SIKUKUU YA PASAKA NI NINI.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe  ndugu zangu wote. 

Tunapoelekea sikukuu ya Pasaka kuna marafiki kadhaa waliniandikia ujumbe wakitaka niwatumie masomo yangu   kuhusu pasaka,  niliwajibu kwamba muda ukifika nitafundisha  hivyo wasubiri.

Tunapozungumzia  sikukuu ya Pasaka ni vyema tukaanza  kujua kwanza maana ya "sikukuu" na maana ya "Pasaka"

Sikukuu ni nini? 

●Sikukuu ni siku ya kuadhimisha tukio fulani lililotokea siku  nyingi zilizopita. 

●Sikukuu pia ni siku ya kufurahia tukio fulani lililotokea zamani. 

Kwa Kanisa la KRISTO  duniani inatupasa  kufurahia katika MUNGU  au kuadhimisha katika MUNGU kile ambacho tunaadhimisha, na kama tunaadhimisha katika MUNGU basi lazima tuadhimishe tu kile kinachompendeza MUNGU na kitu hicho tukiadhimishe katika mpango wa MUNGU,  mpango wa MUNGU ni utakatifu. 

Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

Pasaka ni nini? 

●Kwa kifupi tunaweza kusema pasaka ni sikukuu ambayo Wakristo huadhimishwa ufufuo wa YESU KRISTO Mwokozi wao,  hiyo ni tafsiri ya kamusi ya kiswahili.

Kibiblia Pasaka ni nini? 

1. Pasaka ni mwana kondoo  aliyechinjwa kuwa upatanisho  kati ya MUNGU na wanadamu. 

Kutoka 12:21 "Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka."

Kondoo hawa walichinjwa na damu yao ndio iliwekwa katika miimo ya milango hata wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli hawakufa, maana Malaika alipoiona hiyo damu ya kondoo hakuwagusa hao ili kuwaua, unaweza kusoma zaidi kuhusu hilo katika sura nzima ya Kutoka 12.

Kwa hiyo kondoo hao kupitia damu yao kulifanyika upatanisho kati ya MUNGU  na waisraeli hata Waisraeli wasipate madhara.

Waebrania 11:28 "Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao."

2. Pasaka ni jina lingine la Bwana wetu YESU KRISTO likimaanisha kwamba Bwana YESU alikufa na kisha kufufuka ili sisi wanadamu tupatane na MUNGU muumbaji wetu.

1 Wakorintho 5:7" Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana PASAKA wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, KRISTO;"

Kwa jinsi hiyo tunajua na kugundua kwamba Bwana YESU KRISTO ndiye Pasaka wetu, alikufa msalabani  na kwa damu yake ya agano jipya tunapata msamaha wa dhambi, na kupitia damu ya YESU KRISTO dhambi za mtu yoyote  hata kama ni dhambi nyingi kiasi gani zinafutwa kama tu mtu huyo akiamua kutubu na KUMPOKEA YESU KRISTO KAMA MWOKOZI WAKE. 

Damu ya YESU aliye Pasaka wetu,  hiyo damu ya Pasaka  ina kazi ya ajabu sana kwetu. 

Inatufanya tuwe karibu na MUNGU muumba wetu. 

Waefeso 2:13 "Lakini sasa, katika KRISTO YESU, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake KRISTO."

Waisraeli waliamuriwa na MUNGU kuiadhimisha sikukuu hii wakikumbuka walivyotoka utumwani  Misri.  Hivyo Waisraeli walisherekea Pasaka wakikumbuka  kutoka utumwani Misri. 

Kutoka 12:14 "Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele"

Sisi kama Kanisa tunaadhimisha pasaka kama kukumbuka tulivyookolewa na Bwana YESU KRISTO  aliye Pasaka wetu.

1 Wakorintho 5:7 -8 "Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, KRISTO; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli."

●Ninachotaka uone hapo ni kwamba "KRISTO ndiye Pasaka wetu" na "Tuifanye karamu si kwa chachu ya kale"

●Biblia inaturuhusu Kanisa kuifanya karamu maana Pasaka wetu alikwisha kutolewa kuwa sadaka, pasaka wetu ni ni KRISTO.

●Sasa kwanini Biblia inasema  "Tuifanye karamu?" 

Tuangalie neno karamu lina maana gani. 

Karamu ni nini? 

■Ukiangalia Kamusi ya kiswahili sanifu neno karamu lina maana ya sherehe ambazo watu hula na kunywa kwa ajili ya kuadhimisha jambo maalumu.

Kwa Kanisa Ninaposema "Kunywa kwa ajili ya kuadhimisha " sina maana unywe pombe,  pombe hapo haihusiki,  pombe ni dhambi hivyo kunywa vinywaji vingine isipokuwa vileo, ukishindwa kunywa juisi na soda bado kunywa maji, pombe usiguse. 

 Biblia haikatazi kuadhimisha ila muhimu ni kwamba unaadhimisha nini? 

Kitu kingine ambacho watu wengi huuliza ni kwanini tunaadhimisha pasaka tukisema tuakumbuka ukombozi wakati hata mkombozi wetu YESU KRISTO aliadhimisha Pasaka? 

Jibu ni rahisi tu kwamba Bwana YESU KRISTO alipokuja katika mwili alisherekea siku ya Pasaka ja Kiyahudi ambayo ilikuwa ya Mwisho. 

Luka 22:15 -16 "Akawaambia, Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa MUNGU."

Ndio maana Pasaka hii ya Kiyahudi baada ya wakati huu haipewi tena kipaumbele katika maandiko ya Agano jipya. 

Lakini pia kuna tukio la kukumbuka hapo kwamba Bwana YESU alipokuwa anaadhimisha pasaka hii ya mwisho ya kiyahudi, ni siku hiyo hiyo Bwana YESU alidhihirisha Agano jipya litakavyokuwa. 

Luka 22:17-20 " Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa MUNGU utakapokuja. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]"

Bwana YESU  alifanya ishara hizi akijua kwamba yeye ndiye Pasaka wetu yaani mwana kondoo wa MUNGU atakayechinjwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi kwetu tunaomtii. 

Ufunuo 5:9-10 " Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe(YESU) kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia MUNGU kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa MUNGU wetu; nao wanamiliki juu ya nchi."

Kwa hiyo sikukuu ya Pasaka kwa Waisraeli ilikuwa siku ya kuadhimisha na kusherehekea ukombozi wao. 

Hesabu 9:2 "Tena, wana wa Israeli na washike sikukuu ya Pasaka kwa wakati wake ulioagizwa."

Kwa Kanisa  ni siku ya kuadhimisha ukombozi wetu. 

Ni wazi kwamba hakuna andiko katika Biblia linalotoa mwezi wala tarehe ya Sikukuu ya Pasaka  lakini tukio la Pasaka lipo ndani ya Biblia(1 Kor 5:7-8) na ni Biblia katika kuadhimisha tukio lolote inasema kwamba kila mmoja athibitike mwenyewe yaani hakuna anayelazimishwa kuadhimisha siku kwa MUNGU na hakuna mtu anakatazwa kuiadhimisha siku katika MUNGU. 

Warumi 14:5-6 " Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru MUNGU; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru MUNGU."

Hivyo sio kosa kimaandiko kuiadhimisha siku katika MUNGU. 

Tunasherekea pasaka katika MUNGU, tukimtukuza MUNGU na kumwinua Mwokozi wetu YESU KRISTO,  hivyo kama yuko mtu anasherekea pasaka vibaya ni makosa na kwa uangamivu wake mwenyewe. 

Lakini jambo muhimu katika siku kama hii ni mtu kutengeneza maisha yake kwa YESU KRISTO ambaye damu yake ya Pasaka ndio damu ya ukombozi wetu. 

Waefeso 1:7" Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake."

Ndugu hakikisha unaadhimisha sikukuu hii kwa utakatifu na adabu njema mbele za MUNGU. 

Jitenge mbali na kila dhambi,  uovu na makosa katika sikukuu hii na siku zote zinazofuata. 

Ikatae mitoko ya kishetani na kataa mialiko ya watu wabaya walio na lengo la kukuangusha katika dhambi. 

Mtii MUNGU katika hali zote. 

Muhimu ni nini kwako katika Pasaka ya mwaka huu? 

1 Kor 5:7-8 inajibu. 

1 Wakorintho 5:7 -8 "Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, KRISTO; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli."

1. Basi tujisafishe yaani tutubu  na kutakaswa na damu ya YESU KRISTO.

1 Yohana 1:7 "bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote."

2. Tutoe chachu ya kale yaani tuondoe dhambi na tujitenge mbali na dhambi. 

1 Wathesalonike 5:22 " jitengeni na ubaya wa kila namna."

3. YESU KRISTO tayari ndiye alifanyika sadaka ya ukombozi wetu,  hivyo kila mtu akubali kukombolewa na damu ya YESU KRISTO Mwokozi. 

Wakolosai 1:14-15 " ambaye katika yeye(YESU) tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa MUNGU asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote."

4. Tuifanye karamu/sherehe sio kwa dhambi na maovu bali kwa weupe wa moyo na kweli. 

Wakolosai 3:17" Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

Zingatia hayo katika pasaka hii na endelea kuzingatia siku zote za maisha yako. 

Kumbu 13:4 "Tembeeni kwa kumfuata BWANA, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye."

Nakutakia maandalizi mema ya Pasaka na nakutakia Pasaka njema. 
MUNGU akubariki sana. 
By Peter Mabula. 
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments