USIOGOPE.

na Mwl Peter Mabula



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wetu aliye hai.

Moja ya vitu vibaya kwa Mteule wa KRISTO ni mtu huyo kuwa mwoga.

Kuogopa ni dhambi kwa wateule wa KRISTO.

Kanisa la watu waoga hawawezi kufanikiwa kihuduma kamwe.

Neno "Kuogopa" likiondoka kwa wateule wa MUNGU basi wateule hao wa KRISTO watafanya mambo makubwa sana.

Isaya 41:13 "Kwa maana mimi, BWANA, MUNGU wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia."

■MUNGU anapomuita mtu ili amtumikie, neno la mapema kabisa ambalo MUNGU humtaka mtumishi huyo ni kwamba asiogope.

●Mfano Ibrahimu alipoitwa aliambiwa asiogope.

Mwanzo 15:1 "Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, USIOGOPE, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana."

●Joshua alipoitwa na MUNGU moja ya maneno ya mapema kabisa ya MUNGU kwa Joshua ni kwamba asiogope.

Yoshua 1:9 "Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; USIOGOPE wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako."

●Yeremia alipoitwa katika utumishi moja ya maneno ya mwanzo mwanzo aliyoambiwa na MUNGU ni kwamba asiogope.

Yeremia 1:8 "USIOGOPE kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA."

Kwanini MUNGU alipowaita watumishi ili wamtumikie aliwaambia wasiogope?

●●Sababu kuu ni kwamba wakiwa waoga hawatafanikiwa katika utumishi wao kwa MUNGU.

Kila aliyeokolewa na YESU KRISTO ni Mtumishi wa MUNGU lakini Wateule wengi ni waoga kupita kawaida.

●●MUNGU anataka watumishi wake wawe majasiri.

●Uoga huleta hofu na hofu ni tatizo kuu linalosababisha mtu asiendelee katika kile alichoitiwa na MUNGU katika KRISTO YESU.

Katika maisha yako hakikisha unaishinda hofu na ushinde woga.

●Ukitaka ufanikiwe katika huduma njema aliyokupa ROHO MTAKATIFU basi ishinde hofu na woga.

Huduma nyingi za Injili ya KRISTO zimedumaa kwa sababu ya uoga na hofu.

Wateule wengi hawatimizi wajibu wao kwa KRISTO kwa sababu ya hofu pamoja na uoga.

■Ili Suleimani ajenge hekalu na atumike katika utumishi uliokusudiwa ilibidi Daudi amshauri mwanaye asiogope.

1 Nyakati 28:20" Kisha Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Uwe hodari, mwenye moyo mkuu, ukatende hivyo; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu, MUNGU wangu, yu pamoja nawe; yeye hatakupungukia wala kukuacha, hata itakapomalizika kazi yote ya huo utumishi wa nyumba ya BWANA."

Nimejifunza kwa wateule wengi kwamba uoga ndio tatizo lao .

Wengine wanasubiri hadi mtu awanyanyue ndipo Watanyanyuka.

Ngoja nikupe shuhuda kutoka katika huduma yangu kwa KRISTO.
Mimi Peter Mabula ni Mwalimu wa kufundisha Neno la MUNGU.
Kwa sababu kuna marafiki zangu hujifunza kwangu basi wakati mwingine hunipigia simu ili niwashauri, hapo ndipo huwa nagundua uoga unavyozuia huduma nyingi njema.

●Mtumishi mmoja aliniambia siku moja kwamba amesikia msukumo rohoni kwamba akashuhudie injili mitaani ili watu waokoke lakini kwa zaidi ya miaka miwili sasa hajui pa kuanzia, niliduwaa rohoni mwangu maana hata muda huo huo angechukua Biblia na kuchagua nyumba 15 ambazo angezifikia kwa siku hiyo hata akiwa tu na maandiko mawili yaani Yohana 3:16-18 na Mathayo 11:28.

Sasa huyu mtumishi sio mchanga kiroho na anajua kuhubiri kabisa lakini kwa miaka 2 bado hajui ataanzia wapi utumishi alioitiwa, na hata baraka zake zimeambatanishwa na utumishi huo.

✓✓Tatizo kuu ni uoga na hofu.

●Nimewahi kupigiwa simu na Wachungaji sio chini ya watano wakitaka wajiunge katika huduma yangu, nilishtuka sana, yaani mimi niwe Askofu wao mkuu na wao wawe matawi ya huduma yangu, nilishtuka sana maana mimi sio Mchungaji ninayechunga Kanisala mahali, Mimi ni Mwalimu wa Neno la MUNGU tu kwa sasa ingawa ninaifanyia kazi huduma aliyonipa ROHOMTAKATIFU.

