UKIITWA NA YESU ITIKA NA FANYIA KAZI WITO WA MUNGU NDANI YAKO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu nikujuze  jambo hili muhimu sana.

◼️Mtu yeyote aliyeokoka ameitwa na MUNGU na MUNGU huweka wito fulani ndani yake.

✓✓Sio lazima wito wa Mtumishi mmoja uwe sawa na wito aliopewa Mtumishi mwingine.

✓✓Uko wito wa namna mbalimbali kulingana na maagizo ya MUNGU kwa mtu husika.

Mfano ni huu.
Isaya 42:6-7 " Mimi, BWANA, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa."

✓✓Huu ni mfano hai wa wito wa MUNGU kwa aliyekusudiwa.

◼️Huyu wito wake unamtaka kuyafunua macho ya vipofu ili yaanze kuona, kuwatoa gizani waliofungwa na kuwatoa watu katika magereza ya kiroho.

✓✓Huyu akisimama katika Wito wake aliopewa na Bwana YESU KRISTO lazima hayo mambo yanayoambatana na Wito wake yatatokea katika utumishi wake kwa KRISTO.

Isaya 35:5-6 " Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa.  Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani."

✓✓Wito huu unahitaji sana maombi binafsi, kumsikiliza sana ROHO MTAKATIFU na kuwafundisha sana watu Neno la MUNGU ili watoke gizani kisha unawaombea.

◼️Wito wa Musa aliopewa na MUNGU ulikuwa kuwatoa Misri Watu wa MUNGU.
Kutoka 3:10 " Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri."

✓✓Wito wa Musa ulimtaka kuijua Misri, kujua njia za kutoka Misri, kuwajua viongozi wa Misri na kumsikiliza sana ROHO MTAKATIFU.

◼️Wito wa Yona ulimtaka Yona kwenda Niwawi na kutembea mji mzima akipaaza sauti yake akiwaambia watu watubu dhambi na kuziacha maana wasipotubu MUNGU ataangamiza.

Yona 3:1-4 " Neno la BWANA likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama BWANA alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu. Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa."

✓✓Wito wa Yona haukuwa kama wito wa Musa.

✓✓Uko wito wa namna nyingi sana MUNGU huwapa wateule wake katika KRISTO YESU.

✓✓Kuna walio na wito wa kuhubiri, wengine kufundisha n.k

◼️Mfano wa walioitwa kuhubiri hata wao wito kwa mmoja unaweza kuwa tofauti na mwingine, kuna anayehubiri kwa nyimbo za injili, mwingine anahubiri kwa pesa zake, mwingine anahubiri kwa vitabu au majarida au vipeperushi, kuna anayehubiri kwa kushuhudia mitaani, kuna anayehubiri kwa kuhubiri mitaani au mikutano ya injili au semina.

◼️Lengo ni Moja Mtu anayempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake anaokoka haijalishi amehubiriwa kwa njia gani.

Marko 16:15-7 " Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;"

✓✓Hivyo japokuwa wote wito wao ni kuhubiri lakini kila mtu wito wake una maelekezo binafsi ya ROHO MTAKATIFU yanayoambana na karama au kipawa MUNGU amekupa.

◼️Muhimu tu wito wa MUNGU ni katika KRISTO YESU tu na kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.

✓✓Hata ulipoitwa na kupewa wito ni baada ya wewe kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.

✓✓Ndugu timiza wito wako katika Kanisa la MUNGU.

✓✓Ndugu timiza wito wako katika injili ya YESU KRISTO Mwokozi.

 Wakolosai 2:6-7 " Basi kama mlivyompokea KRISTO YESU, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani."

✓✓MUNGU akikuita lazima akupe agizo.

✓✓Kila aliyeitwa na MUNGU katika KRISTO huyo ndugu ana wito ndani yake maana Wokovu wa KRISTO huambatana na wito wa MUNGU na maagizo ya MUNGU ndani ya mtu husika.

