MAELEKEZO YA KIBIBLIA YA MUME KWENYE NDOA YAKE.

Mr & Mrs Peter Mabula 
Watendakazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote. 
 Karibuni tujifunze Neno la MUNGU. 
Leo Nazungumzia baadhi ya mambo muhimu sana ya Mume kujua na kuzingatia katika ndoa yake.

✓✓Kuoa au kuolewa Kikristo kwa ndoa takatifu sio jambo linalojitokeza tu bali ni mpango wa MUNGU. 
Mwanzo 2:24 "Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja."

Katika ndoa MUNGU ametoa maelekezo katika kila jinsia ndani ya ndoa. 
✓✓Kuna maelekezo kwa ajili ya Mume na kuna maelekezo kwa ajili ya mke. 

Leo tutaangalia baadhi ya maelekezo ya kibiblia  kwa Mume mwema. 

1. MUNGU anataka Mume ampe upendo Mkewe. 

Waefeso 5:25 "Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama KRISTO naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;"

Mume kumpenda Mkewe ndio Kusudi la MUNGU.
Mpende mkeo Kimwili,  kihisia na kiroho. 
Wewe Mume hakikisha unampenda mke wako,  huyo ndiye uliyepewa na MUNGU hivyo mpende
Mpende mkeo hata kama inakugharimu.
 
Mpende mkeo  kama nafsi yako.
Waefeso 5:33 "Lakini KILA MTU AMPENDE MKE WAKE kama nafsi yake mwenyewe; ............."

Kama ambavyo unaitunza nafsi yako hata nafsi ya mkeo ipende na itunze. 

2. Usiwe na uchungu na mkeo. 

Wakolosai 3:19 "Ninyi waume, wapendeni wake zenu MSIWE NA UCHUNGU NAO."

Uchungu ni nini? 
Uchungu ni masikitiko au masononeko ya ndani moyo wa mtu ambayo hayana mwisho wa haraka.

Uchungu unaweza kuleta madhara makubwa katika ndoa yako kama wewe Mume utakuwa mtu wa kubeba uchungu. 
Hata kama yamkini kuna kitu kidogo hakijaenda Sawa achilia na samehe ili usimezwe na dhambi ya uchungu.
Sio mkeo kakukosea kidogo tu wewe unakaa na uchungu wiki nzima au mwezi,  na katika huo muda una uchungu utamchukia mkeo,  hutatimiza baadhi ya majukumu yako katika ndoa yako na familia hivyo kusababisha madhara makubwa. 

Biblia inakusaidia wewe Mume kwamba  usiwe na uchungu na mkeo. 
Na dawa ya uchungu ni kuachilia tu,  achilia na songeni mbele. 
Sio mkeo ameweka chumvi nyingi kwenye mboga unachukia na kujaa uchungu wiki nzima,  hutoi matumizi na mke na watoto wanaanza kutafuta chakula kwa majirani kisa tu Baba wa familia Kwa sababu ya uchungu amesusa kuwajibika katika familia yake. 
Biblia inasema Mume hakikisha huwi na uchungu na mkeo bali Mpende mkeo kama nafsi yako.  

3. Mvumilie mkeo.

Kuvumilia maana yake ni kustahimili Shida,  tatizo na mateso yanayoweza kujitokeza. 
Hivyo Mume hakikisha unakuwa na uvumilivu wa kudumu kwa mkeo. 

Hakikisha kwa mke wako unakuwa na upendo unaovumilia maana Kuvumilia ni Moja ya sifa kuu za upendo. 

1 Wakorintho 13:4 "UPENDO HUVUMILIA, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;"

Sio mkeo hajabeba mimba katika Miaka miwili tu ya ndoa unaanza kumnyanyasa na kumtisha kwamba utaachana naye kwa sababu tu hajazaa,  Vipi kama tatizo la kukosekana uzao ni lako Mume,  hata kama tatizo kweli ni la mke bado Kibiblia ni wajibu wako Kuvumilia huku mkiomba na MUNGU atawapa uzao. 

Ukisoma katika Waebrania 6:15 unaona ujumbe ukimhusu Ibrahimu ambaye Mkewe alikuwa tasa,  ila kwa kumhusisha MUNGU na kuvumilia aliipata Ahadi ya kupata uzao katika ndoa pale walipompata Isaka. 
 
Waebrania 6:15 "Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi."

Japokuwa tunajua kwamba Ibrahimu kabla ya kumpata Isaka alimzaa Ishumaeli lakini ukisoma Biblia unaona kabisa kwamba Ishumaeli alipatikana kwa Sababu Sarah ndiye alikosa uvumilivu na sio Ibrahimu kukosa uvumilivu. 

Mwanzo 16:2 "Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai."

Yaani mke ndiye alikosa uvumilivu na kumruhusu mumewe kuzaa na mwanamke wa nje aitwaye Hajiri, haikuwa mpango wa MUNGU na ni dhambi mwanandoa kuzaa nje ya ndoa.
   
Kuvumilia Katika ndoa ni jambo jema sana na litaifanya ndoa yenu kuwa hai daima.

Kuna vitu vingi vidogo tu huwafanya Watu kukosa uvumilivu kwa wake zao,  haipasi kuwa hivyo katika ndoa za waenda mbinguni waliokolewa na Bwana YESU KRISTO Mwokozi. 
Mume hakikisha unakuwa na uvumilivu mkubwa kwa mkeo. 
Katika ndoa ni lazima kuvumiliana. 

4. Ishi na mke wako kwa akili.

1 Petro 3:7 "Kadhalika ninyi waume, KAENI NA WAKE ZENU KWA AKILI; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe."

Mume kuishi na mke kwa akili ni nini? 

✓✓Kuishi na mke kwa akili Kibiblia  ni kuhakikisha katika maisha ya ndoa yenu hamtoki katika Kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU.

Hiyo ndio maana ya kwanza ya Mume kuishi na mke wake Kwa akili. 

Ili tupate majibu ya maana ya Pili ya Mume kuishi na mke wake kwa akili tuangalie maana ya neno "akili"
Akili ni uwezo wa kujua kitu au jambo. 

✓✓Hivyo Mume kuishi na Mkewe kwa akili maana yake ni Mume kuishi na Mke wake huku akiwa na uwezo wa kujua vitu au mambo mbalimbali muhimu katika mambo yote yanayohusu ndoa yao na familia. 

Kumbuka Mume ndiye kiongozi wa familia, alikosa akili ni hatari sana kwa ndoa hiyo. 

Mfano wakati mwingine sio wanawake wote Katika ndoa zao   wana ujasiri wa Kuwaambia waume zao kwamba wanataka tendo la ndoa,  hivyo mume inakupasa uwe na akili yaani uwe na uwezo wa kutambua ili utimize wajibu wako kwa mke wako. 
Inawezekana kabisa unafanya kazi ngumu na hivyo ukifika nyumbani umechoka sana,  lakini tumia akili vyema  maana uko katika ndoa na wahusika wa ndoa sio wewe peke yako bali ni wewe ni mkeo. 

Nimewahi kuongea na Watu wengi kwa simu kwenye huduma za maombezi, ni kawaida kabisa mama kukuomba umuombee Mume wake maana wana Mwaka au miezi 6 au miezi 4 bila kukutana Kimwili,  Mume kila siku kachoka na ana stress za kazini. 
Mwanaume ni muhimu uishi na mke wako kwa akili katika utakatifu. 

Kuna wanaume kwa kukosa akili waliwafanyisha kazi ngumu wake zao walio wajawazito na kupelekea kuharibika mimba na hata kutokea madhara zaidi,  yaani kuna wanawake wanaenda shambani kulima hata kama mimba muda wa kujifungua umefika,  yaani Mume anaamrisha tu.

Akili njema inahitajika sana kwa Mume katika ndoa yake. 
Vipo vitu vingi sana vinahitaji akili njema ya Mume katika ndoa yake ili ndoa yake istatawi. 

 5. Mkubali mkeo alivyo na ridhika naye.

1 Timotheo 6:6 "Walakini UTAUWA PAMOJA NA KURIDHIKA ni faida kubwa."

✓✓Maana ya kuridhika ni kutosheka. 
Hivyo ridhika na mkeo yaani tosheka na yeye tu. 

Mkubali mkeo maana huyo ndiye mke wako uliyepewa na MUNGU Baba. 

Usimkubali mkeo kwa anayokufanyia bali mkubali alivyo. 
Onyesha mahali pote kwamba huyo ndiye mkeo umpendaye. 
Ukimkubali mkeo huwezi kamwe kumsaliti.
Ukiridhika na mkeo hiyo itakuwa faida ya ndoa yako na watoto wenu pia. 

6. Msikilize mkeo. 

Yakobo 3:17-18 "Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, TAYARI KUSIKILIZA MANENO YA WATU, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani."

Kama wanandoa ni vyema sana mkiwa Watu wa kusikilizana, hasa wewe Mume Inakupasa uwe mtu wa kumsikiliza sana mkeo maana hana mtu wa kumwambia zaidi isipokuwa wewe. 

Kwa asili wanawake huongea zaidi kuliko wanaume hivyo Msikilize mkeo maana ni mkeo. 

Wanawake wanapenda kusikilizwa.
Tumia maneno laini unapoongea na mkeo. 
 Tumia maneno laini  na sio maneno mazito na ya kuumiza. 
Mpe amani na ajisikie yuko na Mume bora. 
Sikiliza ushauri wa mkeo na jadiliana naye kwa amani na upendo. 

7. Ishi kwa amani na mke wako. 

Waebrania 12:14 "Tafuteni kwa bidii KUWA NA AMANI NA WATU WOTE, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona BWANA asipokuwa nao;"

Biblia inapokuagiza utafute kuwa na amani na Watu wote ujue hata mkeo ni sehemu ya Watu wote. 
Ishi kwa amani na mkeo maana ni huyo ndiye ulipewa na MUNGU.

Kuna wanandoa huishi kama kondoo na simba,  hakuna amani, ni vita, matukano na hata kupigana,  haifai kuwa hivyo kamwe.  
Lakini wewe Mume uliye na YESU KRISTO hakikisha unaishi kwa amani na Mke mwema wako. 
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By  Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii  kupiga, Sadaka, kuandika meseji na hadi whatsapp).

Comments