●Nilimhubiri mtu mmoja akaokoka, kisha baadae akaanzisha Kanisa na ilipofika kipindi cha usajili wa Kanisa nilimwambia kwamba amuone mchungaji mmoja wa dhehebu ambalo wala sio langu ili awe chini yake na ikawa hivyo, sasa kuna Mchungaji mmoja rafiki yangu alipogundua hivyo alinilaumu sana akisema "Usingewaachia watu uliowazaa kiroho ili wakuze huduma nyingine, ni heri ungewakabidhi kwangu "

nilimwambia juu ya wito wangu wa sasa kwamba ni kufundishia Neno la MUNGU na sio kujifunga na dhehebu, nilimwambia kwamba nimeshazaa kiroho Watumishi wengi walioanzisha huduma zao huku wakifundisha kwa kutumia masomo yangu na huwa wananihimiza niandae masomo zaidi maana wanayatumia hayo kufundishia katika huduma zao huku wakijifunza zaidi juu ya wito wao maana wao ni wachanga kiroho, hawajaokoka muda mrefu na hawajakulia katika wokovu, kwa wale tu ambao nimewasiliana nao na wakaanzisha huduma basi hadi sasa ningekuwa na zaidi ya makanisa kumi, hapo bila kuwahusisha ambao hawakunijulisha.

Nini nataka kusema?

Hata wewe ukitaka kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi basi ishinde hofu na jitenge mbali na uoga.

●Akina Petro walipoitwa katika utumishi waliambiwa na Bwana YESU kwamba wasiogope, na hao kwa kuukataa uoga ndio maana Neno la MUNGU limetufikia mimi na wewe leo.

Luka 5:10-11 "na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. YESU akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata."

●Mtumishi mmoja aliniambia kwamba bila mimi hawezi kufanikiwa katika huduma yake ya kuchunga Kanisa, nilimkemea sana maana niliona amekosea sana kusema hivyo.

Mtumishi yule akaendelea kusema kwamba yeye ameitwa kumtumikia MUNGU ila hadi aje kuishi na mimi ndipo anadhani atafanikiwa, ameshamaliza masomo ya Biblia na anaweza kutumika vyema katika kazi ya MUNGU, nilimshangaa sana na nikamkatalia ombi lake, nikakataa hata tu kuonana naye, nikamwambia kwamba aanze kuzunguka nyumba kwa nyumba akihubiri na MUNGU atamtendea mema mengi.

●Kuna watu wawili wako nje ya Tanzania lakini kila mara wanasema wanatafuta nauli ili waje kwangu niwafundishe utumishi maana wana mzigo wa kumtumikia MUNGU, niliwakatalia na kuwaambia waanze huko huko kuhubiri Injili, nilichojifunza ni kwamba wateule wengi ni waoga na wamejaa hofu hivyo huduma zao zimebaki wakizitaja midomoni tu lakini utekelezaji hakuna.

Kwanini nimekupa shuhuda hizi za kweli?

Ni ili ugundue kwamba watu wengi hata Watumishi wa MUNGU wamekwamwa katika utumishi wao kwa sababu tu ya hofu na uoga.

Ndio maana nikakumbuka kwanini MUNGU alipokuwa anawaita baadhi ya watumishi wake baadhi ya maneno ya kwanza kwanza aliyowaambia ni pamoja na "USIOGOPE "

Ninachojua mimi kila mtumishi wa kweli wa Bwana YESU KRISTO inampasa kuanza kumtumikia MUNGU katika hali hiyo hiyo aliyonayo.

Sasa uoga na hofu ndizo zimefuta huduma nyingi za watu.

●Wako wateule leo ni waimbaji wazuri wa nyimbo za injili ila hawajaanza kuimba na wanaogopa waanzie wapi.

Kuchelewa kwao kuingia katika uimbaji kunazuia mambo mengi sana katika mwili wa KRISTO.

●Kuna watu wana wito wa kazi ya MUNGU ila wanaogopa kuanza kuifanya kazi hiyo ya MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.

Ndugu, je wewe umeitwa kufanya nini katika mwili wa KRISTO?

Je kwanini sasa ni miaka mingi ukiwa na huo mzigo wa kazi ya MUNGU ila huingia katika utumishi huo?

Inawezekana wewe umeitwa kutoa mali zako ili injili iende, je unasubiri hadi siku ukiwa hoi kitandani karibia na kufa ndipo utoe mali zako kwa ajili ya kazi za MUNGU.?

Je wewe uliyeitwa katika kuhubiri, unasubiri nini?

Wewe mpeleka injili unasubiri nini?
Wewe mshuhudiaji unasubiri nini?
Usiogope anza utumishi haraka maana hujui kwanini MUNGU amekuita huko.

●Hata kama uko kwenye hatari hubiri injili ya KRISTO.

Paulo aliambiwa asinyamaze bali atangaze Neno la MUNGU hata kama yuko kwenye hatari.

Matendo 18:9-10 " BWANA akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu."

●Wapo watu wana wito lakini akili zao ni kwamba hadi siku wakihamia mjini ndipo wataanza kuhubiri, nani alikuambia kwamba watumishi wameitwa mijini tu?

●Yuko mtu anasema siku akipata vyombo vya kuhubiria vya millioni 10 ndipo ataanza kuhubiri, je hujui kwamba MUNGU anaweza kuwapandisha watumishi kutoka kiwango hadi kiwango? Wewe unataka uanze tu juu na sio chini?

Woga na hofu ndivyo vimekuondoa kwenye kusudi la MUNGU.

Ndugu, kama umeitwa na KRISTO YESU usiogope, bali nitumikie maana MUNGU hatakuacha.

Luka 12:7-9 " Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi. Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa MUNGU; na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa MUNGU."

Ushinde uoga unaokuzuia kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU.

Ishinde hofu inayokuzuia kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU KRISTO Kwako.
MUNGU akubariki sana
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292( whatsapp).
ubarikiwe

Comments