FAIDA ZA KUMSHUKURU MUNGU.

Na Mwl Peter Mabula, Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe sana ndugu zangu wote.

Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

Kwanza maana ya ''kumshukuru MUNGU'' ni kuonyesha ishara ya kuridhika na jambo la wema alilokufanyia MUNGU.
Maana ya pili ya kumshukuru MUNGU ni kusema kwa maneno mazuri ya kutoa shukrani kwa kwake kwa wema aliokufanyia.

Yona 2:9 "Lakini mimi nitakutolea sadaka kwa sauti ya shukrani; Nitaziondoa nadhiri zangu. Wokovu hutoka kwa BWANA."

Yapo mambo mengi sana ya kukufanya umshukuru MUNGU.
Inawezekana kalenda ya kichawi mwaka huu juu yako ni kwamba usimalize mwaka huu ukiwa hai, lakini YESU KRISTO amesema uishi ndio maana unaishi, ndugu mshukuru MUNGU.
Mwanamke mmoja alikuwa anaombea mwanamke mwingine aliye kwenye ndoa afe ili aolewe yeye, ni akili za kishetani sana hizo, lakini vipi kama ni wewe ndugu uko kwenye ndoa na kuna mtu nje anatamani ufe ili aoane na mwenzi wako? ndugu unatakiwa sana kumshukuru MUNGU kwa maombi na sadaka.
Mtu mmoja mwenye kazi nzuri kuna watu walikuwa wanamuombea afe ili wachukue nafasi yake, ndugu hakika una kila sababu ya kumshukuru MUNGU aliyeziumba mbingu na dunia, mshukuru Bwana YESU KRISTO kwa neema yake ya Wokovu kwako.
Inawezekana ratiba ya kuzimu kuhusu wewe ilikuwa kwamba uwe kichaa mwaka huu, au ufe, au upoteze vitu vyote au uwe mlemavu n.k lakini MUNGU Baba akasema na uwe salama ndio maana uko salama hadi Leo, ndugu ona umuhimu mkubwa wa kumshukuru MUNGU kwa maombi na sadaka ya shukrani.

Zaburi 95:2-3 " Tuje mbele zake kwa shukrani, Tumfanyie shangwe kwa zaburi. Kwa kuwa BWANA ni Mungu mkuu, Na Mfalme mkuu juu ya miungu yote."

Inawezekana wachawi walichora ramani ya wewe kupitia, ramani hiyo ni magonjwa, vifungo, kuteseka na kila aina ya ubaya lakini MUNGU akakulinda na kukupa uzima, ndugu hakikisha unamshukuru MUNGU kwa maombi na sadaka ya shukrani.

Zaburi 116:17 "Nitakutolea dhabihu ya kushukuru; Na kulitangaza jina la BWAMA;"

Hakuna aliye hai Leo atakayekosa nafasi ya kumshukuru MUNGU kwa ulinzi wa mwaka mzima.

Ndugu zangu, tunaishi tu kwa sababu MUNGU wetu ametaka tuishi, hivyo ni vyema sana kuwa na muda wa kumshukuru MUNGU.

Faida za kumshukuru MUNGU.

1. MUNGU atakuponya na hatari.

Ukisoma Danieli sura ya 6 utaona jinsi ambavyo watu wabaya walitunga sheria ya dharula ya siku 30 ili tu Danieli afe asimalize mwaka huo.
Mfalme bila kutafakari akaipitisha sheria hiyo ambayo imeundwa ili watu wote wasujudie sanamu, watu wale walijua kuwa Danieli ni Mteule wa MUNGU anayejielewa asiyeweza kusujudia sanamu hivyo walijua Danieli atagoma amri mpya hiyo ndio maana wakapitisha kwamba atakayeshindwa kutii sheria hiyo auawe, yaani kwa lugha nyepesi watu wale mawakala wa shetani walitaka Danieli asimalize mwaka huo akiwa hai.
Danieli aliijua siri ya kushinda roho ile ya mauti ni kuingia katika maombi ya kumshukuru MUNGU.

Danieli 6:10 Biblia inasema "Hata Danielii, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za MUNGU wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo."
Maombi ya kushukuru yana nguvu Sana maana hutengeneza ushindi wa ajabu sana.
Biblia inaonyesha kwamba shukrani ya Danieli mbele za MUNGU ilimfanya MUNGU kutuma Malaika waliomwokoa Danieli ili asife mwaka huo.
Biblia inasema katika Danieli 6:22 kwamba "MUNGU wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno."
Kuna nguvu kubwa sana katika kumshukuru MUNGU.
Biblia inaonyesha kwamba Danieli alikuwa anasali na kushukuru kwa MUNGU Mara tatu kila siku, matokeo yake aliponywa na hatari mbaya iliyokuwa mbele yake.
Hata wewe kwa kumshukuru MUNGU unaweza kuponywa na hatari yeyote iliyo mbele yako, kumshukuru MUNGU ni muhimu sana.
Ndugu hakikisha unamshukuru MUNGU kwa kukulinda mwaka mzima.

2. Kumshukuru MUNGU huleta ongezeko.
Marko 6:41 "Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote."

Bwana YESU katika andiko hilo anatufundisha jambo muhimu sana kwamba kuna nguvu ya ajabu katika kumshukuru MUNGU.
Biblia inasema kulikuwa na samaki 2 na mikate 5 ambayo kwa maombi ya kumshukuru MUNGU nguvu ya MUNGU ya ajabu ilishuka hadi kuwafanya watu zaidi ya 5000 wale chakula na kushiba na wengine kubakiza.
Kuna nguvu ya ongezeko katika kumshukuru MUNGU.
Unaweza kumshukuru MUNGU na ukapewa mwaka uliojaa neema kwako.
Hata katika hali ya kawaida kama wewe huwa unawapelekea zawadi ndugu zako kijijini, na ndugu wale ni mmoja tu ambaye kila ukimpa zawadi anakushukuru, siku moja ukawa na zawadi moja tu na unaelekea huko na zawadi hiyo inamtosha mtu mmoja tu huko, je utampa nani?
Ukweli ni kwamba utampa yule ambaye hukushukuru.
Hata kwa MUNGU iko hivyo.
Kushukuru ni jambo la muhimu sana.
Biblia inasema kwamba ni mapenzi ya MUNGU kwamba tumshukuru yaani ni agizo la MUNGU kwamba tumshukuru.

1 Thesalonike 5:18 ''shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya MUNGU kwenu katika KRISTO YESU.''

Neno mapenzi ya MUNGU ni sawa na neno matakwa ya MUNGU.
Neno ''matakwa'' maana yake jambo ambalo mtu analitaka.
Matakwa ya MUNGU maana yake ni jambo ambalo MUNGU analitaka, hivyo moja ya jambo ambalo MUNGU analitaka ni shukrani kutoka kwetu.
Hakikisha unamshukuru MUNGU maana ni mapenzi yake katika KRISTO YESU.

3. Sadaka ya shukrani huleta kukubaliwa na MUNGU.

Walawi 22:29 "Tena mtakapomchinjia BWANA dhabihu ya shukrani, mtamchinja ili mpate kukubaliwa."
Biblia iko wazi sana kwamba moja ya kitu kinachoweza kukufanya ukubaliwe na MUNGU ni sadaka ya shukrani, sadaka ambayo anaitoa mteule wa MUNGU anayeishi pia maisha matakatifu ya Wokovu.
Ndugu sadaka ya shukrani ni sehemu ya Shukrani kwa MUNGU na sadaka hiyo huleta kukubaliwa na MUNGU hivyo ndugu tafuta nafasi ya kumshukuru MUNGU hata kwa sadaka yako njema ya shukrani.
Sadaka ya shukrani kwa MUNGU haijaanza leo, ni utaratibu wa Kibiblia kabisa, Mfano ni huu.

2 Nyakati 29:31 "Ndipo Hezekia akajibu, akasema, Sasa mmejifanya wakfu kwa BWANA, karibuni mkalete dhabihu na matoleo ya shukrani nyumbani mwa Bwana. Basi kusanyiko wakaleta dhabihu na matoleo ya shukrani; na wote wenye moyo wa ukarimu, wakaleta sadaka za kuteketezwa.

4. Kumshukuru MUNGU ni kumtukuza.

Luka 17:12-19 " Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee YESU, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.
Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza MUNGU kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. YESU akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa MUNGU utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa."
Bwana YESU katika maandiko hata anatujulisha kwamba kumshukuru MUNGU ni muhimu sana, hapa waliponywa watu 10 ili aliyemshukuru MUNGU kwa uponyaji alikuwa ni mmoja tu.
Ndugu hakikisha unamshukuru MUNGU na kumpa utukufu wote.
Kuna faida nyingi katika kumtukuza MUNGU na faida mojawapo inaletwa na kumshukuru MUNGU.
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
By Mwl Peter  Mabula.
0714252292(whatsap, sadaka, ushauri na maombi)
MUNGU akubariki sana kwa kusoma somo hili.

Comments