YATAKAYOTOKEA BAADA YA NGUVU ZA GIZA KUONDOLEWA KWAKO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu ujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

◼️Somo hili ni kwa ajili ya aliyefungwa na nguvu za giza.

◼️Kwa yule ambaye hajafungwa na nguvu za giza anaweza kusoma tu kama sehemu ya kuongeza Maarifa ya ki MUNGU ili awasaidie kiroho waliofungwa na nguvu za giza.

✓✓Baada tu ya shetani kutupwa kuzimu, mambo 4 yaliyokea kule alikoondolewa.

Ufunuo 12:10 "Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa MUNGU wetu, na mamlaka ya KRISTO wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za MUNGU wetu, mchana na usiku."

◼️Ukisoma andiko hapo juu unagundua kwamba mara tu baada ya shetani kutupwa kuzimu mambo 4 yalitokea kule alikoondolewa.

Mambo haya sawasawa na Ufunuo 12:10 ni haya.

1. Wokovu ulitokea.

2. Nguvu za MUNGU zilianza kuonekana.

3. Ufalme wa MUNGU ulichukua nafasi.

4. Mamlaka ya ki MUNGU ilichukua  nafasi.

Nini nataka kusema?

✓✓Shetani akiondolewa katika maisha ya Mtu ujue Mtu huyo anapata wokovu, anapata Nguvu za kiroho na za kusonga mbele, kisha ufalme wa MUNGU katika KRISTO YESU unamhudumia mtu huyo na Mtu huyo anakuwa na Mamlaka ya ki MUNGU dhidi ya shetani.

◼️Shetani hana kitu kwako kama wewe umeokolewa na YESU KRISTO Mwokozi maana MUNGU atakuwa upande wako na MUNGU atamuondolea shetani nguvu mbele zako.

Warumi 16:20" Naye MUNGU wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu YESU KRISTO na iwe pamoja nanyi. [Amina.]"

✓✓Kama mashetani(majini) wakiondolewa kwako wewe leo(kama unateswa na mapepo) ndipo utakuwa huru katika Wokovu wa KRISTO, utakuwa na nguvu za kiroho, ufalme wa MUNGU utaanza kukuhudumia na Mamlaka ya Jina la YESU KRISTO itaanza kufanya kazi kwako.

✓✓Shetani akiondolewa mahali popote ujue mahali hapo Wokovu wa MUNGU utaingia, nguvu za MUNGU zitaingia na ufalme wa MUNGU utawahudumia Wateule wa KRISTO hapo.

✓✓Wewe Mteule wa KRISTO unayeishi maisha matakatifu una kibali cha kuomba na kushinda, ishi tu maisha matakatifu tu na uwe Mtu wa Maombi.

Zaburi 4:3 "Bali jueni ya kuwa BWANA amejiteulia mtauwa; BWANA atasikia nimwitapo."

✓✓Majini yakimwacha mtu ujue mtu huyo anapata Wokovu, anapata nguvu za kiroho na ufalme wa MUNGU unamhudumia mteule huyo na Mtu huyo anakuwa na Mamlaka ya ki MUNGU dhidi ya Nguvu za giza.

◼️Hivyo ni vizuri sana kila Mtu aliyefungwa na Nguvu za giza amhitaji sana YESU KRISTO ili Mtu huyo afunguliwe na kuwa huru dhidi ya Nguvu za giza.

✓✓Nguvu za giza zikiachia maisha yako au ya Familia yako au ya Ndoa yako au ya Ukoo wako ujue hizo nguvu za giza zikiachia tu basi hapo panaingia Wokovu, nguvu na ufalme wa KRISTO YESU Mwokozi.

✓✓Shetani na mawakala wake wote ni vizuizi vya mema, shetani akiondolewa tu ujue Wokovu unaingia, nguvu za kiroho zinaingia na ufalme wa MUNGU unaanza kuwahudumia wateule wa MUNGU.

Kwanini nasema shetani na mawakala zake ni vizuizi? 

Biblia inasema kazi zao ni kuzuia.

2 Wathesalonike 2:7 "Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa."

✓✓Inawezekana nguvu za giza zinakuzuilia kufunga ndoa, kufanikiwa, kupata kazi, kuzaa, kupona magonjwa n.k.
Mhitaji sana YESU KRISTO ili akuweke huru maana Sasa umeshajua ukiwekwa huru Nini kitatokea


✓✓Nguvu za giza zikiondolewa tu basi wokovu utaingia kwako, kwenye ndoa na kwenye kila baraka yako iliyokuwa imeshikiliwa na kuzuiliwa na nguvu za giza.

◼️Ili nguvu za giza ziachie maisha yako basi zingatia haya.

1. Ishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.

1 Petro 1:15 "bali kama yeye(YESU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

2. Fanya maombi ya kuziondoa nguvu za giza kwako au kwa ndoa yako au kwa familia yako au kwenye baraka yako yoyote.

Yeremia 5:14 "Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala."

3. Futa uhalali wa hizo nguvu za giza kuwa hapo.

Kutoka 22:18 '' Usimwache mwanamke mchawi kuishi.''

✓✓Unaweza kufuta uhalali huo kwa Maombi tu katika Jina la YESU KRISTO au wakati Mwingine kwa maombi yanayoambatana na sadaka.

Zaburi 4:5 "Toeni dhabihu za haki, Na kumtumaini BWANA."

4. Omba MUNGU katika KRISTO YESU azifukuze kwako hizo nguvu za giza.

Zaburi 6:9-10 " BWANA ameisikia dua yangu; BWANA atayatakabali maombi yangu. Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika."

Omba leo na MUNGU atakuonekania.

Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments