![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna kipindi nilfundisha somo kuhusu mikono kiroho na nikaahidi kwamba nitazungumzia pia miguu kiroho, ni leo ndio nazungumzia miguu kiroho, fuatilia somo hili hadi mwisho na utafaidika sana kiroho.
Njia mojawapo aliyotupa MUNGU ili tutambue kilichopo kwenye ulimwengu wa roho ni kwa kupitia ndoto na maono.
Watu wengi sana wanaomba maombi ya kujinasua na vifungo mbalimbali lakini walipojulishwa kwa ndoto au maono juu ya vifungo hivyo vya giza kwa kupitia kuona mashambulizi katika maeneo ya miili yao hawakushughulikia kimaombi hivyo tatizo likaendelea kuwapata hata kama wanatamani tatizo hilo litoke au liishe, ila tu hawakujua wanatakiwa kupambana na nini kwenye maombi.
Leo tunaangalia maana ya kushambuliwa miguu kwenye ulimwengu wa roho.
Miguu ina maana gani kwenye ulimwengu wa roho?
1. Miguu kiroho inabeba utayari na ina maana ya kuwa na utayari.
Waefeso 6:15 "na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;"
Miguu imebeba utayari kiroho sasa kwa sababu tunaangalia ni nini maana ya kushambuliwa miguu ndotoni au kwenye maono ni vyema tujue ni nani tunamuona ndotoni akitushambulia miguu yetu.
Ukishambuliwa miguu maana yake ni nguvu za giza wanakuondolea utayari.
Adui akikuondolewa ujue hutafanikiwa.
Utayari ni nini?
Utayari ni kukubali na kutii na kutenda ulichoambiwa.
Utayari ni kufanya jambo kwa ujasiri kutoka mazingira ambayo wengine wameshindwa kufanya jambo hilo.
Utayari ni kufanya maagizo uliyopewa.
Kuna watu wameondolewa utayari wa kupokea injili na wao wamekubali na kubakiza tu lawama.
Kuna watu kipepo wameondolewa utayari wa kufunga ndoa, mtu wa hivyo hata kama ana mchumba lakini mpango wa kufunga ndoa hana.
Yaani unakuta mtu ana mchumba miaka 7 na kila wakati mchumba wake akimwambia wafunge ndoa yeye anakuwa hana utayari, ndugu vingine sio kawaida ila ni vifungo vya giza ambapo nguvu za giza wamemuondolea utayari mtu huyo, sasa wewe mwenye utayari utahangaika sana huku mchumba wako hana utayari na hajui kwanini hana utayari.
Ngoja nikupe mfano hai kuhusu mimi mwenyewe.
Katika maisha yangu nilipanga nikifikisha miaka 24 nitaoa, nilikuwa tayari kabisa kuoa wakati huo lakini nilikuja kuoa nikiwa na miaka 28. Nini kilisababisha ikapita miaka 4 sina tena mpango wa kuoa?
Kuna mambo mengi yalitokea lakini hata sijui kwanini akili yangu kuhusu suala la kuoa ilikuwa kama haipo, kwanini nasema hivyo?
Nikiwa na miaka 27 Baba yangu mdogo mzee Moses Mabula alinipigia simu na kuniambia " Mwanangu Peter inakupasa kuoa sasa" baada ya kuambiwa hivyo niliona akili yangu ndio kama imerudi, niligundua kabisa ufahamu wangu kuhusu kuoa na kiu ya kuoa haikuwepo kabisa, baada ya muda tena kuna Mtumishi mmoja rafiki yangu aliniambia "Mtumishi unatakiwa uoe sasa" Maneno hayo na ya mzee wangu niliona ni kama yananichanganya na yalinitesa moyoni kwa miezi kadhaa, sio rahisi kunielewa lakini Nilichogundua ni kwamba watu wengi hasa wanaume hufungwa kiroho kwa kuondolewa kiroho utayari wa kufunga ndoa, kwa anayehusika na hili naamini anaposoma ujumbe huu ananielewa vyema mno. Sasa jiulize ninaambiwa suala la kuoa moyo wangu unaumia, nakuwa na wasiwasi naona kabisa ndio naanza kuzinduka, najiuliza mbona miaka mingi napanga kuoa nikiwa na miaka 24 mbona miaka imevuka sana na ndio utayari wa kuoa moyoni mwangu sina hata asilimia moja. Baadae nilipata ufunuo wa andiko la Mithali 19:14 ambalo ndio lilinifinyanga kiasi kwamba Nikasema " sasa ngoja nioe".
Inakuwaje jambo lako na lenye faida kwako hadi watu wengine ndio watumie juhudi kubwa kukushawishi ndipo utekeleze?
Ndugu zangu, vingine ni vifungo vya giza.
Ndugu zangu wako watu wengi sana wameondolewa na nguvu za giza utayari wa kuoa au kuolewa, leo unaweza kukutana mwanaume ana miaka 45 ana kazi nzuri, hana tatizo la kisaikolojia wala hana tatizo lakini ukimuuliza utaoa lini anakuambia labda miaka 8 ijayo.
Huyu ndugu ikiwa ni hivyo si mtoto wake akiingia kidato cha nne yeye atakuwa anakaribia kufikisha miaka 80?
Ndugu zangu mambo mengine ni vifungo vya giza.
Kuna wengine wanamilikiwa kiroho na majini mahaba hivyo majini hayo yamewaondolea utayari wa kuoa au kuolewa.
Unakuta Mwanamke ana miaka 44 hana mtoto, hajaumizwa katika mahusiano, hajawahi kuolewa lakini , hajakosa wachumba wala hana tatizo la kisaikolojia lakini hana mpango wa kuolewa, hivi ni vifungo vya giza, nguvu za giza zikikuondolea utayari wa kuingia katika ndoa utaona hata ndugu wanaokushauri uoe au uolewe, hao ndugu unaweza hata kuwachukia bila sababu kumbe tatizo ni wewe nguvu za giza zimekuondolea utayari.
Ndugu, upo utayari aina nyingi sana hivyo unapoona adui kwenye ulimwengu wa roho anashambulia miguu au anahusika na miguu ujue inawezekana anaharibu utayari wako wa mambo mema kwako.
Kuna watu huwa nawasiliana nao hadi nabaki nimeduwaa, mtu mmoja aliniambia amefunuliwa yeye ni Mtumishi wa MUNGU mkubwa sana, ana karama, ameokoka lakini hajui aanzeje kufanya kazi ya MUNGU, nikamwambia "Mimi ningekuwa wewe ningeanza leo leo "
Yeye anasema "Sijui jinsi ya kuanza"
Mwingine anasema ana msukumo wa kuhubiri Injili ila hajui ataanzaje, nikamwambia anza leo kwa kuhubiri mitaani, kuna mwingine amejiandaa kwa miaka zaidi 7 ili amtumikie Bwana YESU lakini hajui ataanzaje.
Ndugu zangu, mengine ni adui amekuondolea utayari pambana kiroho kisha anza haraka majukumu yako ambayo MUNGU katika KRISTO amekupa.
Kuna wengine wameondolewa utayari wa kujenga, wengine wameondolewa utayari wa kitu fulani chema chenye faida kwao.
Mwingine ana mtaji miaka 5 lakini hana utayari wa kuanza biashara.
Ndugu, Kuna nguvu ndani yetu na hiyo nguvu ipo katika maeneo mbalimbali ya kiroho.
Waefeso 3:20 "Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;"
Hivyo ukimwona adui kwenye ulimwengu wa roho anahusika na miguu yako ujue kuna kitu kinawindwa .
Mjue adui huyo ili ujue kupamana naye na kumshinda.
Wako maadui wengi unaoweza kuwaona ndotoni au kwa njia ya maono, baadhi ya maadui hao ni;
✓✓Nyoka maana yake mashetani, majini, mizimu, na kila roho ya kuzimu.
Hivyo kama nyoka anashambulia miguu tambua ni nani anataka kukuondolea utayari .
✓✓Mbwa maana yake roho ya uzinzi na uasherati, epuka dhambi hiyo maana inaweza kukuondolea utayari.
✓✓Mtu kama adui huyo ni wakala wa shetani au anawakilisha anataka kuna mtu anataka kukuondolea utayari kipepo.
Wakati mwingine unaweza usione wakati adui yako anapigana na miguu yako ila ukiona tu miguu yako imefungwa kamba au ukiona mtego umetegwa mahali na wewe unatembea kuelekea huko tambua miguu yako inawindwa kiroho ili kuondolewa utayari.
Zipo kwaya makanisani wana mpango wa kurekodi huu ni mwaka wa kumi bila mafanikio, wanafahamu kabisa kwamba kurekodi wimbo mmoja ni Tshs 70,000 wana uwezo wa kupata laki 3 ya safari kwa mda mfupi tu lakini kurekodi kumebaki kuzungumzwa tu, inawezekana walikusanya haraka pesa kubwa ya sare na wakanunua sare lakini kurekodi tu ndio imeshindikana kupata 70,000 kwa muda mrefu sana, tatizo ningeweza kwamba kwenye ulimwengu wa roho adui amewaondolea utayari kwenye eneo moja tu la kurekodi.
Je wewe unahisi adui kakuondolea utayari kwenye nini?
Na je kakuondolea utayari wa kupeleka injili?
Je kakuondolea utayari wa kununua kiwanja?
Je kakuondolea utayari wa wa kujenga, au kumalizia ujenzi?
je ni utayari upi adui kakuondolea?
Leo kimaombi katika jina la YESU KRISTO hakikisha utayari wako wa ki MUNGU unarudi ndani yako.
Hata Mimi nitajiombea utayari na kuwaombea marafiki zangu utayari
2. Maana ya pili ya miguu kwenye ulimwengu wa roho ni mlango wa kuingia kwenye nafsi ya mtu.
Zaburi 56:6 “Hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa wameniotea nafsi yangu.”
Kwa namna hiyo ndotoni unaweza kuona nyoka kajiviringisha mguuni kwako kumbe ni julisho kwamba kwamba nafsi yako imeshikiliwa au imekamatwa na nguvu za giza.
Unaweza ukashangaa kila unaliwaza au unalotamani ni baya tu siku zote, unajaribu kuomba unaona kwenye ulimwengu wa roho miguu yako ina tatizo, kumbe hilo ni julisho kwamba nafsi yako imekamatwa na nguvu za giza ndio maana badala ya kuwaza ya MUNGU wewe unawaza ya shetani aliyeikamata nafsi yako.
Kumbuka maamuzi yote na mipango yote unayofanya juu ya maisha yako vinatokea kwenye nafsi yako. Hivyo nguvu za giza zikiikamata nafsi yako zimekamata maisha yako maana maamuzi yako yote hutoka kwenye nafsi yako, mipango yako yote hutokea kwenye nafsi yako.
Hivyo ikikamatwa kipepo nafsi yako ujue umekamatwa wewe, sasa kwa neema ya MUNGU huwa unaonyeshwa kwa njia ya ndoto au maono ukiona mashambulizi miguuni au tatizo mguuni kwako na kumbe unajulishwa tatizo ni nini kwenye nafsi yako.
Ndugu, kwa maarifa haya ya kiroho fanyia kazi kimaombi ili ufunguliwe kifungo cha nafsi kinachokutesa.
Kumbuka kila jambo huanzia katika ulimwengu wa roho kabla ya kuonekana katika ulimwengu wa kimwili, mtu hufa katika ulimwengu wa roho kwanza kabla ya kufa katika ulimwengu wa mwili, mtu hufungwa vifungo kwanza katika ulimwengu wa roho kabla ya tatizo kuonekana katika ulimwengu wa mwili, hivyo kama ni nafsi yako imefungwa katika ulimwengu wa roho na umewahi kuona ndotoni mashambulizi miguuni, nakuomba shughulikia kimaombi jambo hilo na nafsi yako itaachiwa na hizo nguvu za giza.
Naamini kuna mtu anaenda kufunguliwa katika jina la YESU KRISTO kama mtu huyo akifanyia kazi.
Kumbuka pia kwamba siku zote miguu kiroho ni lango la kupitisha vitu kwenda kwenye nafsi hivyo unaweza ukashangaa unakuwa mchovu na huwezi kuomba kwa sababu ya adui amedhibiti miguu yako kiroho.
Sasa ni muhimu sana ujue umefungwa nini, inawezekana umefungwa utayari, inawezekana umefungwa nafsi na inawezekana umefungwa vyote viwili yaani umefungwa utayari na umefungwa nafsi kiroho.
Leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO kupitia maombi hakikisha unafunguliwa, fanyia kazi somo hili na utakuwa huru.
3. Maana ya tatu ya miguu kwenye ulimwengu wa roho ni ishara ya kumiliki.
Miguu kiroho imebeba nguvu za kumiliki.
Kumbu 11:24-25 " Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; tokea hilo jangwa, na Lebanoni, na tokea mto wa Frati, mpaka bahari ya magharibi, itakuwa ndiyo mipaka yenu.Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama mbele yenu; BWANA, Mungu wenu, ataweka utisho wenu na kuhofiwa kwenu juu ya nchi yote mtakayoikanyaga, kama alivyowaambia."
Maana yake mahali ambapo wateule wa KRISTO watakanyaga au wataishi, hilo eneo kwenye ulimwengu wa roho wao watakuwa watawala hivyo nguvu za giza hazitakuwa na uwezo tena kufanya chochote pale, maana wateule wa MUNGU wako pale.
Miguu hiyo ya kumiliki ni miguu ya kiroho hivyo mahali ambapo mteule wa KRISTO yuko haitakiwi nguvu za giza kutawala hapo maana mwenye nguvu za MUNGU yuko hapo, ni mmiliki kwenye ulimwengu wa roho.
Nguvu hiyo ya miguu kiroho inakuwezesha kumiliki.
Pia ni vyema kujua kwamba vipo vitu vingi vya kumiliki mojawapo ni uchumi.
Kumbu 28:6 "Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo."
Mawakala wa shetani wakati mwingine ndotoni unaweza kuwaona wanamiliki miguu yako kiroho na kuifunga kipepo watakavyo.
Ayubu 13:27 "Waitia miguu yangu katika mkatale, na kuyaaua mapito yangu yote; Wajiandikia alama kuzizunguka nyayo za miguu yangu;"
Hapo inakupasa upambane kiroho kwa njia ya maombi ili kufungua vifungo vya giza na kuwashambulia wao Kwa maombi ya vita katika jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Unapoona kwenye ulimwengu wa roho unafungwa miguu ujue maana mojawapo ni kwamba unazuiliwa kumiliki na kutawala ama unaondolewa uwezo wa kumiliki ili kufanikisha kusudi jema.
Kumbuka shetani huwinda kusudi hivyo anaweza kukufunga miguu kiroho ili azuie kusudi.
Je unakusudia nini mwaka huu?
Unakusudia kusoma, kufunga ndoa, kupata kazi, kuanzisha mradi, kuhubiri Injili, kuanza huduma n.k
Ukiona adui anashambulia miguu ujue wakati mwingine lengo lake azuie kusudi jema, omba ndugu ili kuharibu nguvu za giza na kujikomboa.
Wakati mwingine nguvu za giza huiwinda ardhi ambayo wewe utaikanyaga kwa miguu yako kiroho ndio maana unaona adui akiwa na vita kwenye miguu yako.
Kumbuka ardhi hutumika kujenga hivyo adui anaweza kukuzuia kujenga
Kumbuka pia kama ambavyo MUNGU hutumia ardhi fulani hivi kujenga ufalme wake, shetani nae hutumia ardhi kusimamisha ufalme wake.
Kwa sababu wewe uliyeokoka unaweza kwenda mahali na ukafika katika ardhi ambayo nguvu za giza zimetawala, unachotakiwa kufanya ni kumiliki eneo hilo kiroho kwa maombi katika jina la YESU KRISTO huku ukitumia damu ya YESU KRISTO ili nguvu za giza zisiinuke tena hapo.
Inakupsa wewe kumiliki eneo hilo kwenye ulimwengu wa roho ndipo nguvu za giza zitaliachie hilo eneo.
Yoshua 1:3 "Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa."
Kumbuka maisha ya kiroho yanategemea nani anamiliki eneo ulilopo kiroho.
Unaweza ukaenda sehemu na kila kitu kwako kikabadilika kwa sababu ya mmiliki wa eneo hilo kiroho, hakikisha kila unapoenda unapamiliki eneo hilo kiroho ili nguvu za giza zisikuzuie kufanikisha kusudi lako.
Kuna Wakati nilimshangaa sana MUNGU, ilikuwa hivi, kwa siku mbili niliamua tu kulala Kanisani usiku, kipindi hicho familia yangu walikuwa wamesafiri, siku ya kwanza niliota ndoto kadhaa Nikijulishwa mambo yatakayotekea siku chache zijazo, kesho yake niliwasimulia rafiki zangu na mambo yakaja kutokea kama nilivyoota wakaanza kusema "wewe ni nabii " nikawa tu nacheka na kusema mimi sio nabii, siri ilikuwa kulala Kanisani.
Mwaka jana pia niliingia maombi ya kufunga siku tatu kavu, nikaamua kuishi kanisani kwa siku hizo tatu, siku ya kwanza niliota ndoto 7 na zote za kweli na sikusahau hata ndoto moja. Nilichogundua ni kwamba kuna uhusiano wa kiroho kati ya ardhi ya eneo ulilolala na wewe, fanyia mazoezi katika hilo na utanipa majibu.
Ardhi kiroho kama inamilikiwa na nguvu za giza usipoomba vyema unaweza kushangaa unaota ndoto za vitisho na za ajabu ajabu lakini ukiwa katika ardhi ambayo kuna nguvu za MUNGU pale ndoto zake ni ujumbe wa MUNGU moja kwa moja.
Unaweza kwenda mahali na ukashangaa ndoto unazoota ni za kufukuzwa tu kwa sababu ardhi ya eneo hilo inamilikiwa kiroho na nguvu za giza hivyo hawakuihitaji hapo wewe mteule wa KRISTO.
Sasa ndugu, nakupa ushauri huu, hakikisha ulitembelea popote, kwa maombi miliki kwanza eneo hilo ndipo kusudi la MUNGU kwako itatimia.
Mnaweza mkaandaa mkutano wa Injili na mkautangaza sana lakini kama hamjashughulikia kiroho ardhi msishangae kuona hakuna mtu anakuja mkutanoni, ndugu miliki kwanza ardhi kiroho ndipo kusudi jema ulilobeba litatimia.
Miguu kiroho ina nguvu za kukunyaga nguvu za giza na kuzishinda.
Luka 10:19 "Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru."
Wakati mwingine unapoona shambulio kwenye miguu yako ujue adui kakuondolea nguvu za wewe kumshambulia yeye kiroho.
Wachawi huloga pia aridhi ili anayekanyaga basi adhuhurike.
Mfano hai ni huu,
Ezekieli 21:21 "Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini."
Hivyo ombea ardhi yako au ya eneo lako la biashara au ya eneo unalohamia n.k
Shetani akitaka kukuondolea na kukuzuia njia moja wapo anashika miguu yako kiroho na anafanya iwe miepesi kufuata mabaya yanayokutenga na MUNGU.
Mithali 1:16" Maana miguu yao huenda mbio maovuni, Nao hufanya haraka ili kumwaga damu."
Nini ufanye kuhusu miguu yako kiroho inaposhambuliwa.
1. Tubu kwa ajili ya dhambi zako au makosa yako yaliyo kufungulia nguvu za giza kuondoa utayari wako.
Rejea kwa MUNGU kwa toba ili akusamehe na kukusaidia.
Isaya 55:7 "Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa."
Je miguu yako kiroho imevalishwa nini hata kusudi la MUNGU limezuilika kwako?
Na kama miguu yako imevalishwa vitu vibaya tubu.
Yoshua 5:14-15 " Akasema, La, lakini nimekuja sasa, nili amiri wa jeshi la BWANA. Yoshua akapomoka kiusouso hata nchi, naye akasujudu, akamwuliza, Bwana wangu aniambia nini mimi mtumishi wake? Huyo amiri wa jeshi la BWANA akamwambia Yoshua, Vua viatu vyako miguuni m
wako; kwa kuwa mahali hapo usimamapo ni patakatifu. Yoshua akafanya vivyo."
2. Pambana kimaombi na adui uliyemwona kwenye ulimwengu wa roho akihusika na miguu yako juu ya ardhi fulani akitaka kukizuia.
Kumbu 2:24 "Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano."
Anza kumiliki kwa maombi huku ukipambana na adui aliyeshikilia eneo hilo kiroho.
Pambana na adui aliyekufunga utayari.
Pambana na adui aliyekufunga nafsi.
Pambana na adui aliyeishikilia ardhi kiroho.
Kumbuka ni adui gani unapambana naye, ni nani, amevaa sura ya nini n.k,
Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."
Pambana naye kwa jina la YESU KRISTO.
3. Takasa miguu yako kiroho ili utayari wa ki MUNGU uje kwako.
Walawi 11:44 "Kwa kuwa mimi ni BWANA, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yo yote, kiendacho juu ya nchi."
4. Muombe MUNGU akupe utayari katika yote yanayohitaji utayari.
Mfano ni utayari wa kufanya kazi ya MUNGU.
Waefeso 6:15 "na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;"
Kumbuka pia kulifuata Neno la MUNGU ili mkono wa MUNGU ukusaidie kufanikiwa.
Zaburi 119:173 "Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, Maana nimeyachagua mausia yako."
5. Mwambiye MUNGU akuongoze kwenye njia ya Amani.
Luka 1:79 "Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani."
6. Omba MUNGU aifanye miguu yako kiroho ipitie katika kusudi lake.
Mfano ni huu.
Zaburi 18:32-33 " MUNGU ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu. Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu."
Omba MUNGU aifanye miguu yako kuwa miguu ya kilungu.
Kulungu ni mnyama ambaye miguu ya nyuma hukanyaga sehemu miguu ya mbele ilikanyaga.
Hivyo MUNGU anataka tukanyage kwenye hatua zake.
Jifunze sana Neno la MUNGU katika KRISTO YESU ili ujue kutembelea kwenye kusudi la MUNGU.
7. Mshukuru MUNGU maana umefunguliwa na uko huru sasa.
1 Nyakati 29:13 "Basi sasa, MUNGU wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu."
MUNGU akubariki Sana kwa kujifunza somo hili na kulifanyia kazi.
MUNGU akufungue miguu yako kiroho wewe uliyefungwa.
Bwana YESU KRISTO akurudishie utayari wako katika yote yaliyo yako katika kusudi la MUNGU.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi Katika shamba la MUNGU.
+255714252292
Ubarikiwe.

Comments