![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.
Ukisoma Waamuzi 11 Kuna mambo mengi Biblia inazungumza kuhusu Yeftha, baadhi ni haya;
Waamuzi 11:1-3 " Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine. Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; na watu mabaradhuli walikwenda na kutangamana na Yeftha, wakatoka kwenda pamoja naye."
✓✓Yeftha alikuwa mtoto wa Mwanamke Kahaba ila alikulia kwa Baba yake mzazi Aitwaye Gileadi, Baba yake alikuwa na mke na watoto lakini hao watoto walipokuwa wakubwa hawakumpenda Yeftha wakasema hana chake katika nyumba ya Baba yao kisha wakamfukuza kisha akaenda Tobu kuishi katika maisha yasiyotakiwa kuwa yake.
✓✓Inawezekana waliamua vyema kabisa kumfukuza kulingana na mitazamo yao lakini nafasi ya Yeftha ni kuja kuwa kiongozi wa Taifa na sio familia tu.
Ndugu zake walimuondoa kwenye nafasi yake akaenda kuishi kama Mtumwa au mkimbizi asiye na ndugu, inauma lakini ndivyo ilivyomtokea.
Lakini kumbe nafasi yake kwenye ulimwengu wa roho ilikuwa awe kiongozi sio wa familia yake tu au ukoo wake bali awe kiongozi wa jamii nzima ya kwao.
Yeftha alikuwa Mcha MUNGU na nafasi yake sahihi iliyopangwa na mbingu, hiyo nafasi ikamrudia kwa namna ya ajabu sana.
Nchi yake ilipovamiwa na Taifa la wana wa Amoni ndipo waligundua kwamba anayeweza kuwashindia vita ni Yeftha shujaa na mcha MUNGU.
Ilikuwa hivi;
Waamuzi 11:5-11 " Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu; wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni. Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu? Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi. Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi Kwamba mwanirejeza kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye BWANA akiwatoa mbele yangu, je! Mimi nitakuwa kichwa chenu? Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye BWANA atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako. Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kichwa, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya BWANA huko Mispa."
✓✓Watu wengi leo hawako katika nafasi zao.
✓✓Watu wengi wameruhusu maadui kuwaondoa katika nafasi zao sahihi.
✓✓Kuna mahali MUNGU anaweza kukuweka, ni mahali sahihi ila sijui kama uko katika nafasi yako.
Yeftha alikuwa mtoto wa mwanamke kahaba, alitengwa na kuondolewa katika nafasi yake.
Yeftha alipoondolewa kwenye nafasi yake wala hakulalamika wala kukata tamaa maana alijua MUNGU anaweza kumrejesha katika nafasi yake.
◼️Malalamiko hayawezi kumsaidia mtu ila maombi ndiyo yanaweza kumsaidia.
Yeftha alimtegemea MUNGU.
Yeftha ni mmoja wa Waamuzi ambao MUNGU aliwainua ili kuwa viongozi wa Israeli.
Nafasi yake kiuongozi ilikuwa kubwa sana kwenye ulimwengu wa roho ndio maana unaona shetani akiwatumia Watu wa Karibu ili kuhakikisha tu Yeftha hawi kiongozi wa Waisraeli.
Hata wewe Inawezekana kwenye ulimwengu wa roho unajulikana na kutambulika kama kiongozi mkubwa, Mtumishi mkubwa, Mfanyabiashara mkubwa n.k lakini shetani mapema kabisa amefanya kila mbinu ili wewe usikae kwenye nafasi yako.
Amua ndugu kuomba katika jina la YESU KRISTO ili ukae katika nafasi yako halisi.
Ndugu zake Yeftha walimuondolea nafasi yake katika ukoo na taifa lakini baadae wakapata wakati mgumu ndipo wakajua kwamba ni Yeftha tu ndio anaweza kuwasaidia, ndipo wakamwita Yeftha wakatubu kisha wakamrudisha katika nafasi yake.
Kuna watu leo nafasi zao ni kuolewa na kupata watoto katika ndoa zao lakini shetani amewaondolea nafasi zao za kuolewa ndio maana hakuna nafasi kwao ya kuolewa, kama ni wewe leo Omba kwa jina la YESU KRISTO ukisema ''Nitarejea katika nafasi ya kupata Mchumba na kuolewa na kuzaa watoto''
Kuna wamama wako katika ndoa lakini hawara wa mume amechukua nafasi ya mke katika ndoa, Leo mfukuze huyo wakala wa shetani ambaye ni hawara ili amwachie mume wako na uwe na imani ndani yako ukisema ''Nitarejea katika nafasi yangu kwenye ndoa''
Kuna nafasi nyingi pia katika ulimwengu wa roho MUNGU ametupa lakini mashetani kazi yao ni kuiba na kuharibu hivyo kama kuna nafasi yako imeibiwa kichawi leo irudishe kwa jina la YESU KRISTO na aamini ukisema ''Leo nitarejea katika nafasi yangu''
Inawezekana nafasi yako ni kupata kazi lakini wachawi wamekuloga kiasi kwamba wengine wote wanapata kazi isipokuwa wewe, Omba Kwa jina la YESU KRISTO kwamba ''Nitarejea katika nafasi yangu ya kupata kazi''
Inawezekana nguvu za giza wamekuandika kufa mwaka huu, Mtumainie MUNGU maana Biblia inasema anaweza kuwapa kuishi hata walioandikiwa kufa,
Zaburi 102:20 "Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa."
Ndugu leo Omba Kwa jina la YESU KRISTO ukisema ''kwa jina la YESU KRISTO nitaishi wala sitakufa hadi ratiba ya MUNGU ifike na sio ratiba ya mchawi''
Ndugu ukiwa vizuri na YESU KRISTO hakika anaweza kukurudisha katika nafasi yako ya kupona ugonjwa.
◼️Mfano ni huyu aliyerudishwa katika nafasi yake ya kuwa mzima.
Marko 5:34 "Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena."
◼️YESU anaweza kukurudisha katika nafasi yako ya kupata kibali.
Wafilipi 4:13 "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu."
YESU anaweza kukurudisha katika nafasi yako ya kuingia katika ndoa takatifu.
Marko 10:7-9 " Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha MUNGU, mwanadamu asikitenganishe.
◼️YESU anaweza kukurudisha katika nafasi yako ya kuishi.
Mfano ni huu wa Lazaro
Yohana 11:44 "Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye YESU akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake."
◼️YESU KRISTO anaweza kukurudisha katika nafasi yako ya kuzaa watoto wa kiume wa wa kike.
Zaburi 113:9 "Huweka nyumbani mwanamke aliye tasa, Awe mama ya watoto mwenye furaha."
◼️YESU KRISTO anaweza kukupa nafasi yako na kupata kazi.
Kumbu 28:3 "Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani."
◼️YESU KRISTO anaweza kukurudisha katika nafasi yako ya kumtumikia MUNGU.
Kumbu 13:4 "Tembeeni kwa kumfuata BWANA, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye."
✓✓✓Nakuambia hivi YESU KRISTO anaweza kukurudisha katika kila nafasi yako uliyoumbiwa na MUNGU ambayo shetani na mawakala zake waliichukua. Amua tu kuomba katika jina la YESU KRISTO huku ukiishi maisha matakatifu ya Wokovu.
Ukikaa vizuri na YESU KRISTO hakika anaweza kukurudisha katika nafasi yako ambayo watu walikuondolea kwa hila zao, wivu wao na chuki zao.
YESU KRISTO anaweza kukurudisha katika nafasi yako ndani ya moyo wa mume wako au mke wako.
YESU KRISTO anaweza kukurudisha katika nafasi yako ndani ya ndoa yako au familia yako au ukoo wako.
YESU KRISTO anaweza kukurudisha katika nafasi yako ya kuheshimiwa na kuthaminiwa.
YESU KRISTO anaweza kukurudisha katika nafasi yako ya kazi, nafasi yako ya ndoa, nafasi yako ya kuzaa, nafasi ya kiuchumi n.k
◼️Mtu wa maombi hashindwi labda tu aache kuomba.
✓✓Waambie wanadamu ''Nipeni muda nitarudi katika nafasi yangu''
✓✓Waambie adui zako katika ulimwengu wa roho ''Nipeni muda maana nitarejea katika nafasi yangu na hakuna atayeniondoa''
MUNGU pia ni MUNGU wa nafasi ya pili, atakupa kurudi katika nafasi yako ambayo wachawi na waganga waliiharibu au kuipindisha au kuiondoa.
Inawezekana pia ni wewe mwenyewe uliharibu maisha yako mwenyewe kwa uovu au kushawishiwa, ndugu hakika MUNGU ni MUNGU wa nafasi ya pili, tubu na okoka kisha omba kurudishwa katika nafasi yako njema na utarudi katika nafasi yako njema.
Omba MUNGU akupe kurudi katika nafasi yako kiroho na kimwili.
Omba MUNGU akupe kurejea katika nafasi yako ambayo MUNGU alikupangia hata kabla hajakuuumba, kumbuka MUNGU hajawahi kumpangia mtu mabaya hivyo tubia maovu yalikuletea mabaya na omba Bwana YESU akupe sasa kurejea Katika nafasi yako uliyoambiwa nayo na MUNGU.
Yusufu akina Potifa walimuona ni Mtumwa lakini MUNGU alimuona ni mkuu wa nchi namba mbili baada ya farao, hakina Yusufu alikuja kukaa kwenye nafasi yake.
Mwanzo 41:40-41 " Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.
Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri."
Waambie watu "Nipeni muda nitarudi katika nafasi yangu"
Hana walimuona kama tasa lakini MUNGU alimuona kuwa ni mama wa watoto 6 na ikaja kuwa hivyo.
1 Samweli 2:21 "Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA."
Waambie watu "Nipeni muda nitarudi katika nafasi yangu"
Bartimayo walimuona kama kipofu lakini asiyeweza kuona tena lakini Bwana YESU alimrudisha katika nafasi yake ya kuona.
Marko 10:52" YESU akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani."
Waambie wanaodhani kwamba baraka kwako haiwezekani , waambie"Nipeni muda nitarudi katika nafasi yangu"
Lazaro walimuona kama marehemu lakini YESU alimuona kama mzima wa afya na hakika akamfufua na kumrudisha katika nafasi yake ya kuisha.
MUNGU ni MUNGU wa nafasi ya pili kama ukiamua kuambatana naye katika KRISTO YESU.
Mimi Peter Mabula nsipenda sana habari ya Nabii Amosi, ni kwamba Watu walimuona Amosi kama Mchungaji wa mifuko na mtunzaji wa Bustani lakini MUNGU alimuona kama Nabii na akampeleka katika nafasi yake ya kuwa Nabii mkubwa katika taifa na wakarti wake.
Amosi 7:14-15 "Ndipo Amosii akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu;
naye BWANA akanitwaa, katika kufuatana na kundi; BWANA akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli."
Waambie wanakuwazia mabaya "Nipeni muda nitarudi katika nafasi yangu"
Ndugu, Kesho yako iko mikononi mwa MUNGU na sio mikononi mwa watu. wambie watu wakupe muda tu maana MUNGU anaenda kubadilisha historia ya maisha yako.
◼️Ndugu, Mche MUNGU na zingatia kanuni za ki MUNGU na ndipo MUNGU atakupa kurejea katika nafasi aliyokuumbia.
◼️Inawezekana kabisa tajiri wa leo ndio akawa masikini wa kesho na inawezekana kabisa masikini wa leo ndio akawa kuwa tajiri wa kesho, Ndugu fanya kazi halali huku ukimcha MUNGU katika KRISTO YESU, hata kama ni kazi ndogo lakini MUNGU Baba atakuinua na utakaa katika nafasi yako uliyoumbiwa nayo.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na whatsapp).
Ubarikiwe.

Comments