BAADHI YA MAKOSA MAKUBWA SANA WANAYOYAFANYA BAADHI YA WATUMISHI WA MUNGU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 




Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

✓✓Ni Muhimu sana Mtumishi wa MUNGU kumpa MUNGU Utukufu katika Mambo yote ya huduma.

Zaburi 29:1-2 " Mpeni BWANA, enyi wana wa Mungu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu; Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu."

✓✓Kama Malaika alikataa kusujudiwa na Mwanadamu kwanini Wewe Mwanadamu utake kusujudiwa na watu?

Ufunuo  22:9 "Naye akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako, na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. Msujudie MUNGU."

✓✓Ni Muhimu sana Mtumishi kufanya kila juhudi ili YESU KRISTO ajulikane na sio yeye Mtumishi ajulikane.

2 Wakorintho 4:5 "Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali KRISTO YESU ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya YESU."

✓✓Ni Muhimu sana kuwafanya watu wote kuwa wa YESU KRISTO na sio kuwafanya kuwa wa kwako au wa dhehebu lako.

Yohana 10:16 "Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.'

Hapo chini ni baadhi ya makosa makubwa wanayoyafanya baadhi ya Watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU.

1. Kuwafanya waamini wawe wanafunzi wao na sio wanafunzi wa YESU KRISTO.

✓✓Bwana YESU aliagiza kwamba tuwafanye watu wote wawe wanafunzi wake na sio wetu sisi watumishi.

Mathayo 28:19-20 " Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari."

Leo kuna mtu wa Kanisani ukiongea naye robo saa utashangaa anamtaja Mchungaji wake mara 20 huku katika robo saa hiyo anamtaja Bwana YESU mara moja tena katika mifano tu, haya ndio makosa na madhara ya mtumishi kuwafanya waamini kuwa wanafunzi wao na sio wa YESU KRISTO, haya ni makosa katika KRISTO.

2. Kuwafanya waamini wawe wanafunzi wa dhehebu na sio kuwafanya wawe wanafunzi wa YESU KRISTO Mwokozi.

Madhehebu yanayofundisha watu kuwaona dhehebu lao tu ndio waenda mbinguni hivyo kuwafanya waamini walione dhehebu ndio tiketi ya uzima wa milele wakati si kweli.

✓✓Kumbuka YESU KRISTO hakuwahi kufundisha kwamba tuwafanye waamini wawe wanafunzi wa dhehebu bali tuwafanye wawe wanafunzi wake.

Yohana 8:31-32 " Basi YESU akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru."

Hata ukisoma Biblia utashangaa katika Biblia nzima neno "Dhehebu " linapatikana mara tano tu, hiyo ni kuonyesha kwamba kwa MUNGU madhehebu sio kipaumbele bali kipaumbele ni watu Kuokoka na kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Mwanaye huku wakiwa watu wa ibada Kanisani, sasa katika wakati huu watumishi wengi wamewafundisha waamini kuliona dhehebu ndio msaada kuliko hata YESU, huo ni upungufu mkubwa wa kulielewa kusudi la MUNGU.

Kuna watu leo hadi wamefundishwa kutokusalimiana wala kukaribiana na watu wa madhehebu mengine.

Kuna watu wamefundishwa kuyachukia madhehebu mengine.

Ninaposema madhehebu sina maana kwamba ujiunge kila dhehebu bali hakikisha dhehebu hilo unalojiunga nalo injili yao ni YESU KRISTO anayeokoa na wanalitumia kwa haki neno la MUNGU katika ROHO MTAKATIFU.

Sasa ajabu ni kwamba madhehebu hayo hayo ambayo yanaisimamia kweli ya MUNGU na wanahubiri Wokovu wa KRISTO bado Wachungaji wanawafundisha waamini kulithamini dhehebu kuliko hata Biblia, ni hatari sana.

Ni heri kuwafanya waamini kuwa wanafunzi wa YESU KRISTO hivyo hata kama hawako katika dhehebu lenu lakini popote watakapokuwa watabaki na YESU KRISTO Mwokozi huku wamkitii MUNGU katika mambo yote.

3. Kuwafanya waamini wawe wanafunzi wa vitu na sio kuwafanya waamini wawe wanafunzi wa YESU KRISTO.

◼️Hii ni hatari sana sana katika Kanisa.

Kuna watu nimewahi kuongea nao na niliishia kuduwaa.

Mtu mmoja siku moja aliniambia nimuombee maana ajali zinamwandama hata kama kila siku anapaka nyumba na gari yake kwa maji ya upako.

Nilimuuliza maswali mengi sana lakini alinihakikishia kwamba ana zaidi ya mwaka mmoja hajawahi kufanya maombi hata dakika moja bali kila siku huwa ananyunyuzia chumba chake cha kulala na gari yake kwa maji aliyopewa kanisani.

 Maji yakiishia anafuata tena maji, siku zote yako ndani ya gari lake lakini akaniambia mara kwa mara anakabwa kichawi usiku na ajali za gari zinamwandama.

 Nilipomwambia kwamba inawezekana hayo maji ya upako ndio mlango wa nguvu za giza kumtesa alinishangaa sana. Sasa kwake yeye YESU KRISTO sio Muhimu tena maana maji ya upako yameshachukua nafasi ya YESU na nafasi ya MUNGU.

◼️Ndugu zangu ni vyema sana kujua mbamba MUNGU huwa hahitaji visaidizi ili kutenda miujiza au kukutendea kitu, unahitaji maombi tu katika jina la YESU KRISTO.

◼️YESU KRISTO hahitaji visaidizi kutenda miujiza.

Ufunuo upo lakini ufunuo huwa ni wa siku moja tu na sio wa kudumu, na mtumishi ujiridhishe kwamba ni kweli ni ROHO MTAKATIFU amekufunulia na sio zaidi ya hapo.

Leo kuna watu wamefanywa kuwa wanafunzi wa vitu na sio kuwa wanafunzi wa YESU KRISTO, hiyo ni mbaya sana.

Leo kuna watu hawahitaji tena Neno la MUNGU ila wanahitaji mafuta ya upako, chumvi za upako, keki za upako, barafu za upako n.k, haya ni makosa makubwa ya baadhi ya watumishi.

Kuna watu leo hawamhitaji YESU hata kidogo ila wanahitaji tu miujiza yake, ni hatari sana.

Kuna hadi watumishi wamewafanya waamini wawe wanafunzi wa shetani na sio kuwafanya kuwa wanafunzi wa YESU KRISTO maana watumishi hao hawahubiri wokovu tena bali wanahubiri vitu vya upako na madhehebu na taratibu za Kanisa ambazo haziendani na Biblia.

Watumishi wamewabadilisha waamini wa kuwafanya wajue tegemeo lao sio YESU KRISTO tena bali tegemeo lao ni vitu vya upako na miujiza.

Lengo kuu la Biblia ni kuwafanya Wakristo wawe wanafunzi wa YESU KRISTO na sio vinginevyo.

Yohana 13:35 "Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi."

Nini nataka kusema?

" mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana(YESU), mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya MUNGU; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba(MUNGU), aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye(YESU) tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;
naye ni mfano wa MUNGU asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.-Wakolosai 1:10-15"

Nini YESU KRISTO anataka kusema kwako?

" Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo3:5-6 "

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments