HATUA SITA(6) ZA KUMPATA KIONGOZI SAFI WA KIROHO ILI AONGOZE VYEMA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.
Kazi ya kiongozi wa kiroho ni kuongoza, ndilo somo la leo.

✓✓Kuongoza ni nini?

◼️Kuongoza ni kuwa mbele ya kikundi ili kuelekeza njia au kuelekeza kitu.

◼️Kuongoza ni kutoa maelekezo ili mambo fulani yatendeke.

Ni utaratibu wa MUNGU kwamba viongozi wawepo mfano hai ni hapa ambapo mchakato wa kumfanya Joshua kuwa kiongozi ulianza 

Hesabu 27:18-22 " BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii. Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za BWANA; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia. Musa akafanya kama BWANA alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote;"

HATUA ZA KUPATIKANA KIONGOZI SAFI WA KIROHO:

Ukisoma maandiko hapo juu unagundua hatua kadhaa za kiongozi kupatikana.

1. Hatua ya kwanza ya kiongozi safi kupatikana ni MUNGU kumchagua mtu huyo ili awe kiongozi.

Hesabu 27:18 "BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ......"

◼️Hapa aliyemchagua Yoshua ni MUNGU mwenyewe.

✓✓✓Ni vyema sana kuwa na viongozi wa kiroho waliochaguliwa na MUNGU mwenyewe katika KRISTO YESU.

Hii inamhusu kila kiongozi wa kiroho iwe ni katika vyeo vya Kikanisa, Idara mbalimbali Kanisani au hata huduma na karama.

2. Hatua ya pili ni kiongozi safi kupatikana ni Kuwekewa mikono yaani kuombewa na Watumishi wa MUNGU.

Hesabu 27:18 ".......... ukamwekee mkono wako;"

◼️Musa aliambiwa na MUNGU amwekee mikono Joshua, hivyo viongozi wa kiroho inawapasa kuwekewa mikono yaani kuombewa.

Hii ya kuwekewa mikono ina maana nyingi, baadhi ya ni hizi;

✓✓Ili waanze na MUNGU katika uongozi wao

✓✓ili kuwakabidhi chini ya uongozi wa ROHO MTAKATIFU

✓✓ili kuwabariki wafanikiwe katika kazi ya uongozi ambayo Bwana YESU KRISTO amewapa.

Nimesema hii inawahusu viongozi wote wa kiroho na hata watu wenye karama, huduma na vipawa mbalimbali ambavyo watavitumia  kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU.

Mfano ni mtu ni Mwinjilisti anataka aanze kuwa anahubiri mitaani, inatakiwa kuwekewa mikono na kuombewa maana huko anakoenda kufanyia kazi hatakuwa tu Mwinjilisti bali kwa baadhi ya watu atakuwa kiongozi wa kiroho.

3. Hatua ya tatu ya baadhi ya viongozi kupatikana ni Kumweka huyo kiongozi mpya mbele ya wanaotakiwa kusaidiana nae na anaotakiwa kuwaongoza.

Hesabu 27:19 "kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; .........."

Kiongozi ni vyema sana hatua hii itokee kwake, hii ni Muhimu sana.
Haiwezekani Askofu au Mchungaji au Mzee wa Kanisa au Katibu wa Kanisa au Mwenyekiti wa Vijana au kiongozi wa Wanawake, haiwezekani Kiongozi wa namna hiyo apewe nafasi hiyo kimya kimya kisha yeye ndio aende kwa wasaidizi wake au kwa washirika kisha aseme "Kuanzia leo mimi ndio kiongozi wetu naomba tushirikiane katika kazi ya MUNGU " watu hao hawawezi kumwelewa vyema hata kama anafaa, watakuwa na maswali mengi sana, hawatamwamwini, wataona hajaitwa na MUNGU ila amejiita au ameletwa na shetani n.k
Kumbe tatizo tu hazijafuatwa Kanuni na hatua za Kibiblia za kupatikana kwa kiongozi wa kiroho hata aanze kazi.
Hivyo ni muhimu sana wenye mamlaka juu ya Kiongozi husika kufuata Kanuni hii ya kabla Kiongozi mpya hajaanza kufanya kazi basi wamweke mbele ya watakaosaidiana naye kazi na mbele ya atakaowaongoza.
MUNGU alimwambia Musa ampeleke Joshua mbele ya Eliazari ambaye watasaidiana na ampeleke kwanza mbele ya Waisraeli ambayo ndio atakuwa kiongozi wao.
Hii ni kanuni ya Biblia ya kuifuata katika mwili wa KRISTO wanapowekwa viongozi wapya.

◼️Kiongozi inabidi kwanza atambulishwe mbele ya atakaowaongoza ndipo ataaminika na mambo mengi yataenda vyema.

◼️ Kiongozi kabla ya kuanza kazi atambulishwe sio ajitambulishe yeye.

Sasa leo unaweza kukuta Kwaya ina migogoro kwa sababu tu Mchungaji amemteua kimya kimya mwenyekiti wa Kwaya, hivyo inafika siku ya Kwaya mwenyekiti hata hakuna anayemtii au kumsikiliza, watu wanadhani anajipendekeza ili awe Kiongozi kumbe ameshapewa uongozi tayari.

Itakuwaje mfano Mchungaji anajipeleka Kanisani na akifika tu anasema mimi ndio Mchungaji wenu mpya kuanzia leo maana Askofu amenipa nafasi hii. Hata kama ni kweli Mchungaji huyo amepewa nafasi hiyo na Askofu lakini atakuwa na mlima mrefu Sana wa kuuvuka hata kazi yake mpya eneo hilo ikae sawa, kanuni hizi za Kibiblia zisipofuatwa uongozi unaweza ukawa mgumu sana.

4. Hatua ya nne ya kiongozi safi kupatikana hata aanze majukumu ni kupewa usia mbele ya kundi.

Hesabu 27:19 "........... ukampe mausia mbele ya macho yao."

◼️Usia ni nini?

✓✓Usia ni kitendo cha kumwagiza mtu ili afanye jambo fulani na pia kumkataza kwa maneno ya hekima ili asifanye jambo fulani.

Mausia ni ya muhimu sana kuelezwa Kiongozi mpya mbele ya kundi atakaloliongoza, lakini ni lazima yawe maneno ya hekima kama maana ya neno usia inavyosema.

✓✓Musa alimhusia Joshua mbele ya Waisraeli wote.
Hata katika Kanisa la leo viongozi wapya wanatakiwa kupewa mausia kwa hekima kwamba ni nini wafanye katika uongozi wao na ni nini wasifanye kibaya katika uongozi wao.

Ni muhimu tu kumuusia kiongozi kwa hekima, ikiondoka hekima utakuwa unamharibia kiongozi huyo.

Hivyo hakikisha wewe mkuu wake unamuusia kwa hekima sana huyo kiongozi anayechukua nafasi fulani katika kundi la watu wa KRISTO YESU Mwokozi wetu aliye hai.

5. Hatua ya tano ya kupatikana kwa kiongozi safi ni kumfanya kiongozi huyo aheshimike ili watu wamtii.

Hesabu 27:20 "Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii."

Musa aliambiwa aweke sehemu ya heshima yake juu ya Yoshua ili watu waweze kumtii Yoshua ambaye ndiye Kiongozi mpya.

Hii maana yake nini?

✓✓Hii maana yake ni kwamba Musa ampe Joshua sehemu ya madaraka yake yaani Joshua achukue baadhi ya madaraka ya Musa.

Hiyo inatakiwa kufanyika pia leo katika Kanisa la MUNGU.
Mnapompa mtu Uchungaji mpeni na madaraka Kanisani hapo, sio Mchungaji anamtenga mtu kwa sababu ya dhambi harafu Askofu utamrudisha mtu huyo hata kama mnajua ni kweli katenda dhambi na inampasa kuwekwa chini ya marudio, ikiwa ni hivyo maana yake huyo Mchungaji hamjampatia madaraka.

✓✓Usimpe mtu uongozi kama haujampatia na madaraka pia, wewe unaweza kumshauri tu.

Hadi mtu anapewa uongozi naamini anakuwa amehakikishwa ana ROHO MTAKATIFU, ni mkweli, analitumia kwa haki Neno la MUNGU, anajitambua na anafuata kanuni za Kibiblia vyema.

Haiwezekani wewe Mchungaji umempa mtu uenyekiti wa Praise team(Kundi la kusifu na kuabudu) harafu ni wewe kila siku ndio unachagua Nyimbo za kusifu na Kuabudu na Tenzi hapo utakuwa hujampatia madaraka kiongozi huyo.

Haiwezekani wewe Mama Mchungaji ndio unasimamia mambo yote ya idara ya wamama Kanisani wakati Viongozi wa Wanawake wapo, hapo ni kwa sababu mmewapa uongozi bila kuwapa madaraka.

✓✓Viongozi ukiwapa uongozi bila madaraka ujue watu hawatawatii kamwe.

Kama kila kijana Kanisani jambo lake hadi apeleke kwa Mchungaji tu au mzee wa Kanisa ujue Mwenyekiti wa vijana ana cheo bila madaraka yeyote.
Kuna vitu vikubwa sana na vizito hivyo vinaweza kupelekwa kwa Mchungaji au Askofu au baraza la wazee wa Kanisa lakini kuna vitu vinatakiwa kupelekwa kwa viongozi wa idara, ukiona hata vitu vinavyotakiwa kwa kiongozi wa idara vinapelekwa kwa Mchungaji ujue Viongozi wa idara wana vyeo bila madaraka.

Musa alimpa Joshua baadhi ya madaraka yake ili Waisraeli wamtii, hata katika Kanisa leo inatakiwa iwe hivyo hivyo.
Mfano kama yamkini  Madaraka ya kufundisha, kuelekeza na kutoa mpango kazi yalikuwa ya Musa tu, sasa tunaona Joshua akiyafanya huku na Musa yupo, huko ndio kutoa Madaraka kwa Viongozi wanaochukua nafasi.

Unapomweka mtu fulani awe Kiongozi hakikisha unampa na madaraka ili aheshimiwe hata atimize vyema majukumu yake ya uongozi.

6. Hatua ya sita ya Kiongozi safi kupatikana ni Kiongozi huyo mpya kupewe nguvu ya kuwa na maamuzi ya mwisho kwenye eneo lake analoongoza .

Hesabu 27:21 "Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za BWANA; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia."

Mimi Peter Mabula nayapenda Maneno haya "KWA NENO LAKE watatoka, NA KWA NENO LAKE wataingia"

Unajifunza nini juu ya neno hili " kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia"?

Hii maana yake Joshua anapopewa uongozi anapewa na kuwa na madaraka na anapewa kuwa mwamuzi mkuu zaidi ndani ya kundi la watu anaowaongoza.

Maana ya kiongozi ni muongoza njia hivyo haiwezekani mfano Mchungaji anasema tutakutana Kanisani jumatano ijayo kwa ajili ya maombi ya kufunga harafu Askofu aseme mkutane Alhamisi kwa ajili ya maombi ya kufunga, hapo Mchungaji atakuwa anaingiliwa ili asiwe mwamuzi wa mwisho kwenye kundi lake.

Haiwezekani mwenyekiti wa Vijana anatangaza kwa Vijana kwamba jumamosi ijayo tukutane kanisani asubuhi ili kwenda kushuhudia mitaani kisha mzee wa Kanisa au Mama Mchungaji au Mchungaji atangaze kwamba Vijana jumamosi wasiende kushuhudia kwa sababu tu Mchungaji hataki wakati kiongozi huyo kabla ya kuwatangazia vijana alimjulisha Mchungaji na akakubaliwa.
◼️Ndugu zangu ni vyema sana katika kazi ya MUNGU na katika Kanisa la YESU KRISTO Duniani mambo yote yatendeke kwa kusudi la MUNGU, utakatifu na kwa ajili ya kuleta faida katika mwili wa KRISTO.

1 Wakorintho 14:26 "Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga."

◼️Ndugu zangu ni vyema mambo yote yatendeke kwa uzuri na utaratibu mzuri unaomwinua KRISTO na kuzaa matunda mema kwa Kanisa la MUNGU.

1 Wakorintho 14:40 "Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu."

Ndugu zangu ni vyema kanuni hizi za Kibiblia zikafanya kazi ndani ya Kanisa.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.
+255714252292( whatsapp, Sadaka ya kuipeleka Injili, Maombezi na ushauri wa kiroho).
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
Amen Amen 

Comments