UMEOMBA UPEWE MKE/MUME MWEMA. JE MUNGU HUJIBUJE MAOMBI HAYO?

Peter Mabula na Jemimah William
Watendakazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO 



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.

◼️MUNGU hujibuje maombi ukiwa umemuomba akupe mke/mume mwema?

✓✓Ni swali ambalo huwasumbua watu wengi ambao hawajaingia katika ndoa, ni sawa kabisa swali hilo liwasumbue maana unapohitaji Mke au Mume ujue unamhitaji mtu wa karibu zaidi atakayekuwa na wewe karibu zaidi kuliko wote na ambaye itakubidi kukaa naye hadi tu kifo kitakapowatengasha.

✓✓Ni kweli kabisa utaratibu wa ki MUNGU upo kwamba Mwanaume ambaye hana Mke na Mwanamke ambaye hana Mume wanaweza wakapendana katika hali takatifu na baada ya hapo wakaenda kuanzisha familia yao wenyewe baada ya kufunga ndoa takatifu.

Mwanzo 2:24 "Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja."

✓✓Neno "Kuoa" kwa ujumla lina maana ya Mwanaume kufanya muunganiko na Mwanamke ili kukaa pamoja kama Mume na Mke kulingana na taratibu za dini, sheria, desturi au taratibu za ndoa za mahali husika.

◼️Kwa sababu sisi ni Kanisa hai la KRISTO basi inatupasa kuoa na kuolewa kulingana na taratibu za dini yaani taratibu za Kanisa hai la MUNGU duniani, na namshukuru MUNGU maana hata sheria za nchi haziendi kinyume na taratibu za Kanisa maana sheria hazisemi kwamba mtu aoe au kuolewa akiwa mtoto, sheria hazisemi kwamba mtu aoe au kuolewa kwa kulazimishwa au kuolewa na asiyempenda, lazima watu husika wapendane na kuwepo na makubaliano rasmi yaliyo katika hali ya haki na utakatifu.

Mithali 5:18-19 "Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezaye; Maziwa yake yakutoshe sikuzote; Na kwa upendo wake ushangilie daima."

✓✓Neno "Kuoana" lina maana ya Mwanaume na Mwanamke kukubaliana kuishi kama Mume na Mke kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
 Taratibu hizo kwa sisi Wakristo ni taratibu za Kanisa ambazo ni taratibu za ki MUNGU kabisa, hapa nazungumzia Kanisa linalomtii MUNGU katika KRISTO YESU.

◼️Kumpata mwenzi wako wa ndoa na kufunga naye ndoa takatifu ni jambo zuri na la kupendeza mbele za MUNGU na mbele za wanadamu.

✓✓Kufunga ndoa takatifu ni jambo jema sana, hakuna haja ya Mwanaume umeshafikia umri wa kuoa lakini huna hata mpango wa kuoa, unateswa tu na mawazo ya dhambi ya zinaa,ni heri kuoa.

1 Wakorintho 7:2 "Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe."

✓✓Ni muhimu sana wewe kijana ambaye umri wa kuoa umefika inakupasa uoe.
Ili usiwe tu mtu wa kuwaka tamaa chafu.

1 Wakorintho 7:9" Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa."

✓✓Lakini pia umakini sasa unahitaji juu ya mtu wa kufunga naye ndoa, Kijana uwe makini na Binti uwe makini sana.

◼️Uwe makini Kwa sababu sio kila mtu ambaye hajafunga ndoa anafaa kuwa mwenzi wako wa ndoa.

◼️Sio kila Kijana au Binti mnayesali naye anakufaa kuwa mwenzi wako wa ndoa.

◼️Sio kila mtu asiye na mchumba basi sasa awe mchumba wako kwa sababu tu unatafuta mchumba.

✓✓Ni kweli kabisa kwamba kila asiye na mchumba sio dhambi wewe ukichumbiana naye, ni kweli huyo ni halali lakini sio wote waliohalali wanakufaa wewe.

1 Wakorintho 6:12 "Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote."

Mtu mmoja aliniuliza "Mtumishi Mabula hapo Kanisani kweni ni nani anafaa kuwa mke mwema?"

Nikamjibu kwamba Kanisani popote mabinti wote wanaoishi maisha matakatifu wanafaa kuwa wake wema sana, Kanisani hakuna binti asiyefaa kuwa mke mwema maana wameokoka na wanaoishi maisha matakatifu ya Wokovu, ila sio wote wanakufaa wewe.

✓✓Ndio maana Biblia inasema kwamba vitu vyote vinaweza kuwa halali kabisa ila sio vyote vinamfaa kila mtu.

✓✓Mabinti wote Kanisani ni halali ila anayekufaa ni mmoja tu.

◼️Inakupasa kumjua anayekufaa wewe, ndio maana inakupasa kujifunza somo hili hadi mwisho yamkini utapata maarifa ya kiroho ya kukusaidia unapoelekea katika uchumba kisha ndoa.

◼️Inawezekana kabisa vijana au mabinti wote waliookoka ni halali kwako mmoja katika wao akawa mchumba wako, lakini ukweli ni kwamba sio kila kijana au binti anakufaa wewe kulingana na hali yako, kulingana na huduma yako, kulingana na kazi yako n.k

✓✓Ndio maana inakupasa kujua kwamba Mke mwema wako Kaka au Mume mwema wako Dada hutoka kwa MUNGU.

✓✓Ndio maana vijana wengi na mabinti wengi huingia katika maombi ili MUNGU awape wenzi wema na sahihi kutoka kwake.

Lakini changamoto ya vijana wengi na mabinti wengi hawamjui MUNGU anawajibuje kuhusu mke mwema au mume mwema.
Wengi wanasubiri tu kuota ndoto ndipo waamini kwamba wamepewa mwenzi mwema, wakati ndoto ni "lango" hivyo anaweza akalitumia MUNGU au hata shetani anaweza kulitumia lango hilo kulingana na maisha ya mtu husika na uelewa wake wa kiroho.

Vijana wengi sana na mabinti wengi sana wamepata madhara kutokana na ndoto ambazo ni shetani aliwaletea ili kuwadanganya, watu hawa hubaki kujifariji na kumbe wanafanyia kazi ujumbe wa ndoto wa shetani.

Zekaria 10:2 "Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji."

Dada mmoja baada ya maombi aliota ndoto kwamba mume mwema wake ni kijana mmoja ambaye wakati huo alikuwa nje ya nchi. Dada yule baada ya ndoto hiyo alitangaza kila mahali, aliwakataa vijana sahihi waliomjia na kuwatukana wengine maana alijipa uhakika kwamba mwenzi wake yuko nje ya nchi na siku akirudi atafunga naye ndoa maana ana uhakika aliyemwambia kwa ndoto ni MUNGU,kumbe hakuwa MUNGU.
Dada huyu alijisahau kwamba kuna vyanzo vitatu vya ndoto.

Kuna ndoto chanzo chake ni MUNGU, kuna ndoto chanzo chake ni mawazo ya mtu husika mwenyewe kutokana na dhughuli za mchana au kutokana na kile alichokiwaza sana. Kumbuka ubongo wa mwanadamu ni kama memory card ambayo hutunza vitu hivyo kichwani hutunzwa matukio uliyoyaona mchana, mambo uliyoongea au kuwaza sana na hayo yote yanaweza kujirudia usiku kwa njia ya ndoto yakiwa kama ulivyoona mchana au ulivyowaza au yakawa na tofauti kidogo sana ila ni Yale Yale.

Sasa unaweza ukawazia mwenzi na fikra zako kwa njia ya ndoto zikakuchagulia Mke/Mume hata kama ni Mume/Mke wa mtu.

Mhubiri 5:3 "Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno."

✓✓Na chanzo cha tatu cha ndoto ni shetani.

Hiki chanzo kiko wazi sana maana shetani ni baba wa uongo.

Yohana 8:44 "Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo."

Kuhusu huyu Dada ambaye nimekuambia habari zake kwamba mchumba wake yuko nje ya nchi, kilichotokea ni hiki, baada ya muda kama mwaka na miezi baadaye yule kijana wa nje ya nchi alirudi Tanzania akiwa na Mke na Mtoto, Dada huyu nusura ahame mji.

✓✓Ni kweli kabisa kwamba ni fumbo kumjua Mke/Mume mwema wako.
Mithali 31:10 "Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? ........"

◼️Na fumbo hili anayeweza kulifumbua ni MUNGU.

✓✓MUNGU anaweza kulifumbua fumbo hili kirahisi sana baada ya wewe kuomba huku unaishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU Mwokozi.

Sasa baada ya WEWE KUOMBA ILI UPEWE MKE/MUME MWEMA. MUNGU HUJIBUJE MAOMBI HAYO?

Njia 5 ambazo MUNGU anaweza kukujibu Baada ya  wewe  kuomba  Mke mwema au  Mume mwema ni  hizi.

1. ROHO MTAKATIFU kukujulisha.

1 Wakorintho 2:10 "Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."

◼️Kwa njia gani ROHO MTAKATIFU atakujulisha baada ya kuomba upewe Mke au Mume mwema?

A. Binti utakapofuatwa na kijana sahihi ROHO MTAKATIFU anakupa amani rohoni mwako juu ya kijana huyo.

Wafilipi 4:7" Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU."

✓✓Yaani ukiwa na amani ya KRISTO ndani yako basi hiyo ni njia mojawapo ya MUNGU kukujibu juu ya hitaji lako la mume mwema kwako.

✓✓Kama huielewi vyema amani ya MUNGU basi unaweza kujipa muda jambo hilo huku ukiomba na baada ya muda utaielewe vyema amani ya MUNGU inayokusaidia kuamua ndani yako ambayo ROHO MTAKATIFU amekupa.

✓✓Unaweza kuwa umeomba upewe mke mwema au mume mwema na anapojitokeza iwe katika mwili au katika mawazo ukiona amani ya KRISTO, hilo ni jibu la MUNGU kwako la maombi yako, fanyia kazi jibu la MUNGU la maombi yako.

✓✓kama amani itaondoka kwako binti wakati ukiambiwa na kijana husika basi utakuwa umeshajua kabisa kwamba unachotaka kuamua yaani kumkubalia sio sahihi kwako kulingana na mbingu.

Hapo unakuwa umeshajua kabisa huyo kijana japo ni halali ila hakufai wewe.

Hata kama umeota ndoto kisha amani ikaondoka ujue hapo unajulishwa kwamba huyo hakufai au usifanyie kazi.

B. Kijana anapowaza au kupanga kumwambia binti fulani kwamba katika hali takatifu anataka kumchumbia ili wafunge ndoa, katika mazingira hayo hayo ROHO MTAKATIFU hujifunua kupitia kukupa amani ya KRISTO kama Binti huyo ni sahihi kwako.

Wakolosai 3:15 "Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani."

✓✓Hiyo amani ya KRISTO ambayo ROHO MTAKATIFU anakupa ndio inakusaidia katika maamuzi.

Sasa unaweza kuwa umeomba upewe Mke mwema au Mume mwema na anapojitokeza iwe katika mwili au katika mawazo ukiona amani ya KRISTO inafanya kazi ndani yako , hilo ni jibu la MUNGU kwako kutokana na maombi yako.

✓✓Kama amani itaondoka utakuwa umeshajua kabisa kwamba unachotaka kufanya sio sahihi kulingana na mbingu.

Hata kama kijana utaota ndoto yaani umeota ndoto kwamba huyo ndio wako, ukiona baada baada ya ndoto huna amani, au kila ukiiwazia ndoto hiyo unakosa amani basi ndoto hiyo haikuwa ya MUNGU na unakuwa umeshajulishwa kwa njia ya amani ya KRISTO kwamba huyo mtu sio wako.

Na kwa mabinti ni vile vile kuhusu ndoto unazokoseshwa amani.

C. ROHO MTAKATIFU kukupa huzuni moyoni kama huyo binti au kijana sio kusudi la MUNGU kwako.

2 Wakorintho 7:10 "Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya MUNGU hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti."

✓✓Ninachotaka ujue hapa ni kwamba kuna huzuni iliyo kwa jinsi ya MUNGU, huzuni hii ROHO MTAKATIFU anaweza kukupa kama njia ya kukujulisha kwamba kama ni kijana usimchumbie binti huyo maana wa kwako yupo, kama ni binti huzuni hiyo inakujulisha kwamba usikubali kuoana na huyo maana sio mpango wa MUNGU, hapo unakuwa umeshajua kabisa kwamba huyo hakufai.

✓✓Sasa unaweza kuwa umeomba upewe mke mwema au mume mwema na anapojitokeza iwe katika mwili au katika mawazo ukiona huzuni iliyo kwa jinsi ya MUNGU, hilo ni jibu la MUNGU kwako.

D. ROHO MTAKATIFU kukusemesha kwa sauti au maono ya wazi.

Yeremia 29:6" oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue."

✓✓Andiko hili linaonyesha MUNGU akisema kwa sauti kwa ujumla juu ya watu kuoa, kuolewa na wazazi kuwaozesha watoto wao.

✓✓Hapa MUNGU anaposema oeni anawaambia vijana wote nchi nzima sasa kwa kijana mmoja akiisikia sauti hii ya MUNGU ikimsemesha binafsi atasikia ikisema "Oa mke" hivyo MUNGU anaweza kusema kwa sauti na wewe kijana kwamba "Fulani ni mkeo hivyo fungeni ndoa" hata Yusufu pia aliambiwa kwa sauti ya Malaika aliyetumwa na MUNGU, ufafanuzi wake ni kama aliambiwa hivi na Malaika " Yusufu Usimwache huyo Mariamu,huyo ndio mkeo kulingana na mbingu, huyo ndio Mke mwema wako wewe Yusufu"

Mathayo 1:20 "Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa BWANA alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, ......."

✓✓Yusufu aliambiwa hayo kipindi hajamuoa Mariamu, hivyo hata wewe unaweza kuambiwa kwa sauti juu ya nani ndio mwenzi wako wa ndoa.

✓✓Waulize ambao wako katika ndoa takatifu, baadhi yao walisikia sauti kabisa zikiwaambia kwamba ni akina nani watakuwa wenzi wao wa ndoa.

◼️Unaweza ukapata neema hiyo pia, endelea kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU Mwokozi na endelea na maombi.

2. MUNGU kukujulisha kwa ndoto au maono.

◼️Unaweza kuwa umeomba juu ya kupata mwenzi wa ndoa na MUNGU akanijibu kwa ndoto.

Kwanini MUNGU akujulishe kwa ndoto?

A. Anakujulisha kwa ndoto au maono ili umjue Mwenzi wako.

✓✓Mfano hai ni Yusufu ambaye alijulishwa kwa ndoto ili amjue mke mwema wake kutoka kwa MUNGU.

Mathayo 1:20" Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa BWANA alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa ROHO MTAKATIFU."

✓✓Hata wewe inawezekana kabisa umeomba kwa MUNGU kuhusu mwenzi wa ndoa na MUNGU akakujulisha kwa ndoto.

B. MUNGU anakujulisha kwa ndoto au maono kuhusu mwenzi wako ili umfahamu mwenzi wako kisha usubiri majira ya MUNGU ya nyie kufunga ndoa.

Habakuki 2:3 "Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia."

C. MUNGU anakujulisha kwa ndoto au maono kuhusu mwenzi wako ili uchukue maamuzi ya kumwambia na kuwaambia watumishi wa MUNGU kisha mipango ya kufunga ndoa ianze.

Ayubu 33:14-15 " Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;"

3. Baada ya maombi na muda wa MUNGU ukafika utashangaa mwenzi wako anakuwa karibu yako, anakujulisha kuhusu suala la kufunga ndoa.

Mwanzo 24:7 "BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko;"

Baada ya kukujulisha unapata amani naye na kisha unafunga naye ndoa.

✓✓Hilo linaweza kuwa ndilo jibu la MUNGU kwako baada ya wewe kufanya maombi ya kumpata mke/mume mwema.

Kama umeomba upate mke mwema katika kipengele hiki kitakachomleta karibu na wewe huyo Mume/Mke mwema wako ni hiki.

A. Malaika.

Mwanzo 24:40 "Akaniambia, BWANA, ambaye naenenda machoni pake, atapeleka malaika wake pamoja nawe, atafanikisha njia yako; nawe umtwalie mwanangu mke katika jamaa zangu, na wa nyumba ya babangu."

B. Tabia yako njema itamvuta kwako huyo mtu sahihi uliyopewa na MUNGU.

Mithali 11:16a " Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; ....."

C. Kuishi kwako maisha matakatifu kutamsogeza karibu yako mwenzi mwema uliyepewa na MUNGU.

Mithali 22:11 "Apendaye usafi wa moyo, na neema ya midomo; Mfalme atakuwa rafiki yake."

D. Ushuhuda wako mzuri wa maisha yako ya wokovu unaweza kumsogeza mwenzi wako karibu na wewe hata mkaoana.

1 Timotheo 4:12 "Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi."

E. Wewe kupata neema ya kibali mbele za kijana huyo au binti huyo.

Esta 2:17 "Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata NEEMA na KIBALI machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti."

✓✓Usipopata neema na kibali kwa kijana au binti husika hawezi kukubali kufunga ndoa na wewe, hivyo maombi unapoomba ya kupata mwenzi yanaweza kumfungua hata wewe upate kibali na neema machoni pake ili mfunge Ndoa.

4. MUNGU kukupa rohoni upendo wa dhati kwa ajili ya mwenzi wako huyo ajaye na yeye pia anakuwa na upendo kuhusu wewe.

1 Wakorintho 13:4 "Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;"

Unaweza kuwa umefanya maombi ya kumpata mke mwema au mume mwema na MUNGU akakujibu njia hiyo tu, wengi huwa hawaelewi kama hilo tu linaweza kuwa jibu la MUNGU kwao kuhusu mwenzi wako wa ndoa unayemtafuta.

Kwa nini ujibiwe kwa njia hiyo kuhusu mwenzi wa ndoa umtakaye?

A. Ili umfahamu mwenzi anayekufaa wewe hata mfunge ndoa.

Wimbo 8:6 "Nitie kama muhuri moyoni mwako, Kama muhuri juu ya mkono wako; Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu."

B. Unapewa rohoni kumpenda huyo kijana au binti ili kukuondolea mawazo kwa mabinti au vijana wengine .

1 Wakorintho 16:14 "Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo."

C. Ili uanze taratibu za kikanisa zitakazopelekea mfunge ndoa.

Waefeso 4:2" kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo;"

5. MUNGU anakupa wazo ndani yako juu ya ni nani anakufaa ufunge naye ndoa.

Yeremia 29:11 "Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho."

◼️MUNGU anakuwazia mema wewe maana u mteule wake katika KRISTO YESU.
Na kwa sababu wewe ni Mteule wa KRISTO uliye muombaji basi MUNGU wakati mwingine husema kwa njia ya wazo hivyo anaweza kukupa wazo ndani yako likakusaidia katika kuamua ni nani mke mwema wako au ni nani mume mwema wako.

Inakuwaje katika kupewa wazo baada ya maombi juu ya mwenzi?

A. Unawaza rohoni kwamba Binti fulani au Kijana fulani anakufaa kufunga naye ndoa.

Mwanzo 24:67" Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; ........."

B. Unapewa wazo kuhusu huyo tu ili kukuondolea wengine ambao labda huwa unawafikilia.

Yakobo 2:4" je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?"

✓✓Ili usiwe na hitilafu kwenye mawazo wakati mwingine unajulishwa kwa njia ya wazo juu ya ni nani anakufaa hivyo unajitenga mbali na wengine wote.

Zingatia mteule wa KRISTO na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments