![]() |
Peter na Jemimah Mabula Watendakazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna mamlaka nne za MUNGU kwa Mkristo ambazo mamlaka hizo humfanya Mkristo kuwa mshindi daima.
Mamlaka hizo ni Jina la YESU KRISTO, Nguvu za ROHO MTAKATIFU, Damu ya YESU KRISTO na Neno la MUNGU la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
Leo nazungumzia Damu ya YESU KRISTO Katika kipengele kiitwacho Kazi za Damu ya YESU KRISTO.
Kwanza kabisa ni muhimu kila mtu kujua kwamba Damu ya YESU KRISTO ni kwa ajili ya Watu wote duniani, cha kufanya tu ni kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.
Ufunuo 5:9 "Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe(YESU) kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia MUNGU kwa DAMU yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,"
Damu ya YESU KRISTO ina kazi kubwa mno katika ulimwengu wa roho na matokeo ni makubwa sana katika ulimwengu wa mwili kwa Wateule wa MUNGU.
Wakolosai 1:19-20 " Kwa kuwa katika yeye(YESU) ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa DAMU ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni."
Lengo la somo hili ni wewe uwe unaomba katika jina la YESU KRISTO huku ukitumia Damu ya YESU KRISTO ili uwe huru na uwe mshindi dhidi ya nguvu za giza.
Pia lengo la somo hili ujue kazi za damu ya YESU KRISTO maana hata ujasiri tu wa kupaingia patakatifu, huo ujasiri utakuwa nao ukiwa tu na Damu ya YESU KRISTO.
Waebrania 10:19 "Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa DAMU YA YESU,"
Kuna kazi nyingi za Damu ya YESU KRISTO kwa Mkristo aliye na YESU KRISTO na anajua kuomba maombi akitumia damu ya YESU KRISTO.
Hivyo ukiona Watu au dhehebu wanajitenga mbali na damu ya YESU KRISTO ujue upo mahali pasipo sahihi.
Waebrania 13:20 "Basi, MUNGU wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu YESU,"
Damu ya YESU KRISTO sio vitu vya duniani , hivyo mtu asikudanganye lakini damu ya YESU KRISTO ipo tayari kwenye ulimwengu wa roho kwa ajili yako.
Damu ya YESU KRISTO ni ya muhimu Sana maana hata Mbinguni watakatifu walioko huko ni wale tu waliosafishwa Kwa damu ya YESU KRISTO.
Ufunuo 7:14 "Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika DAMU YA Mwana-Kondoo(YESU KRISTO)."
Baadhi ya kazi za Damu ya YESU KRISTO.
1. Damu ya YESU KRISTO hutengeneza agano jipya kati ya MUNGU na Mwanadamu aliyemwamini KRISTO.
Marko 14:24 "Akawaambia, Hii ndiyo DAMU YANGU YA AGANO, imwagikayo kwa ajili ya wengi."
Agano maana yake ni patana au kupatana hivyo tunapatana na MUNGU muumbaji wetu kwa damu ya YESU KRISTO.
Kuna maagano ya kabla ya YESU KRISTO kuja duniani lakini ni MUNGU mwenyewe ndiye aliyezungumzia agano jipya ambalo atalileta.
Yeremia 31:31-33 " Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya AGANO JIPYA na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema BWANA. Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema BWANA; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa MUNGU wao, nao watakuwa watu wangu."
Kwa hiyo ni kwamba kwa sasa sisi tuko katika agano jipya katika damu ya YESU KRISTO na hili agano jipya linaenda hadi kurudi kwa Bwana YESU mara ya pili.
2. Damu ya YESU KRISTO hufuta dhambi zote za mtu anayetubu kwa MUNGU katika KRISTO YESU.
Mathayo 26:28 "kwa maana hii ndiyo DAMU YANGU YA AGANO, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi."
Yaani Damu ya YESU KRISTO ina uwezo wa kulipa madeni yote ya dhambi ya Watu wote duniani wanaoamua kuokoka.
Ufunuo 1:5 "tena zitokazo kwa YESU KRISTO, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika DAMU YAKE,"
3. Damu ya YESU KRISTO huleta upatanisho kati ya Mwanadamu anayeokoka na MUNGU.
Warumi 3:25 "ambaye MUNGU amekwisha kumweka AWE UPATANISHO KWA NJIA YA IMANI KATIKA DAMU YAKE,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa."
MUNGU amemweka YESU KRISTO ili awe upatanisho kwetu kwa njia ya imani katika damu yake ya agano jipya.
Hivyo kama unahitaji upatanisho ujue unaihitaji damu ya YESU KRISTO ya upatanisho.
Wakolosai 1:20 "na kwa yeye(YESU) kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa DAMU YA MSALABA WAKE; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.
4. Damu ya YESU KRISTO husafisha Dhamiri, nafsi na mioyo yetu.
Waebrania 9:13-14 " Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake KRISTO, ambaye kwamba kwa ROHO wa milele alijitoa nafsi yake kwa MUNGU kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu MUNGU aliye hai?"
Damu ya YESU KRISTO husafisha dhamiri.
Dhamiri ni nini?
Dhamiri ni nia ya kufanya jambo.
Watu wengi wana nia mbaya tu Katika nafsi zao, hao wana dhamiri mbaya.
Inawezekana moyoni mwako unawaza mabaya tu, hutaki kuyawaza lakini uajikuta unayawaza, ndugu dhamiri yako inatakiwa kusafishwa kwa damu ya YESU KRISTO.
Ndugu, Omba maombi leo katika Jina la YESU KRISTO huku ukitumia damu ya YESU KRISTO kukusafisha dhamiri yako, ili uwe na dhamiri njema kuanzia sasa.
1 Yohana 1:7 "bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na DAMU yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote."
5. Damu ya YESU KRISTO inaleta ulinzi katika mwili, afya, familia, biashara, ndoa n.k kulingana na maombi ya mkristo mhitaji anayeomba.
Ufunuo 12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."
Hapa unahitaji tu kufanya maombi ili damu ya YESU KRISTO ifanye kazi kama ulivyoomba katika maombi yako.
6. Damu ya YESU KRISTO hututakasa na kutufanya tuwe huru.
Waebrania 13:12 "Kwa ajili hii YESU naye, ili awatakase watu kwa DAMU yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango."
Damu ya YESU KRISTO hutakasa.
Kutakasa ni nini?
Kutakasa ni kuondoa uchafu na kufanya kitu au mtu au eneo kuwa safi kiroho.
Damu ya YESU KRISTO kwa maombi yako inaweza kutakasa eneo la mwili wako unalotaka litakaswe, afya, ndoa, nyumba, ardhi n.k
7. Damu ya YESU KRISTO hutufanya tukae ndani ya YESU KRISTO.
Yohana 6:54-56 " Aulaye mwili wangu na KUINYWA DAMU YANGU anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake."
Kuinywa Damu ya YESU KRISTO ni kutafakari uwezo ulioko ndani ya Damu YESU KRISTO na kuutumia huo uwezo ulio ndani ya damu katika damu ya YESU KRISTO.
Pia ni muhimu kujua kwamba Mtu ambaye ameula mwili wa KRISTO na kuinywa damu yake ile iliyomwagika msalabani, ni yule ambaye anakaa ndani ya YESU KRISTO, na YESU KRISTO anakaa ndani yake.
8. Damu ya YESU KRISTO imetununua tuliokoka ili tuwe wa MUNGU kwa ajili ya uzima wa milele.
Matendo 20:28 "Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo ROHO MtakaTtifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, alilolinunua kwa DAMU YAKE mwenyewe."
Biblia inasema MUNGU ametununua sisi Kanisa kwa damu yake, hiyo ni kupitia YESU KRISTO Mwokozi wetu.
9. Damu ya YESU KRISTO hutufanya tuhesabiwe haki mbele za MUNGU.
Warumi 5:9 "Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika DAMU yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye."
10. Damu ya YESU KRISTO huleta ukombozi kwetu tuliompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wetu.
Waefeso 1:7 "Katika yeye huyo, kwa DAMU yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake."
Yako maeneo yako mengi yanahitaji ukombozi wa damu ya YESU KRISTO, kazi yako ni kufanya maombi ya ukombozi na damu ya YESU KRISTO itakukomboa.
Damu ya YESU KRISTO huleta ukombozi.
1 Petro 1:18-19 " Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa DAMU YA THAMANI, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO."
11. Damu ya YESU KRISTO hutufanya tuwe karibu na YESU KRISTO.
Waefeso 2:13 "Lakini sasa, katika KRISTO YESU, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa DAMU yake KRISTO."
12. Damu ya YESU KRISTO hunena mema.
Waebrania 12:24 "na YESU mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili."
Ni jukumu lako tu kuishi maisha matakatifu ya Wokovu na kuomba katika jina la YESU KRISTO ukiomba damu ya YESU KRISTO inene mema na itanena.
Inawezekana unasemwa vibaya sana na Watu, Omba damu ya YESU KRISTO inene mema kwako.
Inawezekana unataka damu ya YESU inene mema kwenye ndoa yako, biashara yako, afya yako, kibali chako, kazi yako, mwili wako, Familia yako, Ardhi yako n.k
Ndugu Omba na damu ya YESU KRISTO itanena mema.
Ndugu, husika na YESU KRISTO na damu yake kwenye maisha yako.
Warumi 6:22 "Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa MUNGU, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.'
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka, kuandika meseji na hadi whatsapp).
Ubarikiwe
Comments