![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Baada ya mtu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake mtu huyo huwa anakuwa kiumbe kipya maana sasa anaanza kuishi kwa kulifuata neno la MUNGU na sio mambo ya kidunia.
◼️Mtu baada ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake na kusamehewa dhambi mtu huyo anakuwa amezaliwa mara ya pili.
1 Petro 1:22-23 " Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo. Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la MUNGU lenye uzima, lidumulo hata milele."
Baada ya mtu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake hivi ndivyo inavyompasa kuishi mtu huyo.
1. Mtu huyo anaanza kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Waefeso 3:16-19 " awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya ROHO wake katika utu wa ndani. KRISTO akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake KRISTO, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa MUNGU."
2. Mtu huyo anazichukia dhambi zote na anachukua hatua ya kujitenga nazo mbali.
1 Petro 1:14" Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu."
3. Mtu huyo anaanza kujitolea kikamilifu mbele za MUNGU.
1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."
4. Mtu huyo anaanza kuwaza mema, kutenda mema, kupanga mema na kufikiri mema.
1 Yohana 3:9 "Kila mtu aliyezaliwa na MUNGU hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na MUNGU."
Ndio maana kama umeokoka kweli ni rahisi kuwasikia watu wakisema "Huyu ndugu amebadilika kweli, hata kuongea amebadilika kweli maana haongei mabaya tena, hanywi pombe tena n.k
5. Mtu huyo anakuwa mtu wa kufanya kazi Kisha baada ya kazi ibada na maombi.
Waebrania 10:25 "wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia."
6. Mtu huyo anakuwa mtu wa kulitafakari Neno la MUNGU na kuliweka moyoni ili limsaidie kila muda.
Zaburi 1:1-3 " Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa."
7. Msingi wa mtu huyo unakuwa ni YESU KRISTO.
1 Wakorintho 3:11 "Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, YESU KRISTO."
Msingi ni nini?
✓✓Kuna maana mbili za neno "msingi"
Maana ya kwanza msingi "ni jambo la muhimu."
◼️Kama YESU KRISTO ndiye msingi wako basi yeye ndiye atakuwa wa muhimu kwako kuliko vitu vyote, kuliko dhehebu lako, kuliko Mchungaji wako,kuliko nabii wako, kuliko mtume wako, kuliko mke wako au mume wako, kuliko mchunba wako, kuliko taratibu zenu za ibada, kuliko ndugu zako, kuliko wazazi wako na kuliko watu wote na kuliko vitu vyote.
◼️Hivyo kama wewe msingi wako ni YESU KRISTO basi mpe nafasi ya kwanza katika maisha yako maana ni yeye atakupa uzima wa milele ukishinda duniani, tena ndio matakwa ya MUNGU kwamba msingi wako uwe Mwanaye wa pekee.
Yohana 6:40 "Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho."
◼️YESU KRISTO kuwa wa muhimu kwako kuliko vyote ina maana sawa na MUNGU kuwa wa muhimu kwako kuliko vyote, hivyo mkimfuata KRISTO umemfuata MUNGU Mwenyezi.
✓✓Maana ya pili ya Neno "Msingi" ni kitu cha mwanzo ambacho ni muhimu kuwepo kabla vitu vingine kujengwa juu yake.
◼️Hivyo kama YESU KRISTO ni msingi wako basi katika fundisho lolote inatakiwa kipaumbele awe ni YESU KRISTO na kusiwepo na fundisho lolote ambalo nafasi ya kwanza hapewi YESU KRISTO kama Mwokozi.
Leo kuna watu msingi wao ni wachungaji wao, hata mchungaji akiwadanganya wao watafuata uongo huo.
Wengine msingi wao ni vitu vya upako kama maji ya upako, mafuta ya upako n.k, hawa hawaifuati kweli ya MUNGU ambayo inasema kwamba "Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, YESU KRISTO.- 1 Wakorintho 3:11 "
Wengine misingi yao ni siku mfano sabato, wengine msingi wao ni dhehebu, wengine msingi wao ni dini, Biblia inasema kwamba haitakiwi kuwapo na msingi mwingine kwa mtu katika suala la imani na wokovu.
"Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, YESU KRISTO.- 1 Wakorintho 3:11 "
✓✓Kitu chochote cha kiroho ni muhimu kisiende kinyume na KRISTO.
✓✓Fundisho lolote la Neno la MUNGU ni muhimu fundisho hilo limfunue YESU KRISTO kama msingi mkuu na Mwokozi anayeokoa wanadamu wote.
Ukiona dini yeyote au dhehebu lolote au mtumishi yeyote anahubiri kinyume na KRISTO yaani hamtii KRISTO wala kumfuata ujue mtumishi huyo msingi wake ni shetani na sio MUNGU.
Mwenye sikio la kusikia naamini ameelewae leo nini kinachompasa.
Pia mimi naamini ukiokoka utaishi kama iwapasavyo waliokoka.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji na hadi whatsapp).
Ubarikiwe

Comments