 5:15-16 "Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na BWANA atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii."

Kumbe kwa sababu tu ya Baba yao au mama yao aliye vizuri na MUNGU na huwaombea watoto wake, siku Akifariki huyo mtu wa MUNGU ndipo utaona hatari kwa watoto hao maana hawakuadhibiwa kwa sababu tu ya muombaji aliyekuwa anawaombea na kutubu kwa ajili yao na hata kutoa sadaka kwa ajili yao.

✓✓Ni vyema kila mtu akafikia maamuzi binafsi ya kutubu kwa KRISTO na kuacha dhambi zote.

✓✓Ukitaka jina lako liandikwe kwenye kitabu cha uzima tubu mwenyewe na kuokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU.

Warumi 10:9-11 " Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika."

Swali la tatu.

◾Je ndugu zangu waliokufa zamani ninaweza kuonana nao baadae?

✓✓Kama mtu huyo alikuwa ameokoka na akamaliza safari yake katika Wokovu wa KRISTO, kisha na wewe umeokoka na unaishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU na ukamaliza safari ya duniani ukiwa unaishi maisha matakatifu basi mtaonana mbinguni.

Luka 16:22-23 " Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake."

Hapa tunaona watu wawili waliokufa na mmoja akapelekwa paradiso maana alikuwa anaishi maisha matakatifu na mwingine akapelekwa kuzimu kwa sababu alikuwa mwovu.

Nini nataka kusema?

✓✓Kama wewe ni mtenda dhambi na ukamaliza safari ukiwa dhambini basi hutamuona kamwe aliyeenda uzima wa milele.

✓✓Jambo la kujua ni kwamba kila mwanadamu akifa anaenda ama paradiso au kuzimu,
Paradiso wanaenda waliookolewa na Bwana YESU KRISTO na kuzimu wanaenda waliokataa YESU KRISTO kama Mwokozi wao na ambao hawakuishi maisha matakatifu ya wokovu hata kama waliitwa Wakristo.

✓✓hivyo kama ndugu yako Ameenda kuzimu na wewe unaenda paradiso ujue hutaonana naye.

◼️Wasaidie ndugu zako walio hai sasa ili wasiende jehanamu na wewe pia ishi maisha matakatifu ya Wokovu ili usiende jehanamu, bali uende mbinguni aliko YESU KRISTO Mwokozi wetu anayetuandalia makao.

Yohana 14:2-3 "Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo."

Swali la nne
Je mtu anapokufa, tukimuombea anatuona? au anatusikia?

✓✓Hakuna mtu aliyekufa hata mmoja anaweza kusikia maombi na wale walio duniani, hawezi kamwe kuona duniani.

✓✓Wanaoombea wafu huwa wanafanya hivyo kujifurahisha tu nafsi zao ila hakuna jibu hata moja la MUNGU kwa ajili ya aliyekufa.

◼️Biblia inasema mtu akifa kumbukumbu lake linasahaulika yaani linafutika.

Mhubiri 9:5-6 " kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua."

MUNGU awabariki sana wote mliofuatilia maswali haya na majibu yote.
pia kama uliuliza swali na haukujibiwa inawezekana siku moja Nitakujibu maana huwa natunza maswali ya watu kama yalivyo.
Mbarikiwe sana wote.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU.

Comments