![]() |
Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tena karibu sana ujifunze maarifa haya ya rohoni yatakayokupa akili ya rohoni na kuchochea msukumo ndani yako ili uombe na kufanikiwa.
Nini nataka ujue?
✓✓Kama mtu uliye na KRISTO YESU Biblia inataka ufanikiwe katika mambo yote katika ulimwengu wa roho na yadhihirike katika ulimwengu wa mwili.
3 Yohana 1:2 "Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo."
◼️Sasa kuna baraka haziwezi kuonekana katika macho ya kawaida, zimefichwa, zinahitaji tu hadi ROHO MTAKATIFU akupe akili na akufumbue macho ili uzione baraka hizo.
Isaya 45:3 "nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, MUNGU wa Israeli."
Biblia inaposema kwamba "hazina za gizani " maana yake zilikuwa zimefichwa au hazionekani hadi MUNGU tu katika KRISTO YESU akusaidie.
Inakuwaje hadi tunaweza kumaliza hata muda mrefu bila kuziona hizo baraka zitupasazo sisi, nani alizificha hata hatuzioni?
Jambo la kwanza nataka ujue hapa ni kwamba MUNGU hazifichi baraka zetu ila;
A. Dhambi zetu zinaweza kutufanya tusizione baraka hizo maana dhambi zitaondoa msaada wa MUNGU kwetu.
Isaya 59:1-2 "Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."
Na tunajua wazi kwamba sisi bila YESU hatuwezi kuweza chochote.
Yohana 15:5 "Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote."
◼️Hivyo kumkimbia MUNGU ni kuzikimbia pia baraka zake.
B. Tunapokaa mbali na MUNGU tutakosa akili sahihi na maarifa sahihi ya kutufanya tuzione baraka hizo hivyo zinakuwa kama zimefichwa machoni petu ni sisi ndio hatuko vizuri na MUNGU.
Mithali 1:7 "Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu."
C. Kuna wengine pia MUNGU hawapi kabisa hazina hizo za gizani yaani hizo baraka kwa sababu tu MUNGU anakuwa anajua akiwapa watamkimbia, hivyo MUNGU anaanza kuwajenga kwanza kiroho ili hata akija kuwapa baraka hizo, hizo baraka zisiwe tanzi kwao.
Mfano kuna watu leo ni matajiri sana au wameinuliwa sana, wana walinzi wengi na hawaonekani mitaani na Kanisani hawaendi, hawa hata wewe Mtumishi ukipewa ujumbe kwa ajili yao ili kuwaonya hutaweza kuwafikia maana mali zao na ufahari wao unawafanya wasisogelewe, hivyo hao baraka zao zimetengeneza jehanamu yao maana hawasikia ya MUNGJ tena hata wakatii.
Hivyo MUNGU anaweza kuzuia kwa muda baraka fulani kwa mtu fulani ili mtu huyo aongeze ukaribu na MUNGU hata afikie hatua ya kutokumwacha YESU hata akifanikiwa.
✓✓Ndugu ongeza kiwango cha kumpenda MUNGU katika KRISTO YESU.
Sasa kwanini baadhi ya watu wasio na YESU nao baadhi yao wamefanikiwa sana?
Jibu ni kwamba wengi zaidi wamefanikiwa sio katika MUNGU bali katika shetani.
Waliofanikiwa nje na MUNGU wengi wao ama wameingia katika mikataba ya kishetani au kwa sababu wako katika utawala wa shetani, aliye katika utawala wa shetani hufanya baadhi haya; kuiba ndipo anafanikiwa, kuuza vitu viovu mfano madawa ya kulevya, pombe, bangi nk ndipo anafanikiwa lakini ni vitu ama vibaya au pia vitu vya wizi au anafanya mchanganyiko, kufanya kazi isiyo halali au kuchanganya kazi halali na isiyo halali, kufanya biashara haramu, kufanya unyama fulani ili kufanikiwa, utapeli, ulaghai, Wengi wao wameenda kwa waganga, wanatumia kazi zao vibaya na vitu vingi sana vya kishetani.
Hawa Biblia inasema hivi juu yao " Siku zao hutumia katika kufanikiwa, Kisha hushuka kuzimuni ghafula. Walakini walimwambia MUNGU. Tuondokee; Kwani hatutaki kuzijua njia zako. Huyo -Ayubu 21:13-14
Hao ni wa kuzimu na sio mbinguni.
Kama ni ndugu zako au watu wa karibu yako waambie warejee kwa YESU sasa, waache ushetani na waache mambo mabaya.
Siku moja Mimi Peter Mabula nilienda kununua kitu dukani, nilienda nikiwa nimechelewa sana maana mwenye duka alikuwa anafunga, nilipomweleza aliingia ndani ya duka kunichukulia bidhaa hiyo maana tulikuwa na sherehe ya Vijana Kanisani na kitu hicho kilikuwa muhimu sana, wakati anaingia ndani ya duka nilichungulia nikaona kuna paka wengi mle na amewasha vitu, yaani kumbe huwa anafungia paka wengi dukani, nilishangaa mno na nilipopata kitu hicho niliomba sana.
Kuna watu wameloga ofisini kwao ili wawe na vibali n.k hizo ndizo baraka za kipepo.
Yaani kwa ujumla mtu aliyefanikiwa nje na MUNGU lazima kuna kitu kibaya cha dhambi alihusika nacho, ni wachache sana waliofanikiwa kwa juhudi njema au kwa kujaariwa elimu hata wakawa na kazi nzuri na bila kujihusisha na shetani, na hao naweza kusema ni neema ya MUNGU tu ilikuwa nao hata kama hawakumjua MUNGU.
✓✓Kumbuka shetani anamiliki baadhi ya hazina hivyo humgawia mtu anayemsujudia.
Mathayo 4:8-9 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia."
Shetani anamiliki hazina ila anahitaji wa kumsujudia ili baadae waende jehanamu.
Unajua maana ya kumsujudia shetani?
Waliofanikiwa katika shetani wote humsujudia shetani kupitia kazi zao hata wafanikiwe.
Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu alitupa akili sisi akisema " Ndipo YESU alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie BWANA Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.-Mathayo 4:10 "
Ndio maana Biblia pia inasema katika
Mithali 1:32 kwamba "Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza."
◼️Na wote katika KRISTO tunajua kabisa kwamba tunao maadui katika ulimwengu wa roho ambao kazi yao mojawapo ni kuzuia mafanikio kwetu.
Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."
Ngoja nikupe mifano hai kazaa ili uelewe ya kuwa hazina au baraka kufichwa na nguvu za giza.
Ukisoma katika Isaya 45:2-3 unaona MUNGU akimpa mtumishi wake hazina za gizani yaani baraka zilizokuwa zimefichwa.
Isaya 45:2-3 " Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, MUNGU wa Israeli."
Lakini ili MUNGU ampe mtumishi huyo hizo hazina unaona MUNGU akifanya mambo haya matatu.
1. Kupasawazisha mahali palipoparuza.
2. Kuivunja milango ya shaba.
3. Uyakatakata mapingo ya chuma.
Hivyo inawezekana hata wewe kuna baraka yako imefichwa na ulimwengu wa roho wa giza, ili ipatikane inakupasa uombe maombi ya kusawazisha, kuvunja milango ya shaba na kuyakata mapingo ya chuma.
✓✓Ndio maana leo nasema omba MUNGU akufumbue macho ya rohoni ili uzione baraka zako.
Mfano wa pili ni huu.
Mwanzo 21:19 "MUNGU akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana."
Ukisoma hii mwanzo 21 unaona kabisa Hajiri na Ishumaeli walikuwa karibia na kufa kwa sababu tu ya kukosa maji Maana walikuwa jangwani, ilifika kipindi Hajiri alijificha ili asimuone mtoto wake akifa, kilichofanyika kijana alimuomba MUNGU na MUNGU alichokifanya ni kumfumbua macho ndipo akakiona kisima wakapata maji.
Maji hayo yalikuwa ni baraka iliyofichwa hadi pale MUNGU alipojibu maombi kwa kumfumbua macho Hajiri.
✓✓Hata wewe inawezekana kuna baraka hadi ufumbuliwe macho na ROHO MTAKATIFU ndipo utaziona baraka hizo na kuzipata.
✓✓Kuna watu ni baraka kwako ila huwajui au unawadharau, omba ufumbuliwe macho ndipo utawajua na kushirikiana nao kisha ndipo utafanikiwa.
Ndugu, unahitaji sana kufumbuliwa macho ya rohoni, mwambie Bwana YESU KRISTO akufumbue macho ya rohoni.
◼️Ishi maisha matakatifu maana msaada wa MUNGU huambatana na utakatifu, acha dhambi maovu na makosa, mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako kisha Omba MUNGU akufumbue macho uzione baraka zako.
✓✓Kuna mambo mengine yamefichwa katika macho ya kimwili, unahitaji macho ya rohoni ili uone na kujua.
✓✓Ndugu kuna mahali unahitaji sana ufumbuliwe macho ya rohoni kwa faida yako.
Jifunze kwa Balaamu ambaye ukaidi wake na tamaa mbaya nusura vimuue, neema ya MUNGU akafumbuliwa macho katikati ya hatari ndipo akasalimika.
Hesabu 22:31 "Ndipo BWANA akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi."
Vipi asingefumbuliwa macho?
Hakika angekufa.
Ndugu, unahitaji sana kufumbuliwa macho ya rohoni.
Ni kusudi la MUNGU kabisa kwamba tufumbuliwe macho ya rohoni sisi tulio Kanisa hai la KRISTO.
Waefeso 1:17-18 " MUNGU wa Bwana wetu YESU KRISTO, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;"
◼️Kufumbuliwa huko kutatokea tu kwa maombi na utakatifu na kumsikiliza ROHO MTAKATIFU.
Ndugu unahitaji sana kufumbuliwa macho ya rohoni ili uone rohoni vyema.
◼️Hata kumjua Mke mwema wako au Mume mwema wako unahitaji kufumbuliwa macho ya rohoni wewe ambaye hauko kwenye ndoa.
✓✓Hata kuwajua maadui zako katika ulimwengu wa roho unahitaji sana kufumbuliwa macho ya rohoni ndipo utajua.
Inawezekana huyo mtu wako wa karibu sana ndiye mchawi anayekuroga, anarogaa familia yako, anaroga uchumi wako na afya yako, unahitaji tu kufumbuliwa macho ya rohoni ndipo utamgundua na kujitenga mbali naye.
Kuna Mtu uzao ulikosekana kwa miaka mingi na kumbe aliyemfunga huo uzao ni mama mkwe wake ambaye anampenda sana na kumpa kila siri na zawadi.
Kuna mtu maisha yake yalifungwa na mama yake mzazi, mchawi hana akili hata moja.
Kuna mtu mmoja kila akifika kazini kuna mtu anamkimbilia na kumshika mkono akimsalimia, kumbe alikwa anatekeleza jambo la kipepo la kumfunga huyu.
✓✓Ndugu, unahitaji sana macho ya rohoni.
Sio mialiko yote unaenda tu, mwenye macho ya rohoni anaweza kuona kabla juu ya jambo la kishetani lililobebwa na mwaliko huo.
Hata zawadi za kichawi zipo pia, uwe mtu wa rohoni ili ujue kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho.
✓✓Ndugu unahitaji macho ya rohoni ili uwe mshindi.
Kuna watu wamefungwa kwenye madhabahu za giza, kuna watu wamefungwa baharini au juu ya milima au vilima.
Kuna watu wamefungwa ardhini na kuna watu wamefumgwa kipepo kwenye miili yao wenyewe.
Ndugu, kuna mengine unahitaji kuomba upewe na MUNGU macho ya rohoni yanayoona.
Ndugu unahitaji sana macho ya rohoni.
Macho ya rohoni ndio yatakufanya uone mambo makubwa na hata magumu usiyoyajua kabla hivyo omba.
Yeremia 33:3 "Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua."
Kama hujawahi kupigana na adui usiyemjua katika ulimwengu wa roho unaweza usinielewe.
Kuna watu wana matatizo mabaya sana na vifungo vibaya sana na hawajui ni adui gani anayewatesa, ndugu unahitaji macho ya rohoni yanayoona ndipo utamjua adui na kumshinda kwa maombi katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na whatsapp).
Ubarikiwe.
Comments