AHADI YA MUNGU KWAKO NI UHAKIKA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

✓✓Ahadi ya MUNGU siku zote ni ndio na kweli.

✓✓MUNGU kama alisema na wewe kitu kwamba atakutendea hakika atakutendea.

✓✓MUNGU hawezi kamwe kusema uongo bali akisema kitu lazima atakitimiza.

Hesabu 23:19 "MUNGU si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?"

✓✓MUNGU akikuahidi jambo hakika atalitimiza.

◼️Ahadi ya MUNGU ni nini?

✓✓Ahadi ya MUNGU ni sharti alilojipa MUNGU ili kulitimiza.

Ahadi ya MUNGU ndani yake imebeba agano na kauli yake juu ya kutimiza hicho alichoahidi.

Ngoja tuangalie kidogo juu ya ahadi ya MUNGU kwa Waisraeli.

Yoshua 21:43-45 " Basi BWANA aliwapa Israeli nchi hiyo yote, ambayo aliapa kwamba atawapa baba zao; nao wakaimiliki, na kukaa mumo. Kisha BWANA akawapa raha pande zote, sawasawa na hayo yote aliyokuwa amewaapia baba zao; wala katika adui zao wote hakusimama hata mtu mmoja miongoni mwao mbele zao; yeye BWANA akawatia adui zao wote mikononi mwao.
Halikuanguka neno lo lote katika jambo lo lote lililokuwa ni jema ambalo BWANA alikuwa amelinena katika habari ya nyumba ya Israeli; yalitimia mambo yote."

Biblia inasema kwamba halikutanguka hata neno moja katika yale aliyoyaahidi MUNGU kwa Waisraeli.

Kwanini halikutanguka neno?

✓✓Ni kwa sababu ahadi ya MUNGU imebeba agano ndani yake hivyo MUNGU atalitimiza agano hilo la ahadi.

MUNGU alitimiza kile alichoahidi kwa Waisraeli.

Biblia inasema kwamba MUNGU alitenda kama alivyowaapia.

MUNGU akikuahidi kitu hutimiza, ukiona amechelewa usidhani amesahau bali kwa majira yake lazima atatimiza.

Hata kama wewe utaona MUNGU amechelewa lakini kama ni yeye alisema basi hakika atatimiza.

◼️Ahadi za MUNGU kwa watoto wake katika KRISTO YESU hutumia.

Biblia inasema katika Yoshua 21:45 kwamba "Halikuanguka neno lo lote katika jambo lo lote lililokuwa ni jema ambalo BWANA alikuwa amelinena katika habari ya nyumba ya Israeli; yalitimia mambo yote."

◼️Ahadi za MUNGU zilizo katika yeye ni ndio na kweli.

2 Wakorintho 1:20 "Maana ahadi zote za MUNGU zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; MUNGU apate kutukuzwa kwa sisi."

◼️YESU KRISTO akikuahidi hakika atatimiza.

✓✓MUNGU akisema na wewe kwa ndoto au kwa maono juu ya kukutendea kitu fulani chema hakika atatimiza.

Uwe tu na uhakika kwamba aliyesema na wewe ni MUNGU mwenyewe katika KRISTO YESU na kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.

Hata kama utaona ndoto hiyo imechelewa ingoje maana hakika itatimia kama ni MUNGU alisema na wewe.

Habakuki 2:3 "Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia."

✓✓MUNGU akisema amesema na atatimiza hakika.

✓✓Bwana YESU KRISTO ni mwaminifu na wa haki hakika akisema kitu kwako atatimiza.

Ahadi za MUNGU ni ndio na kweli hivyo jitenge tu mbali na vitu vinavyoweza kuzuia ahadi hizo za MUNGU zisitimie kwako.

Mfano sasa umeokoka na unaishi matakatifu ya Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana, na kwa sababu kwa sasa uko katika kusudi la MUNGU basi MUNGU anasema na wewe kwamba atakupa kitu fulani unachokihitaji, ahadi hiyo ni halisi kabisa lakini mfano kama MUNGU amekusudia kukupa baraka hiyo mwishoni mwa mwaka ujao na wakati huo ukifika MUNGU anamtuma Malaika ili akuletee baraka yako hiyo uliyoahidiwa na yeye lakini Malaika anapofika tu anakukuta umeshaacha Wokovu, umekuwa mwabudu shetani na humtaki YESU KRISTO tena, anakukuta unazini au unaiba n. K, hakika Malaika hatakupa baraka hiyo maana umelikimbia kusudi la MUNGU.

✓✓Hivyo ukilikimbia kusudi la MUNGU ujue umeikimbia na baraka ya MUNGU hata kama alikuahidi kwamba ataitimiza.

Anayekuwa amezuia kutimia kwa baraka hiyo kwako ni wewe na sio MUNGU.

Yoshua 24:20 "Kama mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema."

✓✓Hivyo unapoingoja ahadi ya MUNGU kwako basi baki katika kusudi la MUNGU.

✓✓Kumbuka ahadi anayotoa MUNGU ndio hiyo hiyo anayotoa YESU KRISTO na ni ndio hiyo hiyo anayotoa ROHO MTAKATIFU hivyo ahadi hiyo lazima itimie.

Ahadi ya YESU KRISTO kwako ndio pia ahadi ya MUNGU kwako na ndio pia ahadi ya ROHO MTAKATIFU kwako.

Ndugu hakikisha tu unajitenga mbali na vitu vinavyoweza kuzuia ahadi za MUNGU kutimia kwako.

Vitu vinavyoweza kuzuia ahadi za MUNGU kutimia kwako ni hivi.

1. Dhambi

Isaya 1:4 "Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha BWANA, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma."

2. Kutoka kwenye kusudi la MUNGU.

2 Nyakati 15:2 ".............. " BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi."

3. Kutokumsikiliza ROHO MTAKATIFU.

Wagalatia 5:16 "Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."

4. Kuacha Wokovu wa KRISTO.

Wagalatia 1:6-7 " Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya KRISTO, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya KRISTO."

5. Kutokuifanyia kazi sauti ya Neno la MUNGU inayopelekea kutokuzijua kanuni za ki MUNGU za kukufanya ahadi za MUNGU kutimia kwako.

Kumbu 28:15-19 " Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani. Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,"

Nini ufanye?

1. Mgonje MUNGU maana atatimiza ahadi yake kwako.

Zaburi 37:7 "Ukae kimya mbele za BWANA, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanyaye hila."

2. Ishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi.

1 Petro 1:15 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

3. Endelea na maombi na uwe mtu wa shukrani kwa MUNGU.

1 Wathesalonike 5:17-18 "ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya MUNGU kwenu katika KRISTO YESU."

4. Msikilize ROHO MTAKATIFU na mtii sana ili akupeleke kwenye kutimia ahadi za MUNGU kwako.

Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments