ISHI MAISHA MATAKATIFU.


Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele 




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

✓✓Nakuomba ishi maisha ya Kikristo ya Wokovu huku ukilitumia Neno la MUNGU kwa usahihi.

1 Petro 1:15 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

✓✓Kumbuka kwamba uthamani wako kwa MUNGU unatokana na namna unavyolitumia Neno la MUNGU kwa usahihi, yaani ishi kama Neno la KRISTO linavyokutaka uishi.

✓✓Kumbuka kiini cha kile Neno la MUNGU linaagiza ni wewe kuwa ndani ya YESU na kuishi maisha matakatifu katika yeye.

Yohana 15:4 '' Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.''

◼️Kuwa ndani ya YESU ni kukubali kuokolewa na yeye kisha unampokea kama Mwokozi wako Binafsi na kisha unaanza kuishi maisha ya kulitii Neno la MUNGU.

✓✓Kama kweli wewe umeshampokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako basi inakupasa sana kuishi maisha matakatifu.

✓✓Achana na dhambi ulizokuwa unazitenda kabla hujaokoka.

✓✓Achana na dhambi mpya zinazokunyemelea.

✓✓Usikubali ku-share chochote na shetani.

Unapokuwa mtu wa ku-share kitu na shetani ujue shetani atatumia ufahamu wako ili kukuletea uharibifu.

Kitu muhimu kwa mwanadamu ni ufahamu wake, shetani hujaribu sana kutumia ufahamu wa wanadamu, hivyo kitu cha thamani sana cha mwanadamu kiitwacho ufahamu huharibika.

Wapo watu muda wote wanawaza kufanya dhambi kwa sababu tu shetani amevamia fahamu zao.

Ndugu, Biblia inasema juu yako kwamba ''wala msimpe Ibilisi nafasi. -Waefeso 4:27''

Wako watu ni wasaliti wa ndoa zao, wako watu ni wasaliti wa uchumba mtakatifu, wako watu ni makahaba, wako watu ni waenda kwa waganga, kwa sababu tu shetani amekamata fahamu zao ili wasiende uzima wa milele.

◼️Wewe rafiki yangu amua kuishi Maisha matakatifu katika KRISTO YESU KRISTO Mwokozi.

Wako watu ni waongo, wezi, matapeli, waasherati, wachawi na hata yule anayesoma somo hili ila dhambi yake sijaitaja, hao wanafanya dhambi hizo kwa sababu tu shetani amekamata fahamu zao na anazitumia fahamu hizo ili kuwakosesha mbingu.

Ndugu, kumbuka kama wewe unatenda dhambi basi wewe ni wa shetani na sio wa YESU hata kama wewe ni mtu wa Kanisani, Biblia ndio inasema hivyo.

1 Yohana 3:8a '' tendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. ''

Ndugu, usimruhusu shetani atumie fahamu zako.
Yakobo 4:7b '' Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''



✓✓Wakati wengine wanaanguka dhambini, wewe simama vyema katika utakatifu.

✓✓Wakati wengine wanaangukia katika maovu, wewe ongeza juhudi katika kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.

✓✓Wakati wengine wanamwacha YESU, wewe ongeza juhudi kwa YESU kwa kumtumikia zaidi na zaidi.

1 Kor 15:58 '' Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA. ''

✓✓Wakati wengine wametekwa katika mafundisho ya mashetani yanayowakataza kuokoka, wewe Tembea kwenye Wokovu huku ukilitii Neno la KRISTO katika MUNGU aliye hai.

Wakolosai 3:16-17 '' Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye. ''

✓✓Wakati wengine wanamkataa ROHO MTAKATIFU au kumpinga, wewe mpokee ROHO MTAKATIFU na kubali kuongozwa na yeye siku zote za maisha yako.

Yohana 16: 13-15 ''
 Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi(YESU KRISTO), kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba(MUNGU) ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari. ''

✔️✔️Ishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

✓✓Wakati wengine wako busy na dunia, wewe hakikisha unakuwa busy na YESU Mwokozi wako.
Wakati wengine wanatangaza biashara zao kwa juhudi kubwa, wewe tangaza Neno la MUNGU la injili kwa juhudi kubwa.

◼️Amua kumwishia YESU KRISTO kwa utakatifu wote.

✓✓Kama kweli unaitaka mbingu mpya iliyoumbwa na MUNGU ambayo wateule wa KRISTO tutakaa basi amua kuishi maisha matakatifu.

✓✓Wakati wanaomkataa YESU sasa na kuishi maisha ya dhambi sasa baada ya siku ya mwisho watakuwa wanalia jehanamu, wewe okoka sasa na ishi maisha matakatifu sasa ili baada ya siku ya mwisho ushangilie uzima wa milele.

✓✓Ndugu, hakikisha sana unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU ulio wa thamani sana.

1 Petro 1:14-15 ''Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''

Jinsi ya kuweza kuishi maisha matakatifu fanya yafuatayo.

1. Mpokee YESU KRISTO na anza kuishi maisha inayoagiza Biblia kwa wateule wa MUNGU.

Matendo 16:31 '' ..... Mwamini Bwana YESU, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.''

2. Tafuta Kanisa la kiroho wanakofundisha kweli ya KRISTO na anza kuwa unahudhuria ibada na uwe sasa unafanyia kazi Neno la MUNGU unalofundishwa.

Waebrania 10:25 ''wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.''

3. Uwe na muda wa kuisoma Biblia kwa jinsi ya KRISTO na fanyia kazi Neno hilo la MUNGU.

Zaburi 1:2 ''Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.''

4. Uwe mtu wa maombi na usiache kuhudhuria ibada za maombi au mikesha ili kuimalisha kiroho chako kuhusu Maombi.

Isaya 43:26 ''Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako. ''

5. Mhitaji ROHO MTAKATIFU ili akusaidie kuwa mshindi dunaini.

Yohana 16:13 '' Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. ''

6. Kataa dhambi zote, jitenge na dhambi, zikimbie dhambi, kataa ushawishi wote wa dhambi na usitende dhambi.

2 Kor 4:2 '' lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la MUNGU na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za MUNGU.''

7. Jitenge mbali na marafiki wanaokushawishi kufanya dhambi au wanakushawishi kukaa mbali na ibada.

Zaburi 1:1 ''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. ''

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.



Comments