![]()  | 
| Na Mwl Peter Mabula  Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi  | 
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
◼️Ukiwa mteule wa KRISTO hakikisha una ROHO MTAKATIFU maana ndio ahadi kuu kwa wateule iliyoahidiwa na Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu.
✓✓Bila ROHO MTAKATIFU hatuwezi kuwa Kanisa hai la MUNGU.
✓✓Bila ROHO MTAKATIFU Kanisa haliwezi kutimiza kusudi la MUNGU, ndio maana Bwana YESU KRISTO ahadi kuu kabla ya kuondoka kwenda mbinguni ni ahadi ya kuja kwa ROHO MTAKATIFU.
Yohana 16:13 "Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake."
◼️Baada ya wewe kujazwa ROHO MTAKATIFU basi enenda katika ROHO MTAKATIFU.
Matendo 2:4 "Wote wakajazwa ROHO MTAKATIFU, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama ROHO alivyowajalia kutamka."
✓✓Baada ya kujazwa ROHO MTAKATIFU hakikisha unaenenda katika yeye siku zote.
Wagalatia 5:16 "Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."
✓✓Mambo mengi ya kiroho hutayaweza kamwe kama hauna ROHO MTAKATIFU.
Zekaria 4:6 " ........... Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema BWANA wa majeshi."
Sasa tatizo kwa Wateule wa MUNGU wengi sio kuwa na ROHO MTAKATIFU bali ni jinsi ya kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Niko hapa leo kwa neema ya MUNGU ili nikujulishe namna za kuenenda katika ROHO MTAKATIFU hata uwe wa MUNGU milele.
Inakupasa kuzingatia mambo haya yote chini, usiishie jambo moja tu bali hakikisha yote yanakuhusu siku zote za maisha yako ya wokovu wa KRISTO.
Jinsi ya kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
1. Kukubali kila ushauri wake siku zote na wakati wote.
Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."
Iga hata mfano huu kwa kutii ushauri wa ROHO MTAKATIFU.
Matendo 13:2 "Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia."
✓✓Hawa walitii maagizo ya ROHO MTAKATIFU kiasi ambacho hadi leo kwenye Biblia tuna vitabu 13 alivyoviandika huyo Sauli(Paulo) aliyepewa kazi maalumu na ROHO MTAKATIFU.
Hata  viongozi wa kiroho wa Paulo walitii maagizo ya ROHO MTAKATIFU ndio maana wakamwacha Paulo amtumikie MUNGU.
Kuna mahali mitume walikatazwa na ROHO MTAKATIFU wasihubiri kwanza katika mji fulani.
Matendo 16:6 "Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia."
Walitii sauti ya ROHO MTAKATIFU maana ROHO MTAKATIFU alikuwa anajua kila kitu kuhusu eneo hilo na watu wa eneo hilo ndio maana akawakataza mitume kwa wakati huo ili wasipate hasara, ni jambo jema sana kutii maagizo ya ROHO MTAKATIFU.
Kutii shauri la ROHO MTAKATIFU ndio kuenenda katika ROHO MTAKATIFU .
2. Kwa wewe kumruhusu ROHO MTAKATIFU aseme kupitia wewe.
Mathayo 10:20 "Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni ROHO wa Baba yenu asemaye ndani yenu."
✓✓Unapomruhusu ROHO MTAKATIFU aseme na wewe kupitia Kunena kwa lugha, kuhubiri, kufundisha n.k hapo unakuwa unaenenda katika ROHO MTAKATIFU.
3. Kwa wewe kukubali kuongozwa na ROHO MTAKATIFU siku zote.
Warumi 8:14 "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU."
Kukubali kuongozwa na ROHO MTAKATIFU ina maana mbili.
A. Wewe kukubali kuelekezwa njia ya kila kitu cha kiroho na ROHO MTAKATIFU, kwa pale ROHO MTAKATIFU atataka kukuelekeza.
B. Wewe kukubali kusimamiwa na ROHO MTAKATIFU katika mambo yote ya kiroho.
Mfano ni huu
Luka 2:27 "Basi akaja hekaluni ameongozwa na ROHO; ......."
Unapokubali kuongozwa na ROHO MTAKATIFU katika yale yote ROHO MTAKATIFU anataka kukuongoza, hapo hakika unaenda katika ROHO MTAKATIFU.
4. Kwa wewe kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU.
Luka 4:18 "ROHO wa BWANA yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,"
✓✓Unapokubali kumtumikia Bwana YESU KRISTO katika kweli yake ya injili ya Wokovu huku ukiongozwa na ROHO MTAKATIFU hakika hapo unakuwa unaenenda kwa ROHO MTAKATIFU.
5. Kwa wewe kukubali kufundishwa na ROHO MTAKATIFU.
Luka 12:12 "kwa kuwa ROHO MTAKATIFU atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema."
Kufundishwa na ROHO MTAKATIFU ina maana ya ROHO MTAKATIFU kukupa mafunzo, kukuelimisha na kukuwezesha kufanya jambo la ki MUNGU kulingana na kusudi la MUNGU.
✓✓Unapokubali kufundishwa na ROHO MTAKATIFU hakika hapo unaenenda katika ROHO MTAKATIFU.
6. Unapofanyia kazi kile ROHO MTAKATIFU anakukumbusha.
Yohana 14:26 "Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia."
ROHO MTAKATIFU kukukumbusha ina maana ya yeye kukuambia ufanye jambo ambalo umelisahau.
Mfano umtumikie MUNGU kama alivyokuambia, utimize nadhiri, usiende ulikokatazwa na MUNGU, utimize ahadi uliyoahidi mbele za MUNGU mfano matoleo n.k
✓✓Yaani ROHO MTAKATIFU kazi yake mojawapo ni kukufanya ukumbuke ili utimize kusudi la MUNGU au ili ufanikiwe.
Unapofanyia kazi kile ROHO MTAKATIFU anakukumbusha hapo hakika unaenenda katika ROHO MTAKATIFU.
7. Kwa wewe kukubali kuomba katika ROHO MTAKATIFU.
Yuda 1:20 "Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU,"
Kuomba katika ROHO MTAKATIFU ina maana mbili.
A. Kunena kwa lugha.
✓✓Kunena kwa lugha ni udhihirisho wa ROHO MTAKATIFU hivyo unapokuwa mtu wa kunena kwa lugha na kumcha MUNGU hapo unaenenda katika ROHO MTAKATIFU.
B. Kuomba kwa kufuata maelekezo ya ROHO MTAKATIFU.
Kuzingatia anachokuelekeza ukiwa katika maombi, kile anakujulisha uombee, Neno analokupa katika maombi.
✓✓Ukiwa ni mtu wa kuomba katika ROHO MTAKATIFU hapo unaenenda katika ROHO MTAKATIFU.
8. Kwa wewe kumtii MUNGU katika mambo yote.
Matendo 5:32 "Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na ROHO MTAKATIFU ambaye MUNGU amewapa wote wamtiio."
◼️Kwanza MUNGU huwapa ROHO wake wale tu wanaomtii, na unapokuwa mtu wa kumtii MUNGU katika KRISTO YESU katika mambo yote yaipasayo injili ya KRISTO, hapo unakuwa unaenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Zingatia pia kwamba kumtiii MUNGU ni kutii Neno lake.
1 Petro 1:23 "Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la MUNGU lenye uzima, lidumulo hata milele."
9. Unapokubali ROHO MTAKATIFU akufanye uwe mpya uliyetimia katika kusudi la MUNGU.
Tito 3:5 "si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na ROHO MTAKATIFU;"
ROHO MTAKATIFU kukufanya wewe kuwa mpya ina maana kwamba ROHO MTAKATIFU kukufanya usiishi tena katika maisha ya zamani, yaani maisha ya dhambi , yaani maisha ya kabla hujaokoka, yaani maisha ya zamani kabla hujampokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili,whatsapp, ushauri n.k).
Ubarikiwe

Comments