KILA MWANANDOA AWE KAMA HAYUKO KWENYE NDOA.

Peter na Jemimah Mabula 
Watendakazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Siku moja niliona maono ya ajabu sana, siku hiyo kwenye maono nilijiona napita katikati ya uwanja  wa taifa uliopo Dar es salaam hapa Tanzania, yaani ule uwanja ulio pembeni ya uwanja wa uhuru, uwanjani pale nilitoka kona moja nikapita katikati ya uwanja hadi kona nyingine, nikasikia sauti ikisema "utahubiri injili ya KRISTO Tanzania nzima" Baada ya hapo nikajiona nikienda maeneo mengi mbalimbali ya Tanzania, mijini na vijijini nikihubiri na baada ya muda mrefu wa kuzunguka Tanzania nzima kuhubiri nikajiona narudi Dar es salaam na kuingia Kanisa moja siku ya ibada.

Nilijua vyema MUNGU alikuwa ananifundisha nini juu ya maono hayo na kutembea Tanzania nzima nikihubiri lakini kuhusu kuingia ndani ya Kanisa ndio chanzo cha somo hili.
Ndani ya maono hayo nikajikuta naingia Kanisani hapo na kumkuta Mchungaji akiwa nje ya Kanisa ila ndani ya uwanja wa Kanisa, nikamsalimia na wakati tunaongea tukasikia watu wanaongea ndani ya Kanisa, tukasogea mimi na Mchungaji kisha Mchungaji akauliza ''Kuna kipindi gani Kanisani muda huu?''

Mimi sikumjibu bali nikaingia Kanisani nikamkuta mama Mchungaji akiwa na mabinti kama saba, yaani akiwa na wanawake ambao hawajaolewa, binti mmoja kati yao alikuwa amekaa karibu na mlango wa kutokea, yaani mlango wa Kanisa wa kuingia na kutoka. Binti yule alikuwa hana furaha kisha mimi nikaanza kumsemesha maneno mazuri mazuri akafurahi kisha nikasema ''Natamani ningeitwa kufundisha mkesha wa mabinti'' kisha nikatoka pale Kanisani nikaenda Nyumbani kwangu kwa lengo la kuandaa masomo yaani mafundisho ya Neno la MUNGU. Nikafika nyumbani lakini ghafla nikajiona tena niko Kanisani pale nikitaka kuwafundisha watu somo fulani japokuwa walikuwa watu nwachache sana ibadani, walikuwa wachache na wengi wao walikuwa ni wanaume, mwanamke niliona kama mmoja tu. Nikasema ''Sasa nawaletea Neno la MUNGU '' na nilipomaliza tu kusema hivyo ROHO MTAKATIFU muda ule ule akaniambia kwa sauti kwamba ''fundisha watu wangu ujumbe huu KWA AJILI YA UZIMA WA MILELE KILA ALIYE KWENYE NDOA NA AWE KAMA HAYUKO KWENYE NDOA'' Nikapewa points za kufundisha. Na ujumbe huo niliosemeshwa na ROHO MTAKATIFU kwa maono ya wazi ndio huo nakuletea leo ndugu.

Ndugu nakuomba sana zingatia Neno hili.

1 Wakorintho 7:29 " Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana; "

Sio kwamba MUNGU anaichukia ndoa bali MUNGU anataka sana watu wake wawe katika ndoa zao takatifu.
MUNGU anataka kila mtu afunge ndoa takatifu.
MUNGU anataka kila mwanaume awe na mke wake waliyefunga nae ndoa Kanisani, MUNGU anataka kila mwanamke awe na mume wake waliyefunga nae ndoa kanisani.

◼️Lakini ROHO MTAKATIFU kupitia somo hili hataki ndoa imbadilishe mtu hata akasahau wajibu wake kwa MUNGU.

✓✓Hakikisha Ndoa haikubadilishi katika wito wako wa kwenda uzima wa milele.

✓✓Hakikisha Ndoa haikuondoi katika kusudi la MUNGU.

Baadhi ya maneno ambayo nilifunuliwa kwamba yanawakosesha baadhi ya watu walio katika ndoa ni haya.

1. Kutokutoa fungu la kumi.

Mwanamke anaolewa ila ana kazi zake zinazomwingizia kipato lakini akiwa ndani ya ndoa mume wake hutoa zaka kamili ya kipato chake lakini mke hatoi zaka akidhani kwamba kutoa kwa mume wake kunatosha japokuwa anajua kabisa kwamba fungu la kumi alilotoa mume halihusiki na kazi ya mke au biashara ya mke.

Kuna wengine mume hatoi zaka akisema kwamba alichotoa mke wake kinatosha, yaani mfano mke anatoa zaka elfu 10 iliyotokana na biashara zake au iliyotokana na pesa aliyopewa na mume wake ya matumizi yake binafsi na mume ana kazi inayompa mshahara wa milioni moja lakini yeye huwa hatoi zaka.
Kwa sababu tu mkewe katika kidogo chake anakitolea zaka.

Ndugu, inawezekana kabla hujaoa au kabla hujaolewa ulikuwa mwaminifu wa kutoa zaka, dhabihu na sadaka lakini baada tu ya kuingia katika ndoa umeacha kutoa kwa sababu tu mwenzi wako hutoa kutokana na kipato chake.

Biblia inasema usiache kutoa zaka mwaka hadi mwaka.

Kumbu 14:22 "Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka."

Kila aliye katika ndoa na awe kama kama hayuko katika ndoa ili tu kuendelea kubaki katika kusudi la MUNGU.

2. Kwenda ibadani.

Nilijulishwa kwenye maono kwamba wapo wamama siku ya ibada huwa hawaendi Kanisani.

Yaani mume anaenda Kanisani akimwacha mke wake anafua nguo au anapika n.k

Kwa mazingira hayo hayo inafika kipindi Mwanamke kila siku ya ibada anapanga kazi za kufanya maana mume wake amemwakilisha Kanisani.

◼️Ndugu zangu kwenda Kanisani hakuhitaji uwakilishi bali kwenda Kanisani kunamhitaji mtu binafsi na kwa faida ya roho yake.

✓✓Ndugu zangu, mambo ya ufalme wa MUNGU yanamhitaji kila mmoja hivyo kila mmoja kwa nafsi yake inampasa kuhusika.

Unakuta mke anaenda Kanisani lakini mume anabaki nyumbani bila sababu na kwa sababu mume huyo anampa mke sadaka ili ampelekee basi yeye anadhani hiyo inatosha.

 Yuko tayari siku zote sadaka yake iiende Kanisani ila yeye haendi, kwa mazingira hayo mnaweza kuwaambukiza hadi watoto wenu tabia hiyo ya mwenzi mmoja tu ndio anaenda Kanisani.

Ndugu zangu, Biblia inasema tusiache kukusanyikana wote ibadani.
Waebrania 10:25 "wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia."

Mwenzi mmoja katika ndoa akianza kutokwenda Kanisani itapelekea moyo wa ibada kuondoka kwake kisha baada ya hapo hata kazi alizotakiwa azifanye siku ambazo sio za ibada yeye ataziacha ili kazi hizo azifanye wakati wengine wakiwa ibadani siku ya ibada.

Ndugu, z kwa ajili ya mambo ya ufalme wa MUNGU kila aliye katika ndoa na awe kama hayuko katika ndoa ili tu kubaki katika kusudi la MUNGU LA UZIMA WA MILELE.

Inawezekana kabla hujaingia katika ndoa ulikuwa unahudhuria ibada zote za mafundisho ya Neno la MUNGU, ulikuwa unahudhuria ibada za katikati ya wiki, ibada za mikesha, ibada ya jumapili lakini baada ya kuingia tu katika ndoa huna tena muda na ibada, huwa unaenda jumapili moja moja ambayo utajisikia.

Huna tena kiu ya haki yaani kiu ya kujifunza Mambo ya ufalme wa MUNGU.

Mathayo 5:6 "Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa."

Huna tena njaa ya mambo ya rohoni hata uyahitaji hayo mambo ya rohoni.

Mathayo 5:3 "Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao."

Ndoa imekubadilishia msimamo wako thabiti wa kiroho, ni hatari sana.

◼️Ndugu yangu, MUNGU anakutaka juhudi yako uliyokuwa nayo kabla ya ndoa kuhusu mambo ya ufalme wa MUNGU uendelee nayo hata ukiwa ndani ya ndoa.

Hata kama hukuwa na juhudi ya ibada kabla ya ndoa basi hakikisha unakuwa na juhudi kubwa baada ya ndoa.

Warumi 13:11-14 " Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini. Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru. Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni Bwana YESU KRISTO, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake."

Kwa ajili ya mambo ya ufalme wa MUNGU kila aliye katika ndoa na awe kama hayuko katika ndoa.

Kuna watu wengine unaweza ukadhani alikuja kanisani ili apate tu mke au mume kisha aondoke maana kabla hajaingia katika ndoa alikuwa mwaminifu sana katika kazi ya MUNGU lakini baada tu ya kuingia katika ndoa amemsahau MUNGU wa Wokovu wake, ni hatari sana.

3. Utumishi kwa KRISTO.

Kuna watu kabla hawajaingia katika ndoa walikuwa na juhudi sana ya kumtumikia MUNGU ila ndoa ndio imewaondolea utumishi wao kwa MUNGU, ni hatari sana.

Bwana YESU anasema "Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.- Luka 14:26"

Ni ajabu sana ndoa tu ndio ikufanye usiwe tena mtumishi wa MUNGU?

Najua kuna kuwa na mimba kubwa na kuna kuzaa na kuna kuwa na mtoto mchanga, ni sawa katika mazingira hayo huwezi kumtumikia MUNGU kama mwanzo.
Jambo hilo la kuzaa na kulea ni la muda mfupi na ni sababu muhimu lakini nje na sababu hiyo hakuna sababu ambayo inaweza kukufanya mwanandoa uache kumtumikia MUNGU vyema.
Ni sababu hiyo tu moja ambayo inaweza kukufanya kwa muda fulani usitumikie kwa MUNGU kwa kasi lakini baada ya hapo inakupa kuendelea kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU.

Jiulize kwanini wafanyakazi baada ya miezi mitatu tu baada ya kujifungua anarejea kazini, wewe unashindwa kurejea katika kazi ya MUNGU kwa muda huo?

Angalau kama mhubiri unahubiri muda mfupi kisha unarejea nyumbani, hiyo inashindikana?

Hata kuna wamama akishajifungua anakaa hata miezi 10 bila kugusa Kanisani, huo sio utaratibu wa kibiblia, lakini pia ashukuriwe MUNGU maana kuna wamama wiki 2 tu baada ya kujifungua mnamuona Kanisani anakuja kumwabudu MUNGU.

Ndugu, inatupasa kuishindania imani ya wokovu wa KRISTO kwa ajili ya uzima wa milele, imani hiyo ni moja tu na ilitolewa na MUNGU mara moja tu.

Yuda 1:3 "Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu."

Hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuishindania imani hiyo kwa ajili ya uzima wa milele.
Kuna wanandoa hata kabla ya kuzaa wameshaacha ibada, na hao ndio wengi yaani ndoa imewabadilisha.
Kuna watu ana mtoto wa miaka mitatu lakini huwezi kumuona Kanisani hata kama mtoto ndio anataka kuja kanisani mama au baba anamkataza, tatizo ni moyo wa ibada ulishaondoka ndani ya mzazi huyo.

Mtoto hadi anamuuliza mama ''Mama tutaenda lini Kanisani?'' mama hata majibu hana maana moyo wa ibada ulishaondoka ndani yake, ni hatari sana.

Kuna watu kabla ya ndoa walikuwa waombaji, walikuwa waimbaji, walikuwa wahuburi, walikuwa washuhudiaji lakini ndoa imewabadilisha.
Ndugu yangu, ujumbe wa leo unasema kwa ajili ya ufalme wa MUNGU kila aliyeoa au kuolewa na awe kama hajaolewa au kuoa katika mambo ya MUNGU.
Biblia inamtaka kila mteule wa KRISTO amtumikie MUNGU siku zote

1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

Wewe mbona ndoa inakutoa kwenye utumishi?

4. Kusoma Neno la MUNGU na kulitafakari.

Kuna watu kabla ya ndoa walikuwa na muda wa kusoma Neno la MUNGU na kulitafakari na kulifanyia kazi lakini baada ya kuingia katika ndoa wameacha, wanajiona wako busy sana hivyo hawahitaji tena Neno la MUNGU, ni hatari sana.

Wafilipi 4:8 "Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo."

Ndugu, Biblia inakutaka kulisoma Neno la MUNGU na kulitafakari.
Biblia inakutaka ulifanyie kazi Neno la MUNGU.

Yakobo 1:22 "Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu."

Mbona ndoa imekubadilisha wewe ndugu?
Hakikisha kwa ajili ya ufalme wa MUNGU kisitokee chochote cha kukutenga na KRISTO YESU bali mtumikie kwa kweli na juhudi.

Warumi 8:38-39 " Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu."

◼️Ndugu zangu, kwa ajili ya uzima wa milele, kwa ajili ya kusudi la MUNGU, kwa ajili ya ufalme wa MUNGU aliye katika ndoa na awe kama hayuko katika ndoa ili tu asimkose MUNGU katika KRISTO.
Mwenye sikio la kusikia na asikie.
Ufunuo 3:22 "Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa."
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji na hadi whatsapp).
Share kwa rafiki zako ujumbe huu.

Comments