Sitasahau siku moja Mimi Peter Mabula katika maono nilijiona niko katika eneo ambalo kuna maelfu ya watu wamefungwa na nguvu za giza, wako utumwani na MUNGU ameweka wito ndani yangu ili nihakikishe watu wale wanatoka huko kwenye utumwa wa nguvu za giza, nilianza kuwaamrisha wakuu wa giza wawaachie watu wa MUNGU, katika harakati hizo sikujua kwamba nilipoitwa na MUNGU nilipewa na fimbo, nikashangaa ndipo nimeshika fimbo mkononi tayari kuwatoa watu kwenye utumwa wa nguvu za giza.
Siku hiyo niligundua aina mojawapo ya wito ambao MUNGU ameniitia kwamba kuhakikisha watu wote wanatoka katika utumwa wa Nguvu za giza na utumwa wa dhambi.

✓✓Inawezekana wito wangu na wako ndugu unayesoma somo ni wito mmoja ila kila mmoja ana utendaji kazi wake.

✓✓Ninachkuomba hakikisha unafanyia kazi wito wa MUNGU ulio ndani yako kwa ajili ya kazi ya MUNGU katika Kanisa la MUNGU na katika injili ya KRISTO.

Siku moja tena katika maono  nikajikuta niko katika nchi nzuri sana nikishangaa, Bwana YESU akanitokea hapo na kuniambia nikawaambie watu wote wampokee kama Mwokozi na waishi maisha matakatifu ya Wokovu wake, ghafla nikajiona nawafuata watu na kila ninayemuona namwambia "Okoka, YESU KRISTO anakuita kwenye ufalme wake" waliokubali niliwaona wanaanza safari kwenda Bwana YESU alipo, waliokataa niliachana nao. Baadae Bwana YESU KRISTO akaniambia "Peter rudi kwangu maana muda umeisha" nikaacha kuwahubiri watu nikamfuata Bwana YESU alipo.

✓✓Hapo napo nilijua ni nini wito wa MUNGU ndani yangu unachotaka.
Ni kuhubiri watu kuokoka na kuhubiri utakatifu.

Je wewe umeitwa kufanya nini?

✓✓Ndugu timiza wito wako kwa uaminifu.

✓✓Ishi maisha matakatifu ya Wokovu ili utumize wito wako.

✓✓Wito huanza na msukumo wa ndani unaokuelekeza jambo la ki MUNGU la kufanya.

✓✓Wito pia unaweza ukaanza kama wazo rohoni linalokuelekeza kufanya kazi ya MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi 

◼️Ndugu, Wokovu wa KRISTO YESU ulioupokea, huo Wokovu huambatana na wito.
Ndugu fanyia kazi wito wako.
Mimi Peter Mabula siwezi kunyamaza ikiwa MUNGU Baba amenipa agizo.

Yeremia 47:7 Utawezaje kutulia, Ikiwa BWANA amekupa agizo? Juu ya Ashkeloni na juu ya pwani, Ndipo alipoyaamuru hayo."

Wewe je? 
Unaendelea kunyamaza wakati MUNGU amekupa agizo?

Wewe je, hata sasa hutaki kumtumikia Bwana YESU wakati amekupa agizo?

Je hata kuhubiri kwa pesa yako huwezi?

Hata kuwaleta kwa YESU watu 10 kwa mwaka huwezi?

Hata kualika watu 2 kila jumapili ili waende Kanisani huwezi?

Bado unaendelea kunyamaza wakati ROHO wa MUNGU amekupa agizo rohoni?

Hata tu kutoa kipande kidogo cha shamba kubwa lako ili pajengwe Kanisa huwezi?

Hata tu kumnunulia pikipiki used mhubiri mmoja ili aipeleke injili vijiji vya mbali huwezi?.

Je bado unaendelea kunyamaza wakati rohoni mwako ROHO wa MUNGU amekupa agizo la kiroho la kazi ya MUNGU?

Je hata kununua mic moja ya kuhubiria huwezi?

Hata kununua kiti kimoja cha kukalia Kanisani huwezi?

Hata kuwasapoti wanaohubiri huwezi?

◼️Ndugu, wito wa MUNGU ndani ya Mkristo, huo wito huambatana na maagizo ya MUNGU.

Nisamehe kama nimeongea lugha ngumu sana Leo ila fanyia kazi na utaitwa heri duniani na mbinguni.

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments