NADHIRI NA HATIMA NJEMA YA MTU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

Hesabu 30:2 "Mtu atakapomwekea BWANA nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake."

◼️Kuna watu wa MUNGU ili kufikia hatima yao njema ilibidi waweke nadhiri.

Nadhiri ni nini?

[✓Nadhiri ni ahadi ambayo mtu huitoa au huahidi mbele za MUNGU kwamba akijibiwa maombi yake atafanya kama alivyoahidi.

✓✓Nadhiri inaweza kuwa sadaka au kitu au jambo jema kulingana na anayeweka ahadi hiyo mbele za MUNGU ili akitendewa kitu fulani na atatenda alivyoahidi.

✓✓Nadhiri ya sadaka ni aina ya sadaka isiyo na kiwango maalumu ambayo inaahidiwa kwa MUNGU ili itolewe baada ya MUNGU kutenda au kujibu hitaji la mhusika.

✓✓Watu wengine hutoa nadhiri siku tu ya kuweka nadhiri hiyo na kabla ya kutendewa na MUNGU, inategemea na kiwango Cha Imani Cha Mtu husika.

◼️Sio lazima uweke nadhiri lakini wapo watu walijaribu kufanikiwa kwa njia zingine za kiroho haikuwezekana hadi walipotumia Kanuni hii ya kiroho ya kuweka nadhiri mbele za MUNGU.
Hata Mimi Peter Mabula niliwahi kuweka nadhiri kwa MUNGU inayohusu mambo matatu na nadhiri yangu ni ya Maisha yangu yote, namshukuru MUNGU wa Mbinguni kwa Neema yake kwangu alitenda kwa jinsi ya tofauti sana na nilivyodhani.

✔️✔️ Narudia tena kuna watu wa MUNGU ili kufikia hatima yao njema ilibidi waweke nadhiri.

Ngoja nikupe mifano 

◾ Yakobo aliweka nadhiri akuwa hana mali yeyote yaani alikuwa maskini sana.

Mwanzo 28:20" Yakobo akaweka nadhiri akisema, MUNGU akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae;"

✓✓MUNGU akatimiza nadhiri ya Yakobo kwa kumbariki sana.

Mwanzo 30:43 "Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno, akawa na wanyama wengi, na vijakazi, na watumwa, na ngamia, na punda."

Hiyo ndio nguvu za nadhiri.

◾Hana alikuwa tasa/asiye na uwezo wa kuzaa ila nadhiri yake ikamfanya azae watoto sita.

1 Samweli 1:11 "Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe."

✓✓Nadhiri ilimfanya Hana afunguliwe tumbo la uzao na kupata mimba na kumzaa Mtumishi wa MUNGU.

✓✓Hana kufanikiwa kwake Katika uzao kulitokana na nadhiri yake kuitimiza mbele za MUNGU kama alivyoahidi.

1 Samweli 1:19-20 "Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA."

Inawezekana wewe ni tasa wa kufanikiwa biashara, inawezekana wewe ni tasa wa kukosa furaha ya ndoa yako, inawezekana wewe ni tasa wa uzao au kupata kazi, inawezekana wewe ni tasa wa kupata wa kufunga naye ndoa takatifu.
Mwenzaki Hana alikuwa tasa wa uzao na nadhiri yake ikasababisha akazaa hata kama mwanzo alikuwa tasa.

Na Hana hakuishia kupata mtoto mmoja Bali akipata jumla watoto sita hata kama alianza kuzaa akiwa mama Mtu mzima.

1 Samweli 2:21" Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA."

◼️Huyu ndiye MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo na ni MUNGU wa Kanisa hai la YESU KRISTO duniani.

✓✓Nadhiri yako wakati mwingine inaweza kuwa ndio ufunguo wa kufanikiwa kwako.

✓✓Sio kika jambo lazima uliwekee Nadhiri ila pale unaposikia msukumo wa rohoni kuweka nadhiri basi unaweza kufanya hivyo.

Nadhiri ina nguvu sana.

✓✓Nadhiri inaweza kuondoa vifungo vyako, vikwazo na vipingamizi vyote vinavyozuia kufanikiwa Katika hitaji la moyo wako.

✓✓Nadhiri ni njia inayoweza kutumika kwako ili kuzuia utendaji kazi wake shetani kwako.

Muhimu tu timiza nadhiri zako, iwe uliahidi kwa kutamka au uliahidi moyoni kimya kimya, timiza nadhiri zako kwa MUNGU.

Kumbu 23 : 21 - "Utakapoweka nadhiri kwa BWANA, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako."

◼️Sio lazima uweke nadhiri ila kuna waliofanikiwa kwa kutumia nadhiri mahali palipokuwa pameshindikana.
Ila zingatia ukiweka nadhiri itimize.

Zaburi 116:18 "Nitaziondoa nadhiri zangu kwa BWANA, Naam, mbele ya watu wake wote."

Ipo mifano mingi kibiblia ya watu wa MUNGU walioweka nadhiri.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments